Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Primary Question

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Katika kijiji cha Fanusi, Kata ya Kisiwani, Wilayani Muheza wapo wananchi wanaofanya biashara ya kutega vipepeo na kuvipeleka nje ya nchi kwa ajili ya kupata kipato na pia njia ya kukuza utalii:- (a) Je, ni lini wataruhusiwa kupeleka tena vipepeo nje ya nchi badala ya Serikali kuzuia kama ni wanyama hai? (b) Je, Serikali ipo tayari kuboresha maeneo hayo ili kuwavutia watalii waweze kuja kwa wingi?

Supplementary Question 1

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ambayo sijaridhika nayo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali la kuzuia wanyama hai kusafirishwa nje ya nchi nina hakika lilikuwa ni zuri lakini lilikuwa linalenga wanyama hai wakubwa, sidhani kama Serikali ilikuwa inalenga vipepeo ambao ni kama wadudu. Wananchi hawa wa Fanusi wamekuwa wakifanya biashara hii ya kupeleka vipepeo nje ya nchi kwa muda na walikuwa wanapata pato zuri tu, karibu shilingi laki tatu mpaka nne kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki ambacho Serikali imezuia biashara hii wananchi wamepata matatizo sana. Naibu Waziri mmepiga marufuku biashara hii kwa muda wa miaka mitatu ambayo inakwisha Mei mwaka huu. Je, baada ya muda huo Wizara itakuwa tayari kuwapelekea rasmi barua wanakijiji wa Fanusi ili biashara hiyo iweze kuanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Waziri mwenyewe alifika kwenye maeneo haya na alitembea pale kwenye Kijiji cha Fanusi na kuona wananchi namna walivyobuni na kuanza huu mradi wa kufuga hawa vipepeo. Aliahidi na kumwelekeza Mkurungezi Mkuu wa TFS apeleke wataalam ili aweze kuwasaidia wale wananchi kukuza ubunifu wao na pia kuboresha mazingira yale. Ni lini wataalam hao na uboreshaji huo utaanza? Nakushukuru sana.

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wakati tunazuia uuzwaji wa wanyama hawa hai nje ya nchi wapo wananchi wa vikundi mbalimbali walikuwa na vikundi vyao na walikuwa wanapata mapato na kulipa kodi kutoka na mauzo hayo. Hata hivyo, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi ni kwamba ulitokea ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu na Serikali ikaona itafute utaratibu mwingine wa kusimamia zoezi hili. Kama alivyosema itakapofika Mei, Serikali itatoa tamko sasa ni kwa namna gani tutaendelea na zoezi hili ili kutoaathiri kabisa shughuli hii hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusu Mheshimiwa Waziri kuagiza kupelekwa wataalam, ni imani yangu kwamba baada ya agizo la Mheshimiwa Waziri wataalam hao walielekezwa kwenda lakini kama bado hawajafika nitahakikisha kwamba wanakwenda kutoa elimu kwenye vikundi hivi ambavyo vinashughulika na biashara hii.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuongezea ziada ifuatayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifika katika Kijiji cha Fanusi, niliona jitihada za akina mama wale katika kikundi kile na niliona adha wanayoipata kwa Serikali kuzuia kusafirisha vipepeo nje ya nchi kutokana na ile blanket ban ambayo kama Serikali tuliitoa miaka mitatu iliyopita. Naomba kuweka sawa tu rekodi kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa hatutaruhusu tena usafirishaji wa wanyama hai kutoka nchini mwetu kwenda nchi yoyote ile na tutafanya mabadiliko ya sheria ili kuzuia jambo hilo lisitokee tena katika nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, utaratibu ambao tunaushauri kwa wananchi wote ambao wamekuwa wakifuga wanyamapori hawa watafute namna nyingine ya kupata faida kutokana na maliasili hiyo na siyo kutegemea kusafirisha kwenda nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa akina mama wa pale Fanusi niliwashauri Halmashauri na nikaagiza washirikiane na
TFS kutafuta namna ya kufanya shughuli ya utalii wa vipepeo katika eneo lile kwa sababu kwa kweli vipepeo walioko pale ni wazuri mno na watu wangeweza kwenda kuwaona pale na kingekuwa ni kivutio cha utalii na wangepata kipato ambacho walikuwa wanakitarajia. Kwa hiyo, huo ndiyo uelekeo, waondokane na mentality kwamba kuna siku tutafungulia vibali vya kusafirisha nje ya nchi kwa sababu tumezuia na hatutafungua tena.

Name

Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Primary Question

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Katika kijiji cha Fanusi, Kata ya Kisiwani, Wilayani Muheza wapo wananchi wanaofanya biashara ya kutega vipepeo na kuvipeleka nje ya nchi kwa ajili ya kupata kipato na pia njia ya kukuza utalii:- (a) Je, ni lini wataruhusiwa kupeleka tena vipepeo nje ya nchi badala ya Serikali kuzuia kama ni wanyama hai? (b) Je, Serikali ipo tayari kuboresha maeneo hayo ili kuwavutia watalii waweze kuja kwa wingi?

Supplementary Question 2

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo swali, nashukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na faida ya watalii kuja kuona vipepeo, nimegundua watalii wengi wakishaona wanafanya identification na wanachukua sample za vipepeo na kuondoka nazo. Je, Serikali yetu imeshafanya utafiti wanaenda kufanyia nini hivyo vipepeo wanavyochukua ili kuhakikisha hatupotezi rasilimali ya Taifa?

Name

Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yussuf, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba watalii wengi baada ya kuona vipepeo hutamani kuondoka nao na baada ya kuondoka nao kitu ambacho tumegundua ni kwamba nao wanakwenda kufanya biashara ileile ambayo sisi tunafanya ili watalii waje Tanzania. Kwa hiyo, ni kwa sababu hiyo Wizara ikaona hamna sababu tena ya kuendelea kuuza wanyama hai nje ya nchi.