Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Primary Question

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:- Wananchi wa Wilaya ya Chunya wameanza kujenga uwanja wa michezo wa kisasa wa Wilaya. Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi huu ili ukamilike haraka?

Supplementary Question 1

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina mswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, katika uwanja huo mimi kama Mbunge nilitoa hela yangu mwenyewe shilingi milioni kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukimuona mtu anatoa hela yake mfukoni kupeleka kwenye project ya wananchi kwa zama hizi ujue kilio hicho ni kikubwa sana. Chunya ni Wilaya ambayo ni kongwe sana, sasa hivi ina miaka 76. Viongozi wengi wa nchi hii akiwemo Profesa Mark Mwandosya amesoma Chunya na viongozi wa kidunia akiwemo aliyekuwa Rais wa makaburu wa mwisho Pieter Botha alizaliwa Chunya na kusoma Chunya. Kwa hiyo, Chunya ni Wilaya ambayo inatakiwa iangaliwe kwa huruma sana. Serikali inasemaje kuhusu kututafutia Chunya wafanyabiashara wakubwa wanaoweza kutusaidia kujenga uwanja huo ili waweze kutangaza biashara zao? La kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri anasemaje kuhusu kuja Chunya aje auone uwanja huo ili awe na uelewa mkubwa na mpana kuhusu uwanja huo? (Makofi)

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa dhati kabisa mzee wangu Mheshimiwa Mwambalaswa kwa jitihada zake kubwa ambazo amekuwa akizifanya katika kuboresha miundombinu ya michezo katika jimbo lake. Niseme wazi kabisa kwamba Wizara yangu pia inayo taarifa kwamba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na wananchi wa Wilaya ya Chunya na Jimbo la Lupa wamechangia kiasi cha shilingi milioni 224, ambazo kati ya hizo milioni kumi ametoa Mbunge wa Jimbo la Lupa Mheshimiwa Mwambalaswa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pia nichukue nafasi hii kuweza kuomba Wabunge wote kuiga mfano huu mzuri ambao Mheshimiwa Mbunge ameuonesha, lakini vilevile kuiga Halmashauri zote nchini zichukue mfano huu mzuri ambao umeonyeshwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya katika kuwashirikisha wadau katika kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu ya michezo.
Kuhusu swali lake la kwanza ambalo ameuliza kuomba wadau, kwamba Wizara imsaidie kuweza kutafuta wadau. Mimi niseme kwamba Mheshimiwa Mbunge Wizara yangu iko tayari kabisa kushirikiana pamoja na wewe, lakini vilevile na Halmashauri ya Wilaya ya Chunya na Jimbo la Lupa kuhakikisha kwamba tunahamasisha wadau mbalimbali waweze kujitokeza katika kuchangia ujenzi huo wa uwanja wa michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ombi lake la pili, niseme kwamba Mheshimiwa Mbunge mimi nikutoe wasiwasi, na ni mwezi wa 12 tu nilikuwa katika Wilaya ya Mbeya Vijijini. Kwa hiyo, niseme kwamba tutakapotoka hapa naomba tukutane tukae, tujadili, tuongelee ratiba kwamba ni lini ili na mimi niweze kuja kujione uwanja huo wa Lupa.

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:- Wananchi wa Wilaya ya Chunya wameanza kujenga uwanja wa michezo wa kisasa wa Wilaya. Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi huu ili ukamilike haraka?

Supplementary Question 2

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa vijana wetu wanaanza vipaji wakiwa mashuleni, je, Serikali ina mpango gani kuipa sekta ya michezo hasa mashuleni ili angalau vijana hao tuwakuze katika vipaji vya michezo ili tuweze kufikia kama nchi ya Brazil?

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri ambalo ameuliza.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba Wizara kupitia Serikali tuna mpango mzuri sana wa kuhakikisha kwamba vijana wetu waliopo shuleni wanashiriki katika michezo. Sasa hivi ninavyoongea tayari Wizara kwa kushirikiana na Serikali tumesharejesha ile michezo ya UMISETA na UMITASHUMTA katika mashule yetu. Haya ni mashindano ambayo kwa kiasi kikubwa sana yanasaidia kuibua vipaji vya vijana. Tumeshuhudia kwamba michezo hiyo inakwenda vizuri na wanafunzi wengi wamekuwa wakishiriki na vipaji vingi vya vijana vimeendelea kujitokeza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikutoe hofu kwamba Wizara tuna mikakati mizuri na tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba tunaedelea kuinua vipaji vya vijana wetu ambao wapo mashuleni, ahsante sana.