Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme wa REA; je, ni lini sasa vijiji vyote vya Jimbo la Busanda vitapata umeme?

Supplementary Question 1

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumza vizuri sana kuhusiana na habari ya kupeleka umeme katika Jimbo Busanda, lakini vijiji hivi ambavyo amevitaja bado hatujamwona mkandarasi, hajafika. Napenda kujua ni lini sasa mkandarasi ataanza rasmi kufanya kazi katika vijiji hivyo vya Ntono na Bugogo ambavyo amevitaja katika jibu la msingi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sera ya nchi ni kwamba mahali popote ambapo nguzo zinapita na nyaya juu, lazima wananchi waweze kupata umeme. Kwenye Jimbo la Busanda kuna vijiji ambavyo vimepitiwa na nguzo; kwa mfano, Nyaruyeye pamoja na vijiji vingine sehemu za Busaka vimepitiwa na nguzo juu lakini havina umeme. Ndiyo maana nilimfuata Mheshimiwa Waziri ofisini nikapeleka vijiji 30 vya nyongeza kwa ajili ya kupatiwa umeme, lakini hapa sijavisikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua sasa Wizara inasemaje kuhusu kuvipatia umeme vijiji 30 ambavyo nimeongea na Mheshimiwa Waziri?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninampongeza Mheshimiwa Bukwimba kwa kufuatilia masuala ya umeme katika Jimbo lake akiwa Mbunge mwanamke wa Jimbo pia. Ameulizia ni lini mkandarasi ataripoti katika Jimbo lake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nirejee kama nilivyosema awali, tutakutana nao wakandarasi tena kwamba maelekezo ni yale yale, mkandarasi asikae sehemu moja. Kwa hiyo, pengine kama yuko katika maeneo mengine, tumesema wawe na magenge na kila Wilaya wakandarasi kazi ionekane imeanza kwa sababu hakuna kikwazo tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kutokana na changamoto iliyokuwepo ya uwepo wa vijiji ambavyo vimepitiwa na miundombinu ya umeme na umeme hakuna, imekuja densification ya awamu ya pili ambapo Geita ni Mkoa mmojawapo katika densification ya awamu ya pili pamoja na mikoa mingine, jumla 11.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba la hilo, vijiji vyake 30 tumeviwasilisha REA kwa ajili ya mchakato na ninamthibitishia vitakuwepo katika hiyo orodha kama ambavyo amefuatilia Mheshimiwa Mbunge. Nakushukuru.

Name

Fakharia Shomar Khamis

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme wa REA; je, ni lini sasa vijiji vyote vya Jimbo la Busanda vitapata umeme?

Supplementary Question 2

MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Dodoma ni Mji Mkuu, pia ni Jiji, lakini kukatika kwa umeme ni jambo la kawaida.
Je, nini kinachosababisha hata kukatika kwa umeme Sengia na Site Two kuwa ni jambo la kawaida? (Makofi)

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba nijibu swali la mama yangu Mheshimiwa Fakharia kwamba kukatika kwa umeme kwa Mkoa wa Dodoma naomba nilichukue na tunalishughulikia, lakini wakati mwingine ni kutokana na kubadilisha tu nguzo ambazo zimeoza, nyaya na kadhalika, lakini kwa kuwa ni Jiji kwa kweli tunalifanyia kazi kwa karibu. Ahsante.

Name

Zuberi Mohamedi Kuchauka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Liwale

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme wa REA; je, ni lini sasa vijiji vyote vya Jimbo la Busanda vitapata umeme?

Supplementary Question 3

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu kwenye Mkoa wa Lindi tumepata Mkandarasi ambaye uwezo wake ni mdogo sana. Mpaka sasa hivi awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu ishafika nusu ya wakati wake lakini bado yuko kwenye Wilaya moja tu ya Ruangwa. Ni lini mkandarasi huyu ataweza kufika Liwale?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Kuchauka juu ya changamoto za utekelezaji wa miradi hii ya REA Awamu ya Tatu na mkandarasi. Lazima nikiri kwamba mkandarasi wa Mkoa wa Lindi State Grid kuna matatizo ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi.
Kwa hiyo, nimthibitishie tu, hivi karibu Mkandarasi huyu zitakapoisha changamoto hizi atafanya kazi kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapa tukutane na Mheshimiwa Mbunge na wote wa Mkoa wa Lindi ili tuweze kujadili suala hili. Ahsante.

Name

Hamidu Hassan Bobali

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mchinga

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme wa REA; je, ni lini sasa vijiji vyote vya Jimbo la Busanda vitapata umeme?

Supplementary Question 4

MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru, Jimbo la Mchinga halina Mamlaka ya Mji Mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua tu kwa Mheshimiwa Waziri, ni kigezo gani kinachotumiwa na TANESCO Lindi kuwalipisha watu wa Mchinga fedha nyingi ya kuunganisha umeme tofauti na vijiji vingine wakati Mchinga yenyewe ni kijiji kama maeneo mengine?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, uunganishwaji wa umeme katika maeneo ya vijijini bei yake ni shilingi 177,000, umeme ambao unaunganishwa kupitia TANESCO na ile shilingi 27,000 ni kwa umeme vijijini. Kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mbunge kwamba hakuna tofauti, ila mijini ni shilingi 377,000 na vijijini ni shilingi 177,000. Kama wanakuwa-charged zaidi ya hizo, naomba tuonane ili niweze kulishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba radhi kwa Waheshimiwa Wabunge kwa tatizo lililojitokeza sasa hivi. Ahsante. (Kicheko/Makofi)

Name

Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme wa REA; je, ni lini sasa vijiji vyote vya Jimbo la Busanda vitapata umeme?

Supplementary Question 5

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Tabora Manispaa mpaka leo hii kuna baadhi ya Kata hazina umeme na Serikali ilituahidi hapa Bungeni kuanzia mwaka 2013 itatuletea umeme wa REA, lakini cha kushangaza Makao Makuu ya Kata hizo yote yamewekewa umeme wa REA ambapo vijiji vyake mpaka leo hii havijawekewa umeme wa REA. Umeme wa REA umewekwa Itonjala, Ifucha, Kalunde, Ntalikwe, Tetemia, Misha, Kakola na baadhi ya Makao Makuu ya Kata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itatuletea umeme wa REA kwenye baadhi ya vijiji ambavyo mpaka leo hii havijawekewa umeme wa REA ukizingatia ile ni Manispaa?

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Munde Abdallah Tambwe swali lake la msingi linahusu maeneo ambayo tulipeleka umeme kwenye Makao Makuu ya Kata na bado vijiji. Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo alipata kuja ofisi akaelezea na ninampongeza kwamba vitongoji na vijiji vya Kata zile vitapata umeme kupitia mradi wa densification awamu ya pili. Mkoa wa Tabora ni miongoni mwa mikoa 11 ambapo mradi huu utaanza mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama nilivyoomba Wabunge wote wa Viti Maalum kwa sababu ni wahanga, ni wafaidika wa umeme kwa kuwa wanawake wakipata umeme wamefaidika wote, waendelee kufuatilia ili umeme upatikane katika maeneo yote. Ahsante. (Makofi)

Name

Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila kijiji kinapata umeme wa REA; je, ni lini sasa vijiji vyote vya Jimbo la Busanda vitapata umeme?

Supplementary Question 6

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru. Mwaka 2016 mwezi wa kumi, Mkoa wa Mara ndiyo walizindua REA Awamu ya Tatu na densification. Mpaka naongea sasa hivi, Jimbo la Tarime Mjini maeneo mengi, maeneo ya Kanyamanyori, Kata ya Nyandoto, Kitale na Nkende mradi huu haujaanza na ni kwa asilimia 90 hawa watu hawana umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujua sasa ni lini Serikali itaenda kuelekeza maana imepita takribani miaka miwili ili miradi iweze kufanyika kwa ufanisi na wananchi waweze kupata umeme? (Makofi)

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nijibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko kuhusu masuala ya umeme katika Mkoa wa Mara hususan katika Jimbo lake, kwanza, kwa kuwa nimeona ndani ya Bunge bado changamoto za wakandarasi kuanza kuendelea na kazi, inaonekana Wabunge wengi hawaridhiki kwamba speed inaonekana ni ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, mara baada ya kutupitishia bajeti yetu, sisi tunaendelea na ziara. Ndiyo maana leo Mheshimiwa Waziri hayupo, ameshafanya ziara pia katika Mkoa wa Mara. Kutokana na tatizo hili, naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya ziara Mkoa wa Mara tena ili kuona kwa nini wakandarasi mpaka sasa hivi wanasuasua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba wakandarasi hili ni onyo la mwisho kwa kweli kama speed itaendelea Serikali ya Awamu ya Tano itasita kuvunja mikataba nao kKwa sababu miezi iliyobaki ni michache na tumeshawapa hela kwa nini inashindikana. Nashukuru ahsante.