Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Venant Daud Protas (1 total)

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri Nishati lakini nina swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri ya Wilaya ya Uyui hasa Jimbo la Igalula tuko nyuma sana katika kuunganishiwa nishati ya umeme. Wakati wa kampeni Mheshimiwa Waziri alikuja tukazindua mradi mkubwa lakini mara baada ya kuondoka yule mkandarasi hakuendelea na kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa kupeleka umeme kwenye kata zaidi ya sita zilizoko katika Jimbo la Igalula na vijiji vyake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa umeme jazilizi katika vijiji vya kata ya Goeko Msasani, Igalula Stesheni na Kigwa Majengo Mapya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Protas Venant wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye jibu la msingi kwamba vijiji vyote 46 vilivyobaki katika Jimbo la Igalula vitapatiwa umeme kuanzia mwezi Februari kwa miezi 18 kwenye mradi wa REA III mzunguko wa pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili ambalo nadhani ndilo la nyongeza alikuwa anasema kwamba mwaka jana Mheshimiwa Waziri alizindua mradi wa umeme jazilizi (Densification) awamu ya pili, Densification 2A.

Mheshimiwa Naibu Spika,Jimbo la Igalula, Mkoa wa Tabora ni mojawapo ya mikoa 9 inayonufaika na Densification 2A ambayo ilianza mwaka jana na tayari ilishazinduliwa kwa Mkoa wa Tabora. Mkandarasi anayefanya kazi katika Mkoa wa Tabora anayo Lot moja ambayo ina mikoa miwili; Tabora na Singida na atafanyakazi hiyo kwa shilingi bilioni 9.7. Tayari mobilization imeshaanza, ameshafanya survey katika Jimbo la Igalula na amekamilisha na tunatarajia muda wowote kufikia mwezi wa nne atakuwa tayari ameanza kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge kwamba amekuwa akifuatilia hata ofisini kuulizia Densification 2A itaanza lini kwenye Jimbo lake, tunamhakikishia kabla ya mwezi Aprili upelekaji wa umeme kwenye vitongoji vilivyoko katika Jimbo la Igalula utakuwa umeanza.