Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 46 Industries and Trade Viwanda na Biashara 386 2019-06-17

Name

Frank George Mwakajoka

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Tunduma

Primary Question

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatafuta masoko ya uhakika ya ndani na nje kwa wakulima wanaozalisha mazao ya chakula kama mahindi na mpunga?

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia mmalaka ya maendeleo ya biashara Tanzania yaani TanTrade imekuwa ikiratibu jitihada mbalimbali za upatikanaji wa masoko ya mazao mbalimbali yanayozalishwa Nchini yakiwemo mahindi na mpunga.

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la utafutaji masoko ndani na nje ya nchi ikiwemo masoko ya mazao ya chakula ni jukumu endelevu. Utekelezaji wa jukumu hilo huhusisha Taasisi ya TanTrade, Balozi za Tanzania nje ya nchi, Bodi za Mazao, Soko la Bidhaa za Mazao na sekta binafsi. Lengo la kutumia Balozi zetu nje ya nchi ni kupata taarifa za kina kuhusu mahitaji ya masoko ya mazao na bidhaa za Tanzania katika nchi husika. Kwa jitihada hizo, yamepatikana masoko ya mchele na mahindi katika nchi ya Oman, Misri, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Burundi na Visiwa vya Comoro. Aidha, kupitia TanTrade tulipokea maombi ya sekta binafsi kutoka nchi ya Rwanda ya kununua tani 102,000; nchi ya Burundi tani 100,000; Zambia tani 3000 na Visiwa vya Comoro tani 3000 za mahindi kwa kupindi cha mwaka 2018/2019. Kwa mujibu wa takwimu za TRA tayari tani 39,218 za mahindi zimeshauzwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na Soko la Bidhaa, imeendelea kuhamasisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kutumika katika mazao ya kilimo ikiwemo mahindi na mpunga ili kuyafikia masoko ya ndani na nje ya nchi. Vilevile Wizara imeendelea kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda ili kupata soko la uhakika la mazao ya kilimo. Viwanda vimeendelea kuongezeka vikiwemo vya EPZA, kufufuliwa kwa vinu vya nafaka vya Iringa, Arusha, Mwanza na Dodoma chini ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko na kile cja Mlali - JKT kilichozinduliwa tarehe 8 Aprili, 2019 na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vingine vingi vinavyoendelea kuanzishwa na wafanyabiashara wadogo na wakubwa nchini.