Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Thea Medard Ntara (3 total)

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo yamenikatisha tamaa, nimechanganyikiwa, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Serikali ilianzisha Kitengo cha SUA huko Tunduru, Waziri anijibu, je, ni lini tawi hilo litaanza kufanya kazi kama Chuo Kikuu Kishiriki au Centre na twende wote huko tukaone?

Swali la pili, Vyuo Vikuu Vishiriki vya Taasisi ya Dini vilivyopo Kusini kama hicho alichokitaja, Stella Maris na kile kingine kipo pale Songea kinaitwa AJUCO, vimeendelea kuzorota na vingine vimefungwa. Serikali ndio inatakiwa kusimamia hivyo vyuo ili viweze kusimama kwenye sehemu yake. Mheshimiwa Waziri ataniambia wanasaidiaje hivi vyuo ambavyo watoto wanaosoma ni Serikali hii hii ili viweze kusimama na kufanya kazi yake kikamilifu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Thea, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Chuo chetu cha SUA kilikabidhiwa eneo katika majengo ambayo yalikuwa ya camp ya waliokuwa wanajenga barabara. Serikali imefanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli udahili katika chuo hiki cha Tunduru bado haujaanza na kinachokwamisha kuanza udahili pale ilikuwa bado kuna miundombinu ambayo siyo toshelezi. Bado hakuna mabweni pamoja na maabara katika eneo hili. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Chuo chetu cha SUA kimepanga kuanza kutoa kozi fupi fupi pale katika eneo letu la Tunduru kwa wakulima wetu kwa lengo la kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya korosho, mihogo pamoja na ufuta.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika majengo yale yaliyopo kwa hivi sasa yanatumika kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa wanafunzi wetu wanaosoma Shahada ya Wanyamapori na Utalii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Chuo chetu cha SUA kinaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutosheleza au kujenga miundombinu ili tuweze kuanza kutoa huduma pale mara tu majengo hayo yatakapokuwa yamekamilika.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, amezungumzia juu ya vyuo binafsi ambavyo vipo katika Kanda hiyo ya Kusini, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imekuwa inafanya juhudi tofauti tofauti kuhakikisha vyuo hivi vinaendelea kutoa huduma. Serikali imekuwa ikifanya yafuatayo kupitia Tume ya Vyuo Vikuu:-

Mheshimiwa Spika, tumeendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha kama vyuo hivi vinatoa huduma sawasawa na elimu Bora; Tume yetu imeendelea kutoa ushauri wa kitaalam; na Tumeendelea kutoa mafunzo kwa viongozi pamoja na Wahadhiri wa vyuo hivi. Katika mwaka huu fedha, TCU imeendesha mafunzo ya Wahadhiri pamoja na wamiliki zaidi ya 218 kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinasimama sawasawa. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibuyake, lakini niseme tu kwamba mpaka sasa vyuo vikuu vina shida sana ya wahadhili na mfumo huo unachukua muda mrefu mno, yaani mtu anaomba kibali inachukua miezi sita na zaidi.

Ni lini watarekebisha na kuona kwamba huo mfumo unakuwa mwepesi ili tupate wahadhili wa kutosha katika vyuo vikuu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Dkt. Thea Ntara ni mwakilishi wa vyuo vikuu hapa ndani ya Bunge na kwa kweli anaitendea haki sana nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulitambua kwamba mifumo ambayo tulikuwa nayo nyuma ndiyo iliyokuwa ikileta matatizo na kusababisha ucheleweshaji mkubwa sana wa upataji wa vibali vya wageni. Mfumo ambao ninauzungumza ambao upo kwenye piloting kwa sasa ni mfumo mpya na tulipoanza kufanya majaribio kibali kina uwezo wa kutoka ndani ya siku moja ama siku mbili.

Naomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na amani, tutausimamia vizuri mfumo hu una kuondoa tatizo la upatikanaji wa vibali kwa maprofesa, wahadhili, lakini na wageni wote wanaotaka kupata vibali hapa nchini. (Makofi)
MHE. DKT THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwa mara ya kwanza mimi naona amelitendea haki sana swali hilo, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; ili kuendelea kupunguza uhaba wa wahadhiri;

Je, Serikali haiwezi kurudisha utaratibu wa kuwafanya wahadhiri hao wafundishe hata baada ya miaka 65 kama nchi nyingine za Marekani na Ujerumani?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ntara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wahadhiri wetu kufundisha zaidi ya miaka 65 ni suala la kiutumishi kwenye kanuni zetu za kiutumishi. Nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalichukua suala hili, tutakwenda kukaa na wenzetu wa Wizara ya Utumishi ili tuweze kuangalia namna gani ya kurekebisha sheria zetu zile ili ziendane sasa na mahitaji haya muhimu ya soko letu la wahadhiri nchini. Ahsante sana.