Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:- Je, Serikali imejipangaje kutekeleza mojawapo ya malengo katika Mpango wa Maendeleo wa miaka 5 kwa Taifa 2016/2017, 2020/2021 katika kupanua wigo wa Utalii nchi (diversification)?

Supplementary Question 1

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi na pamoja na vivutio hivyo bado iko nyuma sana kwenye Utalii kwa mfano Utalii wa fukwe kuliko nchi za wenzetu waliotangulia Kenya, Msumbiji na Zanzibar.

Sasa nataka kufahamu ni lini Serikali yetu itayazingatia na kuyapa umuhimu kipaumbele maeneo ya Coco Beach na kuona kwamba yanaendelezwa ili yaweze kufikia malengo hayo na kuleta watalii wengi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili ningependa kufahamu kwamba kwa mfano nchi zinazoongoza kwa kupokea watalii wengi kwa mfano Swaziland, USA Brazil na nchi nyingine za jirani zimewekeza katika aina mbalimbali za Utalii kwa mfano vitu vingine Mheshimiwa Waziri amevitaja kwa mfano, Cable car ikiwemo nchi jirani ya Rwanda balloons.

Je, ni lini sasa Tanzania itaona kipaumbele na kuwekeza katika maeneo hayo ili kuwepo basi kwa mfano kule Kilimanjaro Cable cars watalii waweze kuja wengi na kuliingizia pato nchi yetu ya Tanzania? Ahsante. (Makofi)

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Amina Mollel kwa sababu katika maswali ambayo nimekuwa nikijibu hapa nimeshajibu maswali yake matatu yote yakihamasisha uhifadhi na Utalii nakupongeza sana Mheshimiwa Amina Mollel. Kama nilivyojibu ni kweli kwamba Tanzania tumekuwa na Utalii wetu wa asili ambao umezingatia sana safari kwa maana ya kutembelea mbuga za wanyama na maeneo mengi ambayo yamepatia nchi nyingine pesa nyingi za kigeni kama Utalii wa fukwe na aina nyingine za Utalii kwa kweli zimekuwa hazikuzingatiwa.

Mheshimiwa Spika, sasa ili kufikia katika malengo hayo Wizara imeliona hilo tuliunda kikosi kazi maalum cha kutafiti kwa nini Tanzania imekuwa nyuma katika Utalii wa fukwe na tukagundua kwamba palikuwa na udhaifu katika usimamizi wa hizi fukwe, fukwe nyingi zimevamiwa, lakini fukwe nyingi zimepewa watu ambao wameshindwa kuziendeleza. Katika kulibaini hilo tumependekeza kuanzishwa Mamlaka maalum ambayo itakwenda kusimamia Utalii wa fukwe na kuhakikisha kwamba fukwe hizi zinaundiwa sheria maalum ili zisiweze kuvamiwa.

Mheshimiwa Spika, na katika eneo la Coco beach juhudu mbalimbali zimefanyika lakini kuna mgogoro unaoendelea kati ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika Manispaa ambayo iko katika eneo hilo na mwekezaji katika eneo hilo na Ofisi ya TAMISEMI imeingia na kuelekeza. Aidha, Manispaa wamlipe yule muwekezaji aondoke au amruhusu aendelee na kazi yake lakini kuna ucheleweshaji wa kufanya maamuzi ndio maana Wizara imeona tuanzishe Mamlaka maalum.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kweli kwamba watalii ambao tumekuwa tukiwapata katika Mlima Kilimanjaro karibu kufikia asilimia 100 ni miaka 18 na mpaka miaka 50, chini ya miaka 18 na juu ya miaka 50 hawawezi kuja kwa sababu hawawezi kupanda Mlima Kilimanjaro ili kuweza kuwapata hawa tumefikiria kushauri TANAPA kuangalia uwezekano wa kufikiria kufanya utafiti kuona kama tunaweza kuweka cable car na kama hili litafanikiwa litaweza kutuletea watalii wengi zaidi kama tulivyoona takwimu katika nchi alizozitaja.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.