Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Primary Question

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Mwese?

Supplementary Question 1

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Naomba niipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo imefanya kusema kweli kwa hiki kituo, kilikuwa ni kituo chakavu sana na kinatumika na watu wengi sana. Tunashukuru sana kwa hizi pesa ambazo mmetuletea na kuanzia sasa hivi ukarabati umeanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wafanyakazi wa sekta hii ni wachache sana, hatuna kabisa manesi, madaktari wala wahudumu kabisa; je, ni lini Serikali itatuletea watumishi katika kituo hiki ha Mwese? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ndiyo hospitali inayobeba matatizo yote katika Mkoa wetu wa Katavi; je, ni lini Serikali itatuletea Madaktari Bingwa, kwa sababu Hospitali ya Mpanda haina Madaktari Bingwa? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nipokee pongezi zake kwa fedha ambazo tumepeleka Mwese na nimpongeze naye mwenyewe kwa kufanya kazi za Kibunge hasa katika Mkoa wake wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la watumishi katika Kituo cha Mwese, napenda nimhakikishie kwamba kwa sababu kituo hakijakamilika, Serikali itaweka kipaumbele katika kutenga watumishi ambapo kituo hicho mara kitakapokamailika tu tutawapeleka mara moja ili waweze kutoa huduma kwa wananchi. Hao watumishi tutawaajiri mwezi Julai, wataanza kazi, wataripoti, lakini kuna watumishi ambao tutawa-retain kwa ajili tu ya Kituo hiki cha Mwese.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupeleka Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Manispaa ya Mpanda, kwanza nilitembelea hospitali ile mwezi Novemba, 2017 hospitali yenyewe tu kwanza inahitaji uangalizi wa karibu kwa maana ya ukarabati na mambo mengine. Nimhakikishie kwamba katika ajira ambazo tunaendelea nazo sasa hivi, kati yetu sisi tuna ajira 6,000 ambazo tunaendelea kuziratibu na Wizara ya Afya ina ajira kati ya 1,800 mpaka 2,000 ambazo wanaendelea kuziratibu, basi tutaweka kipaumbele cha kupeleka Madaktari Bingwa kupitia ajira hizi.

Name

Selemani Moshi Kakoso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Vijijini

Primary Question

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Mwese?

Supplementary Question 2

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwanza naishukuru na kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa wanayoifanya baada ya kutoa fedha za kupeleka Kituo cha Afya cha Mwese na Kituo cha Afya cha Mishamo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa jiografia ya Jimbo la Mpanda Vijijini ambalo lipo katika Wilaya ya Tanganyika liko katika mazingira ya mtawanyiko; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka ambulance ambayo itawasaidia kwenye hivyo vituo vya afya; Kituo cha Afya cha Karema, Kituo cha Afya cha Mwese na Kituo cha Afya cha Mishamo? (Makofi)

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kutokana na eneo mtawanyiko mkubwa wa Jimbo la Mpanda Vijijini lililopo katika Wilaya ya Tanganyika ambayo ni Wilaya mpya kunahitajika ambulance kutokana na kwamba maeneo yako mbalimbali sana; Mwese, Mishamo na kile kituo kingine ambacho amekitaja. Tutakapopata mgao wa ambaulance ambao utapatikana kabla ya mwezi wa kumi, basi naomba sana tuendelee na mawasiliano ya karibu ili tumpe kipaumbele.

Name

Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Primary Question

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Mwese?

Supplementary Question 3

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Lushoto yenye tarafa tano ina Vituo vya Afya katika Tarafa ya Mlola, Mlalo, Mnazi pamoja na Lushoto Mjini; je, ni lini sasa Serikali itajenga Kituo cha Afya katika Tarafa pekee iliyobaki ya Mtae?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana ya maswali yote ya awali. Mheshimiwa Shangazi alishafika ofisini kwetu mara kadhaa kuhusu kituo hiki na ndiyo maana tumeanza katika awamu hii kupeleka pale Mnazi. Naomba nimhakikishie kwa sababu wananchi wa Mtae wanapata shida, katika kipindi kinachokuja tutafanya kila liwezekanalo, kuhakikisha eneo lile tunalipatia Kituo cha Afya. Lengo letu ni kupunguza vifo vya mama na watoto. (Makofi)

Name

Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Primary Question

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Mwese?

Supplementary Question 4

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Katika ziara ya Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI mwezi Machi, 2017 katika Halmashauri ya Monduli aliahidi kusaidia juhudi za wananchi katika Kituo cha Afya cha Makuyuni. Pamoja na hayo, katika mwaka wa fedha 2017/2018 fedha zote za ruzuku tulielekeza katika ujenzi wa Vituo vya Afya.
Je, ni lini Serikali italeta fedha za CDG katika Halmashauri ya Monduli kwa ajili ya kumalizia Vituo vya Afya Lemuoti, Nalarani, Makuyuni pamoja na Duka Bovu?

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana Mheshimiwa Julius Kalanga awe na mawasiliano ya karibu na Mkurugenzi wa Halmashauri kwa sababu wakati wowote fedha za ruzuku zinaweza zikaingia. Sasa zikiingia waweke kipaumbele kwenye hayo maeneo.

Name

Dr. Shukuru Jumanne Kawambwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Primary Question

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Mwese?

Supplementary Question 5

MHE. DKT. SHUKURU J. KAWAMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Jimbo la Bagamoyo kata zake zote isipokuwa moja tu ndiyo ina kituo cha afya ambacho ni kipya. Je, ni nini mpango wa Serikali kuweza kutupatia angalau kituo kimoja au viwili zaidi kwa Jimbo zima la Bagamoyo? (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Bagamoyo ina changamoto kubwa na hivi sasa tuliimarisha katika Kituo cha Afya cha Kerege. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadri iwezekanavyo na tukijua kwamba jiografia ya Bagamoyo na mahitaji yake yalivyo, nadhani kabla hatujafika mwezi wa saba, hapa katikati, tutafanya jambo katika kituo kimoja cha afya ambacho yatapendekeza kutoka Wilaya ya Bagamoyo. (Makofi)