Primary Questions from Hon. Nusrat Shaaban Hanje (8 total)
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kurekebisha mfumo wa elimu na kuingiza mbinu tete na stadi za maisha ili kuwajengea uwezo wa kiushindani vijana wanaohitimu na kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; kwa niaba ya Waziri Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwawezesha wanafunzi kupata stadi mbalimbali zikiwemo stadi za maisha na mbinu tete ili kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo suala la ajira na kiteknolojia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali itafanya mapitio ya mitaala ya shule za msingi na sekondari ili kuingiza stadi mbalimbali kama vile stadi za maisha hususan stadi za karne ya 21 na mbinu tete. Stadi za karne ya 21 ni pamoja na fikra tunduizi, ubunifu, ushirikiano, uongozi na stadi za teknolojia ya habari na mawasiliano. Stadi na mbinu hizi zitasaidia kuwajengea vijana uwezo wa kiushindani katika soko la ajira. Ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza:-
Je Serikali ina mpango gani wa kutumia mashamba ya uzalishaji wa mbegu bora hususani za alizeti ambayo ndio zao la uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mchango wa zao la alizeti katika kuongeza upatikanaji wa mafuta ya kula hapa nchini ambapo asilimia 68 ya mafuta ya kula yanatokana na zao hilo ikilinganishwa na mazao mengine ya yanayochangia asilimia 31.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuongeza upatikanaji wa mbegu bora za mafuta nchini kwa kutenga fedha jumla ya shilingi bilioni 40 katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya uzalishaji wa mbegu ya Wakala wa Mbegu wa Serikali ili kuzalishaji mbegu za alizeti na mazao mengine.
Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu hiyo kutawezesha kuongeza uzalishaji wa mbegu za alizeti kutoka tani 538 katika msimu wa 2019/2020 hadi kufikia tani 10,000 za mbegu bora za alizeti mwaka wa fedha 2019/2030 ambazo zitatosha kutumika katika eneo la hekta milioni 1.2 zinazoweza kuzalisha tani 500,000 za mafuta ya kula.
Mheshimiwa Spika, kwa kuthamini umuhimu wa zao la alizeti, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea kugundua na kuzalisha aina mpya ya mbegu bora za alizeti zenye sifa ya kutoa mavuno na mafuta mengi na zenye ukinzani dhidi ya magonjwa kutoka aina 1 hadi 17 za zao la alizeti katika msimu wa 2019/2020.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
(a) Je, kwa nini kipande cha reli ya kati kutoka Manyoni hadi Singida hakipo kwenye mpango wa ukarabati?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kukarabati kipande hicho cha reli ili kusaidia kuchochea ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC) inaendelea na mpango wa ukarabati wa mtandao wa reli iliyopo na kufufua njia za reli zilizofungwa kwa awamu kwa kuanzia na njia kuu (main line). Katika kutekeleza jukumu hilo, Serikali inazingatia Mpango wa Miaka Mitano wa Taifa ambao unaanzia 2021/ 2022 – 2025/2026. Aidha, Serikali itaendelea na ukarabati wa matawi ya reli ikiwemo kipande cha reli kutoka Manyoni hadi Singida kulingana na mahitaji ya ukuajiwa uchumi na uwezo wa kifedha. Lengo la Serikali ni kuboresha miundombinu ya reli ili kurahisisha huduma za uchukuzi nchini.
Mheshimiwa Spika, sehemu (b); Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo na miundombinu ya reli imara katika kuchochea uchumi wa nchi. Hata hivyo, kama nilivyoeleza katika jibu langu la msingi sehemu (a), Serikali itaendelea kufungua njia zote zilizokuwa zimefungwa ikiwa ni mkakati wake wa kurejesha huduma za usafiri wa reli wenye uhakika nchini na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia TRC imepanga kufanya tathmini kwa ajili ya ufunguaji wa njia zilizokuwa zimefungwa kwa lengo la kujua gharama za ukarabati. Maeneo ya reli yatakayohusika ni pamoja na Kilosa – Kidatu na Manyoni – Singida. Hivyo, naomba Mheshimiwa Mbunge aelewe kwamba Serikali inafanya kazi eneo la reli Manyoni – Singida, ahsante.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kutenganisha Mahabusu/Magereza ya Watoto na Watu wazima ili kuwalinda Watoto dhidi ya vitendo vya ukatili wa kingono vinavyoweza kujitokeza?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifutavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kulinda haki ya mtoto, Serikali ilitunga Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 ambayo inakataza kifungo kwa watoto na kuweka mahabusu magerezani na iwapo italazimu kuwekwa mahabusu sharti awe chini ya uangalizi wa Kamishna wa Ustawi wa Jamii au mahabusu za nyumbani au chini ya uangalizi wa taasisi yeyote itakayotamkwa katika amri ya Mahakama.
Mheshimiwa Spika, Kanuni za Kudumu za Jeshi la Magereza za Mwaka 2003 Toleo la 4, chini ya Kanuni 488 zimeweka utaratibu mzuri wa kuwatenga wafungwa na mahabusu katika sehemu maalum na vyumba maalum kwa kuzingatia umri ambapo wafungwa na mahabusu watoto hutengwa katika mabweni yao maalum pasipo kuchanganywa na wakubwa.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali inalo Gereza la Wami ambalo ni maalum kwa watoto ama vijana waliokatika ukinzani wa sheria na kuhukumiwa vifungo ambavyo huhamishiwa huko na kutumikia vifungo vyao wakiwa peke yao kama vijana bila ya kufungwa na watu wazima.
Mheshimiwa Spika, aidha Serikali inaendelea kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kingono na ukatili mwingine na kusimamia ipasavyo Sheria ya Watoto na Sheria zingine nchini zinazotoa ulinzi kwa watoto. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je, ni yapi yalikuwa malengo ya Serikali kuanzisha Chuo cha Diplomasia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Diplomasia hapo awali kilikuwa ni chuo cha kimkakati ambacho kilianzishwa kwa ushirikiano kati Tanzania na Msumbiji kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi mbalimbali katika nyanja za kidiplomasia na uongozi katika ngazi za kitaifa na kimataifa kutoka katika hizo nchi mbili. Kutokana na ubora cha chuo hiki Serikali ilifanya maboresho kwa kuongeza mitaala na kilianzisha kozi katika ngazi ya cheti, stashahada, shahada, stashahada ya uzamili na shahada ya uzamili ambazo zilianza kujumuisha wanafunzi kutoka nje ya mfumo wa watumishi wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa chuo kimezalisha wanadiplomasia wengi ambao wameweza kuajiliwa katika Serikali yetu, sekta binafsi pamoja na jumuiya za kikanda na kimataifa. Hivyo, chuo kimefikia lengo lake baada ya kufanyika kwa maboresho husika na kuweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taifa letu na wananchi kwa ujumla.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani kuiwezesha GST kufanya utafiti wa kisayansi na teknolojia kuhusu Critical Minerals ili kudhibiti mabadiliko ya hali ya hewa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Madini imeielekeza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kuandaa taarifa kuhusiana na madini mkakati (Strategic/Critical Minerals) hasa madini teknolojia ikiwemo madini muhimu kwa ajili ya nishati ya kijani (green energy minerals). GST imeanza kuandaa andiko kuhusiana na madini haya na kuainisha ni madini yapi ndiyo ya kimkakati kwa mtizamo wa dunia na nchi, matumizi ya madini hayo na mahala yanapopatikana.
Aidha, GST imebaini maeneo ya kufanya tafiti za jiofizikia katika maeneo sita (blocks) kwa nishati ya kijani (green energy) na matumizi ya magari ya umeme. Serikali inaendelea kutafuta wadau wa maendeleo ambao watashirikiana katika kufanya tafiti za jiosayansi. Ahsante sana.
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je? Serikali ina mkakati gani wa kuzuia ukatali wa kijinsia na utumikishwaji wa watoto katika makambi yanayotarajiwa kujengwa ili kuwezesha ujenzi wa Bomba la Mafuta Hoima Tanga?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nusrat Shaaban Hanje, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia na utumikishaji wa watoto vinakomeshwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mradi wa bomba la mafuta Hoima Tanga, kupitia MTAKUWWA Wizara yangu imejipanga kuimarisha na kuzijengea uwezo Kamati za Ulinzi na Usalama kwa watoto kwa vile Serikali itaendelea kutumia vyombo vya dola kuhakikisha wale wote wanaotumikisha watoto na kufanya vitendo vya ukatili wanachukuliwa hatua za kisheria. (Makofi)
MHE. NUSRAT S. HANJE aliuliza: -
Je ni lini Serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo vya Kati nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu Swali la Mheshiwa Nusrat Shaaban Hanje, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa elimu ya kati katika maendeleo ya nchi, Serikali imeendelea kugharamia uendeshaji wa vyuo vya kati kupitia ruzuku ambapo kwa mwaka 2022/2023, imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 41.47 kwa wanafunzi 2,435 waliopo katika vyuo vya kati wanaosoma fani za sayansi na ufundi. Aidha, Serikali inakamilisha taratibu za kuwezesha mikopo kutolewa kwa ajili ya elimu ya kati.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.