Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma (5 total)

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kwa Jimbo la Nkasi Kusini, hali ni hiyohiyo ama mbaya zaidi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza ambapo tuna kata 37 na vituo viwili tu vya afya. Sasa swali langu, Serikali ina mpango wowote wa kuongeza vituo vya afya Wilayani Muheza ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Jimbo la Muheza lina kata 37 na vituo vya afya viwili tu na hali hii ipo katika karibu majimbo yote nchini. Tunafahamu tuna kata zaidi ya 3,900 na ndiyo maana Serikali imeweka mpango wa kujenga vituo vya afya kwa awamu. Ni kweli kwamba hatuwezi kukamilisha kujenga vituo katika kata zote ndani ya mwaka mmoja wa fedha, lakini Serikali imedhamiria na inatambua kwamba tuna kazi ya kufanya kwa awamu kwa kadri ya fedha zinavyopatikana na kuendelea kujenga vituo vya afya katika kata zetu na kujenga zahanati katika vijiji na hospitali za halmashauri katika ngazi za halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mwinjuma kwamba katika mipango ya Serikali inayokuja, tutaendelea kuomba kuidhinishiwa fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga vituo vya afya katika kata nchini kote zikiwemo kata katika katika Jimbo hili la Muheza.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Najua barabara yote kilometa 40 ina umuhimu mkubwa, lakini kipande katikati ya Kisiwani na Kibaoni ndiyo kipande hasa ambacho kina matatizo makubwa, Je, Serikali ina mpango wowote wa kukishughulikia kipande hiki kwa namna ya kidharula ili kuhakikisha kwamba kinapitika wakati wote wa mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwinjuma, Mbunge wa Muheza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, barabara hii inaendelea kutengenezwa. Jana nimepita maeneo ya Tanga na nilikuwa na Meneja wa TANROADS na moja ya maelekezo ambayo tumempa ni kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo yana shida likiwepo hili la kati ya Kisiwani na Kibaoni wahakikishe kwamba wanapeleka nguvu zao ili pasije pakatokea tatizo la kutokuwa na mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu barabara hii ipo kwenye matengenezo ndiyo maana tumeendelea kutenga hizo shilingi milioni 600 kwa ajili ya kurekebisha sehemu zozote ambazo ni korofi ikiwemo pamoja na hili eneo kati ya Kisiwani na Kibaoni. Ahsante.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri kwa niaba ya Serikali na ambayo yananipeleka kwenye maswali mawili ya nyongeza. Miongoni mwa matatizo makubwa ya kilimo na biashara ya viungo Wilayani Muheza ni kukosekana kwa ardhi kubwa ya kulimia mazao hayo kule ambako yanastawi. Pia na viwanda vya kuyachakata kulekule kwenye Tarafa ya Amani, ili kuyaongezea thamani kwa vile kule hakuna kiwanda hata kimoja. Sasa kuna ekari 35,063 ambazo ziko chini ya Kampuni ya East Usambara Tea Company ambazo zilikuwa na viwanda viwili ambavyo kwa sasa ni magofu na zinazotumika ni ekari 4,909 tu kwa miaka mingi na viwanda hivi vimegeuka magofu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali haioni hivi sasa ni wakati wa kuvirudisha viwanda hivi kwenye umiliki wake, ili kuwasaidia wananchi ikiwa ni kwa kuwekeza yenyewe ama kwa kushirikiana na wawekezaji wapya serious ili wananchi wa Amani wapate kupata viwanda vya kuongeza thamani mazao yao ya viungo kule? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tatizo la aina hii, Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuwa mashahidi, limekuwa likitokea sehemu nyingi ambapo wawekezaji wamekuwa wakiomba kumilikishwa viwanda hivi kwa ahadi ya kuvifufua na kuzalisha ajira pamoja na kuliongezea pato Taifa, lakini badala yake wamekuwa wanaviuwa na kuvigeuza kuwa magofu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuwa aidha na sheria kali zaidi ama kutunga sheria mpya ili tusiendelee kuchezewa na viwanda vyetu vifanye makusudio yaliyokuwepo wakati vinaanzishwa? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamis Mohamed Mwinjuma, Mbunge wa Jimbo la Muheza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Hamis Mwinjuma kwa kufuatilia sana maendeleo, hasa sekta ya viwanda katika jimbo lake. Amenifuata mara nyingi kuhusiana na viwanda hivi, hasa vya chai hivi vya East Usambara Tea Company Limited, ambavyo viko pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusu suala la ardhi. East Usambara Tea Company Limited ina ekari 35,000 kama alivyosema na katika ekari hizo ni ekari 2,027 tu ndio zimepandwa chai na ekari 600 zimepandwa miti, kwa maana ya miti ile inayotumika kama nishati, kuni kwa ajili ya kutumika katika viwanda hivyo. Pia eneo lingine maeneo yaliyobakia ambayo yanamilikiwa na kampuni hii yanatumika kwanza katika sehemu nyingine ni vyanzo vya maji, lakini maeneo mengine ni natural reserve kulingana na utaratibu wa UNESCO kwamba, huwezi kutumia mazingira yote kulima, kwa hiyo, maeneo mengine makubwa yako katika mazingira ya reserve.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na uhitaji wa wakulima katika Jimbo la Muheza, tutaona namna gani kushirikiana na wenye kampuni, ili tuone kama wanaweza kutoa sehemu kidogo ambayo inaweza kutumika na wakulima wadogowadogo kwa ajili ya kuzalisha viungo ambavyo vitatumika katika viwanda vya kuchakata viungo kama alivyoomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uwekezaji katika viwanda hivyo. Nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na ufuatiliaji huo wote, lakini viwanda hivi sasa vinafanya kazi vizuri. Uwezo uliosimikwa kwa viwanda vile viwili ambavyo vinafanya kazi vya Bukwa na Kwamkoro vina uwezo wa kuchakata kilo 120 kwa siku, lakini sasa hivi vinaweza kupata raw material kwa maana ya malighafi zaidi ya kilo 90,000. Kwa hiyo, maana yake viwanda hivi vinafanya kazi vizuri, lakini kuna viwanda vile viwili ambavyo kutokana na mahitaji haya wenye viwanda, Kampuni ya East Usambara Tea Company Limited, walivigeuza kama ma-godown, ambavyo vilikuwa Viwanda vya Munga na Nderema, lakini pia baadaye, nimjulishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kampuni hii ina mpango sasa wa kuanza ku-pack kwa maana ya blending ya ile chai wanayozalisha pale badala ya kwenda kuuza kwenye minada ya Mombasa na kwingine, wataanza kufanya blending pale. Kwa hiyo, tuna mpango wa kuwasaidia ili wafufue viwanda hivi viwili viweze sasa kufanya blending badala ya kuwa store au magofu kama yalivyo sasa.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, na nina maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni kwamba, kwa vile imeshathibitika kwamba jambo hili halina madhara yoyote kimazingira na kwenye idadi ya vipepeo, na kwamba kwanza ukiachilia mbali kuongeza vipato vya wananchi lilikuwa linasaidia kwenye idadi ya vipepeo kwa vile kwa kawaida kipepeo anayetaga mayai mpaka 500 kwa njia zake za kwaida huweza kuzalisha vipepeo wawili, lakini kwa njia hii ya msaada wa wananchi huweza kuzalisha mpaka vipepeo 300.

Je, Serikali haioni kwamba, ilishauriwa tu vibaya kwenye suala hili kwa kutotenganisha kati ya wanyama wakubwa kama chui, twiga na swala na hawa vipepeo wetu na kwamba inatakiwa kurudi nyuma na kutenganisha sasa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwa vile ni nchi chache sana duniani ambazo zinaweza kuzalisha vipepeo kama sisi, na ni biashara na utalii mkubwa duniani; Serikali haioni haja sasa ya kuwekeza kwenye kuanzisha utalii wa vipepeo, ili kuongeza vivutio vya utalii nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hamis Mwin’juma, Maarufu kama “Mwana FA”, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Hamis Mwin’juma, lakini pia nimpongeze sana kwa kuendelea kusimamia eneo hili la wanyamapori hai, lakini nimpongeze pia kwa kuendelea kupigania wananchi wa Muheza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo ameshauri Mheshimiwa Mwinjuma, kwamba Serikali inawezekana ilishauriwa vibaya. Nimtoe wasiwsi kwamba Serikali iko makini na Serikali iko kazini na ina wataalamu wa kutosha. Suala hili limekuwa likichunguzwa na wataalamu mbalimbali. Muhimu ni kuangalia kipi faida na hasara ambayo inaweza ikapata Serikali. Tunapoendelea kuhamisha wanyama mbalimbali kutoka ndani ya nchi kupeleka nje ya nchi ina maana tunazidi kuuwa utalii wa hapa Tanzania. Hata hivyo nimtoe wasiwasi, kwamba suala hili tunaendelea kulifanyia tathmini, tutachakata kuangalia faida na hasara ya eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze pia, kwa kuendelea kuhamasisha utalii kupitia vipepeo ambavyo amevitamka yeye mwenyewe. Kwa hiyo, kama kweli tutaanzisha utalii wa vipepeo haina haja sasa hata kuendelea kuvitoa hivi vipepeo viende nje ya nchi kwa sababu tunapoendelea kuvitoa tunauwa soko la utalii wa ndani.
MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Hata hivyo, ripoti ya NEMC ya Oktoba, 2018 ambayo Mheshimiwa Waziri anaitaja, ilielezea wazi kwamba kinachokatazwa ni uchimbaji mdogo na inashauriwa ufanyike uchimbaji aidha wa kiwango cha kati ama mkubwa, kwa sababu hizo za kimazingira ambazo Mheshimiwa Waziri amezitaja. Sasa je, Serikali haioni kwamba kwa vile wananchi wa Sakale, Kata ya Mbomole, Wilaya ya Muheza, hawana uwezo wa kufanya uchimbaji wa kiwango cha kati ama mkubwa inafaa sasa iwasaidie kupata mwekezaji mwenye vigezo vinavyotajwa na ripoti hiyo ili uchimbaji ule uweze kufanyika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyikiti, la pili; ni ombi kwa Wizara, kwamba tuna maeneo kadhaa mengine katika Wilaya ya Muheza katika Kata ya Pande Darajani katika Kata ya Magila na katika Kata ya Magoroto hasa Kijiji cha Mwembeni ambayo yanaonyesha dalili za kuwa na madini. Je, Serikali inaweza kututumia watalaam wake ili wakafanye tathmini na kuona kama kuna uwezekano wa kuchimba katika maeneo hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda ujibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge Hamis Mohamed Mwinjuma, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla ya kutoa majibu ya Wizara, napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuwa mwelewa, kwa sababu tulipofanya ziara hii na kukubaliana kwamba uchimbaji mdogo utaleta athari kubwa za mazingira, mara nyingi watu wasingeweza kuamini kwamba mbona kuna mali, lakini tathmini ya kimazingira ilionyesha kwamba uchimbaji mdogo utaleta athari kubwa ambazo yawezekana zisiwe na faida hata kama uchimbaji unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya kuelewa kwa Mheshimiwa Mbunge ndiyo maana hata wananchi wote wakaelewa kwamba huenda kama madini haya lazima yachimbwe basi iwe ni kwa uchimbaji wa kati ambao teknolojia yake inakuwa ni ya kuchukua udongo mahali pale na kuchenjulia sehemu nyingine ili kuendelea kulinda vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, Wizara itatoa ushirikiano wote ambao wananchi wanauhitaji kwa sababu pale tulikwishatoa leseni za uchimbaji mdogo. Kwa hiyo tutawaomba tu wafuate utaratibu, wao watapata muwekezaji halafu watakuja Wizarani, watafanya amalgamation ya uchimbaji mdogo tutazi-upgrade kuwa za uchimbaji wa kati na tutawapa miongozo yote inayostahili ili waweze kufanya uchimbaji ambao bado utazingatia kutoathiri chanzo cha maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili; GST ndiyo taasisi yetu ambayo inakwenda kufanya utafiti wa awali na huwa tunapenda kuhimiza utafiti wa awali kwa sababu hautakuwa ule ambao unaleta na wingi wa mashapo kwa kule chini. Sasa hilo linawezekana, tutawaagiza waje. Mheshimiwa Mbunge hata baada ya hapa anaweza akaja pale ofisini kwetu tukaongea na watu wa GST na wakapanga namna ya kwenda nawe ili awaelekeze katika maeneo ambayo anataka waweze kufanya utafiti ili huo wa awali uweze kuonyesha kama uchimbaji unaweza kuendelea katika vijiji ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja. Nakushukuru. (Makofi)