Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Amber. Mbarouk Nassor Mbarouk (12 total)

MHE. ALI JUMA MOHAMED: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri nilikuwa na swali moja tu la nyongeza.

Serikali ina mpango gani wa kutafuta fursa mbalimbali za ajira ambazo ziko katika nchi mbalimbali duniani, kwa ajili ya Watanzania hususan nchi ya Qatar ambayo mwakani ni wenyeji wa Kombe la Dunia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuchangamkia fursa kwa ajili ya Watanzania kwenda kufanya kazi nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, pili, napenda kukufahamisha kuwa Serikali imeanza mazungumzo na nchi mbalimbali ambazo zina fursa ya ajira hizo, hasa zikiwemo nchi za Ghuba, ili kuwa na utaratibu maalum wa kutoa quarter maalum kwa ajili ya Tanzania. Ninapenda kutoa taarifa pia kwamba tayari Tanzania imesaini mkataba na nchi ya Qatar kwa ajili ya kuwa na quarter maalum ya watanzania kwenda kufanya kazi huko, hasa katika kipindi hiki ambako tunaelekea kwenye mashindano ya World Cup ambayo yanaanza Novemba mwakani 2022. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Kwa kuwa imethibitika kwamba Wilaya ambazo ziko mpakani zinanufaika sana kupitia biashara na majirani zao wa nje, na kwa kuwa katika Wilaya ya Nyasa, kwanza kuna uasilia wa kindugu lakini vilevile kuna changamoto kubwa za kukuza biashara na Malawi ingekuwa ni mkombozi mkubwa.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameonesha kuwa na uwezo mkubwa wa kidiplomasia kwa jinsi ambavyo amenijibu swali langu, namshukuru sana, je, Waziri una mpango gani wa kwenda kuongeza nguvu ya kupeleka ushawishi katika nchi ya Malawi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa…

SPIKA: Ushawishi wa nini?

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ushawishi wa kuhakikisha kwamba suala hilo ambalo tumelizungumzia la kibiashara linafanyika kwa kutumia meli na nyenzo nyingine.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ninapenda pia kumualika Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri kuja Wilaya ya Nyasa ili kuwafahamu wananchi wa kule na shughuli wanazozifanya na kuona namna bora zaidi ya kukamilisha kushughulikia suala hili la kibiashara. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki itafanya kila jitihada kwa kushirikiana na mamlaka husika nchini Malawi ili kuwezesha meli ya MV Mbeya II ianze safari zake kati ya Malawi na Tanzania pale taratibu zote zitakapokamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili ambao ni mwaliko, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba nitakuwa tayari, kwa idhini yako, kufanya safari hiyo ili kuona fursa mbalimbali ambazo ziko katika Wilaya ya Nyasa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FRANCIS L. MTEGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na zaidi nimshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Hata hivyo, nina swali la nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakulima wale mpaka sasa hivi tunavyoongea, bado mazao ya mahindi na mpunga ni mengi sana na kwa kuwa, wanaelekea msimu mpya wa kilimo na bei ya mbolea iko juu na wengine wanashindwa kufanya marejesho ya benki.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana nami kwamba muda umefika sasa wa kuunda task force maalum ya Waheshimiwa Mawaziri. Pengine ikijumuisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wa Kamati za sekta husika, ili waende mahsusi kutafuta masoko kabla ya msimu mpya wa kilimo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA
AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyofuatilia upatikanaji wa masoko ya bidhaa ikiwemo mchele, na mahindi. Lakini pia, ninakubaliana na wazo la Mheshimiwa Mbunge kwa kuunda hiyo task maalum kwa ajili ya kutafuta hayo masoko. Lakini pia ninaomba kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, juhudi nyingi sana hivi sasa zinachukuliwa na Serikali katika kutafuta masoko ya bidhaa hizo. Hivi sasa ninavyosema kuna timu ya Wizara ya Kilimo ambayo iko nchini Comoro, mahsusi kwa kutafuta soko la bidhaa ya mchele na mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni juzi tu, timu hiyo ilitoka South Sudan kwa nia hiyo hiyo ya kutafuta soko la mahindi na mpunga na mwisho ninapenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, TANTRADE wana utaratibu maalum wa kuwasiliana na Balozi zetu ambazo ziko nje mahsusi kwa ajili ya kutafuta soko kwa bidhaa za Tanzania ikiwemo za mpunga na mahindi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali.

Kwa kuwa tatizo la masoko liko pia katika mazao mbalimbali nchini na kwa kuwa sasa hivi, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuweka kitengo cha kutafuta masoko katika Balozi zetu, ili kiweze kushughulikia tatizo la masoko katika mazao mbalimbali nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ritta Kabati kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa tayari Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeunda Idara maalum ya Economic Diplomacy, kwa ajili mahsusi ya kutafuta masoko ya bidhaa zetu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulizie maswali mawili.

Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake lakini pia niwapongeza Watanzania kwa michango mizuri ambayo wamechangia nchi yetu wanaoishi nje ya nchi. Kwa kuwa Diaspora wakirudi nchini huwa wanachukuliwa kama wageni kwenye nchi yao.

Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutoa hadhi maalum kwa Diaspora kushiriki ujenzi katika uchumi na uwekezaji kabla hatujaweza kupewa uraia pacha?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; je, watanzania wanaoishi nje ya nchi wanapopata matatizo kwa mfano kesi, wamekuwa wakipatiwa msaada gani ukiwepo msaada wa kisheria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge ambaye ni mdau mkubwa sana wa diaspora kwa namna anavyowasemea na kuhakikisha fursa nyingi kwa wana diaspora. Wizara yetu kwa kushirikiana na taasisi za Serikali zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar na kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi wanaoshughulika na mambo ya Diaspora tayari imeanza kufanya tafiti ili kupitia sera, sheria na taratibu za nchi kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa watanzania wanaoishi nje kupata hadhi maalum.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la pili la msaada wa kisheria wakati wanapopatwa na matatizo kama vile kesi ni kwamba Serikali kupitia balozi zetu zimekuwa zikiwasaidia watanzania wanapopatwa na kesi nje ya nchi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuwatafutia mawakili mabobezi na waaminifu kwa gharama zao; pili, pale kesi inapokuwa katika Mahakama ubalozi umekuwa ukifuatilia kwa karibu sana kesi hizo ili kuona watanzania hawa wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi husika.

Mheshimiwa Spika, mwisho pale wanapomaliza vifungo vyao au wanapopata msamaha ubalozi unafanya uratibu wa kuhakikisha kwamba wanarudi nyumbani salama, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kimsingi suala la uraia pacha na Diasporas limefanyiwa mjadala mpana sana kwa muda mrefu sana. Sasa kwa sababu Serikali na niipongeze kwa kufanya jitihada ya kutambua mchango wa Diasporas na tunaamini kwamba wakifungua wakipewa hati maalum ama uraia pacha pamoja na kwamba kuna restriction ya katiba hawaoni sana ifike hatua lifike tamati suala la kujadili masuala la uraia pacha na Diaspora tulifanyie kazi sasa kwa sababu tumeona impact yake ni kubwa zaidi kwa sababu Serikali yenyewe ndiyo imetuambia sasa hiyo ni ndogo tu tukifungua tutapata faida nyingi Zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali haioni kama imefika hatua tulifanye sasa kwa vitendo suala la kutambua kuwapa hadhi maalum ama kutambua mchango wa Diaspora kiuhalali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nusrat Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa watanzania wanaoishi nje ya Nchi na kama nilivyojibu hapo awali ni kwamba tayari saa hivi Serikali inafanya tafiti ya kuangalia vipi tunaweza tukaangalia uwezekano wa watanzania hawa kupewa hadhi maalum. Hivyo namuomba Mheshimiwa Mbunge atupe muda kidogo ili kumaliza tafiti na taratibu hizo ahsante sana.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na nichukue nafasi hii kuipongeza Sarikali kwamba imefuata usauri wa wabunge na ushari wa kamati na pia kama Mbunge ni jambo ambalo nimekuwa nikilisema toka mwaka 2016 na hatimae Ubalozi mdogo umefunguliwa katika Jiji la Lubumbashi, kwa hivyo itarahisisha sana utendaji wa kazi na biashara kati ya nchi yetu na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ninaswali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa kwa upande wa Ziwa Tanganyika upande ule wa Kalema tayari Serikali yetu imeshaanza ujenzi wa bandari na inaendelea vizuri, lakini upande wa pili ambao kuna kama mwalo wa moba ambao sio bandari hasa haujawa katika mazingira ambao yanaweza ku-facilitate meli na hivyo sisi kufanya biashara.

Je, Serikali iko tayari kukutana na Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kupitia tume ya pamoja na hivyo kushirikiana na kuangalia uwezekano wa kuona namna gani watashirikiana katika jambo zima la kujenga miundombinu, ili biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iweze kushamiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuimarisha barabara sehemu ya pili ya DRC, na kwa hali hiyo tayari saa hizi mazungumzo yameshaanza kati ya DRC na Tanzania na mazungumzo hayo yataendelezwa pia katika Mkutano wa Pamoja wa Ushirikiano (JPC) ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Mei na maandalizi wa mkutano huo unategemewa kuanza mwezi wa Aprili. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NG’WASI D. KAMANI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Hivi karibuni nchi jirani ya wenzetu imeingia makubaliano na nchi za uingereza za kupeleka wataalam wa afya vijana kwa ajili ya kufanya kazi kule. Majibu ya Serikali ni mazuri, lakini matokeo yake hayaridhishi. Ni lini hasa Serikali itaona haja ya kuja na mikakati mbadala ya kuhakikisha inatumia Balozi zetu tulizonazo katika nchi zaidi ya 25 na Balozi Ndogo kwenye nchi zaidi ya 15 kuhakikisha inaongeza mawanda ya vijana kupata ajira? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Mheshimiwa Rais wa nchi yetu, Mama Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya juhudi kubwa sana za kuhakikisha anapanua mawanda ya mahusiano ya Kimataifa kwa nchi yetu katika nchi za Kimataifa, lakini takwimu zinaonesha kwamba, vijana wachache sana wanapata nafasi za ajira kwenye nchi jirani. Serikali je, inalitambua hili? Na kama inalitambua ni lini hasa itaanza kuchukua hatua ili kuhakikisha juhudi za Mheshimiwa Rais zinapata tija ya ajira kwa vijana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ng’wasi Damas Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna haja ya Serikali yetu kuongeza juhudi katika kuhakikisha kwamba, vijana wetu wanapata fursa za ajira nje ya nchi. Miongoni mwa mbinu hizo ni kuhakikisha kwamba, tunaingia mikataba na nchi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba, fursa zilizopo huko zinapatikana.

Mheshimiwa Spika, mfano hivi sasa tayari tumeshaingia mkataba na nchi ya Qatar mwezi uliopita tu ujumbe mkubwa wa Tanzania ulikwenda Doha mahsusi kwa ajili ya kufuatilia mkataba huo. Katika makubaliano yao tayari nchi ya Qatar imekubali kufungua Visa Centre hapa Tanzania maalum kwa ajili ya vijana wa Tanzania kwenda kufanya kazi Qatar. Pia tumeanza mazungumzo na nchi za Falme za Kiarabu na Oman na Saudi Arabia kwa ajili ya kuingia nao mkataba. Hii mikataba ni muhimu sana kwa sababu ndiyo inayotupa uhakika wa kupata hizo ajira.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba, Serikali imeona kuna umuhimu mkubwa sana wa vijana wetu kupata ujuzi kabla ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi. Hivyo basi, kupitia TAESA ambao ni wakala maalum wa taasisi ya ajira hapa Tanzania, imeanzisha kanzi data na ina portal maalum ili vijana waweze kujiandikisha mara zinapotokea fursa za ajira waweze kuajiriwa.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa tayari portal hiyo ina vijana wanaofika 40,000 na umuhimu wake ni kwamba, hao vijana kabla ya kwenda kufanya kazi nje ya nchi huwa wanapewa mafunzo maalum ili kuhakikisha kwamba, wanapokwenda huko nje hawaharibu katika kazi ambazo wamepelekewa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu hayo naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

(a) Je, wanafunzi wanaosoma Chuo cha Diplomasia wanafanya wapi mafunzo kwa vitendo ili sasa lengo la kuanzisha Chuo cha Diplomasia liwe limetimia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Serikali imekubali kwamba yaliyokuwa malengo ya msingi kuanzia Chuo cha Diplomasia kwa sasa yamebadilika kutokana na mahitaji ya nchi na pia kutokana na masuala mengine ambayo Serikali wanajua kwanini walipadilisha.

(b) Je, ni kwanini sasa Serikali isione haja ya kupitia upya mfumo wa utoaji elimu kwenye chuo hiki ambacho lengo lake lilikuwa ni kutoa viongozi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwasababu hata wanaotolewa katika chuo hiki wahitimu wengi hawatumiwi kama ambavyo lengo la kuanzisha chuo hicho lilivyokuwa. Sasa ni kwanini wasipitie upya ili wanaohitimu katika chuo hicho wawe na tija kwa taifa na Serikali ifikie malengo yake inayosema kwamba inazalisha viongozi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kuhusu mafunzo kwa vitendo. Chuo hiki kimsingi kinapowatoa wale wanafunzi wanakwenda kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya field zao, moja ya eneo ambalo wanapewa nafasi ni Wizara ya Mambo ya Nje yenyewe ambako wanafunzi wachache huwa wanapewa nafasi kutokana na ukweli wa uwezo wa Wizara yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maeneo mengine ni kwenye taasisi mbalimbali zenye sura ya Kimataifa, vile vile kule kwenye NGO na maeneo ambayo utendaji wake upo katika sura ya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la tija, ni kwamba chuo hiki kina tija kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba kwa sasa kimezalisha wanadiplomasia wengi sana ambao wanatumika katika maeneo mbalimbali. Na ukizingatia kwamba tuna hiki chuo kiliboreshwa na kufanyiwa maboresho ya uhakika kimekuwa na sura ya chuo kikuu, na sasa hivi kinatoa hadi shahada ya juu, kama nilivyoieleza hapo, wanatoa hadi masters pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachoweza kusema ni kwamba mafunzo wka vitendo wanapatiwa lakini vile vile tija inaonekana kwenye Nyanja za kimataifa na wasomi wengi sana tumekuwa tukiwatumia katika maeneo mbalimbali, ahsante.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Balozi nyingi nje ya nchi hazifanyi vizuri kwa ufanisi katika kutangaza fursa za nchi yetu vivutio pamoja na utalii. Nini mkakati madhubuti wa Serikali kuhakikisha Balozi hizi zinafanya vizuri?

Swali la pili, kwa kuwa balozi zetu nyingi nje ya nchi hazina watumishi wa kutosha hasa balozi za kimkakati kama Congo na kwingineko, ni lini Serikali itapeleka watumishi wa kutosha ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kama nilivyoelezea katika swali la msingi, kwamba utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ni kipaumbele muhimu cha Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ili kuhakikisha kwamba sera hiyo inatekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati ambayo inafanya kwanza ni Wizara ni kukiimarisha Kitengo chetu cha Mawasiliano ya Serikali ili kuhakikisha kwamba kinatoa taarifa zote muhimu kwa wadau kuhusu fursa zinazopatikana nje ya nchi na pia fursa ambazo zipo katika nchi yetu na hiyo imefanyika kwa ufanisi sana kwa sababu mfano Ubalozi wetu wa China ni ushahidi kwamba kitengo chetu kinafanya kazi vizuri kwa sababu ni taarifa nyingi ambazo Ubalozi wetu wa China zinapatikana kule na pia Serikali hapa na wananchi kwa ujumla wanapata taarifa nyingi za Ubalozi wetu na China na Balozi nyingine pia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la watumishi, ni kweli kwamba ninaungana na Mheshimiwa Mbunge kwamba hapo nyuma kidogo hilo tatizo la ukosefu wa wafanyakazi lilikuwepo na lilikuwa ni kubwa, hata hivyo kwa hivi sasa tayari Serikali imechukua juhudi maalum za kuhakikisha kwamba suala hili halipo. Mfano, katika mwaka uliosha wa 2021/2022 jumla ya wafanyakazi 140 walipelekwa kwenye Balozi zetu mbalimbali nje ya nchi na suala hili ni endelevu, na tayari hivi sasa Wizara yetu imepata kibali cha kuajiri Maafisa wengi tu ambao watakuwepo Makao Makuu kwa ajili baadaye miaka ya mbele huko waweze kwenda kutumikia katika Balozi zetu.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, ikiwa Jumuiya hizi zinapoanzishwa kila Jumuiya inakuwa na lengo lake. Mfano, SADC ukisoma malengo yake ilianzishwa kwa ajili ya siasa na usalama zaidi wa nchi zetu. Ikiwa kama COMESA ilianzishwa kwa ajili ya kuwepo kwa soko la pamoja na katika majibu ya msingi kwenye swali inasema kwamba kuwepo kwa tripartite arrangement kunachangia kuondoa changamoto hizi.

Je, mbona bado wafanyabiashara wetu wanapotaka kuyaendea masoko ya hizo nchi ambao ni wanachama na ambao sisi siyo wanachama, wanaendelea kupitia changamoto. Mfano, wafanyabiashara wa Tanzania wanapotaka kuliendea soko la Congo wanakutana na changamoto nyingi lakini hata mazao yanapokuwa yanauzwa kwenye nchi mfano Misri, tunapata tozo kubwa ya ushuru wa bidhaa zaidi ya 30%.

Swali la pili, je, Serikali haioni sasa ipo haja kwa umuhimu kabisa kwamba toka tujitoe kwenye COMESA mwaka 2000 na sasa hivi ni miaka 13, Serikali inaonaje iende kufanya utafiti kukaa na wafanyabiashara ambao wanafanya biashara kwenye nchi hizi wanachama, zituletee zipi faida ambazo sisi tulipata kutoka kwenye COMESA na zipi hasara ambazo nchi imepata katika kipindi cha miaka 13 kujitoa kwenye COMESA? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwani amekuwa mfuatiliaji mkubwa sana katika masuala ya biashara hasa baina ya sehemu anakotoka huko Momba na soko la DRC. Nianze kwanza na swali la pili alilosema kuhusu utafiti, tuangalie utafiti au tufanye utafiti na tuone kama tumeathirika au hatujaathirika na Tanzania kujitoa katika COMESA.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla ya Tanzania kujitoa COMESA, ilifanya utafiti mkubwa sana na kujiridhisha kwamba hakuna hasara yoyote na hakuna athari yoyote ya Tanzania kujitoa COMESA.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusiana na changamoto ambazo zipo hasa katika soko la Congo. Changamoto hizi hazitokani kabisa na Tanzania kujitoa COMESA. Changamoto na vikwazo vya kibiashara ambavyo siyo vya kiforodha zimekuwepo katika nchi mbalimbali na kila zinapojitokeza basi hushughulikiwa kwa kadri inavyowezekana.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana specific na suala la Congo -DRC ni kwamba, Tanzania imechukua hatua nyingi sana za kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wetu hawapati vikwazo wanapofanya biashara nchini Congo. Hatua hizo ni kwanza kuhakikisha JPC ambayo ni uhusiano wa kibiashara kati ya DRC na Tanzania na ni mwezi Septemba tu last year JPC ilikutana na ilizungumzia masuala mbalimbali ya kukuza biashara. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri aliyoyatoa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali ina mkakati gani wa kutoa elimu ya diplomasia ya uchumi kwa wananchi ambao ndiyo wadau wakubwa wa dhana hii ikilinganishwa na sasa inafahamika Kitaifa zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; tumeona vyombo vingi vya habari na waandishi wa habari wakiwa nje ya nchi wakiripoti matukio hasi tofauti na fursa zilizoko Tanzania na zinazopatikana nje.

Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha waandishi wa habari walioko nje ya nchi wanatangaza nchi yetu na fursa zilizopo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza katika kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ambayo imeweka msisitizo zaidi katika dhana ya diplomasia ya uchumi, Wizara imeendelea kutoa elimu kwa wananchi katika kuelezea fursa mbalimbali zinazopatikana nje ya nchi kupitia makongamano na vyombo vya habari, lakini pia na mitandao ya kijamii. Pia katika maonesho mbalimbali Wizara imekuwa ikitoa hiyo elimu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, Wizara yetu au Serikali inachukua mkakati gani kwa ujumla kwa waandishi wa habari ambao wanapotosha hizi habari nje ya nchi. Kwanza ni kwamba balozi zetu zimekuwa very active mara zinapotokea taarifa hasi, basi mara moja wanashirikiana na vyombo vya habari vya nje katika kuhakikisha kwamba habari zinazotolewa ni za uhakika, ahsante sana.

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri sana aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba tu niongezee kidogo kwamba kuhusu mkakati wa kutoa elimu ya diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu jana wakati Kamati yetu ikitoa taarifa na kama ilivyoelekezwa pia na Kamati, tulieleza kwamba tunaandaa mpango mkakati wa kitaifa wa kutekeleza diplomasia ya uchumi na katika mpango huo, moja ya kitu kitakachojumuishwa ni mpango wa kutoa elimu kwa umma. Kwa hiyo, tutatumia mbinu mbalimbali kuboresha utoaji wa elimu ya umma pamoja na yale tunayoyafanya sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili ambalo ni kuhusu tunafanya nini kushirikisha hivi vyombo vinavyotoa elimu hasi kuhusu Tanzania. Tunalifahamu hilo pamoja na hayo yanayofanyika, tayari tumeanza mazungumzo na vile vyombo vya nje hususani vile vinavyoongea Kiswahili kwa sababu sasa hivi tunakuza pia Kiswahili kuwaomba pia wadau wetu.

Mheshimiwa Spika, juzi nimekutana na Idhaa ya Kiswahili ya Uturuki ambao wamefungua idhaa ya kiswahili na moja ya kitu nilichowaomba na mtaona ni kwamba sasa watusaidie kutoa elimu chanya na taarifa chanya kuhusu Taifa letu hususan vivutio tulivyonavyo, fursa tulizonazo na waachane na kutoa elimu hasi. Wao wamekubali kwamba watatusaidia kushirikiana na idhaa nyingine, ahsante. (Makofi)