Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Primary Question

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa utekelezaji mipango yake pamoja na maelekezo ya Mhe. Rais ya kushughulikia kero za wachimbaji wadogo hususani katika maeneo ya uchimbaji ya Ng’apa Mtoni na Muhuwesi?

Supplementary Question 1

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu ya Serikali lakini pia niipongeze Serikali kwa hatua mbili hizi ya kwanza ya kutufungulia soko la madini Tunduru Mjini hali ambayo imeweza kuboresha shughuli na biashara ya madini kwa ujumla kiasi cha kuwaongezea kipato wachimbaji wadogo Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru lakini na Serikali kwa ujumla. Pia pongezi kwa kututengea maeneo katika eneo la Mbesa lakini pia kwenye eneo la Ngapa Mtoni. Nina maswali mawili madogo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uboreshaji uliokwishafanyika ambao ni mzuri na umetuletea mafanikio makubwa bado ziko changamoto kwenye maeneo ya afya, usalama na mazingira na changamoto nyingine zinazohusiana na ugawanaji wa maeneo kwenye maeneo makubwa yaliyotengwa na Serikali. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana na mimi kwenda kwa wananchi hawa kuwasikiliza kwa karibu sana na kuratibu changamoto zao na kuzipatia majawabu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili wanawake ni mahodari sana wa kuunda vikundi na kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za ujasiriamali ni mahodari sana kwenye ujasiriamali na kuunda vikundi na kujishughulisha katika mambo ya ushirika.

Je, wakinamama wa Tunduru watasaidiwaje na Serikali kuweza kuboresha shughuli za uchimbaji mdogo na kwa kupitia vikundi na njia mbalimbali za ushirika ili kuweza kujiboreshea vipato wao wenyewe na kuboresha kipato cha Halmashauri ya Tunduru?

Name

Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Answer

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunazipokea pongezi hizo alizozitoa na nieleze tu kwamba katika pongezi hizo na yeye anastahili pongezi kwa sababu na yeye ni sehemu ya mchakato huo na nieleze tu kwamba sisi kama Wizara ya Madini na mimi binafsi niko tayari kurudi tena Ngapa kule kukutana na wananchi wa Tunduru kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu kuwasaidia wakina mama nieleze kwamba wakinamama kupitia Chama chao cha Wachimbaji Wanawake - TAHOMA wamekuwa wakifanya juhudi mbalimbali za kuweza kutafuta maeneo kwa ajili ya kuchimba na kutafuta usaidizi wa aina mbalimbali, Wizara tunaendelea kushirikiana nao kwa karibu lakini katika eneo la Tunduru wapo wanawake wanaofanya vizuri sana pengine kuliko hata wanaume, kuna mama mmoja pale anaitwa Mwajuma ameajiri wanaume zaidi ya 40 wanachimba kwenye leseni yake, kuna mama mwingine pale anaitwa Debora Mwikani naye ameajiri wakina baba wengi wanafanya kazi pale, nieleze tu kwamba uchimbaji kwa kweli kinachohitaji ni nidhamu ya matumizi na wakinamama wameonesha nidhamu ya matumizi kwa kiwango kikubwa na kwa kweli nitumie nafasi hii kuwapongeza wanawake kwa kushiriki kwenye shughuli za uchimbaji madini na tunaamini kupitia wanawake uchumi wa madini utatutoa nakushukuru. (Makofi)