Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 11 Sitting 32 Works, Transport and Communication Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 272 2017-05-18

Name

Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Primary Question

MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Wakati akihutubia mkutano wa kampeni Kharumwa Mheshimiwa Rais aliwaahidi wananchi wa Nyang’hwale kwamba barabara ya Kahama – Busangi – Kharumwa – Buyagu – Busisi itajengwa kwa kiwango cha lami; na Ilani ya CCM ya mwaka 2015 - 2020 imesema barabara ya Kahama - Bulige – Solwa – Mwanangwa itafanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
Je, kuna maandalizi gani yanayoendelea ya kutekeleza ahadi hiyo ya Rais na ile ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba kwanza nianze kwa kuwatakia ndugu zangu waislam wote nchini mfungo mwema katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kahama – Busangi – Kharumwa – Buyagu hadi Busisi yenye urefu kilometa 156.68 ni barabara ya mkoa inayounganisha mikoa mitatu ya Shinyanga, Geita na Mwanza. Aidha, barabara ya Kahama - Bulige – Solwa – Mwanangwa yenye urefu wa kilometa 150 ni barabara ya mkoa inayounganisha mikoa ya Shinyanga na Mwanza. Barabara hizi ni miongoni mwa barabara ambazo Serikali imepanga kuzijenga kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako tukufu kuwa Wizara yangu itaendelea kutekeleza ahadi za viongozi wakuu kwa awamu kutegemeana na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, barabara ya Kahama – Busangi – Kharumwa – Buyagu – Busisi itatekelezwa kama Mheshimiwa Rais alivyoahidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara ya Kahama – Bulige – Solwa – Mwanangwa (kilometa 150) ni kweli ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015. Napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kuwa tayari upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii umekamilika, kama ilani inavyoelekeza. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha za kugharamia ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.