Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:- Katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018 Serikali iliondoa kodi kwenye taulo za kike (pads) jambo ambalo ni muhimu sana kwa maisha ya Wanawake na Wasichana mpaka sasa ni mwaka mmoja tangu kodi hizo ziondolewe lakini bei ya taulo za kike haijashuka licha ya kuondolewa kwa kodi hizo Nchi nzima. Je, ni lini Serikali itasimamia kwa ukamilifu suala hilo ili bei za taulo za kike zishuke na kusaidia afya za Wanawake hususani Wasichana?

Supplementary Question 1

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ninasikitika sana kwa majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, tulipoomba Serikali itoe kodi na ikakubali ilikuwa ni furaha kwa Wanawake wengi wa Nchi hii ya Tanzania. Jana ilikuwa ni siku ya hedhi salama kwa wanawake duniani. Tumeonana na wadau wanaoshughulikia pads, hakuna lalamiko walilolitoa juu ya uendeshaji zaidi ya kodi ambayo Serikali imetoa kwa wanao- import na kuwaacha watengenezaji waliko hapa nchini.

Swali langu; ni nini Serikali itafanya kuweza kusaidia wawekezaji wa ndani wanaotengeneza taulo hizi ikiwemo Jessy, HQ na wengineo ili kuweza kupunguza gharama ya taulo za kike?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali itakubali kuweka ulazima wa wauzaji wanaouza taulo hizi kuweka gharama ya bei katika taulo hizo ili kufanya bei zote zifanane kama ilivyo kwa mazao kama ya Coca cola na Pepsi nchi nzima ina bei moja. Serikali itachukua wazo letu la kuona wkamba ni lazima iandikwe bei katika taulo hizo ili kukwepa kwa wale wanaoweza kuongeza hasa wasafirishaji na wauzaji na bei hii iweze kupungua.

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kusahihisha alichokisema kwamba wazalishaji wa ndani bado wanalipa kodi ya ongezeko la thamani kwenye bei ya bidhaa hizi, hapana. Tumeondoa kodi ya ongezeko la thamani kwenye bidhaa hii kwa bidhaa zinazotoka nje ya Nchi na zile zinazozalishwa ndani ya Nchi ndiyo maana nikasisitiza kwenye jibu langu la msingi, majibu ambayo Serikali iliyatoa kwa swali namba 2938 ambalo liliulizwa na Mheshimiwa Stella Ikupa Allex na kwa mwongozo wako naomba kulisoma swali lake liliuliza hivi:-

“Kutokana na umuhimu wa taulo za kike Nchini, Je, Serikali inaonaje ikiondoa kodi kwenye taulo hizi?”

Mheshimiwa Spika, Serikali ilisema kwenye swali hili kwamba ukiondoa kodi haiwezi kuleta atahari moja kwa moja kwenye bei ya bidhaa husika kwa sababu bidhaa husika inategemea mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, tukienda Nchini Botswana, tukaenda Nchini Kenya ambako waliwahi kuondoa kodi kwenye bidhaa hizi hakuna athari yoyote iliyoonekana kwenye taulo hizi za kike. Kama tunataka kweli kumsaidia mtoto wa kike kama kweli tuna dhamira ya dhati ya kumsaidia mtoto wa kike, naomba tuisikilize Serikali inasema nini; Serikali siku zote imekuwa ikisisitiza kwamba, sisi kama Serikali tuna mpango na tayari tumeanza kufanya mchakato wa kuona ni jinsi gani ya kutoa bidhaa hii bure kwa watoto wa kike na siyo kuondoa kodi jambo ambalo halina athari yoyote zaidi ya kupunguza mapato ya Serikali. Jambo hili lilipelekwa kisiasa zaidi na mimi nawaomba kwenye mambo ya msingi yanayogusa Watanzania tusiingize siasa, hilo ndiyo suala ambalo nataka kuliweka hivyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili baada ya majibu yangu haya ya swali lake la kwanza, hakuna ulazima wowote wa kuandika bei kwenye bidhaa hizi kwa sababu tuko kwenye soko huria na Serikali yetu hatutaki kuingilia jambo hili, tunachohitaji ni kuja na mpango wa kibajeti wa ku-deal na jambo hili ili tuwasaidie watoto wetu wa kike.