Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Sheria ya Tawala za Mikoa Sura ya 97 inawapa mamlaka ya kipolisi Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwatia nguvuni watu wa muda wa saa 48, lakini sheria hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kutoa amri za kukamata Wabunge, Wenyeviti wa Halmashauri, Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na hata watumishi wa umma wakiwemo madaktari. • Je, Serikali inawachukulia hatua gani Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaotumia vibaya madaraka na sheria hiyo? • Je, ni lini Serikali itaifanyia marekebisho sheria hiyo ili kuwaondolea Wakuu wa Mikoa na Wilaya mamlaka ya kuwaweka watu ndani kwa kuwa ni kandamizi, inakiuka haki za binadamu na inatumika vibaya?

Supplementary Question 1

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa kuwa Serikali inakiri kwamba kuna baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wamekuwa wakiitumia sheria hii vibaya.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuleta mabadiliko ya Sheria hii hapa Bungeni?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wamewasimamisha baadhi ya Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa ambao wamechaguliwa kihalali kwa muda mrefu na kukaimisha nafasi hizo kwa watu wengine, jambo ambalo linakwenda kinyume kabisa na sheria, kanuni na taratibu bora za uendeshaji wa Serikali za Mitaa. Je, Serikali inatoa kauli gani dhidi ya jambo hili? (Makofi)

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, hivi sasa sheria hii inajitosheleza. Changamoto kubwa ni matumizi ya ile sheria. Ndiyo maana tumesema kwamba ofisi yetu na kupitia Waziri wangu hapa, aliitisha kikao maalum cha kupeana maelekezo ya jinsi ya kutekeleza vizuri sheria hii. Lengo kubwa ni kwamba makusudio ya sheria hii yaweze kufikiwa kama vilivyo.
Kwa hiyo ukiangalia, muktadha wa sheria yenyewe haina matatizo isipokuwa katika implementation ya sheria. Ndiyo maana tumesema kwamba maelekezo maalum yametolewa na sasa hivi hatutarajii kwamba kama kutakuwa na mapungufu yoyote mara baada ya maelekezo hayo ambapo ofisi yetu imefanya kazi kubwa sana katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la Wenyeviti wa Vijiji kusimamishwa na baadhi ya Wakuu wa Wilaya, naomba ikiwezekana tupate taarifa ya eneo specific, liko wapi, halafu tuangalie kesi gani ambayo imejitokeza katika eneo husika tuweze kuangalia tatizo gani limesababisha kusimamishwa. Hata hivyo tuna imani kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya jukumu lao kubwa ni kuhakikisha kwamba utaratibu wote unasimamiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na wakati mwingine inawezekana baadhi ya vijiji kuna baadhi ya Wenyeviti wa Vijiji huenda wameuza ardhi ya kijiji au kufanya jambo lingine ambalo lilikuwa tofauti na utaratibu, ndiyo maana utakuta Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa anafanya taratibu za kisheria. Lakini kama kuna jambo ambalo limekiukwa basi naomba ofisi yetu tupate taarifa hizo tuweze kulifanyia kazi kwa misingi ya kisheria.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Sheria hii ya Mikoa inatoa mamlaka kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuweza kumkamata mtu katika mazingira ambayo wanaamini kwamba mtu huyo ama anatenda kosa la jinai, ama kwa ufahamu wao ametenda kosa la jina, ama anafanya kitendo chochote kinachovunja amani na utulivu, ama anaona mtu huyu anatarajia kutenda au kuhatarisha amani, hivyo ndio tafsiri ya sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu hili wamepewa hawa kwa sababu ya ku-maintain law and order. Utaiona leo hii inapokuwa ipo kinyume na wewe kama mbaya, lakini ikiwa inakusaidi katika wakati ambapo amani yako, haki yako au jinai dhidi yako inataka kutokea, mkuu huyu anapochukua zile hatua ndipo utakapoona msingi wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa ni wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama, mamlaka haya yanatokana na nguvu kubwa waliyonayo katika msingi wa Katiba. Halikadhalika, mtu yoyote anayo haki ya kuomba mtu mwingine ambae anaweza kutenda kosa la jinai dhidi ya mtu fulani au ya watu fulani kuomba wakamatwe.
Kwa hiyo haki hii sio tu wamepewa hawa peke yao, ukisoma vizuri sheria nyingine tulizonazo pia zinakupa wewe nguvu ya kusema wewe hapana, Simbachawene mimi naona huyu anatarajia au anahatarisha amani au anataka kutenda kosa, akakamatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, isipokuwa cha msingi ni pale tu ambapo inapaswa kutumika kwa kuzingatia sheria. Mtu huyo awe ana mtarajio ya kupelekwa mahakamani immediately baada ya kukamatwa na baada ya muda ule kupita. Isikamatwe kwa ajili ya show off tu, asikamatwe mtu kwa ajili ya ku-show, asikamatwe kwa ajili tu ya kuonesha kwamba wewe una madaraka. Lazima akamatwe mtu huyo kama kweli kitendo chake kinahatarisha amani na utulivu. Hapa ndipo ninapotaka nisisitize kwamba Wakuu wetu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kwa kutumia sheria hii, wawe makini na kuhakikisha kwamba wanaitumia kama vile sheria inavyotaka. (Makofi)

Name

Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Primary Question

MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:- Sheria ya Tawala za Mikoa Sura ya 97 inawapa mamlaka ya kipolisi Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwatia nguvuni watu wa muda wa saa 48, lakini sheria hiyo imekuwa ikitumiwa vibaya na Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa kutoa amri za kukamata Wabunge, Wenyeviti wa Halmashauri, Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na hata watumishi wa umma wakiwemo madaktari. • Je, Serikali inawachukulia hatua gani Wakuu wa Mikoa na Wilaya wanaotumia vibaya madaraka na sheria hiyo? • Je, ni lini Serikali itaifanyia marekebisho sheria hiyo ili kuwaondolea Wakuu wa Mikoa na Wilaya mamlaka ya kuwaweka watu ndani kwa kuwa ni kandamizi, inakiuka haki za binadamu na inatumika vibaya?

Supplementary Question 2

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna la ziada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa Wakuu wa Wilaya wanatumia madaraka vibaya ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini ambapo amemsimamisha kazi Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) wa Mtaa wa Mlimwa Kusini, kwa hila na ujanja na mpango wa kutengeneza. Jambo ambalo inapelekea kunakuwa na malalamiko makubwa miongoni mwa wananchi wa Mtaa wa Mlimwa Kusini ambapo ni Kiongozi wao wamemchagua na wanampenda. Je, tabia hii mbaya ya Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, ni lini ataacha kusimamisha watu kiholela? (Makofi)

Name

George Boniface Simbachawene

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibakwe

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, scenario anayoizungumzia is a very specific scenario na pengine tungeweza kuisikiliza chanzo chake, imekuwaje, ilitokeaje. Si rahisi kwa muda huu kuweza kufanya hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote humu Wabunge tunafahamu, namna ambavyo Wenyeviti wetu wa Vijiji na Mitaa wanavyouza maeneo, wanavyoharibu mali za umma, wanavyochezea mali za umma. Kwa hiyo, kuna mambo mengi yanayotokea huko; na sisi kama nchi tumewapa madaraka hawa watu wawakilishe mamlaka ili kuhakikisha kwamba maslahi ya umma inalindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa kutekeleza majukumu haya, mazingira hayawezi yakafanana, yanatofautiana kutoka sehemu moja na sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tunayosimamia, Utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, tupo tayari kupokea jambo lolote mahsusi na kulishughulikia namna ilivyo. Lakini si kweli kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya hawa wanafanya mambo ya ovyo. Wanafanya mambo ambayo yanasababisha tunakuwa na amani katika nchi hii na tunawapongeza wanafanya mambo haya katika mazingira ambayo ni tata, kwa sababu pia kuna siasa ndani, kuna mambo mengi; tuwasaidie lakini pia tulete mambo ambayo yamekwenda sio sawa ili tuweze kuyashughulikia kulingana na yalivyo. (Makofi)