Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ally Seif Ungando

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Primary Question

MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:- Wananchi wanaoishi katika Jimbo la Kibiti hutumia nishati ya mkaa na kuni kwa matumizi ya nyumbani, shuleni, gerezani na kadhalika, hivyo kusababibisha uharibifu mkubwa wamazingira kwa kukata miti hovyo:- (i) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka nishati mbadala? (ii) Je, ni aina gani ya nishati itakayotumka badala ya kuni na mkaa?

Supplementary Question 1

MHE. ALLY S. UNGANDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa wananchi wa Kibiti wanategemea sana nishati yao ya mkaa na kuni, je, ni lini sasa wataunganishiwa hii gesi asilia katika Miji ya Kibiti, Bungu na Jaribu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali sasa inajenga mradi mkubwa wa umeme kule Mloka wa Stiegler’s, je wananchi wa Kibiti ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea kukata kuni na mkaa wanaweza wakapatiwa upendeleo wa kupata vibarua?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuruku kwa kunipa nafasi ya kujibu swali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeza kwa kazi nzuri anayofanya katika Jimbo la Kibiti, hususan katika sekta hii ya nishati. Maswali yake ya nyongeza kwanza ameuliza ni lini sasa Serikali itasambaza gesi katika Wilaya hii ya Kibiti, katika jibu letu la msingi tumesema katika kipindi hiki cha muda wa kati kati ya mwaka 2010 mpaka 2020 tumekuwa tukutekeleza miradi ya muda wa kati na muda mfupi wa kusambaza gesi katika maeneo mbalimbali. Mpaka sasa Mheshimiwa Waziri wa Nishati wiki mbili zilizopita amezindua uunganishaji wa gesi nyumba mpya 26. Matarajio yetu mpaka ifikapo Septemba, 2019 kuunganisha nyumba kama 333 katika Mkoa wa Mtwara na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mkoa wa Lindi na Pwani, Serikali kupitia TPDC imekuja na mradi mkubwa kabambe wa kusambaza gesi asilia. Mradi huu utafanywa na mashirikiano baina ya sekta binafsi na Serikali na kwa sasa hatua ambao imefikia tumeshampata Mshauri Mwelekezi, anaandaa makabrasha na kufanya feasibility study ya mradi mzima, matarajio yetu mwezi wa Tano mwakani kuwapata wakandarasi wa sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri niwakaribishe sekta binafsi katika maeneo mbalimbali ili kujumuika na Serikali katika mradi mkubwa wa kusambaza gesi asilia kwa matumizi ya majumbani na viwandani na hususan katika Wilaya ya Kibiti kwa kuwa nayo imepitiwa na bomba la gesi hususan katika maeneo ambayo ameyataja Jaribu, Kibiti maeneo ya Nyamwimbe, Kata ya Mlanzi, maeneo ya Mangwi, Kata ya Mchukwi na maeneo mengine kama ambavyo anafahamu Mheshimiwa Mbunge, kwa hiyo nimwaidi hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza mradi wa Stiegler’s Gorge Rufiji Hydro Power unaotekelezwa katika Kata ya Mwaseni, Kijiji cha Mloka. Ni kweli mradi ule una matarajio makubwa ya kutoa ajira na kwa kuwa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, utekelezaji huu wa miradi hii mikubwa ya mikakati, lengo kubwa ni kuzalisha ajira na katika maeneo ambayo mradi unatekelezwa na kwa Watanzania wote kwa ujumla. Kwa hiyo nimwahidi na hata yeye anafahamu, hata zile kazi za awali za madereva zilizotangazwa, zimetangazwa kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kibiti na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Rufiji na Wakuu wa Wilaya wa Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo ni wazi kabisa kipaumbele kwa watakaokuwa na sifa wanaostahili, lakini zipo kazi za kawaida za vibarua mbalimbali, watapata wananchi wa Kibiti na wananchi wa Wilaya ya Rufiji na wa maeneo ya Mkoa wa Morogoro. Kwa hiyo hilo kwa kweli halina mjadala, ndivyo ambavyo tumelipangilia. Ahsante sana.

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:- Wananchi wanaoishi katika Jimbo la Kibiti hutumia nishati ya mkaa na kuni kwa matumizi ya nyumbani, shuleni, gerezani na kadhalika, hivyo kusababibisha uharibifu mkubwa wamazingira kwa kukata miti hovyo:- (i) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka nishati mbadala? (ii) Je, ni aina gani ya nishati itakayotumka badala ya kuni na mkaa?

Supplementary Question 2

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Baada ya Mtwara kupatikana kwa gesi Mheshimiwa Waziri akatangaza kwamba Liwale nao tutapata umeme wa gesi kutoka Mtwara. Wakati ambapo Mheshimiwa Waziri anatangaza nikamwomba nikamwambia kwa umeme ule wa Mtwara nafuu Liwale wakatuachia umeme wetu wa mafuta, lakini jambo hilo halikutekelezwa, matokeo yake sasa Liwale umeme unapatikana kwa shida sana.

Je, Mheshimiwa Waziri anatuahidi nini sisi watu wa Liwale shida hii tunayoipata mwisho lini? Maana sasa hivi umeme haupatikani kabisa, unawaka masaa mawili au matano.

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuruku kwa kunipa nafasi ya kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Kuchauka Mbunge wa Liwale kupitia Chama cha Mapinduzi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kuchauka ameelezea katika swali lake la nyongeza kwamba tulitoa ahadi ya kuunganisha Wilaya ya Liwale katika umeme wa gesi, lakini kwa sasa nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge ni kweli kuwa Wilaya ya Liwale kwa mara ya kwanza imeunganishwa na grid ya Taifa kupitia Kituo cha Maumbika, lakini tunatambua changamoto iliyojitokeza katika maeneo mbalimbali ambapo tumeunganisha grid ya Taifa lakini inatokana na umbali wa kusafirisha umeme huyo kufikia katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Shirika la TANESCO lipo katika hatua ya manunuzi ya kifaa ambacho kitakuwa na uwezo wa kurekebisha hali hiyo ili isiendee. Kwa hiyo niwathibitishie wakazi wa Wilaya ya Liwale, wakazi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ambao wameunganishwa kwenye grid ya Taifa, wakazi pia wa Mkoa wa Ruvuma na wakazi wa Biharamulo, Ngara kwamba tatizo ni muda na limepatiwa ufumbuzi na kwamba likishashughulikiwa wataona faida ya umeme wa uhakika ambao unatokana na grid ya Taifa, kuliko huu ambao ni wa mafuta ambao kwa kweli umelisaidia shirika kuokoa kiasi cha pesa na kuweza kuendelea kuwekeza katika maeneo mengine. Kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na kwa kuwa hivi karibuni kwenye tarehe 21 nitafanya ziara katika jimbo lake, nitatoa hayo maelezo. Ahsante sana.

Name

Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Primary Question

MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:- Wananchi wanaoishi katika Jimbo la Kibiti hutumia nishati ya mkaa na kuni kwa matumizi ya nyumbani, shuleni, gerezani na kadhalika, hivyo kusababibisha uharibifu mkubwa wamazingira kwa kukata miti hovyo:- (i) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka nishati mbadala? (ii) Je, ni aina gani ya nishati itakayotumka badala ya kuni na mkaa?

Supplementary Question 3

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuumuliza Mheshimiwa Waziri kwamba suala hili la nishati mbadala tuliaminishwa kwa ugunduzi ule wa gesi, basi wananchi wa vijiji wangefikishiwa ile gesi wakaachana kabisa na mambo ya kutumia mkaa ili kuweza sasa kutumia gesi ambayo inapatikana maeneo ya Mtwara. Hata hivyo, mpaka sasa hivi hata Mtwara kwenyewe matumizi ya gesi si makubwa kwa sababu ile miradi ni kama imekuwa abandoned, Serikali haiifanyii tena kazi. Sasa nataka kufahamu kutoka kwa Naibu Waziri, je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na masuala ya gesi iliyopo Mtwara?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimshuruku sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya maswali ya msingi ya Waheshimiwa Wabunge. Pia napenda niungane na Mbunge Mwambe kwa matumizi ya gesi kule Mtwara na nimpongeze kwa ufuatiliaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibu mwezi uliopita tumeanza kutekeleza rasmi, mwaka jana tulizindua usambazaji wa gesi Mtwara na katika maeneo 12 ambayo tunaanza nayo vifaa tayari vimepatikana na tarehe 30 mwezi huu ujenzi wa usambazaji gesi Mtwara unaanza. Tunaanza na vituo cha Chuo cha Ufundi pamoja na maeneo yote yanayokwenda mpaka gerezani na maeneo ya Mtwara Mikindani. Nitake tu kuwapa taarifa na uhakika wananchi wa Mtwara kwamba yataanza sasa mwezi huu tarehe 30 na yatachukua takribani miezi 15 ili wananchi wa Mtwara waweze kupata gesi kama ambavyo tumepanga.

Name

Jerome Dismas Bwanausi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Primary Question

MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:- Wananchi wanaoishi katika Jimbo la Kibiti hutumia nishati ya mkaa na kuni kwa matumizi ya nyumbani, shuleni, gerezani na kadhalika, hivyo kusababibisha uharibifu mkubwa wamazingira kwa kukata miti hovyo:- (i) Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka nishati mbadala? (ii) Je, ni aina gani ya nishati itakayotumka badala ya kuni na mkaa?

Supplementary Question 4

MHE. JEROME D. BWANAUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi. Tatizo lililopo Kibiti pia lipo katika Jimbo la Lulindi na sisi hatujapitiwa na utaratibu huo wa kupewa umeme mbadala na kutumia gesi kwa ajili ya majumbani. Sasa nataka kumwomba Mheshimiwa Naibu Waziri atueleze maana sisi tunategemea umeme hali ya usambazaji umeme katika jimbo la Lulindi inasikitisha na iko katika kiwango cha chini sana. Je, nini kauli ya Serikali?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Bwanausi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika baadhi ya maeneo utekelezaji wa kandarasi umesuasua hasa mwanzoni lakini kwa upande wa Mheshimiwa Bwanausi yapo maeneo ambayo yalikuwa mbali sana na mtandao wa umeme, kwa hiyo, imechukua muda mrefu kwa wakandarasi kuyafikia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Bwanausi kwa ushirikiano na Waheshimiwa Wabunge wa Mtwara pamoja na mkandarasi, sasa hivi mkandarasi mkandarasi anakamilisha shughuli za kusimika nguzo katika maeneo 22 ya Mheshimiwa Bwanausi. Ni matarajio yetu katika Jimbo la Bwanausi, maeoneo ya vijiji 22 yatawashwa kabla ya mwezi Septemba, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafanya kila namna kuhakikisha kwamba wakandarasi wanaongeza kasi. Tarehe 22, mimi mwenyewe nitakuwa Mtwara ili kuweka msukumo mkali kwa wakandarasi ili waweze kukamilisha kazi hizo kwa wakati.