Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Nusrat Shaaban Hanje (7 total)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa Naibu Waziri amekiri kwamba anatambua uhitaji wa kuweka life skills na soft skills kwenye elimu yetu Tanzania.

Je, Serikali iko tayari sasa kwa ajili ya kuendana na mabadiliko ya mfumo ya Sayansi na Teknolojia pamoja kizazi kipya kwa sababu generation inabadilika. Serikali sasa ipo tayari kulifanya, kuifanya topic ya soft skills ambayo inafundishwa kwenye somo la civic kwa form one topic ya kwanza form two topic ya kwanza na form three topic ya kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari sasa kufanya topic ya life skills iwe somo maalum sasa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inatengenezewa utaratibu mzuri wa upimaji wa uelewa na kuhakikisha kwamba vijana wanapata maarifa zaidi kuliko kusoma kwa ajili ya kujibu mtihani?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, je, lini sasa Serikali itaanza mchakato wa kushirikisha wadau wa elimu wakiwemo wanafunzi wenyewe na watu wa ku-develop mitaala ili kuhakikisha kwamba wanayoyasema yanatekelezwa kwa vitendo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nilivyoeleza katika jibu langu la msingi kwamba katika mwaka wa fedha 2021/2022 tunakwenda kufanya maboresho na mapitio ya mitaala kama nilivyozungumza hapo awali. Kwa hiyo, suala la kuingiza life skills, suala la kuhuisha mitaala ni suala ambalo lina mchakato mrefu ukiwemo na huo Mheshimiwa Mbunge aliouzungumza.

Kwa hiyo, tutahakikisha tunaenda ku-absolve au kuhusisha na mawazo hayo ambayo ulikuwa nayo maadam tayari hili lilishakuwa ni topic kwenye masomo naweza vilevile tukaifanya kama somo kwa kadri utafiti utakavyotuelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala kwamba ni lini, kama nilivyoeleza kwenye majibu ya msingi kwamba katika mwaka wa fedha 2021/2022 tutakwenda kuianza kazi hiyo kwa kadri itakavyowezekana. Ahsante.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyotoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika mwaka ujao wa fedha tutafanya mapitio ya mitaala. Lakini swali la nyongeza la pili la Mheshimiwa Nusrat alikuwa ameomba kwamba wadau washirikishwe. Nilikuwa nataka kumtoa hofu kwamba Serikali inapoandaa mitaala huwa inawashirikisha wadau na hata sasa hivi tutawashirikisha. (Makofi)

Kwa hiyo, nitumie Bunge lako Tukufu kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kama kuna mambo yoyote ambayo wanadhani yanapaswa kuingia katika mitaala yetu Wizara ya Elimu tupo tayari kupokea maoni yenu. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa kuna umuhimu sana katika barabara ya Singida – Supuka – Ndago ambayo kimsingi inapita katika Jimbo la Waziri wa Fedha pia.

Je, ni lini sasa Serikali itaichimba angalau kwa kiwango cha changarawe barabara hii ambayo zaidi ya miaka kumi haijafanyiwa marekebisho yoyote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge ameuliza barabara ya Supuka – Ndago ambako ni Jimbo la Iramba Magharibi ambapo anatokea Waziri wa Fedha wa sasa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba. Niseme tu kabisa kwamba barabara hiyo itajengwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na upatikanaji wa mbegu ya alizeti kwa wananchi wa Mkoa wa Singida naomba nimuulize swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, wananchi wa Mkoa wa Singida wamekuwa wakilima kwa utaratibu wa kawaida kabisa ule ambao wanalima wakimaliza wanaweka mbegu baada ya kuuza wanabakiza kidogo kwa ajili ya kwenda kulima tena mwakani ndio utaratibu wanaoutumia mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Naibu Waziri sasa yupo tayari kwa ajili ya kwenda kukutana na wakulima wa alizeti wa Mkoa wa Singida hususan jimbo la Singida Magharibi kwenye kata za Mwaru, Mgungia, Muhintiri, Minyukhe kwa ajili ya kwenda kuzungumza nao sasa kuona namna gani ambavyo ku-in cooperate mawazo yao na ya Wizara kwa ajili ya kuhakikisha kwamba upatikanaji wa mbegu ya alizeti, zinapatikana zenye tija ili walime kilimo ambacho sio cha desturi? Ahsante sana.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hanje kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwenda ku-visit tupo tayari na tutafanya hivyo na Mwenyezi Mungu akijaalia mwezi huu wa Juni tutakuwa na Mkutano mkubwa utakaoongozwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu katika Mkoa wa Sindiga kwa ajili ya suala la zao la alizeti na kukutana na wazalishaji na wakulima wa alizeti. (Makofi)
MHE. NUSRAT SH. HANJE: Mheshimiwa Spika ahsante, pamoja na majibu Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mkoa wa Singida ni mkoa muhimu sana pamoja na Mkoa wa Dodoma na Simiyu katika uchumi wa nchi, kwa sababu inatambulika kwamba Singida sasa hivi ni pilot kwenye zao la alizeti mahususi kwa ajili ya nchi, kwa hiyo pamoja na jibu lake kwamba mwaka 2022/2023 kwamba ndio ataweka kwenye mpango.

Je, Wizara haioni umuhimu wa kutafakari upya jambo hili kulinganisha na umuhimu wa Mkoa wa Singida kwa sasa kwenye bajeti ya mwaka huu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mkoa wa Singida kwenye miundombinu ya barabara bado kuna changamoto sana. Je, Wizara ina mpago gani wa kuhakikisha kwamba inaunganisha Mkoa wa Singida kwa barabara za lami ili kuhakikisha kwamba wakulima wa alizeti na vitunguu wanafikiwa mpaka kwenye vijiji vyao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante na naomba nijibu mswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge Nusrat kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nifanye marekebisho huu mwaka unasomeka 2021/2022; maana yake kuanzia Julai tathmini inafanyika tuweze kupata gharama ili tulipishe eneo la kipande cha reli ambacho kimetajwa.

Sehemu ya pili; Mheshimiwa Mbunge amesema kuunganisha barabara hizi za lami kwenye eneo lake Mkoa wake wa Singida, ni kweli kwamba tunao utaratibu mzuri wa kila Mkoa, kwa maana Meneja wa TANROADS Mkoa anapaswa kuratibu zoezi la barabara katika Mkoa wake husika. Sasa tupokee hoja yako kama kuna eneo ambalo halipitiki kabisa kwa sasa, nielekeze Meneja wa TANROADS wa Mkoa wa Singida afanyie kazi kama kuna sehemu ya kuchukua dharura tufanye hivyo ili kufanya maboresho kwa wakulima wa alizeti, vitunguu na maeneo mengine wapate huduma nzuri ya usafiri, ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri kuhusiana na hatua mbalimbali ambazo, tayari wameshaanza kuzichukua kwa kuona umuhimu wa kufanya mapitio ya mitaala yetu ya elimu.

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nikufahamu kwa sababu kimsingi wameshafanya makongamano kadhaa ya wadau na marafiki wa elimu kwa ajili ya kukusanya maoni. Lakini wamepitia elimu ya awali, msingi na sekondari kimsingi vyuo na vyuo vikuu bado. Kwa hiyo, niulize sasa Wizara ama Serikali ina mpango gani wa kutuletea pia kufanya mapitio ya kozi ambazo zinatolewa kwenye vyuo vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu, kuna maoni ya watanzania wametoa mbalimbali kuna masuala ya kilimo, kuna masuala ya ujasiriamali pamoja na stadi za kimaisha na mambo mengine mengi yote yamejadiliwa. Lakini vyuo na vyuo vikuu ambavyo ndio kimsingi vinatoa watu ambao ndio watenda kazi kwenye nchi. Ni lini sasa Serikali italeta kufanya marekebisho pia ya mtaala na masuala ya kozi ambazo zinatolewa kwenye vyuo hivyo. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nitoe ufafanuzi na kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Hanje. Utaratibu wa vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu wana taratibu zao za kuanzisha mitaala.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano katika vyuo vikuu seneti ndio chombo kikuu ambacho kina mamlaka ya kuangalia mitaala katika vyuo vikuu na vyuo vya kati vina nyanja tofauti, vyuo vya kilimo viko chini ya Wizara ya Kilimo, vyuo vya utalii viko chini ya Wizara ya Utalii, vyuo vya afya viko chini ya Wizara ya Afya na wote wana taratibu zao. Wizara husika ndio zinakuwa na mabaraza kwa mfano Wizara ya Afya, Baraza la Madaktari ndio linaangalia mitaala ya madaktari, Baraza la Wauguzi linaangalia mitaala ya manesi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kiasi fulani hili jambo labda nilipokee kama Serikali tuangalie namna ya kuliratibu. Kwa sababu, kwa sasa hivi sio vyuo vyote vya kati vinasimamiwa moja kwa moja na Wizara ya Elimu na wala Wizara haihusiki moja kwa moja na kuidhinisha mitaala. Ila imekasimisha mamlaka kwa seneti za vyuo vikuu pamoja na vyombo ambavyo vimewekwa, kwa mujibu wa sheria katika vyuo husika kushughulika na mitaala.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba tu tuangalie namna gani labda kwa kuongezea kabla sijamalizia. Ni kwamba nako pia tumeelekeza wafanye mapitio ya mitaala na katika huu Mradi wa Higher Education tuna fedha ambazo tumetenga, kwa ajili ya kufanya mapitio makubwa na ndio maana mradi unaitwa mageuzi ya kiuchumi na yanajikita katika kuimarisha uchumi wa viwanda. Kwa hiyo, mapitio ya mitaala yanafanyika kwa hiyo tutaangalia utaratibu mzuri wa kuratibu tupate mapitio yanayofanyika. Ili tuweze kuja kutoa taarifa kwenye chombo muhimu, ambacho ndio kinasimamia sheria na kusimamia utendaji wa shughuli za Serikali. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante kimsingi suala la uraia pacha na Diasporas limefanyiwa mjadala mpana sana kwa muda mrefu sana. Sasa kwa sababu Serikali na niipongeze kwa kufanya jitihada ya kutambua mchango wa Diasporas na tunaamini kwamba wakifungua wakipewa hati maalum ama uraia pacha pamoja na kwamba kuna restriction ya katiba hawaoni sana ifike hatua lifike tamati suala la kujadili masuala la uraia pacha na Diaspora tulifanyie kazi sasa kwa sababu tumeona impact yake ni kubwa zaidi kwa sababu Serikali yenyewe ndiyo imetuambia sasa hiyo ni ndogo tu tukifungua tutapata faida nyingi Zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali haioni kama imefika hatua tulifanye sasa kwa vitendo suala la kutambua kuwapa hadhi maalum ama kutambua mchango wa Diaspora kiuhalali? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nusrat Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa watanzania wanaoishi nje ya Nchi na kama nilivyojibu hapo awali ni kwamba tayari saa hivi Serikali inafanya tafiti ya kuangalia vipi tunaweza tukaangalia uwezekano wa watanzania hawa kupewa hadhi maalum. Hivyo namuomba Mheshimiwa Mbunge atupe muda kidogo ili kumaliza tafiti na taratibu hizo ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nitauliza maswali pamoja na majibu hayo, nitauliza maswali mawili ya nyongeza kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na kwamba amezungumiza suala la Kanuni za Magereza ambazo zinataka watoto watengwe tofauti na watu wazima wanapokuwepo Mahabusu. Mlundikano wa Mahabusu kwenye magereza zetu hauruhusu jambo hilo ni kwa nini sasa Serikali isiongeze au isipeleke Maafisa Ustawi wa Jamii ambao watakuwa wanashughulika na Watoto wanapokuwa kule kwa sababu ni vigumu sana ku-monitor. Kwa mfano, Gereza la Segerea kuna mahabusu si chini ya mia moja watoto na Maafisa wapo wawili tu ME na KE. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili; kwa nini sasa Serikali isipitie upya kujua idadi ya watoto ambao wana kesi kwenye Mahakama zetu na kwenye Mahabusu zetu yaani kwa maana ya Magereza ili sasa ile sheria kwa jinsi ilivyowekwa na ni nzuri, lakini utekelezaji wake ni mgumu ni kwa nini sasa wasipitie upya ili kuhakikisha kwamba watoto hawa wanasaidiwa kwa sababu hali za watoto wetu kwenye Magereza zetu ni mbaya mno. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje Mbunge wa Viti Maalum, nayo nayajibu kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa atarejea kwenye jibu langu la msingi atagundua kwamba kuna sehemu nimesema kutakuwa kuna Maafisa wa Ustawi ambao watakuwepo maalum katika magereza kwa ajili ya kusimamia haki na maslahi na kuwalinda watoto hawa. Kwa hiyo, kama changamoto ni Maafisa hawa kuwa kidogo basi nimhakikishie tutajitahidi Serikali kupitia Jeshi la Magereza ili kuona kwamba tunaongeza Maafisa hawa ili watoto wetu waweze kupata huduma nzuri za kuweza kusaidiwa na Maafisa hawa pamoja na kwamba kuna nafasi nyingine ya kushughulikiwa na wazee wao na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine Mheshimiwa amegusia suala la kwa nini isipitiwe upya sheria au tuone namna, nimwambie kwamba sheria hii kwamba ipo vizuri, lakini kwa kuwa na yeye ameshauri tuipitie upya basi tutakaa tutaipitia sheria hii ili kama kutakuwa kuna mapungufu basi tutajua namna ya kuifanyia marekebisho.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge pia aliuliza umuhimu wa kujua idadi ya kesi za watoto. Kesi zote zinazokwenda Mahakamani zinasajiliwa kwa namba, kwa hiyo kama atauliza swali mahsusi kwa Mahakama maalumu au kwa Gereza maalum idadi hiyo itapatikana kwa namba na kwa majina ya wahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili; Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 inaweka misingi ya kulinda maslahi ya mtoto. Kwa hiyo, kwa mtu aliyechini ya kizuizi cha magereza anapopelekwa mahakamani kama hapati huduma inayostahili akiwa magereza anayohaki ya kutoa hiyo hoja kwa Hakimu ambapo shauri hilo lipo mbele yake na maelezo ya kisheria kwenda kwa wanaosimamia hizo selo yakatolewa. Nninakushukuru. (Makofi)