Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, nyumba bora ya kuishi inatakiwa kuwa na sifa zipi na ni kwa nini Serikali haiweki ruzuku kwenye vifaa vya ujenzi?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza; kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kabisa ambayo yamekwenda shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa ya sensa ya mwaka 2012 nchi yetu ina jumla ya nyumba 11,873,1950; kati ya hizo, nyumba bora ni 3,444,519 sawasawa na asilimia 37.1 maana yake tuna nyumba 8,429,431 ambazo ni sawa na asilimia 62.9 nyumba hizi sio bora, lakini kati ya hizo nyumba 2,359,906 sawasawa na asilimia 25.4 ni nyumba zimeezekwa kwa nyasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa swali langu; nyumba ya kawaida ya vyumba viwili inahitaji shilingi 400,000 kwa maana ya kununua bundle mbili za mabati. Je, kwa nini Serikali isiweke pale shilingi 200,000 kwa mtu ili na yeye achangie shilingi 200,000 ili hatimaye Serikali itumie kama shilingi bilioni 432 kuondoa kabisa nyumba za nyasi katika nchi hii? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili; ni kwa nini Serikali isiweke viwango vya nyumba bora, ili kila mwananchi awe anazingatia ujenzi wa nyumba bora? Ahsante.

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Joseph George Kakunda, maswali yake mawili kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakapokuwa tumekamilisha sera ya nyumba na makazi jibu lako litakuwepo ndani yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye swali la pili; ni kwamba Wizara imeendelea kuandaa rasimu ya Taifa ya Nyumba ambayo pamoja na mambo mengine itatoa mwongozo wa viwango vya nyumba bora vinavyotakiwa kuzingatiwa na wadau wote. Aidha, sera hiyo itaweka uratibu rahisi wa upatikanaji wa vifaa vya ujenzi vya gharama nafuu, upatikanaji wa mikopo ya nyumba, mfumo wa uratibu wa wadau wa sekta ya nyumba na hivyo kuwezesha upatikanaji wa nyumba bora kuwa za gharama nafuu, ahsante.

Name

Lucy Thomas Mayenga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza: - Je, nyumba bora ya kuishi inatakiwa kuwa na sifa zipi na ni kwa nini Serikali haiweki ruzuku kwenye vifaa vya ujenzi?

Supplementary Question 2

MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa sababu kubwa ambayo inasababisha wananchi waweze kushindwa kujenga nyumba bora ni gharama kubwa ya vifaa vya ujenzi, lakini vifaa hivi ni suala ambalo haliko Wizara ya Ardhi, liko Wizara ya Viwanda na Biashara.

Je, Wizara hii iko tayari sasa kukaa na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kuangalia zile sababu zote zinazofanya vifaa kuwa bei kubwa ikiwemo matamko ya viongozi, gharama kubwa za kodi na changamoto nyingine? (Makofi)

Name

Ridhiwani Jakaya Kikwete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chalinze

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa mawazo yake mazuri, lakini nataka nimhakikishie tu kwamba yako maelekezo toka kwa Mheshimiwa Rais na Serikali kwa ujumla kukaa na Wizara zote zinazohusika katika eneo hili la ujenzi wa nyumba ikiwemo Wizara ya Ujenzi, ili kuhakikisha kwamba gharama zinakuwa nafuu katika ujenzi, lakini pia katika vifaa na kuhakikisha mazingira yanakuwa mazuri ya upatikanaji wa nyumba zilizo bora na salama.