Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:- Kuna upungufu mkubwa wa Walimu katika Shule za Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba:- Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba?

Supplementary Question 1

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba sasa niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika Mkoa wa Kagera, Halmashauri ya Bukoba na hasa Jimbo la Bukoba Vijijini ni mahali ambapo hawafanyi vizuri kielimu katika matokeo na hasa darasa la saba lakini pamoja mambo mengine ni ukosefu wa walimu na ni tatizo la muda mrefu. Kutokana na jibu la msingi bado kuna mahitaji ya walimu zaidi ya 500. Je, Serikali inalichukuliaje jambo hili na kuhakikisha walimu wanapatikana ili Bukoba Vijijini na yenyewe iweze kwenda mbele kielimu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, yapo maeneo mengine katika Halmashauri mbalimbali za Tanzania ambapo yako mbali kabisa yaani tuseme ni remote areas ambapo walimu wakipelekwa hawaendi. Je, Serikali ina mpango gani kufanya uwiano kwa kuhakikisha walimu wanaenda katika maeneo hayo ili Watanzania wote waweze kufaidika na mfumo wa elimu uliopo katika nchi?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema ni kwamba tutaendelea kufanya kila liwezekanalo na hasa katika mpango wa kuajiri walimu. Naomba nimhakikishie kwamba tutaweka kipaumbele katika Mkoa wetu wa Kagera tukijua kwamba mkoa huu ni miongoni mwa mikoa ya pembezoni na tunajua kwamba lazima tufanye juhudi ya kutosha. Kwa hiyo, katika mipango ya baadaye suala la walimu katika Halmashauri ya Bukoba tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la nini Serikali inafanya kuhakikisha usambazaji wa walimu unafanyika, kutokana na changamoto hiyo, tulichokifanya kupitia mpango wa PforR tumehakikisha tunafanya msawazo wa walimu. Tulipeleka fedha katika maeneo mbalimbali kuhakikisha walimu wanatawanya na tuliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wale walimu waliojazana mijini wanahamishwa kwenda maeneo ya pembezoni kwa kupewa posho maalumu za kuwahamisha walimu ili hata watu wa pembezoni wafaidike na programu hii ya elimu bila malipo ambapo ni jambo jema kwa ajili ya vijana wetu. Kwa hiyo, suala hili tunalifanyia kazi kwa nguvu zote Mheshimiwa.

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:- Kuna upungufu mkubwa wa Walimu katika Shule za Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba:- Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba?

Supplementary Question 2

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwanza naomba nitoe pongezi zangu na niwatakie kheri wanafunzi wote wa kidato cha pili kote nchini kwa kuanza mitihani yao ya taifa leo hii.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, nataka nijikite kwenye swali la msingi. Kwenye Halmsahauri ya Lindi Vijijini sasa hivi ni Halmshauri ya Lindi Mjini kwenye Jimbo la Mchinga, Kata ya Mpingo kuna shule shikizi. Bahati nzuri hiyo shule shikizi wananchi wamejitahidi, wamejenga na kule kuna wafugaji huenda mwakani ikaanza. Tatizo letu ni vifaa vya vitakavyotumika kwa ajili ya wanafunzi wale kujifunza na kujifunzia.

Je, Serikali itatusaidiaje kwenye tatizo hili kwa ajili ya wale wafugaji waliopo kule? Ahsante.

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Salma Kikwete ambapo namuita kama Balozi wa Elimu katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu Mheshimiwa mama Salma amechukua muda wake mwingi sana ku-invest kusaidia watoto wa Kitanzania wapate elimu. Kwa hiyo, mama tunakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, eneo hili ambalo amelizungumzia ni eneo la wafugaji, ni shule shikizi, kwa heshima ya mama yetu, naomba nimuagize Mkurugenzi wangu wa Elimu amuagize Afisa Elimu Mkoa atembelee haraka Shule hiyo Mpingo kwenda kufanya needs assessment kuona kuna jambo gani la haraka linatakiwa kurekebishwa mapema ili itakapofika Januari watoto waweze kupata matunda mazuri ya swali hili.

Kwa hiyo, namuagiza Mkurugenzi wangu aweze kufanya kazi hiyo haraka iwezekanavyo.