Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 12 Sitting 5 Defence and National Service Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa 71 2023-09-04

Name

Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-

Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Vijiji vya Msata, Kihangaiko na Pongwe Msungura kutokana na maeneo yao kuchukuliwa na Jeshi la Wananchi?

Name

Dr. Stergomena Lawrence Tax

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu tangu niteuliwe tena kuwa Waziri wa Ulinzi na na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake, lakini nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini kuendelea kumsaidia katika nafasi hii. Niahidi kwamba nitaendelea kufanya kazi zangu kwa uwezo wangu wote, kwa uaminifu, kwa uadilifu na kwa kujituma.

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo ya Vijiji vilivyotajwa yaani Msata, Kihangaiko, na Pongwe Msungura yapo katika Makambi mawili ya Jeshi ambayo ni RTS Kihangaiko na Msata Military Training Base katika Wilaya ya Chalinze. Serikali imeendelea na kutatua migogoro hii ya ardhi katika maeneo haya na katika mwaka 2021 ulifanyika uthamini wa awamu ya kwanza uliojumuisha Vijiji vya Msata, Pongwe Msungura na baadhi vitongoji katika Kijiji cha Kihangaiko. Uthamini awamu ya pili ulifanyika mwaka 2022 ukijumuisha vitongoji viiyosalia katika Kijiji cha Kihangaiko.

Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Uthamini uliofanyika mwaka 2021 iliwasilishwa katika Ofisi ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ili kukamilisha taratibu. Taratibu zitakapokamilishwa na Halmashauri ya Wilaya hii itawasilisha jedwali la malipo kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa kuidhinishwa na hatimaye kufanyiwa uhakiki na malipo na Wizara ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, katika uthamini uliofanywa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mwaka 2022, Wizara ya Fedha imekwishafanya uhakiki kwa Vitongoji vya Funta, Chokozeni na Kudikongo, vilivyopo katika Kijiji cha Kihangaiko kwa ajili ya kulipa fidia na malipo ya shilingi 330,788,467 yameshafanyika kwa wananchi katika Kitongoji cha Funta.

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, lakini pia na Halmashauri ya Chalinze ili kuhakikisha ulipaji wa fidia unakamilika.