Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Kasuku Samson Bilago

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Buyungu

Primary Question

MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:- Walimu wa Elimu Maalum wanapohitimu kwenye Vyuo vya Patandi na SEKOMU hawapelekwi kwenye shule za vitengo vya elimu maalum:- (a) Je, Serikali haioni kama inapoteza rasilimali fedha na watu kwa kutoa elimu isiyo na tija kwa Walimu hao? (b) Je, ni lini Serikali itawapanga walimu wenye elimu maalum kwenye shule na vitengo vyenye mahitaji hayo?

Supplementary Question 1

MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. Maagizo yaliyotolewa na Serikali ya kuhamishia watoto wenye uhitaji wa elimu maalum ifikapo Desemba 31 mwaka huu hayatekelezeki; kwa sababu hata kwangu Wilaya ya Kakonko hakuna shule hiyo. Swali la kwanza, Serikali iko tayari kujenga shule ya watoto wenye uhitaji wa elimu maalum katika Wilaya ya Kakonko ikizingatiwa kwamba kuna watoto zaidi ya 200, Walimu wako watano tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa maelezo hayo hayo ambayo nchi nzima itaathiriwa na agizo hili la Serikali, je, Serikali inaweza ikajiridhisha kwamba kila wilaya inapata shule ya watoto wenye vipaji maalum yenye mabweni ili kuwaokoa katika usumbufu wanaoupata? Ahsante.

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Kasuku Samson Bilago, hajasahau taaluma yake licha ya kuwa Mbunge. Sasa naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kasuku kama ifuatavyo:-
Serikali imeshatoa maagizo tangu mwaka jana kwamba kila halmashauri iteue shule angalau moja ili watoto wenye mahitaji maalum waweze kusomeshwa vizuri kwa mujibu wa mazingira ya mahitaji yao. Sasa kama kwenye wilaya yake hakuna hata shule moja, natoa agizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ili aweze kutekeleza agizo la Serikali lililotolewa tangu mwaka jana mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, amezungumza kwamba kwenye eneo lake la Ubunge wapo Walimu watano tu ambao wana taaluma ya elimu maalum. Namhakikishia kwa agizo ambalo limetolewa na Serikali leo; mimi nimesisitiza tu lilishatolewa siku nyingi, nasisitiza na kuwapa muda kwamba ifikapo Desemba 31, 2018 agizo hili linatekelezeka. Ndiyo maana tumewapa muda mrefu vinginevyo tungeweza kuwapa mwisho tarehe 30 mwezi wa Juni, lakini tumewapa muda mrefu hadi Desemba ya 2018 ili Halmashauri ziweze kujipanga vizuri kuhakikisha agizo linatekelezeka. (Makofi)

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. KASUKU S. BILAGO aliuliza:- Walimu wa Elimu Maalum wanapohitimu kwenye Vyuo vya Patandi na SEKOMU hawapelekwi kwenye shule za vitengo vya elimu maalum:- (a) Je, Serikali haioni kama inapoteza rasilimali fedha na watu kwa kutoa elimu isiyo na tija kwa Walimu hao? (b) Je, ni lini Serikali itawapanga walimu wenye elimu maalum kwenye shule na vitengo vyenye mahitaji hayo?

Supplementary Question 2

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ni kweli baadhi ya halmashauri zimetekeleza agizo la Serikali la kutenga shule moja kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum, lakini ni kweli pia kwamba shule hizi hazina vitendea kazi pamoja na Walimu wa kutosha na matokeo yake hata ufaulu wa watoto umekuwa ukitia shaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitatoa mfano Shule ya Sekondari ya Viziwi Njombe ambayo matokeo ya Form Four ya mwaka uliopita shule nzima wamepata division zero. Sasa je, Serikali iko tayari pamoja na agizo hili kuhakikisha kwamba shule hizi zimepata Walimu wa kutosha na vitendea kazi ili hawa watoto waweze kuangaliwa kwa uzito ule ule wa watoto wengine ambao hawana mahitaji kama hayo? (Makofi)

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru amerejea kauli yangu kwamba agizo hili la kila Halmashauri kuwa na angalau shule moja ambayo watasoma watoto wenye mahitaji maalum. Napenda kumhakikishia kwamba agizo lile lililotolewa tangu mwaka jana lilienda sambamba na maagizo kwamba wahakikishe shule hizo zinakuwa na vifaa na vitendea kazi pamoja na Walimu ambao watawafundisha watoto hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wake wa Njombe alioutoa, namwagiza Mkurugenzi wa Elimu pale ofisini kwangu afuatilie hiyo shule ya Njombe kuona je, ni ukosefu wa vifaa au ukosefu wa Walimu au ni tatizo la wanafunzi wenyewe lililosababisha wote wapate division zero? Hata hivyo, tunafuatilia na naagiza kwamba kila Halmashauri inapoteua shule ya watoto wenye mahitaji maalum wahakikishe kwamba kunakuwa na vifaa vya kutosha vya kuwafundishia. Ndiyo maana tunaita ni mahitaji maalum kwa sababu mtu ambaye ana ulemavu wa macho anahitaji vifaa maalum vya kusomea. Mtu ambaye ana ulemavu wa akili anahitaji vifaa malum vya kusomea. Kwa hiyo wahakikishe vifaa vyote vinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni wakati wa kupanga bajeti, kwa hiyo wahakikishe kwamba ikifika mwezi wa Saba tarehe moja, utekelezaji uanze kufanyika kwa mujibu wa maelezo ya Serikali. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo taarifa kwamba wako Walimu wa kufundisha shule za walemavu wamehitimu hawajaajiriwa bado. Tumefanya mazungumzo na Ofisi ya Waziri Mkuu, nimezungumza na Naibu Waziri anayeshughulika na walemavu, tuletewe orodha ya mahitaji ya Walimu kwa ajili shule za walemavu, tutapata kutoka Wizarani orodha ya wale ambao tayari wamehitimu. Tutawaajiri mara moja ili wanafunzi hao nao wapate elimu kama wanafunzi wengine. (Makofi)