Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Dr. Thea Medard Ntara (4 total)

MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo Kikuu cha Taifa Kusini mwa Tanzania na Kanda nyingine ambazo hazina Vyuo Vikuu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea M. Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, taratibu za uanzishwaji wa Vyuo Vikuu vya Umma hazilengi kuanzisha Vyuo Vikuu vya Kikanda, Kimkoa au Kiwilaya. Vyuo Vikuu vilivyopo nchini, vikiwemo vya Serikali na Binafsi, vinapokea wanafunzi kutoka Kanda zote za Tanzania Bara na Visiwani; na kutoka nje ya nchi. Huu ndio utaratibu wa Vyuo Vikuu Duniani kote. Katika Kanda ya Kusini kuna vituo vitatu vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) vilivyopo katika Makao Makuu ya Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma. Aidha, kipo Chuo Kikuu Kishiriki cha Stella Maris STeMMUCO kilichopo Mkoa wa Mtwara na Taasisi ya Uhasibu Tanzania TIA Kampasi ya Mtwara.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa mpango wa Serikali ni kuboresha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia. Tunafanya hivyo ili kuongeza nafasi za udahili na ubora wa elimu itolewayo na hivyo kukidhi mahitaji ya nchi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha Sheria ya Ajira na kuweka mazingira mazuri ili maprofesa wa kigeni waweze kufanya kazi nchini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuboresha utoaji ajira kwa wageni ilitunga Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni, Namba 1 ya mwaka 2015 pamoja na Kanuni za Kuratibu Ajira za Wageni za mwaka 2016 ili kuratibu ajira za raia wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini ikiwa ni pamoja na kulinda ajira za wazawa na kuruhusu ujuzi adimu kutoka nje kuingia na kurithishwa nchini. Serikali kwa sasa inaendelea na mapitio ya sheria ili kuifanyia maboresho kwa kuzingatia mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Spika, ili kuweka mazingira mazuri ya kuruhusu uwepo wa wafanyakazi wa kigeni nchini, Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi na ukaazi kwa raia wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini na mfumo husika umeanza kutumika kwa majaribio (piloting) kuanzia tarehe 23 Aprili, 2021. Mfumo huu utaongeza Ufanisi katika kushughulikia maombi husika.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu pia utaondoa changamoto ya upatikanaji wa taarifa unganishi za kisekta za kurahisisha upatikanaji wa vibali vya wageni wakiwemo Maprofesa kwa wakati kwa kuzingatia uhitaji.

Mheshimiwa Spika, kulingana kwa taarifa zilizopo mpaka sasa jumla ya vibali vya kazi 74 vimetolewa kwa Maprofesa na Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nchini vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (St. Augustine University) na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Tanzania na vinginevyo.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kusomesha Wahadhiri wengi zaidi katika ngazi ya Shahada ya Uzamivu (Ph.D) kwani waliopo sasa ni wachache?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inao mpango mkakati wa kuongeza rasilimaliwatu katika taasisi za elimu ya juu ikijumuisha wahadhiri, wakutubi na wataalamu wa maabara na karakana ili kukidhi mahitaji ya viwango na ubora wa Elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwezi Julai, 2021 Serikali kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) ina mpango wa kusomesha jumla ya wahadhiri 430 katika kipindi cha miaka mitano (2021-2026) ili kukabiliana na upungufu huu katika fani za kipaumbele (Priority Programs) katika vyuo vikuu vya Serikali nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na mpango huo mahsusi, vyuo vikuu navyo vinaendelea kusomesha wahadhiri wao kupitia vyanzo vingine, ikiwemo mikataba ya kitaalam ya utafiti (collaborative research projects) na scholarship mbalimbali tunazopokea kutoka nchi rafiki ambapo wahadhiri hupewa kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia mipango hiyo, Jumla ya wahadhiri 621 katika ngazi ya shahada ya Uzamivu (PhD) na 241 katika Shahada ya Umahiri wanaendelea na masomo. Aidha kwa mwaka wa masomo 2021/2022 jumla ya wahadhiri 48 wanaendelea na masomo katika nchi mbalimbali. Kwa mfano katika nchi ya China wapo wanafunzi au wahadhiri 30, Uingereza 12 na Hangaria wahadhiri sita. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA K.n.y. MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu hasa katika sekta ya kilimo kwa kuwa mikopo ya elimu ya juu imewezesha wanafunzi wengi kuhitimu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu zinaongezeka hususan katika sekta ya kilimo, Serikali imetekeleza mipango ifuatayo: -

(i) Kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kupitia programu ya kukuza ujuzi nchini, ambapo jumla ya vijana 12,580 katika Mikoa 17 nchini, wakiwemo wahitimu wa fani ya kilimo wamepatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa na sasa wapo tayari kuanza biashara ya kilimo na kutumia teknolojia na ujuzi wa kitalunyumba.

(ii) Kuwezesha wahitimu kupata uzoefu wa kazi nje ya nchi (internship), ambapo Serikali kwa kushirikiana na Ushirika wa Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUGECO), wamewezesha wahitimu 703 kwenda nchini Israeli na Marekani. Kati ya hao, wahitimu 311 wamerudi nchini na wamejiajiri katika maeneo mbalimbali nchini.

(iii) Kupitia Benki ya TADB na mikopo ya Halmashauri, baadhi ya wahitimu waliopatiwa mafunzo nje ya nchi wamepatiwa mikopo ya jumla ya Shilingi Milioni 170 na wanaendelea na shughuli hizo.

(iv) Kupitia Vituo vya Uatamizi kwa wahitimu (Incubator Centres) katika Mikoa ya Morogoro na Pwani, wahitimu 1,000 wamepatiwa mafunzo ya uanzishaji shughuli za kilimo na ujasiriamali na;

(v) Kupitia kilimo cha vizimba (block farming), wahitimu 39 wamepatiwa fursa ya kuanzisha shughuli za kilimo. Kati ya hao, wahitimu 30 wamepatiwa fursa ya kushiriki katika shamba la hekari 1,500 lililopo Mkoani Morogoro Mvomero. Aidha, wahitimu Tisa wamepatiwa fursa ya kushiriki katika shamba la kahawa Mkoani Songwe.

Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha wahitimu wengi zaidi wanaendelea kuwezeshwa kuajirika lakini pia kujiajiri, kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 54 ili kuwawezesha wahitimu 1,500 kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi ikiwemo fani ya kilimo. Ahsante. (Makofi)