Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Khatib Said Haji

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Konde

Primary Question

MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:- Ni kosa la Jinai kwa Mtu au Vyombo vya Habari kutoa, kuandika, kusambaza au kutangaza habari za uongo. Je, Jeshi la Polisi linachukua hatua gani stahiki kwa watu au vyombo vya habari vinavyofanya makosa hayo?

Supplementary Question 1

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 12 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatamka kwamba kila mtu anastahiki heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na matukio ya vyombo vya habari kuwadhalilisha na kuwasingizia uongo baadhi ya watu na katika watu wanaosingiziwa wengine wana uwezo wa kwenda Mahakamani na wengine ni wanyonge ambao hawana uwezo wa kusimamia hizi kesi Mahakamani. Je, Serikali inatoa msaada gani wa kisheria kwa watu ambao wanadhalilika na kukosa haki za utu wao kutokana na kusingiziwa na makosa kama hayo na vyombo vya habari? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mara kadhaa nimeshuhudia baadhi ya magazeti kama Mwanahalisi na Tanzania Daima yakipewa adhabu mara kwa mara ya kufungiwa kutokana na kuzua au kuonekana wamesema uongo, lakini sijawahi kuona magazeti ya Tanzanite, Jamvi la Habari na Fahari Yetu yakichukuliwa hatua yoyote wakati ni kinara wa kuzua na kudhalilisha watu katika nchi yetu: Kwa nini Serikali haichukui hatua kwa vyombo hivi vya habari na mmiliki wake? (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kutoa ufafanuzi kwa maswali ambayo ameuliza Mheshimiwa Mbunge. Kwanza niseme kwamba kitu ambacho anazungumza siyo kweli kwa sababu sisi kama Serikali tunafanya kazi kwa kusimamia sheria pamoja na kanuni. Mara zote ndani ya hili Bunge tumekuwa tukitoa ufafanuzi kwamba sisi kama Wizara tumekuwa tukichukua hatua kwa magazeti yote ambayo yanakiuka sheria ambazo sisi wenyewe Wabunge tumezitunga ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikirudi kwenye swali la Mheshimiwa Mbunge ambapo amesema kwamba hatuchukulii hatua magazeti ya Tanzanite, siyo kweli kwa sababu tumeshajibu mara kadhaa humu ndani kwamba tumeshaandikia onyo gazeti la Tanzanite, vilevile hata gazeti la Tanzania Daima pamoja na
kwamba mara nyingi limekuwa likikiuka hizo kanuni, lakini tumekuwa tukiliandikia onyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Sheria yetu ya Habari inazungumza kwamba kabla ya kuchukua hatua yoyote kwa chombo chochote cha habari, cha kwanza tunachokifanya, tunatoa onyo mara ya kwanza, tunatoa nafasi ya mara ya pili na pale ambapo tunaona sasa hali hiyo imezidi, ndipo ambapo tumekuwa tukichukua hatua ya kuweza kufungia hayo magazeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo kweli kwamba tumekuwa tuna upendeleo. Sheria haina upendeleo, nasi kama Wizara tumekuwa tukichukua hatua pale ambapo tunaona tumeshaonya mara kadhaa lakini bado hawajajirekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

NAIBU WAZIRI YA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kawaida wananchi ambao wamekuwa hawana uwezo wa kifedha wa kupata huduma ya kisheria, wamekuwa wakisaidiwa kupewa huduma hiyo na Serikali kupitia Wanasheria wa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, pale ambapo kuna changamoto yoyote ambayo inahusu malalamiko ya kutotendewa haki katika eneo lolote linalohusu sheria, basi mamlaka ya Serikali kupitia Wizara ya Sheria na Katiba wamekuwa wakichukua hatua ya kuwasaidia, kuwasikiliza na kuwashauri wananchi ambao wamekuwa wakihitaji huduma hizo za kisheria kwa ajili ya kuweza kufanikisha mashauri yao ama kesi zao mbalimbali aidha iwe Mahakamani ama kesi za kawaida za upatanishi na usuluhishi. (Makofi)