Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Minza Simon Mjika (4 total)

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu tuna machine ya X-Ray tuliletewa toka mwaka 2002. Swali langu ni hili, katika hospitali hiyo hatuna mtaalam wa X-Ray:-

Je, ni lini Serikali italeta mtaalam wa X-Ray katika Wilaya hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu wana mashine ya X-Ray ambayo kwa kipindi kirefu imekosa mtumishi kwa maana ya mtalaam wa X-Ray. Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeendelea kuwasiliana kwa karibu na Wizara ya Afya, lakini pia na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuona namna gani tunapata watumishi hawa ili tuweze kupata mtumishi mmoja na kumhamishia katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu. Wataalam hawa bado ni wachache lakini jitihada za Serikali ni kuendelea kuwasomesha ili tuweze kupata wataalam wengi ili waendane na kasi ya ujenzi wa vituo vya afya ambavyo kimsingi vitahitaji kupata watalaam hawa wa X-Ray.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshalifanyia kazi na tulishaainisha mtumishi kwa ajili ya kumpeleka Meatu na wakati wowote atakwenda kuanza kutoa huduma ya X-Ray katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru sana.

Kwa niaba ya wakazi wa Wilaya ya Meatu sasa napenda niulize kwamba ni lini sasa zoezi hili litaanza kwa sababu yapata wiki mbili hivi sasa hatujapata maji katika Wilaya ya Meatu na kuna vijiji ambavyo vinaukame sana kwa mfano Bukale, Mwambegwa na Chambara ni vijiji vingi sana hatuna maji kabisa leo yapata wiki mbili wakazi wa kule tunahangaika, tunapata taabu. Serikali ituambie sasa ni lini itatuletea maji huko kwetu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Minza Mjika kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama jibu langu la msingi nilivyosema mwezi Agosti, 2021 mradi huu unakwenda kuanzwa na suala hili ni jana tu jopo kamili la wizara liliweza kukaa na hawa wenzetu wa KfW na Mheshimiwa Waziri aliwahitaji watoe commitment yao namna ya kuweza kutekeleza mradi huu kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge nafahamu namna ambavyo unafuatilia suala hili ninakupongeza sana. Nikutoe hofu nitaongozana na wewe tutaenda kuhakikisha kwamba kila namna ambavyo ilikuwa imepangwa inakwenda kutekelezwa kwa wakati.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru sana kwa majibu ya Waziri, lakini sasa napenda nijue ni lini zoezi hili litaanza la ujenzi wa hiyo barabara? Naomba kupatiwa majibu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Minza Mjika kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika jibu langu la msingi nimeainisha kwamba tayari tumeshaanza ujenzi kwenye baadhi ya maeneo na katika bajeti tutakayoanza kuitekeleza ambayo Bunge lako limepitisha, tumetenga fedha, kwa hiyo, mara tu bajeti itakapoanza kutumika barabara hiyo itaanza kujengwa, ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, nina penda kushukuru sana kwa majibu mazuri ya Waziri. Lakini nina maswali mawili tu ya nyongeza. Katika Mkoa wa Simiyu kuna Wilaya tano lakini Wilaya ya Meatu ndio ina ukame sana kuliko Wilaya zote hizo tano. Nilipenda kujua ni lini sasa Serikali itachimba visima virefu vya maji na kusambaza katika vijiji hivyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana pamoja nami twende naye katika Wilaya ya Meatu aone wakina mama wanavyopata adha ya maji katika Wilaya ya Meatu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Minza Mjika kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nipende kupokea pongezi kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge. Lakini vile vile nipende kumpongeza na yeye, kwa kazi nzuri anayoifanya kwa ushirikiano mkubwa ndani ya Wizara ya Maji. Amekuwa mfuatiliaji mzuri sana akisaidiana na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo kaka yangu Simon wanafanya kazi nzuri kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali katika mwaka huu wa fedha 2021/2022 ni kuchimba visima virefu katika Wilaya ya Meatu. Tunatambua namna gani wakinamama wanapata shida ya maji katika Mji ule. Hivyo, tumshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan, ameliona hili na ameshatupatia fedha tutaenda sasa kifua mbele kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kuambatana kwangu ni kawaida. Hivyo, niseme Mheshimiwa Minza usiwe na wasiwasi baada ya Bunge hili, baada ya kumaliza ratiba ya Mikoa niliyoipanga nitakuja kwako Simiyu hususani Meatu. Lengo ni kuona hali halisi na kuongeza chachu na ufanisi wa miradi yetu ya maji. (Makofi)