Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya maji katika vijiji 42 vya Jimbo la Momba?

Supplementary Question 1

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa masikitiko makubwa ndani ya Bunge lako Tukufu naomba niseme kwamba Mama yetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ana kauli yake ya kumtua ndoo mwanamke kichwani, lakini Wizara ya Maji ndani ya Jimbo la Momba mmeipinga kauli hii kwa vitendo, imeikataa kabisa hiyo kauli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hapa nimekuja na clip kwenye simu yangu naomba uletewe hapo mbele wewe kama Spika wetu ili angalau wewe uweze kuangalia uone. Kama maji haya ambayo wana-Momba wanatumia, binadamu wa kawaida wanafaa kutumia kutumia haya maji. Mwezi wa sita ulinipa nafasi ya kusimama hapa kuomba mwongozo kwa Wizara ya Maji ili wanichimbie visima vya dharura, mpaka leo hivyo visima pamoja na watoto kuteseka hakuna hata tone la maji.

Mheshimiwa Spika, mradi ambao Wizara ya Maji wanasema huu wa bilioni 9.5 mwaka jana mwezi ya nne waliniondoa hapa Bungeni kwenda kukabidhi mradi kwa mkandarasi na tukaitwa mkutano mkubwa kwa wananchi na wakaahidi kwamba, kufikia mwaka huu mwezi wa sita mradi wa maji utakuwa umekamilika.

Mheshimiwa Spika, leo tunavyoongea wiki moja iliyopita ndiyo wametupatia milioni mia tano kati ya bilioni 9.5 na leo mbele ya Bunge lako tukufu Wizara ya Maji wanasema kwamba mradi huu utakamilika Desemba. Mimi nikienda kwa wananchi ndiyo naonekana tapeli. Sasa kati ya mimi na Wizara ya Maji wakina nani ni waongo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba hii clip uiangalie kwa niaba ya Bunge ili uone hii clip wewe uwe shahidi ikikupendeza ili uoneshwe hapa ili Mheshimiwa Rais aone kama Watanzania tulio mchagua, mimi Mbunge wa kike mtoto wake, wanawake wameniamini wanaweza wakatumia maji haya. Mimi naomba hii clip uone na Mheshimiwa Waziri Mkuu yupo hapa aione hii clip…

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru kwa nafasi hii lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa namna anavyojibu maswali yake vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, kubwa Bunge lililopita tulipata concern ya Mheshimiwa Mbunge, Dada yangu Condester na mimi kama Waziri wa Maji nilifika Jimboni kwake na tukafika maeneo mbalimbali kuona hali ipo miradi ambayo inaendelea lakini kwa udharula nilitoa kiasi cha shilingi bilioni moja kuhakikisha kwamba tuna-support miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe sana Waheshimiwa Wabunge wakati mwingine tunaweza tukawakatisha tamaa watendaji wanaofanya kazi kubwa. Lakini kazi inafanyika na sisi kama Wizara ya Maji na ipo miradi ya kimkakati kuhakikisha kwamba tunalisaidia Jimbo la Momba.

Mheshimiwa Spika, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama viongozi wa Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo kwa Wananchi wa Momba kupata Huduma ya Maji Safi na Salama katika kuhakikisha kwamba tunamtua mwanamama ndoo kichwani. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, nimeletewa hapa hizo clip na nafikiri, hebu msaidizi njoo mfikishie Mheshimiwa Waziri pale ili apate hii picha.

(Hapa Waziri wa Maji alikabidhiwa simu iliyokuwa na clip yenye kuonesha akinamama wa Momba wakichota maji)

SPIKA: Lakini hoja ya Momba Waheshimiwa nadhani mtakumbuka kuna kipindi zilitajwa takwimu hapa ndani kuhusu maji, akasimama Mbunge wa Momba kuelezea kwamba hizi takwimu kwake yeye hazina uhalisia. Akasimama tena kama alivyosema kwenye Bunge nadhani ni Bunge la Bajeti ama lipi? Alisimama tena akaeleza maelezo yakatoka kwamba vikachimbwe visima kwa sababu magari yameishanunuliwa na Mheshimiwa Rais, vikachimbwe visima vya dharura yakatoka majibu hapa.

Mheshimiwa Waziri, anasema alishatoa bilioni moja maana yake hii milioni mia tano ni ya kuongezea kwenye ile bilioni moja ili utekelezaji uendelee. Lakini hali ya hawa wananchi nimekuletea hizo clip hapo siyo hali inayokubalika kwenye hivyo visima wanavyochota maji na kwa hiyo hali iliyoko hapo maana yake kwenye ardhi hiyo yapo maji. Kwa sababu hawa wanawake wametumbukia kwenye hicho kisima maana yake ikienda gari ikachimba hicho kisima hata kama ni kimoja, viwili, vitatu kwa wakati miradi mikubwa ikiendelea wachimbiwe hivyo visima nadhani nimekuletea hiyo clip umeishaipata au umeishaipata clip?

WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, sisi haya ni maelekezo na tunayapokea na kama ana ufahamu Mheshimiwa Mbunge, mimi nilifika na tukatembea maeneo mengi na tukaweka mkakati. Kikubwa hayo ni maelezo jukumu letu ni kwenda kuyatekeleza. (Makofi)

SPIKA: Sawa, sasa kwa sababu kipindi hiki ni cha mvua lazima pia tuwe na uhalisia. Mheshimiwa Condester haya maji yanachotwa kipindi hiki au ni kipindi cha kiangazi? Ili na mimi nitoe maelekezo ambayo yanaeleweka hapa mbele, haya ni ya kipindi hiki cha mvua ama kipindi cha kiangazi? Hizi clip ni za sasa hivi au za kipindi cha kiangazi?

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, hizo clip nimechukua mwaka jana Mwezi wa Kumi na Mbili. Kwa hiyo, kipindi cha mvua watu ambao hawana mabati…

SPIKA: Hamuoni sasa hii yaani ni kipindi hiki?

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

SPIKA: Haya. Mheshimiwa…

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, wakati mvua zimeishaanza.

SPIKA: Sawa. Mheshimiwa Waziri ameishapokea hayo maelekezo kwa sababu magari yapo kila Mkoa, gari lililoenda Songwe ama Mkoa wa jirani liazimwe lipelekwe likawachimbie kisima hawa wamama nadhani umeona hiyo hali iliyoko hapo. Kwa hiyo, nadhani hilo linaweza kufanyika ndani ya muda mfupi. Kwa sababu tayari hapo pana maji yale mambo ya usanifu, yakinifu, upembuzi, sijui nini hapo maji yapo na kwa sababu tayari wanayatumia hayo kawachimbieni hayo hayo wakati mnaendelea na utafiti wenu ili wananchi wa Momba waweze kupata maji. (Makofi)

Name

Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya maji katika vijiji 42 vya Jimbo la Momba?

Supplementary Question 2

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi niulize ni lini Vijiji vya Mdundwalo, Maposeni, Malamala na Kimbango Nyasa vitapatiwa hivyo visima vya maji? Ahsante.

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Ntara, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo haya aliyoyataja Mheshimiwa Dkt. Ntara tayari usanifu unafanyika, gari la kuchimba visima liko kule tumeishachimba kisima kikatoka maji machache sana kiasi kwamba hayawezi hata kupanda kwenye kichotea maji hata kimoja. Niwapongeze sana Regional Manager (RM) Ruvuma niliwaagiza, kwa sababu Dkt. Ntara hili swali ameishaniuliza mara nyingi tukiwa kwenye kiti. Tumeishafanyia kazi na wananchi wametoa ushirikiano kuna mto unaitwa Mpulanginga, huu mto umeonekana una maji ya kutosha kwa maeneo ya Mdundwalo na Maposeni. Lakini vilevile maeneo haya mengine ya Nyasa vilevile baada ya gari kumaliza hapa tunarajia liende huko likaweze kuchimba visima ili wananchi wapate maji safi na salama. (Makofi)

Name

Suma Ikenda Fyandomo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya maji katika vijiji 42 vya Jimbo la Momba?

Supplementary Question 3

MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Wilayani Rungwe kuna tatizo kubwa la maji hasa Kata ya Bulyaga, Makandana, Bagamoyo, Kawatere, Msasani na Ibigi. Sasa je, ni lini ujenzi wa tenki ambalo linatakiwa kuhudumu Kata hizo utakamilika? Ahsante.

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Suma Ikenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Suma Fyandomo kwa kufuatilia Mradi wa Maji Tukuyu lakini ushirikiano mkubwa sana wa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo, Mheshimiwa Mwantona amefuatilia pia kwa karibu Mradi wa Maji Tukuyu Mjini na hili tenki ujenzi unaendelea na fedha milioni mia tano tunarajia kupeleka tena mgao wa mwezi huu. Kwa hiyo, nikutoe hofu Mheshimiwa Mbunge na mradi huu unakwenda kukamilika na wananchi wa Tukuyu wanaenda kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya maji katika vijiji 42 vya Jimbo la Momba?

Supplementary Question 4

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi niulize swali swali la nyongeza. Ningependa kufahamu Serikali mnamkakati gani wa ziada kumaliza changamoto kwenye zile Kata tano za Makao Makuu ya Wilaya ya Nkasi? (Makofi)

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Aida Khenani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, mkakati wa ziadi kuhakikisha zile Kata tano zinapata maji ni kwenda kupeleka miradi ya muda mfupi ya uchimbaji wa visima ili wananchi waendelee kupata maji wakati utaratibu wa kutumia Ziwa Tanganyika unaendelea kufanyiwa kazi.

Name

Shamsia Aziz Mtamba

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya maji katika vijiji 42 vya Jimbo la Momba?

Supplementary Question 5

MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Je, ni lini sasa Serikali itatatua changamoto ya maji ambayo ipo kwa muda mrefu katika Kata ya Lipwidi?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shamsia lini Kata hii aliyoitaja tunapeleka maji? Mheshimiwa Shamsia kwanza nikupongeze kwa sababu umeishafuatilia sana lakini jitihada zinazoendelea pale Jimboni umeziona viongozi wetu wa Mkoa wa Mtwara wanaendelea kufanyia kazi na Kata hii inakwenda kupatiwa huduma ya maji safi na salama muda siyo mrefu.

Name

Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Primary Question

MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya maji katika vijiji 42 vya Jimbo la Momba?

Supplementary Question 6

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Halmashauri ya Itigi haijachimbiwa visima katika bajeti mbili zilizopita na gari la Mkoa wa Singida limekuwa likienda huku huku mara Msomera mara wapi? Sasa lini Serikali itakwenda kuchimba visima katika Halmashauri ya Itigi, katika Jimbo langu?

Name

Maryprisca Winfred Mahundi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, Mbunge wa Itigi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, hili eneo ambalo linatakiwa likachimbwe visima lipo kwenye mpango na kwa sababu gari lipo pale Mkoani tunarajia likimaliza upande umoja liliopo litakwenda katika maeneo haya na maeneo yote ambayo yanatakiwa kuchimbwa visima, visima vitachimbwa.