Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Lolesia Jeremia Maselle Bukwimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Busanda

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Tatizo la uhaba wa watumishi katika sekta ya afya kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni kubwa sana. Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuliondoa tatizo hilo?

Supplementary Question 1

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kutokana na jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri inaonesha kabisa kuna upungufu mkubwa wa watumishi 240. Katika mwaka 2017 wameajiri watu 22 vilevile mwaka ujao wanapanga kuajiri watu 121, hii inaonesha ni mkakati wa kawaida tu na kwa sababu hiyo hawajaweza kukidhi kile ambacho mimi nilikuwa nahitaji kujua. Mimi ninachotaka kujua, ni lini sasa Serikali itakuwa na mkakati wa dharura wa kuhakikisha kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Geita inapata watumishi wa kutosha ili waweze kuwapatia wananchi huduma inayostahiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Halmshauri ya Wilaya ya Geita hasa katika Jimbo la Busanda kuna baadhi ya vituo vya afya ambavyo kwa kweli vina upungufu mkubwa sana hasa katika Kituo cha Afya Katoro ambapo kuna idadi kubwa ya watu vilevile kituo hicho kinahudumia pia na Kata zingine jirani kama Rwamgasa, Busanda pamoja na Kasemye. Kitu hiki kina upungufu mkubwa sana wa wataalam kiasi kwamba inasababisha hata wakati mwingine watu kupoteza maisha yao. Ni lini sasa Serikali itahakikisha inapeleka watumishi kwa dharura katika kituo hiki cha afya? (Makofi)

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza anauliza mkakati wa dharura, ni ukweli usiopingika kama tulivyokiri kwenye jibu letu kwamba upo upungufu mkubwa sana na namna pekee ni kuweza kuajiri na suala la kuajiri ni pamoja na bajeti inaporuhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi tukubaliane kwamba kwa kuanzia na hao ambao tumewataja 121 si haba na kwa sababu katika majibu yangu kwenye swali la msingi nimemueleza sababu zilizosababisha upungufu huu mkubwa, siyo rahisi kwamba kwa mara moja tutaweza kuziba pengo hili kwa sababu suala lenyewe lina budget implication.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba Katoro pale idadi ya watu ni kubwa na iko haja ya kuhakikisha kwamba pamoja na hospitali iliyopo vijengwe na vituo vingine vya afya ili kuweza kuongeza maeneo ya afya kuweza kutibiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe kwa kupitia Halmashauri yake wana uwezo wa kuweza kufanya allocation ndani kutazama maeneo yapi ambayo staff wako wengi ili ndani kwa ndani kwanza kupunguza wakati wanasubiri ajira kutoka Serikali kuu. (Makofi)

Name

Dr. Mary Michael Nagu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Hanang'

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Tatizo la uhaba wa watumishi katika sekta ya afya kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni kubwa sana. Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuliondoa tatizo hilo?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba vituo vya afya na zahanati tunavihitaji sana na Serikali inajitahidi sana katika kusaidiana na wananchi kuvijenga vituo hivi na zahanati hizo. Je, si itakuwa ni kazi bure kama tutakuwa na vituo vya afya na zahanati ambazo hazina watumishi ambao watawapa huduma Watanzania? Naomba Serikali ione hilo kwa sababu huduma ya afya ni ya msingi sana watu wetu wasiendelee kuteseka. (Makofi)

Name

Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa, lakini nataka kutoa majibu ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunahakiki vyeti, watumishi wengi sana imebidi waachishwe kazi na moja kati ya idara ambayo imeathirika sana ni afya. Tumeambiwa katika baadhi ya maeneo hata zahanati zimelazimika kufungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali ilikwishatoa kibali cha ajira watu 50,000. Wizara yangu katika wale 50,000 kipaumbele namba moja ni afya na nataka nisema kama kuna Halmashauri yoyote ambayo huduma zimesimama kwa sababu watu wameondolewa na hawajapata watu mbadala waandike moja kwa moja kwangu watapatikana mara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala alilouliza Mheshimiwa Mary Nagu, nataka niwaambie Watanzania waondoe mashaka. Tuendelee sisi wanasiasa, viongozi kuhimiza ujenzi wa vituo vya afya na zahanati pale ambapo inakaribia kukamilika au wakati inajengwa Wizara yangu ikipata taarifa itafanya maandalizi wapatikane watumishi kabla ujenzi haujakamilika. (Makofi)

Name

Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Tatizo la uhaba wa watumishi katika sekta ya afya kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni kubwa sana. Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuliondoa tatizo hilo?

Supplementary Question 3

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Halmshauri ya Kaliua ina upungufu wa watumishi kwa asilimia 76, waliopo ni asilimia 24 tu. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kuna mkakati gani wa dharura kuhakikisha kwamba angalau kwa Kaliua kabla hata ya kuandika barua maana nasema hapa wanapatiwa watumishi wa afya ili akina mama waache kuteseka kwa kukosa huduma? (Makofi)

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):Mheshimiwa Naibu Spika, umenisaidia kwa sababu majibu aliyotoa Mheshimiwa Waziri wa Nchi na Mheshimiwa Sakaya yuko hapa, sidhani kama itakuchukua muda mrefu kuandika barua kuainisha huo upungufu ili hili jambo liweze kufanyiwa kazi kwa mara moja.

Name

Suleiman Masoud Nchambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Primary Question

MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:- Tatizo la uhaba wa watumishi katika sekta ya afya kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Geita ni kubwa sana. Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuliondoa tatizo hilo?

Supplementary Question 4

MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, wabheja sana.
Kwa kuwa Jimbo la Kishapu lenye watu shapu na Mbunge shapu, ni moja ya Majimbo ama Jimbo lililotekeleza kwa kiwango cha juu sana mpango wa huduma za afya. Tunayo hospitali ya kisasa kabisa katika Wilaya yetu ya Kishapu, tuna vituo vinne vya afya vya kisasa kabisa ambavyo vimekamilika na vinatoa huduma bora katika Jimbo la Kishapu, lakini katika vijiji 118, takribani asilimia 50 mpango wa zahanati katika Jimbo la Kishapu unaendelea vizuri na miongoni mwa vituo hivyo vya zahanati vinatoa huduma bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu je, ndugu yangu, wajina Mheshimiwa Suleiman Jafo na dada yangu Mheshimiwa Ummy, kutokana na malumbano ama tatizo kubwa la mpango wa afya ambalo ni dhahiri limeelezeka na wewe umekiri kuwa watu wengi wanahitaji kuuliza maswali katika jambo hili la afya na kwa kuwa Kishapu tumekwishajitahidi tumepiga hatua…
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Kwa kuwa Kishapu tumepiga hatua kubwa, je, Wizara ya Afya na Ofisi ya TAMISEMI kwa maana ya Wizara hawaoni sasa watoe kipaumbele kwa Jimbo la Kishapu ili kuiweka kuwa ni ajenda maalum na kipaumbele cha kumaliza tatizo hili ili Kishapu iwe mfano katika Wilaya zote nchini kwa kumaliza kabisa tatizo hili kwa kutuongezea michango?

Name

Dr. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

AZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Nchambi kwa kazi kubwa ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati na shughuli kubwa wanayofanya ya uhamasishaji katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba tutamuunga mkono na ajenda ya kwanza ni kwamba Ofisi yangu itafanya utaratibu wa ziara maalum kama ya kiheshima kwenda kule Kishapu ku-recognize juhudi kubwa inayofanywa kule. Baadaye tutaangalia way forward tunafanyaje kwa pamoja kwa lengo kubwa la kuwasaidia wananchi wa Kishapu kwa juhudi hiyo waliyoifanya.