Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Primary Question

MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:- Serikali imeendelea na juhudi mbalimbali za kulinda Nyara za Serikali:- Je, vitalu vya uwindaji vinachangia kiasi gani katika upotevu wa Nyara za Serikali?

Supplementary Question 1

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; katika mapato yanayotokana na uwindaji katika hivi vitalu halmashauri zetu ambazo ziko na maeneo haya zinapata asilimia 25 ya mapato, lakini katika hiyo asilimia 25 ni baada ya kutoa zile gharama za uendeshaji. Sasa kumekuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa haya makusanyo na kiwango hiki kinachotolewa bado ni kidogo na ukizingatia kwamba halmashauri ndizo ambazo zinasimamia kwa ukaribu maeneo haya. Sasa je, Serikali iko tayari kuongeza kiwango toka asilimia 25 mpaka 30 ili tuweze kukidhi gharama za operesheni katika maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika majibu ya Serikali wameeleza namna bora za kudhibiti hizi nyara za Serikali na tunatambua juhudi ambazo Wizara imefanya kwa kushirikisha vyombo vya ulinzi na usalama, kuboresha kanuni na kuvihusisha kwenye kulinda maliasili hizi za Serikali. Hata hivyo, kuna udhaifu waa kibinadamu, yaani watumishi katika hizi kampuni. Je, Serikali itafanya mkakati gani kuhakikisha kwamba watumishi wa hizi kampuni hawachangii katika udhaifu wa kupoteza nyara za Serikali?

Name

Japhet Ngailonga Hasunga (CPA)

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Vwawa

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Richard Mbogo kwa swali zuri na kwa jinsi ambavyo amekuwa akifanya kazi katika kutetea wananchi wake wa eneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kanuni zinavyoelekeza ni kwamba 25% inayotokana na mapato yote ya uwindaji wa kitalii ndio yanakuwa-calculated na yanaenda kwenye halmashauri, si baada ya kutoa gharama. Hivi sasa tunafanya mapitio ya sheria zote zinazohusu uhifadhi na wanyamapori. Baada ya hizo sheria kukamilika kanuni husika pia zitapitiwa tutaangalia kama hilo walilopendekeza litawezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuhusu watumishi ambao wanajihusisha na upotevu wa nyara za Serikali; ni kwamba hivi sasa ofisi yangu tumeunda Kamati ndogo ambayo inapita katika maeneo mbalimbali kubaini makampuni pamoja na watumishi wa ofisi zetu, wale ambao wanakuwa wanahusika na upotevu wa nyara za Taifa. Baada ya Kamati hiyo kukamilisha na mapendekezo kuletwa, hatua stahiki zitachukuliwa kwa watumishi wote wa namna hiyo, kwa sababu tunataka mtumishi afanye kazi yake kwa weledi, kwa kuzingatia kanuni, sheria na maadili ya kazi yake.