Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa ulipwaji fidia kwa wananchi zaidi ya 2,000 wa Wilaya ya Longido na Monduli ambao maeneo yao yalipitiwa na Mradi wa Umeme Vijijini (REA)?

Supplementary Question 1

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba Serikali imesema kwamba hakuna fidia katika miradi hii ya umeme wa REA. Ningependa kujua sasa kwamba je, Serikali ipo tayari kuwaelimisha wananchi kujua kwamba hakuna fidia kabla miradi ile haijaanza kutekelezeka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna vijiji vingi sana hapa Tanzania ambavyo vimepitiwa na nguzo juu lakini umeme haujashuka kwenye vijiji vile na katika nchi yetu ya Tanzania pia hata katika Jimbo langu limeshuhudia kuna vijiji mpaka sasa mradi wa umeme ulipita tangu mwaka 2014, nguzo zimepita juu lakini wananchi hawajashushiwa umeme.

Je, Serikali ipo tayari sasa kuangalia vijiji hivyo vyote Tanzania nzima na kuhakikisha kwamba vijiji hivi vinapatiwa umeme vikiwemo vile vya Jimbo la Busanda ambavyo vipo vingi Nyaruyeye na Busaka hawajapata umeme? Niombe Serikali iweze kunijibu. (Makofi)

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Lolesia kwa kazi nzuri anayoifanya lakini maswali yake amejielekeza kwenye namna gani Serikali itaelimisha wananchi. Nichukue fursa hii kwanza kuwashukuru Watanzania wote kwa maeneo mbalimbali ambapo miradi hii ya REA inatekelezeka, kwa kweli Serikali, REA,TANESCO hata na Wizara yenyewe ya Nishati haijapata changamoto kubwa ya madai ya fidia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwanza Watanzania wenyewe wapo tayari, lakini sisi tutaendelea kuelimisha kadiri tutavyopata fursa kwenye ziara mbalimbali za Mikoa na Wilaya ikiwemo kwenye Jimbo lake la Busanda kwamba wananchi kwa kweli kwa kuwa Serikali inalipia gharama zote na wao wanalipia VAT tu shilingi 27,000 na haijawahi kuwa kikwazo, tutaendelea kutekeleza mradi huu na tunawaomba watupe nafasi zaidi na waiunge mkono Serikali yetu ya Awamu ya Tano yenye nia ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2021 vijiji vyote 12,268 vinapata umeme.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza katika vijiji ambavyo vimepitiwa na umeme wa msongo mkubwa lakini havijashushiwa umeme, nikiri kweli tatizo hilo lipo na hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Nishati alivyofanya ziara katika maeneo mbalimbali ya hapa Dodoma, maeneo ambayo miundombinu ya umeme mkubwa imepita lakini hawajashushiwa, wametoa maelekezo kwa TANESCO kwamba ifikapo Desemba 2019 maeneo yote yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme haijashushwa umeme, ishushwe kwa sababu katika maeneo hayo kinachofanyika ni ujenzi wa line ndogo LV na kuweka transfoma na kuwaunganishia wananchi umeme kwa bei ileile ya shilingi 27,000. Kwa hiyo, nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge ikiwemo vijiji alivyota kwenye Jimbo lake la Busanda, Mkoa wa Geita na mikoa mingine yote nchini kwamba tatizo hilo kwa kweli tunaliona na tumeshaliwekea mikakati kama miradi ya Quiq Wins katika kupelekea utekeezaji wa mradi huo. Nakushukuru sana.

Name

Dr. Stephen Lemomo Kiruswa Mamasita

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Longido

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:- Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa ulipwaji fidia kwa wananchi zaidi ya 2,000 wa Wilaya ya Longido na Monduli ambao maeneo yao yalipitiwa na Mradi wa Umeme Vijijini (REA)?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza kwenye Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, sisi katika Wilaya ya Longido na hata Monduli pia, tumepitiwa na umeme wa msongo mkubwa na napenda kuishukuru Serikali kwa sababu wameshalipa fidia kwa watu wale ambao walistahili kufidiwa, lakini pia naomba kuuliza kwa sababu vijiji vilivyopitiwa katika Wilaya yangu ya Longido ni vitano; Eorendeke, Kimokorwa, Oromomba, Ranchi na Engikaret kuna maeneo mahsusi ambayo jamii iliyatenga kama maeneo ya wazi wakitarajia kwamba fidia yake itakwenda kurudishwa ndani ya kijiji waweze kufanyia miradi ya maendeleo kama kujenga shule, zahanati na kuboresha miundombinu mbalimbali ambayo ni pungufu sana ikiwa ni pamoja na barabara katika vijiji vile.

Mheshimiwa Spika, je, ni lini Wizara itarejesha hizo fedha za maeneo ambayo jamii iliyatenga kama maeneo ya wazi kwa vijiji husika au halmashauri ili tuweze kufanyia hayo maendeleo ambayo tayari wananchi wameshabainisha? Ahsante sana.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa na nimpongeze kwa kufuatilia masuala ya nishati hususan fidia ya wananchi wake.

Mheshimiwa Spika, ni kweli maeneo aliyoyataja ikiwemo Wilaya ya Longido yamepitiwa na njia ya msongo wa KV 400 kutoka Singida – Namanga na tumeshalipa fidia takribani kama shilingi bilioni 44 na maeneo aliyosema ambayo yalikuwa ya maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za jamii, thamani yake ya fidia ni kama shilingi bilioni 10, utaratibu unaendelea wa kuweza kuyalipa katika maeneo mbalimbali ili pesa hizo ziweze kuchangia shughuli za maendeleo, nakushukuru.