Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ignas Aloyce Malocha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwela

Primary Question

MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:- Katika bajeti ya 2016/2017 Serikali ilipanga kujenga baadhi ya Mahakama za Wilaya na za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini. (a) Je, ni hatua ipi imefikiwa katika ujenzi wa Mahakama hizo? (b) Kwa kuwa Mahakama ya Mwanzo Mtowisa katika Wilaya ya Sumbawanga Vijijini ni miongoni mwa Mahakama iliyopangiwa bajeti ya ujenzi kutokana na uchakavu mkubwa na hatarishi kwa wananchi, je, ni lini ujenzi utaanza?

Supplementary Question 1

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mahakama ya Mwanzo Mtowisa ni mahakama iliyojengwa toka enzi za mkoloni na kutokana na hali hiyo imechakaa na inahatarisha maisha ya wananchi. Ndiyo maana Serikali katika bajeti ya mwaka 2015/2016 ni miongoni mwa mahakama iliyopangwa kujengwa upya. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuipa kipaumbele cha pekee kunusuru hali inayoweza kutokea kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa vile vikwazo ulivyovieleza vya upatikanaji wa kiwanja na hati miliki vyote vilishakamilika na uongozi wa Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga ulishathibitisha. Je, ni lini sasa Mahakama hiyo itaanza kujengwa? (Makofi)

Name

Anthony Peter Mavunde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Dodoma mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU - KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi kwamba katika mipango ambayo Wizara tumejiwekea ni kuhakikisha tunatimiza ukarabati wa ujenzi wa Mahakama kadri ya upatikanaji wa fedha za maendeleo. Hivyo kwa sababu katika mwaka huu wa 2017/2018, Mahakama ya Mwanzo Mtowisa ni kati ya Mahakama za Mwanzo ambazo zimewekwa katika mkakati huu, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi fedha zitakapopatikana jambo hili litatekelezeka.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu kwa sasa Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ardhi na Baraza la Ujenzi la Taifa, baada ya utafiti kufanyika kupitia teknolojia mpya ya ujenzi wa Mahakama kupitia Moladi ambapo imeokoa takribani asilimia 50 ya gharama za kawaida naamini kabisa fedha hizi zikipatikana Mahakama ya Mwanzo wa Mtowisa na yenyewe itaguswa pia.