Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Primary Question

MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y. MHE. HUSSEIN N. AMAR) aliuliza:- (a) Je, ni lini walimu wataboreshewa maslahi yao pamoja na nyumba za kuishi? (b) Kwa juhudi za Mbunge wa Jimbo la Nyang’hwale ameweza kujenga madarasa mawili katika Kata ya Izunya kwa lengo la kuanzishwa shule ya sekondari tangu mwaka 2014. Je, ni kwa nini shule hiyo haijafunguliwa hadi sasa ili kuwapa moyo wafadhili?

Supplementary Question 1

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maelekezo yako lakini kipekee nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri japo ni marefu kama ambavyo umesema.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu hayo mazuri, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, wananchi wa Halmashauri na Jimbo la Msalala kama walivyo ndugu zao wa Jimbo la Nyang’hwale na kwa kushirikiana na Mbunge wao hivyo hivyo nao wamefanya kazi kubwa sana ya kuanza kujenga shule mpya za sekondari, Shule za Mwazimba na Nundu ambazo miundombinu aliyoitaja Mheshimiwa Naibu Waziri karibia yote imekamilika, lakini shule hizi hazijapata kibali cha kufunguliwa.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua ni lini shule hizi mbili za Nundu na Mwazimba katika Halmashauri ya Wilaya ya Msalala zitafunguliwa kuanza kupokea wanafunzi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Msalala kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Msalala katika kipindi cha miaka minne iliyopita wamefanikiwa kujenga hosteli kwenye shule saba za sekondari za Kata, shule za Busangi, Baloha, Segese, Lubuya, Bulige, Ntobo…
Mheshimiwa Spika, samahani, naomba nimalizie tu swali langu fupi kwamba shule hizi zina watoto lakini hazitambuliwi na Serikali na hazipati ruzuku ya uendeshaji wa hosteli. Ni lini shule hizi zitatambuliwa na Serikali ili ziwe zinapata ruzuku ya gharama za uendeshaji wa hosteli hizi?

Name

Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimsihi Mheshimiwa Mbunge taratibu zifuatwe ili hizo shule ziweze kufunguliwa. Kwa sababu ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba pale ambapo miundombinu ya shule imekamilika zinaweza kufunguliwa ili wananchi wetu wapate huduma kwa karibu.
Mheshimiwa Spika, katika hilo la pili amesema kwamba hosteli zimejengwa sasa anataka Serikali ianze kuhudumia hosteli.
Mheshimiwa Spika, sina uhakika kama msingi wa swali ni juu ya kwamba hosteli ikishajengwa ianze kupata huduma, lakini kama nimemuelewa sawasawa kwamba anachomaanisha ni kwamba shule hiyo itambuliwe kwamba ni miongoni mwa shule za boarding, naomba tu tufuate taratibu ili wananchi na hasa vijana wetu ambao wana adha ya kutembea umbali mrefu hosteli pale inapokamilika huduma ziweze kutolewa.