Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Maryam Salum Msabaha

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:- Kumekuwa na uuzwaji wa silaha kiholela kama vile mapanga na visu katika barabara zetu ikiwemo Ubungo kwenye mataa hali ambayo inaleta hofu kwa raia wema. Je, Serikali inalichukuliaje suala hilo ambalo ni hatari sana kwa usalama wa raia?

Supplementary Question 1

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kumuuliza Naibu Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania imekuwa kisiwa cha amani, lakini kuna genge la wahuni ambalo hatujui wanapata wapi silaha za kijeshi na kushambulia raia wasiokuwa na hatia.
Je, Serikali haioni sasa imefika wakati muafaka kufanya doria katika sehemu zote za mipaka na barabarani na hata katika vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha genge hili halina nguvu kwa sababu linachafua taswira ya Tanzania katika medali za kitaifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa bado silaha hizi zinaendelea kuuzwa sehemu za starehe kama vile minadani na sehemu mbalimbali na kuhatarisha amani ya ambao wanafika katika kupata huduma katika sehemu hizo.
Je, Serikali ina mikakati gani ya ziada kuhakikisha suala hili kuuza silaha holela linakomeshwa na wale wanaokamatwa wachukuliwe sheria kali ili suala hili likome mara moja? (Makofi)

Name

Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni bahati mbaya sana Mheshimiwa Mbunge hajalitaja jina la kundi ambalo amelizungumza, lakini kimsingi nataka nimueleze tu kwa ufupi kwamba hali ya matumizi ya silaha kufanya uhalifu nchini imepungua, ndiyo maana hata ukiangalia takwimu tokea Juni, 2016 mpaka Agosti, 2017, hakuna matukio makubwa ya mauaji ya kutumia silaha za jadi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utaona ni kazi kubwa ambayo Serikali imefanya kupitia Jeshi la Polisi kuweza kudhibiti wahalifu na magenge mbalimbali ambayo yamekuwa yakitumia silaha hizo za jadi kwa ajili ya kufanya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba mafaniko hayo yamepatikana kwa sababu gani? Kuna mikakati mingi ambayo imefanyika ili kuweza kufikia malengo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tumeendelea kutoa elimu kwa Umma kuhusiana na makundi ambayo yamekuwa yakijitokeza, kwa mfano, maeneo ya Kanda ya Ziwa kuna watu walikuwa wanaitwa wakata mapanga, ukija huku Mbeya na kadhalika, wapo watu ambao walikuwa wanafanya mauaji kwa vikongwe kwa imani za kishirikina. Kwa hiyo, Jeshi la Polisi kwa kupitia utaratibu wake wa ulinzi shirikishi tumekuwa tukifanya jitihada kubwa sana za kutoa elimu kwa jamii ili kufahamu madhara ya matumizi ya silaha za jadi, hasa matumizi ya kujichukulia sheria mkononi kwa jamii, hilo moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, tumekuwa tukiendelea kufanya doria na ukaguzi barabarani kuweza kusimamisha magari na watu ambao wakipita na silaha hizo za jadi na kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria. Hii doria imekuwa ikiendelea na ndiyo maana mpaka sasa hivi tumeweza kufanikiwa kwa mujibu wa takwimu ambazo nimezieleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeendelea kuhakikisha kwamba huduma zetu za Jeshi la Polisi zinashuka katika ngazi ya Tarafa na Kata. Tuna Ofisi za Ukaguzi katika ngazi ya Tarafa na Kata ili kusogeza huduma ya Polisi karibu na wananchi kuweza kukabiliana na matukio mbalimbali ya uhalifu ya aina kama hii ambayo Mheshimiwa Mbunge amezungumza. Kwa hiyo, nikiri tu kwamba kwa jumla kazi kubwa imefanyika na mafanikio yake mpaka sasa hivi ndiyo haya ambayo nimeyaeleza, ni makubwa ya kuridhisha kwa kiasi fulani.

Name

Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Primary Question

MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:- Kumekuwa na uuzwaji wa silaha kiholela kama vile mapanga na visu katika barabara zetu ikiwemo Ubungo kwenye mataa hali ambayo inaleta hofu kwa raia wema. Je, Serikali inalichukuliaje suala hilo ambalo ni hatari sana kwa usalama wa raia?

Supplementary Question 2

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Watanzania wengi ni wakulima, wafugaji na wavuvi. Kwa mantiki hiyo, kisu na panga ni kitendea kazi muhimu na adhimu kwa kukamilisha kazi zao. Kama ni misuse, hata tai inaweza kutoa maisha ya mtu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini tafsiri sahihi ya neno silaha? Naomba majibu.

Name

Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Magharibi

Answer

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri ya silaha tunaitafsiri kufuatana na mazingira inapotumika. Kama mtu amebeba fimbo na anachunga, tunaelewa kwamba mazingira ya anakochunga anastahili kuwa na fimbo hiyo. Leo hii kama mtu anaingia Bungeni na amebeba kisu, ile inageuka kuwa silaha ambayo iko katika matumizi ambapo haitakiwi kuwa na huyo mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo, kama mtu anaenda kuangalia mpira (Ndondo Cup), hata kama kwenye utamaduni wake anatakiwa kuwa na mkuki, hatutarajii aende nao kwenye uwanja wa michezo, tunatarajia aende nao anakochunga ambako anaweza akakutana labda na wanyama wakali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo, hata uholela tunaoungelea kama ambavyo silaha zote zina utaratibu wa maeneo ambapo zinatakiwa kuuzwa, tunatarajia pia hata kwenye matumizi ziwe katika mazingira yanapotakiwa kutumika. Hatuwezi tukaruhusu Watanzania kila mmoja akawa anatembea na silaha popote anapojisikia kuwa nayo kwa sababu udhibiti wake utakuwa ni hatari kwa namna ya kuweza kuhakikisha wale wasiopenda au wasio na silaha wanaweza wakapata athari popote pale ambapo mwenye silaha anaweza akaamua kuitumia. (Makofi)