Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Minza Simon Mjika (3 total)

MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, ni lini Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria utapelekwa katika Mkoa wa Simiyu hususani katika Wilaya ya Meatu kama inavyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la KfW la Serikali ya Ujerumani imekamilisha taratibu za kupatikana kwa wataalam washauri ambao watasimamia utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Mkoa wa Simiyu. Mradi huu unahusisha ujenzi wa bomba kuu kilometa 195, matenki nane yenye ujazo wa lita milioni 11.9 na mabomba ya usambazaji kilometa 49.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi unatarajia kuanza mwezi Agosti, 2021 na miji mikuu ya Wilaya itakayonufaika ni Busega, Bariadi, Itilima, Maswa, Meatu na vijiji vya vilivyoko pembezoni mwa bomba kuu umbali wa kilometa 12 kila upande. Mradi umepangwa kutekelezwa kwa miaka minne. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, ni lini barabara kutoka Kolandoto hadi Meatu itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge Viti Maalum, Simiyu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kolandoto hadi Meatu ni sehemu ya barabara ya Kolandoto – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti hadi Oldeani Junction yenye urefu wa kilometa 328. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ulishakamilika na ujenzi kwa kiwango cha lami utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha.

Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 5,000 zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Kolandoto – Mwanhuzi yenye urefu wa kilometa 62.5 na kipande cha Lalago – Ng’oboko – Mwanhuzi yenye urefu wa kilometa 74.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa Daraja la Mto Sibiti pamoja na barabara unganishi kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 25 mpakani mwa Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu na Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida ni hatua za awali za ujenzi wa barabara hiyo ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itachimba visima vya maji katika Kata ya Mwamanyili Kijiji cha Milambi Wilayani Busega ili kuwapunguzia adha ya maji akina mama wa Kijiji hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Serikali itafanya upanuzi wa mradi wa maji wa Mwamanyili ambao chanzo chake ni Ziwa Victoria kwenda katika Vijiji vya Mwamanyili, Mwanangi, Milambi na maeneo ya Nassa Ginery. Upanuzi huo utahusisha ukarabati wa chanzo cha maji, ulazaji wa bomba la urefu wa kilometa 13.6 na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 15. Kukamilika kwa utekelezaji wa mpango huo kutaboresha huduma ya maji hadi kufikia asilimia 54. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali imepanga kutekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Miji ya Busega, Bariadi na Itilima Mkoani Simiyu. Mradi huo utanufaisha zaidi ya vijiji 200 vya Miji hiyo.