Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Venant Daud Protas (6 total)

MHE. VENANT D. PROTAS Aliuliza:-

Jimbo la Igalula lina jumla ya vijiji 58, ambapo Vijiji 12 vimepata umeme na vijiji 46 bado havijapata umeme:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katika vijiji 46 ambavyo havijapata umeme?

(b) Je, gharama za kuunganisha umeme kwa kila mwananchi ni kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daud Protas Venant, Mbunge wa Igalula, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vilivyobaki 46 katika Jimbo la Igalula vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya III mzunguko wa pili unaoanza katikati ya mwezi Februari 2021. Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba, 2022. Kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huo, kutafanya vijiji vyote katika Jimbo la Igalula kupatiwa umeme.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua ya kuongeza kasi ya kutoa huduma ya umeme nchini mwaka 2019, Serikali kupitia TANESCO ilipunguza bei ya kuunganisha huduma ya umeme kwa wananchi wanaoishi vijijini na maeneo yanayofanana na hayo kutoka wastani wa shilingi 725,000/= kwa mita za njia tatu (three phase) hadi shilingi 139,000/= ikiwa ni punguzo la asilimia 80. Vilevile kwa mita za njia moja (single phase) kutoka wastani wa shilingi shilingi 177,000/= hadi shilingi 27,000/= sawa na punguzo la asilimia
84.75. Kwa ujumla, gharama hizo ni tozo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano ya simu kwenye Vijiji vya Igalula ambavyo havina mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daud Protas Venant, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ina jukumu la kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini ambayo hayana mvuto wa kibiashara. Mpaka sasa Mfuko wa Mawasiliano umeshatekeleza miradi 686 na bado kuna miradi katika kata 371 ikiwa inaendelea na utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Igalula lina kata 11 ambapo Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) imetekeleza miradi sita ya mawasiliano katika Jimbo la Igalula ambapo imejengwa minara sita ambayo imetolewa na watoa huduma katika Kata tano ambazo ni Kizengi, Loya ambayo ina Miradi miwili, Lutende, Miswaki pamoja na Tura.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata zenye watoa huduma wa mawasiliano katika Jimbo la Igalula ni 10 ambazo ni Igalula yenyewe, Kigwa, Loya, Lutende, Miswaki, Kizengi, Miyenze, Tura, Goweko pamoja na Nsololo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada za Serikali, Kata ya Mmale na baadhi ya maeneo ya Jimbo la Igalula bado yana changamoto ya mawasiliano na kupitia Mfuko wetu wa Mawasiliano tunaendelea kufanya tathmini, ili tujiridhishe specifically kwamba kuna changamoto katika maeneo yapi ili yaingizwe katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika siku za usoni kadri upatikanaji wa fedha utakapokuwa unaruhusu. (Makofi)
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara ya Igunga – Miswaki – Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida yenye urefu wa kilometa 89?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daudi Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Igunga – Miswaki –Loya – Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida ni barabara inayouganisha Wilaya za Igunga na Uyui. Kwa upande wa Wilaya ya Igunga, barabara hii inajulikana kama barabara ya Igunga – Itumba – Buhekela – Simbo na ina urefu wa kilometa 107. Kwa upande wa Wilaya ya Uyui barabra hii inaunganisha barabara tatu ambazo ni Simbo - Miswaki - Loya – Migongwa – Magulyati yenye urefu wa kilometa 72.8, hivyo kufanya urefu wa barabara ya Igunga – Miswaki – Loya –Migongwa – Magulyati hadi Iyumbu Singida kuwa na urefu wa kilometa 179.8.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 361.99 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida, kilometa 27, maeneo korofi kilometa 8.7 na matengenezo maalumu kilometa tano na ujenzi unaendelea. Aidha, katika mwaka 2021/2022 TARURA Halmashauri za Wilaya ya Igunga na Uyui zimetenga jumla ya shilingi milioni 235 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilometa 35 na ujenzi wa daraja dogo (box culvert) mawili, makalvati mistari minne ili kuimarisha maeneo korofi ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kuzifanyia matengenezo barabara katika maeneo mbalimbali nchini kulingana na upatikanaji wa fedha, nashukuru sana.

MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Kata za Kigwa, Goweko, Igalula na Nsololo?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa uchimbaji wa mabwawa katika Kata za Mmale, Miswaki, Lutende na Kizengi ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo hayo?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venant Daud Protas, Mbunge wa Igalula lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imepanga kuboresha huduma ya maji kwenye Kata za Kigwa, Goweko, Igalula na Nsololo kupitia bomba kuu linalotoa maji Ziwa Victoria kupeleka Miji ya Nzega, Igunga na Tabora.

Kazi zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa tenki lenye ujazo wa lita 1,000,000 na ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilometa 122. Mradi huu unatarajiwa kukamilika kabla mwezi Juni, 2022 na utanufaisha wananchi wapatao 123,764 kwa kupata huduma ya maji safi, salama na yenye kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2021/2022 kukamilisha usanifu wa ujenzi wa bwawa katika Kata ya Kizengi na wakandarasi watapatikana mwezi Machi, 2022 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo ambapo wananchi wa Kata za Kizenga, Mmale, Miswaki na Lutende zaidi ya 60,000 watanufaika.
MHE. VENANT D. PROTAS aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza agizo la Rais wa Awamu ya Tatu la kuitambua Kizengi kuwa Tarafa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Protas Venant, Mbunge wa Jimbo la Igalula, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala hufanyika kwa mujibu wa mwongozo wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala wa mwaka 2004.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo huu unaelekeza maombi ya kuanzisha maeneo hayo kujadiliwa na kupitishwa kwenye vikao vya kisheria ngazi za Vijiji, Kata (WDC), Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC) kisha kuwasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI haijapokea maombi ya Kizengi kuwa Tarafa. Hivyo, naishauri Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kufuata mwongozo uliotolewa na kuwasilisha maombi hayo Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya tathmini na kufanya maamuzi kwa kadri ya taratibu. Ahsante.