Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mbarouk Salim Ali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wete

Primary Question

MHE. MBAROUK SALIM ALI aliuliza:- Pemba ni Kisiwa kinachozalisha viungo (spices) kwa wingi na wajasiriamali huzalisha bidhaa zinazotokana na viungo hivyo:- Je, ni lini wakulima na wajasiriliamali wa Pemba wataunganishwa na soko la Afrika Mashariki ili waweze kufaidika na soko hilo?

Supplementary Question 1

MHE. MBAROUK SALIM ALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na majibu hayo nina maswali mawili madogo tu ya nyongeza. Katika majibu yake ya msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba wananchi wa Pemba pamoja na wananchi wetu wa Tanzania tayari wameshaunganishwa na soko hili la Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, bado niko kwa Pemba tu, nataka nijue kwamba hii Pemba imeunganishwa kinadharia au kivitendo kwa sababu karibu mwaka wa saba huu Viongozi Wakuu wa Afrika Mashariki walikubaliana kuijenga bandari ya Wete. Hizo ni jitihada na fedha kwa mujibu wa Naibu wa Wizara hii hii aliyepita ambaye kwa sasa hivi ni Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar alisema kwamba fedha tayari zilishakuwepo. Lakini mpaka leo hakuna lolote ambalo limefanyika nilitaka kujua ni nadhalia au ni vitendo.

Mheshimiwa Spika, hizo ni jitihada na fedha. Kwa mujibu wa Waziri wa Wiizara hii aliyepita ambaye sasa hivi ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, alisema kwamba fedha tayari zilishakuwepo, lakini mpaka leo hakuna lolote ambalo limefanyika. Nilitaka kujua, ni nadharia; ni vitendo?

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri katika jibu lake pia amewataka wananchi kwa ujumla watumie fursa zilizopo ili kulitumia soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Niseme tu kwamba kuna vikwazo vikubwa vya tozo nyingi pamoja na ushuru hasa katika uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa hizo:-

Je, ni lini Serikali nitaondoa tatizo hili hasa kwa wajasiliamali?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

Name

Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote, namshukuru Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, Mbunge wa Wete kwa kuuliza maswali yake mawili ya nyongeza. Swali la kwanza amesema: Je, Pemba imeunganishwa kwa nadharia au kwa vitendo? Akitolea mfano ujenzi wa bandari kule Pemba.

Mheshimiwa Spika naomba kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Pemba imeunganishwa kwa vitendo kwa sababu Pemba ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jamhuri yote ya Muungano wa Tanzania imeunganishwa kwa vitendo kwa maana ya soko la pamoja, ambapo ndilo swali lake la msingi. Kwa maana ya mradi ya kimaendeleo ambayo ameisema, miradi hiyo inafanyika sehemu mbalimbali, sehemu zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kuhusiana na Bandari ya Pemba tulishajibu ndani ya Bunge hili kwamba Serikali kwa kushirikiana na Afrika Mashariki inashughulikia mradi huo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, anasema kuna vikwazo vikubwa vya tozo na ushuru. Maana ya soko la pamoja ni kwamba endapo bidhaa inakidhi vigezo vya uasili wa bidhaa (rules of origin), haipaswi kutolewa ushuru au tozo yoyote endapo inasafirishwa au kuuzwa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Bidhaa ambazo hazikidhi vigezo kama niliongea kwenye jibu la msingi, ni kwamba zimetolewa nje ya Jumuiya Afrika Mashariki, lazima zilipe ushuru au common external tariff ambayo imewekwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.