Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 12 Sitting 1 Planning and Investment Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji). 5 2023-08-29

Name

Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, ni fursa gani za uwekezaji zinapatikana Tanzania?

Name

Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Answer

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naomba uniruhusu nitumie dakika moja tu kutoa shukurani. Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa imani kubwa aliyonipa kumsaidia katika ofisi yake katika eneo la mipango na uwekezaji. Nimuahidi kwamba nitafanya kazi hii kwa bidii na utii wa hali ya juu kwake, kwa Serikali yake, kwa nchi yetu na kwa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa ushirikiano ambao ulinipa nikiwa Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati yako, nakushukuru sana lakini niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano na niwaombe wanipe ushirikiano katika hatua hii ambayo ninayo kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, naomba sasa nijibu swali namba tano la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Nchi yetu imejaliwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji kwenye sekta mbalimbali. Naomba nitaje sekta tano tu kwanza, katika sekta ya kilimo tunazo fursa za uwekezaji katika kuongeza thamani ya mazao. Tunayo pia fursa ya kilimo katika mazao ya kipaumbele kama vile mafuta ya kula, sukari na ngano. Tunazo pia fursa katika eneo la utalii hasa katika ujenzi wa hoteli na makazi, tunazo fursa katika eneo la viwanda hasa katika viwanda vinavyolenga uzalishaji wa mbolea, dawa za mifugo na binadamu, nguo na mavazi na bidhaa za ujenzi.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la nishati na gesi tunazo fursa za uwekezaji katika kuzalishaji nishati, katika uvunaji wa gesi na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi. Tunazo pia fursa katika eneo la madini hasa katika maeneo ya utafiti, uchimbaji na uongezaji thamani ya madini.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.