Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Amber. Mbarouk Nassor Mbarouk (10 total)

MHE. ALI JUMA MOHAMED Aliuliza:-

Je, Serikali kupitia Balozi zetu ina mkakati gani wa kusimamia mikataba ya vijana wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ali Juma Mohamed, Mbunge wa Shaurimoyo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha Watanzania wanaopata fursa za ajira nje ya mipaka ya Tanzania wanafanya kazi katika mazingira mazuri na yanayolinda staha na utu wao. Katika kufanikisha azma hiyo Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa vibali vya ajira nje kupitia mamlaka zinazoshughulikia masuala ya ajira, ikiwemo Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) na Kamisheni ya Kazi Zanzibar kwa kushirikiana na Balozi za Tanzania nje.

Mheshimiwa Spika, utaratibu huo pamoja na mambo mengine unaelekeza kila mfanyakazi kuwa na wakala rasmi wa ajira, ambaye anatambuliwa na mamlaka tajwa ambao ndio waandaaji wa mikataba ya ajira nje inayopaswa kukidhi Sheria za Ajira za Tanzania na nchi anayokwenda kufanya kazi. Aidha, kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na Serikali mikataba hiyo pia inapaswa kuandaliwa kwa lugha inayoeleweka na vijana hao, ikiwemo Kiswahili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na Serikali kuweka utaratibu huo bado kumekuwa na changamoto zinazotokana na baadhi ya vijana wanaopata ajira nje kutozingatia utaratibu uliopo. Pia, baadhi ya vijana hao hawajitambulishi kwenye Ofisi za Balozi za Tanzania pindi wanapofika kwenye ajira zao Ughaibuni. Kutokana na hali hiyo Serikali kupitia Balozi zake imeweka mikakati ifuatayo:-

(i) kutambua Kampuni za Uwakala wa Ajira za Nje na kuzitaka ziwe na uhusiano wa kimkataba na Kampuni za Uwakala za Tanzania.

(ii) Kuendelea kutoa elimu kwa vijana wanaopata ajira nje kutoa taarifa zao na kuwasilisha nakala za mikataba yao ya ajira Balozini ili ziweze kuhakikiwa.

(iii) Serikali imeanza mchakato wa kuingia mikataba ya ajira na baadhi ya nchi ili kurasimisha upatikanaji wa ajira katika nchi hizo.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa rai kwa Watanzania ambao wana nia ya kufanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania, kufuata utaratibu uliowekwa na mamlaka husika. Kwa kuwa pamoja na mambo mengine inawapa kinga na kuepuka mazingira mabaya ya kazi ambayo hayatarajiwi na pia kurahisisha kupata msaada pale unapohitajika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha biashara kupitia Diplomasia ya Uchumi kati ya Tanzania na Malawi kwa kutumia meli ya MV Mbeya II?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, meli ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo ilizinduliwa rasmi na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 5 Januari, 2021. Meli hii kwa sasa inafanya safari kati ya Bandari za Tanzania tu za Kyela na Mbambabay.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Sera ya Diplomasia ya Uchumi ni miongoni mwa majukumu makubwa ya Wizara yangu. Kutokana na umuhimu mkubwa wa kukuza biashara kati ya Tanzania na Malawi na katika kuhakikisha kuwa meli ya MV Mbeya II inatumika ipasavyo, Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, ukishirikiana na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imeanza mawasiliano na Serikali ya Malawi na taasisi zake kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ya Malawi ili kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha MV Mbeya II kufanya safari zake nchini Malawi.

Mheshimiwa Spika, ubalozi wetu uliopo Lilongwe, Malawi pia unafuatilia kwa karibu kufikia makubaliano (MoU) baina ya Serikali ya Tanzania na Malawi kuhusiana na uanzishaji wa Ofisi za TPA mjini Lilongwe ambazi zitasimamia utekelezaji na uendeshaji wa shughuli zote za kibiashara zinazotumia huduma za bandari za Tanzania. Hii inatokana na maazimio ya Marais wa Tanzania na Malawi wakati wa ziara ya Mheshimiwa Rais wa Malawi nchini Tanzania iliyofanyika tarehe 7 - 8 Oktoba, 2020.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa taratibu hizo na kukamilika kwa kipindi cha majaribio ya meli hiyo na hivyo kuanza safari zake nchini Malawi, ni dhahiri kuwa biashara kati ya Tanzania na Malawi kwa kutumia Ziwa Nyasa itaimarika. Ahsante sana.
MHE. FRANCIS L. MTEGA aliuliza: -

Je, ni lini viongozi wa Kitaifa wataanza kutembelea nchi za nje mahsusi kwa ajili ya kutafuta masoko ya mazao hususan mpunga na mahindi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Francis Leonard Mtega, Mbunge wa Mbarali, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ziara za Viongozi wa Kitaifa nje zimekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi kati ya Tanzania na nchi rafiki. Kutokana na matunda yanayopatikana kupitia ziara za Viongozi wa Kitaifa, Wizara imeendelea kushauri Mamlaka kutembelea nchi za kimkakati kwa kuzingatia maslahi ya Tanzania katika nchi husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wetu wa Kitaifa tayari wamefanya ziara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na zile za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Ni katika muktadha huo, mwezi Mei, 2021, Wizara iliratibu ziara ya kikazi ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Kenya, ambapo pamoja na mambo mengine alifanikiwa kutanzua, vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiforodha (NTBs) vilivyokuwa vikiwakabili wafanyabiashara wakiwemo waliokuwa wakisafirisha mahindi kwenda Kenya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya ni miongoni mwa wanunuzi wakubwa zaidi wa mahindi ya Tanzania kutokana na sifa zake, ubora wake na bei yake nzuri. Hali kadhalika, Wizara pia iliratibu ziara ya Mheshimiwa Rais Samia nchini Burundi, Rwanda na Uganda, ambapo pamoja na mambo mengine, Mheshimiwa Rais alitumia fursa hiyo kutafuta pia masoko ya bidhaa za mazao kutoka Tanzania ikiwemo mahindi, mpunga na maharage. Aidha, katika ziara ya Burundi, Mheshimiwa Rais aliongozana na ujumbe wa wafanyabiashara ambapo kulifanyika kongamano la biashara kwa lengo la kukuza wigo wa biashara kati ya Tanzania na Burundi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITHA E. KABATI aliuliza: -

(a) Je Serikali inayo database ya kutambua idadi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi?

(b) Je nini mchango wa Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania katika kipindi cha miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitumia mifumo mbalimbali ya kutambua Watanzania wanaoishi nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na usajili wao kupitia Balozi zetu na Idara ya Uhamiaji kwa kutumia usajili wa hati za kusafiria za kielektroniki. Hadi kufikia Januari, 2021 idadi ya Watanzania wapatao Milioni moja na Laki Mbili (1,200,000) wanaishi nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu. Kwa mfano katika kipindi cha miaka mitano iliyopita michango yao imehusisha sekta mbali mbali zikiwemo; Sekta ya Fedha, Sekta ya Afya na Sekta ya Nyumba. Mfano, takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha fedha za kigeni (remittance) ambazo zimetumwa kupitia mfumo rasmi kutoka kwa Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ni takriban Dola za Kimarekani bilioni 2.3 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 5.3.

Mheshimiwa Spika, aidha, michango ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi katika Sekta ya Afya kwa kipindi cha miaka mitano inahusisha utoaji wa vifaa tiba, madawa, vitabu vya masuala mbalimbali ya afya na mafunzo ya elimu ya afya bora kwa wauguzi na madaktari kwenye hospitali za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Sekta ya Nyumba Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano wamenunua nyumba zaidi ya 135 zenye thamani ya shilingi za Tanzania bilioni 29.7 kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Ahsante sana.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza: -

Je, lini Serikali inafungua Ubalozi Mdogo katika Jiji la Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa hii ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili, baada ya Mheshimiwa Rais kuniamini kuendelea na nafasi ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kuchukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini. Nami namwahidi kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na uadilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tayari imefungua Konseli Kuu katika Jiji la Lubumbashi, Jimbo la Haut Katanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Ofisi za Konseli Kuu hiyo kwa sasa zipo katika Kiwanja namba 1174 Avenue Ruwe, Quartier, Makutano, Jijini Lubumbashi. Ninapenda kulijulisha Bunge lako Tukufu Kuwa Konseli Mkuu tayari amewasili Lubumbashi tarehe 7 Februari, 2022. Aidha watumishi wengine wanaendelea kuripoti katika Kituo hicho kwa awamu kulingana na mahitaji na taratibu za kidiplomasia, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NG’WASI D. KAMANI aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia Balozi zetu kuhakikisha Vijana wengi wa Kitanzania wanaajiriwa nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ng’wasi Damasi Kamani, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mkakati maalum wa kuhakikisha kuwa vijana wa Kitanzania wenye sifa zilizowekwa wanapata fursa za ajira nje ya nchi kama ifuatavyo: -

i) Balozi zetu nje ya nchi zimeendelea kutafuta fursa za ajira mbalimbali kwenye maeneo yao ya uwakilishi kwa kuingia mikataba ya ajira nje ya nchi inayowawezesha vijana wetu kupata ajira na kuwahakikishia usalama na maslahi yao katika ajira hizo.

ii) Serikali kupitia Kanzi Data ya Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) inawawezesha vijana na wataalam mbalimbali kujiandikisha ili kuwasadia kuomba nafasi za ajira pindi zinapopatikana nje ya nchi.

iii) Wizara inafuatilia nafasi za ajira ambazo hutangazwa katika Jumuiya za Kikanda na Kimataifa na kuziwasilisha katika mamlaka mbalimbali ili kusaidia kuwatambua vijana ambao wanazo sifa kutoka Serikalini na Sekta Binafsi na kuwashawishi kuomba nafasi hizo. Ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -

Je, ni yapi yalikuwa malengo ya Serikali kuanzisha Chuo cha Diplomasia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Diplomasia hapo awali kilikuwa ni chuo cha kimkakati ambacho kilianzishwa kwa ushirikiano kati Tanzania na Msumbiji kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali katika nyanja za kidiplomasia na uongozi katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutoka katika hizo nchi mbili. Kutokana na ubora cha chuo hiki Serikali ilifanya maboresho kwa kuongeza mitaala na kilianzisha kozi katika ngazi ya cheti, stashahada, shahada, stashahada ya uzamili na shahada ya uzamili ambazo zilianza kujumuisha wanafunzi kutoka nje ya mfumo wa watumishi wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa chuo kimezalisha wanadiplomasia wengi ambao wameweza kuajiliwa katika Serikali yetu, sekta binafsi pamoja na jumuiya za kikanda na kimataifa. Hivyo, chuo kimefikia lengo lake baada ya kufanyika kwa maboresho husika na kuweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taifa letu na wananchi kwa ujumla.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaajiri Maafisa Habari katika Balozi zetu ili kuutangaza nchi na vivutio mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Maofisa wanaopelekwa Ubalozini, moja ya majukumu yao ya msingi ni kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ambayo imeweka msisitizo katika kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Miongoni mwa majukumu ya kila Ofisa na kila Ubalozi ni pamoja na kutangaza vivutio vya utalii wetu, kubidhaisha Kiswahili, kuvutia wawekezaji na kutafuta fursa za masoko kwa bidhaa zetu. Aidha, Wizara ina utaratibu wa kuwajengea Watumishi uwezo kupitia mafunzo ili waweze kufanya kazi zaidi ya moja ikiwemo kuwa na uwezo wa kutoa habari muhimu kwa wadau.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. CONDESTER M. SICHALWE aliuliza: -

Je, Serikali haioni kuna haja ya nchi yetu kurudi COMESA?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Condester Michael Sichalwe, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 19 zilizokuwa mwanzilishi wa Jumuiya ya Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) mwaka 1994. Tanzania ilijitoa katika COMESA mwaka 2000 kwa sababu ilikuwa ni mwanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), ambapo baadhi ya nchi za jumuiya hizo pia ni wanachama wa COMESA.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kujitoa kwa Tanzania kulifikiwa baada ya kujiridhisha kuwa nchi haitaathirika kiuchumi, kwani bado ni mwanachama wa EAC na SADC na kuwa lengo ni kulipunguzia Taifa gharama hasa michango ya wanachama.

Mheshimiwa Spika, tutakumbuka kuwa, mwaka 2008 nchi za COMESA, EAC na SADC zilikubaliana kuanzisha Utatu. Hivyo Tanzania inaendelea kushirikiana na COMESA kupitia Utatu huu (COMESA – EAC - SADC Tripartate Arrangement). Aidha, mwezi Septemba, 2021, Bunge lako Tukufu liliridhia Mkataba wa kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA). Kuwa sehemu ya Utatu wa COMESA – EAC - SADC, na kuridhiwa kwa Mkataba wa AfCFTA kunaifanya Tanzania kuendelea kushirikiana na nchi za COMESA. Ahsante sana.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuainisha nchi ambazo fursa za biashara na uwekezaji zinaweza kuiletea nchi yetu mapato na kupandisha pato la Taifa zinapatikana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Njau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutekeleza dhana ya diplomasia ya uchumi ambayo pamoja na mambo mengine ni kukuza biashara na uwekezaji toka nchi mbalimbali. Dhana hii inahusisha Sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wizara za kisekta na Balozi zetu imeendelea kutangaza fursa za kibiashara na uwekezaji zenye manufaa kwa Taifa letu. Ili kuzitumia fursa hizi kwa tija zaidi, Wizara imeendelea na maandalizi ya Mpango wa Kitaifa wa kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Mpango huo utajumuisha sekta zote husika ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo muhimu ya kisekta yatakayochangia katika kukuza uchumi na Pato la Taifa. Mpango huu utajumuisha pia sekta binafsi na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Desemba, 2023.