Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Nape Moses Nnauye

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtama

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:- Wananchi wa Msalala kwa juhudi zao wamejenga mabweni katika Shule za Sekondari za Bulige, Busangi, Baloha, Mwalimu Nyerere, Lunguya, Ntobo na Isaka. (a) Je, Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo za wananchi kwa kuyatambua mabweni hayo na kuzipatia shule hizo ruzuku za uendeshaji wa mabweni kwa ajili ya umeme, maji, chakula na ulinzi? (b) Je, Serikali ipo tayari kuongeza miundombinu kama mabwalo ya chakula na nyumba za matron katika Shule hizo? (c) Je, ni lini Serikali itasaidia wasichana wa Msalala katika Kata nyingine kama Mwanase, Mwalugulu, Jana, Bugerema na Bulyanhulu kwa kuwajengea Mabweni?

Supplementary Question 1

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, hoja ya msingi hapa ni kwamba tunayo changamoto siyo tu katika Jimbo hili, lakini katika Majimbo mengine pia ya namna ya kusaidia hasa watoto wa kike kuwapunguzia suluba wanayoipata ya kwenda shuleni na kurudi, ndiyo maana hawa wananchi wa Msalala wakawekeza fedha kwa ajili ya kujenga mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu la Serikali ni kwamba mnasaidia kwenye shule ambazo zinachukua wanafunzi wa kitaifa. Hawa ambao wako wengi kwa nini Serikali haioni iko haja sasa ya kuwekeza hata kwenye hizi shule ambazo zinachukua katika eneo dogo lakini kwa lengo la kuwasaidia mabinti zetu wapate mahali pa kukaa na kupata masomo yao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; uwekaji wa miundombinu katika hizi shule na hasa suala la umeme kwa maeneo mengi kwa miradi ya REA imekuwa kama ni hisani ya Wakandarasi, kwa sababu wanaambiwa wakipata nafasi waweke. Maeneo mengi ushahidi unaonesha kwamba hawafanyi mpaka ambapo panakuwa na msukumo maalum. Serikali haioni umefika wakati sasa suala la kuweka umeme kwenye shule liwe ni suala la lazima kwa Wakandarasi waliopewa miradi ya REA na iwe ni kazi ambayo inafanyika bure badala ya kuwa sasa hivi inafanyika kama hisani?

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba nia njema ya Serikali kama tungekuwa na uwezo mkubwa tungepeleka mabweni ama mabwalo katika shule zetu hizi za kutwa. Tumesema hizi shule za kutwa zipo karibu na makazi ya wananchi na tumeelekeza pia Waheshimiwa Wabunge, wananchi wengine na wazazi waendelee kuchukua tahadhari juu ya kulinda watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanza na hizi shule za mabweni za Kitaifa kwa sababu wanafunzi wanatoka maeneo ya mbali sana katika makazi yao huku majumbani kwao kwenda katika hizi shule. Naomba tupokee ari ya Mheshimiwa Mbunge na maoni yake; tukipata uwezo wa kutosha tutafanya kazi na tungependa pia watoto wetu waendelee kusoma vizuri. Ni kweli kwamba kumbukumbu zinaonesha watoto wengi wa kike hawamalizi shule kwa sababu wanapewa mimba wakati wa kutoka nyumbani kwenda shuleni na wakati wa kurudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anazungumzia habari ya umeme kupelekwa katika shule zetu za sekondari za Umma. Ni kweli kwamba tumepata malalamiko mengi katika maeneo mbalimbali, nami nimefanya ziara maeneo hayo. Walimu wetu, Wenyeviti, wazazi, viongozi, Madiwani na Wabunge wanalalamika kwamba kunakuwa na bill kubwa pia ya kuunganisha umeme katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tumesikia mara kadhaa Mheshimiwa Waziri wa Nishati akitoa maelekezo. Tupokee wazo hili pia, tuongee na viongozi wenzetu wa Wizara ya Nishati ili ikiwezekana umeme upelekwe kwenye maeneo ya Umma tena iwe ni bure kwa sababu hii ni huduma ya Serikali. Shule za Serikali, vijana wa Kitanzania, Serikali ni ya kwetu, ipo namna ya kulifanya jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tungependa unapopeleka umeme katika maeneo ya shule za jirani, hata vijana ambao wanakaa maeneo ya jirani, hata wakati wa usiku wanaweza wakajisomea kujiandaa na mitihani yao na kufanya discussion mbalimbali hata kutoka shule mbalimbali za jirani katika maeneo hayo. Ahsante.

Name

Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Primary Question

MHE. NAPE M. NNAUYE (K.n.y. MHE. EZEKIEL M. MAIGE) aliuliza:- Wananchi wa Msalala kwa juhudi zao wamejenga mabweni katika Shule za Sekondari za Bulige, Busangi, Baloha, Mwalimu Nyerere, Lunguya, Ntobo na Isaka. (a) Je, Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi hizo za wananchi kwa kuyatambua mabweni hayo na kuzipatia shule hizo ruzuku za uendeshaji wa mabweni kwa ajili ya umeme, maji, chakula na ulinzi? (b) Je, Serikali ipo tayari kuongeza miundombinu kama mabwalo ya chakula na nyumba za matron katika Shule hizo? (c) Je, ni lini Serikali itasaidia wasichana wa Msalala katika Kata nyingine kama Mwanase, Mwalugulu, Jana, Bugerema na Bulyanhulu kwa kuwajengea Mabweni?

Supplementary Question 2

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ina shule tatu zenye Kidato cha Kwanza mpaka cha Sita; Shule ya Lupembe Sekondari, Magilu Sekondari na Itipingi Sekondari. Katika shule hizi zote kuna uhaba mkubwa sana wa vyumba vya madarasa na mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye shule moja hii ya Itipingi wananchi wameshaanza kujenga bweni moja ambalo sasa hivi limefikia kwenye hatua ya lenta: Je, Serikali ipo tayari kutoa fedha kwa ajili ya kuwasaidia wananchi hawa ili waweze kukamilisha mabweni na hawa vijana waweze kuishi katika mazingira mazuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Name

Mwita Mwikwabe Waitara

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tarime Vijijini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi na wadau mbalimbali wamejenga maboma mengi katika maeneo yao ya Shule za Sekondari na Msingi, kwa maana ya maboma ya shule lakini pia na maboma ya kujenga mabwalo na mabweni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu wa fedha uliopita tumetoa shilingi bilioni 29.9 kukamilisha maboma ya nchi nzima zaidi ya maboma 2,900. Naomba niwaahidi mwaka huu pia, kwenye bajeti ambayo nimesema kwenye jibu langu la msingi tumetenga shilingi bilioni 58.2, pamoja na mambo mengine fedha hiyo imejumuishwa na fedha ya kwenda kukamilisha maboma, mabweni, mabwalo, nyumba za walimu lakini pia na matundu ya vyoo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikutie moyo kwamba wakati ukifika wa kusambaza hizo fedha tutaendelea kuwa tunawasiliana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, fedha zinapoenda katika maeneo yenu, ni muhimu mkapendekeza maeneo ya vipaumbele. Tumepeleka fedha ya kukamilisha maboma, lakini fedha nyingine zimerudishwa kwa sababu kuna shule zimepelekewa kumbe hazikuwa na maboma. Fedha ambayo inapelekwa na Serikali ni kukamilisha maboma na siyo kuanza ngazi ya msingi mpaka kwenye lenta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.