Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Selemani Moshi Kakoso (14 total)

MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Mpanda ndiyo pekee inayotoa huduma za Mkoa katika Mkoa wa Katavi, kwa kutumia bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda;
Je, ni lini Hospitali ya Mkoa itajengwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Suleiman Kakoso Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za awali za ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Katavi zimeshaanza ambapo eneo la ekari 243 limepatikana. Katika bajeti ya mwaka 2014/2015, Mkoa ulipokea shilingi milioni 750, kati ya hizo shilingi milioni 468 zilitumika kulipa fidia kwa wananchi walioachia maeneo yao kupisha ujenzi wa hospitali. Hadi sasa Mkoa upo katika hatua za mwisho kusaini mkataba na kampuni ya Y and P Consultant ikiwa ni hatua muhimu ya kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 1.4 ili kuendelea na ujenzi wa hospitali ya Mkoa katika Mkoa mpya wa Katavi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Vijiji vingi katika Jimbo la Mpanda Vijijini havina huduma ya umeme.
Je, ni lini Serikali itapelekea huduma ya umeme katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Miradi ya REA awamu ya kwanza nay a pili haikuhusisha Jimbo la Mpanda Vijijini. Katika kuhakikisha kwamba wananchi wa Mpanda wanapata umeme wa uhakika Serikali inatarajia sasa kuvipatia umeme vijiji 49 vya Mpanda Vijijini pamoja na Ofisi za Wilaya kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu unaotarajiwa kuanza mwezi Juni, mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme katika Jimbo la Mpanda Vijijini itahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovolt 0.4 yenye urefu wa kilometa 280. Lakini pia ufungaji wa transfoma 64 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 2,452. Gharama ya kazi hii ni shilingi bilioni 9.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uholanzi kupitia Mradi wa ORIO itafunga mitambo mipya ya kuzalisha umeme wa megawatts 2.5 katika Mji wa Mpanda itakayowezesha maeneo mengi kupata umeme wa uhakika. Mradi huu unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2016 na kukamilika mwezi Julai, 2017.
MHE. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:-
Vijiji vya Kabage, Kungwi, Sibwesa, Kasekese na Kaseganyama viko kwenye mgogoro mkubwa wa ardhi na WMA.
Je, ni lini Serikali itaingilia kati na kutatua mgogoro huo unaoleta usumbufu mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kanuni ya Maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori za mwaka 2012 zinaelekeza wananchi kuanzisha maeneo hayo katika ardhi ya kijiji kwa ridhaa yao wenyewe, kwa faida yao kiuchumi na kijamii, lakini pia kwa faida za uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, eneo linalopendekezwa kuwa WMA ya Ubende ilianza na vijiji kumi ambavyo vimeongezeka kufikia vijiji 18. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda lilitoa baraka za kuanzishwa kwa WMA hiyo katika kikao chake cha tarehe 25 Machi, 2005.
Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuanzishwa kwa WMA ya Ubende haukuweza kuendelea katika hatua za mbele baada ya kusajiliwa kwa Chama Wakilishi cha Jumuiya (CBO) mwaka 2006 kwa sababu mbalimbali zikiwemo ukosefu wa fedha, uvamizi wa maeneo yaliyotengwa, mabadiliko ya maeneo ya kiutawala na kutoelewana kwa baadhi ya makundi ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa eneo hili husika kiikolojia na kiuhifadhi kwa ujumla, Wizara yangu itaharakisha kutoa ushauri, msaada wa kitaalam na kushirikiana na Halmashauri za Wilaya ya Mpanda, Manispaa ya Mpanda na Wilaya ya Nsimbo ili kufikia malengo mapana ya kuanzishwa kwa WMA ya Ubende. Aidha, Wizara yangu inaamini kwamba kuanzishwa na kuendeshwa kwa tija kwa Jumuiya ya Uhifadhi ya Ubende kutaleta mafanikio siyo tu ya kiuhifadhi lakini pia ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa vijiji husika na Taifa kwa ujumla.
MHE. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga Barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mpanda hadi Uvinza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mpanda hadi Uvinza yenye urefu wa kilometa 194. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Mpanda – Uvinza – Kanyani yenye urefu wa kilometa 256. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania imesaini mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami mwezi Julai, 2016 kwa sehemu ya Mpanda hadi Usimbili (Vikonge) yenye urefu wa kilometa 35 na Mkandarasi, Kampuni ya China Railway Seventh Group kutoka China ameanza kazi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha za kuendelea na ujenzi wa sehemu iliyobaki ya kutoka Usimbili hadi Uvinza yenye urefu wa kilometa 159.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Barabara ya Mishamo imeombewa kibali ili ipandishwe hadhi na kuwa barabara ya Mkoa lakini hadi sasa hatujui kinachoendelea.
Je, ni lini barabara hiyo itapandishwa hadhi na kuwa chini ya TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Seleman Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upandishwaji hadhi wa barabara hufanywa kulingana na Sheria ya Barabara ya mwaka 2007 pamoja na kanuni zake za mwaka 2009 ambapo maombi yanatakiwa kuwasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana na Wizara ya Ujenzi kupitia kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano haijapokea maombi ya kupandishwa hadhi barabara ya Mishamo. Hata hivyo, Wizara yangu itaifanyia tathmini barabara hii iwapo inakidhi vigezo vya kupandishwa daraja na kuchukua hatua stahiki kulingana na matakwa ya sheria.
ZAINAB A. KATIMBA (K.n.y. MHE. MOSHI S. KAKOSO) aliuliza:-
Wavuvi wadogo wadogo wa Ziwa Tanganyika wana tatizo la vitendea kazi.
Je, ni lini Serikali itawapatia wavuvi hao vitendea kazi vya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako, kwanza naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, kumshukuru Mheshimiwa Spika, wananchi wenzangu wa Mkuranga na kwa namna ya kipekee kabisa kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini kushika nafasi hii ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, naomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, nijibu swali la Mheshimiwa Moshi Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuhamasisha wadau wa uvuvi, ikiwemo sekta binafsi na jamii ya wavuvi wenyewe kuwekeza katika matumizi ya zana bora za uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha mapato yao, baadhi ya mikakati iliyotekelezwa ni kuwawezesha wavuvi wadogo kuanzisha vyama vya ushirika vya msingi kupitia halmashauri husika na pia wawekezaji wakubwa kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza boti na zana mbalimbali za uvuvi hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ziwa Tanganyika, tunacho Kituo chetu cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) pale Kibirizi Kigoma, ambapo tunayo mipango kama Serikali kukiimarisha ili kiweze kuunda boti za kisasa na pia kuendelea kutoa mafunzo na elimu inayohusu sekta ya uvuvi kwa wanafunzi na jamii za wavuvi na wadau wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali inatekeleza Sheria ya VAT ya mwaka 2007 ambayo imetoa msamaha wa kodi ya zana za uvuvi na malighafi nyingine ikiwemo injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu na vifungashio vyake. Vilevile katika jitihada nyingine za kuwasaidia wavuvi, Serikali hii ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, katika mwaka 2015/2016 ilitenga jumla ya fedha shilingi milioni mia nne ambapo jumla ya injini za boti 73 zilinunuliwa na katika hizo boti 49 zilishachukuliwa na vikundi vya wavuvi mbalimbali nchini kupitia Halmshauri zao katika mtindo wa ruzuku ambapo Serikali inachangia asilimia 40 na vikundi vya wavuvi vinachangia asilimia 60.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi sasa tunazo boti takribani 24 ambazo zinawasubiri wavuvi mbalimbali waliopo nchini ikiwa ni pamoja na wavuvi walioko Mpanda na Ziwa Tanganyika lote kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shime kwa Waheshimiwa Wabunge, tuhamasishe vikundi hivi vya wavuvi, mashine hizo bado tunazo, waweze kuja kupitia halmashauri zao kwa kufuata utaratibu kuzipata na kuweza kuimarisha shughuli zao za uvuvi kwa ajili ya kujipatia kipato zaidi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Tangu mradi wa maji katika Kijiji cha Ngomalusambo ukamilike haujawahi kutoa maji hata kidogo:-
Je, ni sababu zipi zilizofanya mradi huo usitoe maji kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Suleiman Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji katika Kijiji cha Ngomalusambo chenye jumla ya wakazi 1,672 ulianza kujengwa mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2015 kwa gharama ya shilingi 268.9. Mradi huo unategemea jenereta ya dizeli inayopampu maji kutoka kwenye kisima kwenda kwenye tenki. Mradi huu umeshindwa kutoa huduma kwa wananchi kutokana na kuibiwa betri ya pampu iliyofungwa katika mradi huo. Ili kukabiliana na changamoto hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imekamilisha ununuzi wa betri mpya na kuifunga wananchi wa Ngomalusambo wameanza kupata maji kuanzia tarehe 22 Juni, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ina mpango wa kuchimba kisima kingine katika mwaka wa Fedha 2017/2018 ili kuwezesha mradi huo ufanye kazi kwa ufanisi kutokana na kisima kilichopo sasa kupoteza uwezo wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na wizi wa betri uliojitokeza hapo awali, Serikali inatoa wito kwa wananchi wa Kijiji cha Ngomalusambo kulinda mradi huo kwa manufaa ya wananchi wote. Napenda kusisitiza kuwa, Serikali haitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria kwa uharibifu wowote wa miradi ya maendeleo kwa maslahi ya watu binafsi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Tatizo la maji katika vijiji vya Mlibansi, Mazwe, Mgamsamansi, Ilangu, Kapemba na Busongola ni kubwa sana.
Je, ni lini Serikali itakarabati visima vilivyochimbwa na UNHCR ili viweze kutatua tatizo la maji katika vijiji hivyo?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza awamu ya pili ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji nchini kote. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.302 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji vijijini inayohusisha ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji. Kupitia fedha hizo zilizotengwa Serikali itakarabati miradi mbalimbali ya maji katika Halmashauri ya Mpanda ikiwemo visima vilivyochimbwa na UNHCR vilivyopo katika Vijiji vya Mlimbasi, Mazwe, Mgamsamansi, Ilangu, Kapemba na Busongola.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa Halmashauri wa miaka mitano yaani kuanzia mwaka 2015 mpaka 2020 wa usambazaji wa maji safi na usafi wa mazingira, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda imepanga kufanya upembuzi yakinifu kwa miradi mikubwa ya usambazaji maji katika kijiji cha Busongola. Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati na kujenga miradi ya maji nchini kulingana na upatikanaji wa fedha ili iweze kutatua kero ya upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Wakulima wa Vijiji vya Vikonge, Bugwe, Majalila na Kupanga wako tayari kulima kilimo cha pamba katika Wilaya ya Tanganyika, tatizo lililopo ni Serikali kutoa kibali cha idhini ya kulima kilimo hicho.
Je, ni lini Serikali itatoa kibali hicho ili wananchi waanze shughuli za kilimo cha pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba niwatakie Waislamu wote nchini Ramadhan Kareem. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iliweka marufuku ya kilimo cha pamba katika badhi ya maeneo ikiwemo Mkoa wa Katavi ili kuzuia kuenea kwa mdudu anayeitwa funza mwekundu. Zuio hilo ni mojawapo ya utekelezaji wa makubaliano ya kimataifa ya kuzuia kuenea kwa wadudu ambao hawako kwenye maeneo mapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali ilipokea taarifa iliyotolewa na Mheshimiwa Kakoso kuhusu uwepo wa wakulima wa pamba katika Wilaya ya Tanganyika. Kutokana na taarifa hiyo, timu ya wataalam kutoka Chuo cha Utafiti cha Ilonga na Bodi ya Pamba ilitumwa kwenda Wilayani Tanganyika na Mpanda ili kupata uthibitisho kuhusu uwepo wa wakulima wa pamba na kufanya tathimini ya mwenendo wa funza mwekundu katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa iliyoandaliwa na wataalam hao imeainishwa kwamba mdudu huyo hayupo katika maeneo ya Mkoa wa Katavi yanayokaliwa na watu. Aidha, taarifa ilibainisha kwamba Wilaya za Tanganyika na Mpanda hazipatikani na eneo lenye zuio na kupendekeza Wilaya hiyo na Wilaya zote hizo ziruhusiwe kulima pamba.
Kutokana na taarifa hiyo, Serikali kwa msimu wa mwaka 2017/2018 imetoa kibali cha kuruhusu zao la pamba lizalishwe katika Wilaya ya Tanganyika na Wilaya ya Mpanda Mkoani Katavi na uzalishaji umeanza katika Wilaya hiyo. Ahsante. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Wilaya ya Tanganyika haina Mahakama ya Wilaya.

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya sanjari na kuboresha Mahakama za Mwanzo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiswa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Wilaya ya Tanganyika iliyo katika Mkoa wa Katavi haina jengo la Mahakama ya Wilaya, wananchi wa Wilaya ya Tanganyika wanategemea huduma ya mahakama ya Wilaya ya Mpanda ambayo ni jirani.

Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa maboresho ya miundombinu wa mahakama katika mikoa yote nchini kwa sasa ujenzi wa Mahakama ya Mkoa wa Katavi na Wilaya ya Mpanda unaendelea. Vilevile Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika ipo kwenye mpango wa ujenzi wa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo ujenzi huo utaenda sanjari na ukarabati wa Mahakama za Mwanzo kuendana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y. MHE. MOSHI S. KAKOSO) aliuliza:-

Vijijini vya Kapanga, Katuma, Simbwesa, Kasekese, Kungwi na Kabage havina mawasiliano ya simu:-

Je, ni lini Serikali itapeleka huduma ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Vijiji vya Kapanga, Katuma Mpembe na Simbwesa vilipatiwa huduma ya mawasiliano mwaka 2016. Mradi huu ulitekelezwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Simu ya Vodacom kwa ufadhili wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote. Vijiji vya Kasekese, Kungwa na Kabage vya Kata ya Sibwesa vilifikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia mradi wa Halotel wa kufikisha huduma ya mawasiliano katika vijiji 4,000 nchini mwezi Septemba, 2018. Hata hivyo, baada ya kukamilika vifaa vya mawasiliano vilivyofungwa vilipata tatizo la kiufundi na kupelekea wananchi wa vijiji hivyo kutopata huduma ya mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, vifaa vya mawasiliano vilivyopata matatizo vimeshaagizwa na vinategemewa kuwasili hivi karibuni na vitafungwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2019 ili wananchi wapate huduma ya mawasiliano itakayowasaidia kujiletea maendeleo.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-

Mradi wa umwagiliaji wa Karema ni wa muda mrefu toka umeanza:-

Je, ni lini mradi huo utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, kama ifuayavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2009/2010 na mwaka 2011/2012 kupitia Mpango wa DADP Mradi wa Umwagiliaji wa Karema ulipatiwa fedha kiasi cha shilingi milioni 742,485,000 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo fedha hizo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa banio, uchimbaji wa mifereji miwili yenye jumla ya urefu wa kilometa nne, ambapo mfereji namba moja ulichimbwa urefu wa mita 3,800 na mfereji namba mbili ulichimbwa mita 200, ujenzi wa tuta la kuzuia maji ya mafuriko lenye urefu wa mita 280, ujenzi wa Ofisi ya Kamati ya Umwagiliaji ya Mradi, ujenzi wa madaraja matatu ya kuvuka kwa miguu (Foot Bridges), ujenzi wa vivusha maji chini ya ardhi viwili, ujenzi wa mifereji katika mfereji namba mbili kwa mita 25 na ujenzi wa kivusha maji kwa juu chenye urefu wa mita 27.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ujenzi huo bado zilihitajika fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mradi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bwawa, ujenzi wa banio la pili, kusakafia mfereji mkuu, kuchimba mifereji ya matoleo ya maji, kuchimba na kujenga mifereji ya mshambani, ujenzi wa vigawa maji vya mashambani na kujenga barabara za mashambani. Aidha, ujenzi huo ulisimama kutokana na kumalizika kwa programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya kwanza (ASDP I) iliyotekeleza mradi huo kupitia mipango ya maendeleo kilimo ya wilaya (DADPS) mwaka 2013/2014.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kumalizika kwa SDP I Serikali imefanya tathmini ya utekelezaji wa programu hiyo, ili kubaini ufanisi na changamoto kabla ya kuanza ujenzi wa miradi iliyobaki. Aidha, mradi huo utatekelezwa kupitia bajeti ya Serikali pamoja na ushirikiano wa wadau wa maendeleo na sekta binafsi katika mwaka 2020/2021 kupitia programu ya kuendeleza sekta ya kilimo Awamu ya II (ASDP
II) iliyoanza kutekelezwa tangu mwaka 2018/2019.
MHE. ANNA R. LUPEMBE (K.n.y. MHE. MOSHI S. KAKOSO) aliuliza:-

Wilaya ya Tanganyika haina Jengo la Polisi Makao Makuu ya Wilaya.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi eneo la Makao Makuu ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa Wilaya mpya zilizoanzishwa na Serikali katika miaka ya hivi karibuni ambazo hazina vituo vya polisi na hata nyumba za kuishi askari.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua hitaji la Kituo cha Polisi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Tanganyika na mpango wa kujenga Vituo vya Polisi katika Makao Makuu ya Wilaya yataanza mara baada ya kufanyika kwa tathmini ya eneo husika.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI K.n.y. MOSHI S. KAKOSO Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya shilingi milioni 400 aliyoahidi Waziri Mkuu kuchangia katika ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kasekese kinachojengwa na wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga na kukarabati vituo vya kutolea huduma za afya kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuboresha utoaji wa huduma za afya ya msingi kwa wananchi ikiwemo upatikanaji wa huduma za upasuaji. Ujenzi na ukarabati huo unahusisha pia utekelezaji wa ahadi za Viongozi Wakuu wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya Serikali kuchangia shilingi milioni 400 ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kasekese imetekelezwa, ambapo fedha hizo zimepelekwa kwenye Kata ya Kasekese tarehe 25/8/2021 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo hicho.

Mheshimiwa Spika, majengo manne yanatarajiwa kujengwa, ambayo ni jengo la wodi ya wazazi, jengo la upasuaji, jengo la kufulia nguo na nyumba ya mtumishi. Aidha, ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje la Kituo cha Afya Kasekese umekamilika kwa gharama ya shilingi 164.9 kupitia fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri. Ahsante sana.