Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Primary Question

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:- (a) Je Ikama ya Wataalam wa Ardhi Katika Halmashauri za Wilaya ni ipi na ni lini Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru itafikia kiwango hicho? (b) Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kurudisha eneo la Hekari takribani 2,000 za Shamba Pori la Nambarapi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili nayo irejeshe ardhi kwa Wananchi wa Vijiji husika kikiwemo Kijiji cha Nambarapi?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimimiwa Spika, nakushukuru, napongeza pia kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo nina maswali ya nyongeza mawili, swali la kwanza kuhusiana na kipengele (a) cha swali langu ili wataalam waweze kufanya kazi zao vizuri na watoe matokeo yanayostaili wanapaswa kutosha kwa idadi, pia wanapaswa kutosha kwa umahili wao yaani vile competence ya utaalam aliyonayo, pia wawe na maadili ya kitaaluma. Bila shaka ni ukweli kwamba wakiwa wachache hawawezi kukamilisha matakwa hayo.

Je, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru inaupungufu wa wataalam wa Sekta ya Ardhi, kwa zaidi ya asilimia 81 na kwa kuwa Serikali ina mpango wa muda mrefu wa kuendelea kutumia bajeti ya kila mwaka. Je katika mpango wa muda mfupi ambao ni wa kuwapanga upya watumishi katika nchi nzima Serikali iko tayari kuweka upendeleo maalum kwa halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa sababu ya changamoto zilizopo hivi sasa?

Mheshimimiwa Spika, swali la pili katika kipengele (b) cha swali langu naona hapa kuna haja ya kupambanua iko shida ya kupata ukweli na uhakika, familia ya watu wanne inayotanjwa inamiki sehemu ndogo sana ya hili eneo ni kama eka 40 tu kati ya zile eka 1,913, eneo kubwa zima linalalamikiwa na halmashauri ya Kijiji.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata kesi inayotajwa siyo kesi ambayo inahusika mahali hapa sasa mimi nafikiri wakati tunaendelea kusubiri kupata uhakika juu ya umiliki wa eneo hili na hapa nitatoa ushauri kwa ufupi. Kwa nini tusiendane na maagizo ya Serikali maagizo ya Chama cha Mapinduzi kupitia ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo kwa kujibu wa Ibara ya 37 inasema Serikali inatakiwa kutekeleza maagizo ya Chama cha Mapinduzi kupitia ilani yake kwamba ni lazima kufanya uhakiki wa mashambapori yasiyoendelezwa kwa kipindi kirefu na kuyagawa upya kwa wananchi. Sasa eneo hili la eka 2,000 kwa zaidi ya miaka 20 limebaki tu likiwa halifanyiwi kaziā€¦

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Injinia sasa swali.

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimimiwa Spika, je Serikali iko tayari sasa kuunda timu maalum kwenda kufuatilia jambo hili kwa nini linachukua miaka mingi bila kupatiwa ufumbuzi huku eneo hili likiwa likitumika kienyeji na baadhi ya watu ikiwa ni pamoja na kuwafanya wananchi walime kwenye eneo hilo katika sehemu ndogo na kuwatoza mazao yanayolimwa katika eneo hilo?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimimiwa Spika, kwanza nikiri wazi kwamba kuna upungufu mkubwa kwa nchi nzima kwa watumishi wa Sekta ya Ardhi. Ukiangalia takwimu za mahitaji tuliyonayo tunatakiwa kuwa na watumishi 2,957 kwa nchi nzima; lakini mpaka sasa tunao 1,546 na hivyo tuna upungufu wa 1,411. Kwa hali hiyo upungufu uko maeneo mengi na kwa Mheshimiwa Engineer Ramo anao watumishi wanne ni kweli ni wachache, lakini kuna halmashauri inawatumishi wawili na nyingine tuliwahi kukuta ina mmoja. Nimuombe tu awe mvumilifu na Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu zoezi hili tumesema tunalipitia upya kwa kuangalia wale tulionao kwa sasa tunaanza kuwapanga upya ili kuweza kuleta uwiano wa kiutendaji katika halmashauri zetu.

Mheshimimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe sana pamoja na kuomba upendeleo nadhani tutaangalia wakati tunapanga tuweze kuona hasa maeneo ya pembezoni ambapo mara nyingi watumishi wengi wanakwepa kwenda kule. Kwa hiyo, tutaangalia na kuwapa umuhimu wale ambao tunajua wanayo shida kubwa katika Sekta hii ya Ardhi.

Mheshimimiwa Spika, jambo la pili swali lake la pili amezungumzia kwamba ile kesi pengine ni ya watu wanne na ni tofauti na suala la wanakijiji. Kesi ile imewekwa kwenye jibu la msingi kwa sababu ndiyo hasa ilikuwa imekwambisha katika mambo yote kufanyika pale, na wale walipofungua kesi maana yake hata Kijiji kisingeweza kufanya jambo lolote kwa sababu eneo lililokuwa linagombewa ni hilo la Kijiji.

Mheshimiwa Spika, lakini tumeshaona hitaji la eneo lile kwamba wananchi wanalalamika na bahati nzuri nakumbuka kama siyo mwaka jana nadhani mwaka juzi nilikwenda pale nikafika mpaka kwenye Kijiji nikafikia kile kilio cha wananchi. Kama Serikali tuliahidi kwamba tutalifanyia kazi na baada ya kukuta kuna kesi na maamuzi yalikuwepo tukawa tumefungwa mikono hatukuweza kufanya ile. Lakini kwa sababu pia kuna agizo la Serikali la kupitia mashamba pori yote na kuweza kuyaletea maelekezo yake kwa maana ya kuleta maepndekezo kwa Mheshimiwa Waziri ili yaweze kufutwa jukumu la kufanya hivyo ni la Halmashauri yenyewe ya Tunduru, ikisha fanya hivyo pamoja na halmashauri zingine chanzo lazima kianzie kwenye halmashauri husika ndipo wizara itaendeleo.

Mheshimimiwa Spika, kwa hiyo, nitoe rai kwa mara nyingine tena kwamba suala hili linahitaji kuanzia katika halmashauri zetu mkileta kwa Waziri, Waziri atamshauri Mheshimiwa Rais kuyafuta pale ambapo tunakuwa tumejiridhisha. Na nitoe rai ni marufuku kwa Serikali yoyote ya Kijiji au kwa watu wote wachache kutumia ardhi ya Umma katika kuwafanya watu kuwa kama vibarua kwa sababu unapompa mtu ardhi na kumtoza pesa maana yake wewe tayari umeshakuwa bepari wa kutaka kunyonya wengine. Ni marufuku na kama kuna maeneo watu wanatozwa pesa kwa matumizi ya ardhi kwa maeneo ambayo wameshindwa kuyaendeleza wenyewe tupate taarifa ili tuweze kuyafanyia kazi.