Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Venant Daud Protas (8 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais iliyotolewa mwezi Novemba, 2020 na mimi nikiwa kama Mbunge, nimesimama hapa kwenye Bunge hili tukufu kwa mara yangu ya kwanza, nianze kumshukuru kwanza Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema aliyetufikisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakishukuru Chama changu cha Mapinduzi ambacho kilinipigania mpaka nimeweza kuingia kwenye chombo hiki muhimu sana. Tatu, nawashukuru familia yangu, walikuwa nami bega kwa bega kupambana katika kuhakikisha mimi nasimama imara kwa maslahi ya Wanaigalula wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa ni dira ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano. Nisiende mbali, kwanza naiunga mkono kwa asilimia mia moja kwa sababu sisi wote wana-CCM tulisimama kote kule tukiinadi Ilani ya Chama cha Mapinduzi na hotuba yake yote imepitia ilani, ndiyo maana akaja na mpangokazi wa miaka mitano, nini Serikali ifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa wasaidizi wake, wameanza kazi vizuri. Tangu ametangaza Baraza la Mawaziri, tumeanza kupishana huko majimboni, wanafanya kazi nzuri sana, tuendelee na mwendo huu huu. Mheshimiwa Rais ameaminika na wananchi wote na Watanzania wote wamemwamini, ndiyo maana wakampa kura zaidi ya asilimia 84, na sisi Wabunge tumeaminiwa na wananchi, wana imani kwa kipindi cha miaka mitano wataona mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie sehemu chake, kutokana na muda, sisi tunaotoka majimbo ya vijijini, katika Halmashauri yetu ya Wilaya yetu ya Uyui, changamoto kubwa ni barabara, ndiyo kero ya Waheshimiwa Wabunge wote walioko humu ndani, kila utakapoenda, shida ni barabara. Katika mtandao huu wa barabara, kuna baadhi tukiwaachia TARURA hawawezi kutekeleza kwa kipindi cha miaka mitano. Kuna barabara gharama yake na bajeti inayokuja kwenye Halmashauri ya TARURA, ukiipa kwa kipindi cha miaka mitano ika-deal na barabara moja, haiwezi kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna barabara yenye urefu wa kilometa 89 ya kutoka Miswaki – Roya kwenda Maguliati mpaka Iyumbu, Mkoa wa Singida. Barabara hii ina madaraja 16 madogo madogo na daraja moja kubwa lenye mita 120. Hii barabara kwa takwimu ya mkandarasi ni zaidi ya shilingi bilioni sita. Halmashauri yetu inapokea shilingi bilioni 1.3 kwa mwaka. Kwa hiyo, ukisema uelekeze nguvu kule, haiwezi ikakidhi kwa kipindi cha miaka sita, barabara nyingi zote zitakuwa zimesimama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kupiga kelele TARURA iongezewe bajeti ili tuweze kukwamua kero za wananchi wetu, wapate barabara. Kwa sababu na kule kuna wapiga kura, tena wanajitokezaga sana kipindi cha kupiga kura. Naomba sana Serikali itusaidie kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye suala lingine. Sisi Wanasiasa na viongozi mbalimbali tumekuwa tukipita kwenye majimbo tukiwahimiza wananchi wetu wachangie baadhi ya maendeleo, lakini…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, muda!

SPIKA: Eeeh! (Kicheko)

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hotuba ya Mheshimiwa Rais, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba ya bajeti Ofisi ya Waziri Mkuu, kwanza nianze kabisa kwa kuunga mkono hoja hotuba nzuri ambayo imewasilishwa na Waziri wetu Mkuu ambaye imetupa matumaini kwa kipindi kilichopita utekelezaji wake na kipindi ambacho tunachokwenda cha bajeti cha mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi hizi tunafahamu Serikali iliyoko inatekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, na Ilani yetu imejipambanua vizuri sana, Ilani ya 2020 – 2025 yenye ukurasa 303 kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu la Igalula Serikali kupitia hotuba ya Waziri Mkuu imewasilisha ni jinsi gani imejali katika sekta ya afya. Na katika hotuba yake imesema kwa kipindi kilichopita wameweza kujenga zahanati zaidi ya elfu moja na mia moja na kidogo. Lakini vilevile wameweza kujenga vituo vya afya zaidi ya mia nne katika nchi nzima ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika Jimbo langu la Igalula, Jimbo lenye wakazi zaidi ya laki tatu waliopiga kura waliojiandikisha mwaka 2020 walikuwa zaidi ya laki moja na kidogo. Lakini Jimbo langu lina zahanati 17 tu ambazo zinatoa huduma kwa wananchi zaidi ya laki tatu, ukigawa uwiano wa zahanati hizo ni zaidi ya kila zahanati inaenda kuhudumia zaidi ya watu 20,000 ambayo kwa kuzingatia Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi kufikia na kufikisha huduma bora kwa wananchi wetu si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Igalula ni waungwana sana wamekuwa wakiibua miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya zahanati na shule. Na wamekuwa wakijitolea sana kwa kuwa wao ndio wanaona ndio vipaumbele vyao. Nilipochaguliwa na wananchi wa Jimbo la Igalula nimefaya ziara katika vijiji takribani 30 kati ya 58 kuangalia nini mahitaji yao na kila nilipokwenda wanahitaji shule na zahanati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia hotuba ya Waziri wetu Mkuu ambayo amewasilisha katika Bunge hili. Niiombe Serikali, juzi wakati tunachangia mpango wakati wa majumuisho Mhehimiwa Ummy Mwalimu alisema mwaka huu atajielekeza katika kutatua na kuweka vifaa tiba katika vituo vyetu vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ni jambo jema zaidi, lakini niwakumbushe kuna maboma mengi ambayo yameibuliwa na wananchi wanahitaji yamalizike. Tukisema twende tukupeleke kwenye vifaa tiba kwenye kituo cha afya kimoja katika jimbo la Igalula hatuwasaidii wana Igalula. Leo hii aliyekuwa Waziri wa Ofisi ya Rais, nani hii Jafo, alikuja katika Kata ya Igalula, aliwakuta wananchi wamechangia kwa nguvu zao wodi ya mama na mtoto akavutiwa na uwekezaji ule na juhudi zile aliweza kutupatia fedha na sasa tumejenga kituo cha afya kilichopo katika Kata ya Igalula. Niwaambie kituo cha afya kimekamilika tangu mwaka 2019 mpaka leo hakijaanza kazi. Sasa lengo la Serikali ni kuongeza huduma kwa wananchi na si kuua huduma kwa wananchi. (Makofi)

Meshimiwa Naibu Spika, wameweka vigezo, kulikuwa kuna zahanati jirani wanasema tuhamishe vifaa tupeleke kwenye kituo cha afya sijajua hayo maelekezo yanatoka huku juu au wenyewe maamuzi yao. Lengo la kuongeza vifaa, vitoa huduma ni lengo la kuwasaidia wananchi, haiwezekani palikuwa na zanahati na tunasema tuna zahanati elfu moja na ushee pamoja na ile zahanati halafu unakwenda kuiua, unasema vile vifaa tuhamishie kwenye vituo vya afya, hata ukiangalia mwongozo wa afya, vifaa vya kwenye zahanati na kituo cha afya ni vitu viwili tofauti.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kupitia kituo chetu cha afya katika Kata ya Igalula tupate vifaa tiba na ile zahanati iendelee kuwepo na wananchi waendelee kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maboma ambayo Serikali imeomba tuwasilishe kupitia halmashauri zetu. Niombe yale maboma yote ambayo yapo katika hatua ya umaliziaji na ni nguvu ya wananchi watu wengine, wananchi wengine baadhi ya kata na vijiji wamejenga zaidi ya miaka sita, mingine miaka minne mitano, wakiwa wanapita pale wanaangalia nguvu zao zimepotea basi Serikali kupitia bajeti hii iweze kuweka fedha ya kwenda kumalizia yale maboma ikiwemo maboma ya zahanati na shule, hivi hivi niombe Serikali iweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la miundombinu juzi wakati wanachangia hapa Wabunge wenzangu kuna mbunge mmoja alisema yeye katika Mkoa wa Dar es Salaam haitaji kilimo kwasababu hana eneo la kulima. Alisema anahitaji barabara ili aweze wanachi wake waende kutafuta kipato warudi nyumbani wakiwa salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wangu wanahitaji miundombinu ya barabara, barabara zetu za vijijini tofauti na za Dar es Salaam. Barabara zetu za vijijini wanahitaji kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika muda wote. Tukija kwenye masuala ya sekta nitachangia zaidi kutokana na muda niseme tu itoshe ninaunga mkono hoja hotuba ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Igalula nianze kuchangia kwasababu ya ufinyu wa muda, nianze kwa kuchangia suala la barabara, Jimbo la Igalula tumekuwa tukipiga kelele mara kadhaa hapa kulalamikia barabara zetu, nyingi hazipitiki hasa wakati wa masika.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto ya baadhi ya barabara na baadhi ya kata tangu dunia iumbwe, tangu tumepata uhuru hawajawahi kuona caterpillar la kusafisha barabara limepita katika maeneo yao. Kwa mfano katika kata ya Male toka tumeanzisha hii kata, halijawahi kupitiwa na barabara yoyote kwa bahati mbaya kupitia Serikali. Pia, Kata ya Nsololo haijawahi kupitiwa na caterpillar ambalo linasafisha barabara katika kata hiyo. Vile vile kuna barabara za Ipururu – Igalula haijawahi kupitiwa kabisa. Barabara za Kawekapina kuja Igalula hazijawahi kupitiwa. Ziko changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kwasababu tuna chombo na taasisi ambayo kimeanzishwa na Serikali TARURA, tuiombe Serikali iongeze fedha kwasababu yawezekana caterpillar haziendi katika maeneo haya kwa sababu ya ufinyu wa bajeti lakini TARURA ikiongezewa fedha na halmashauri yetu ikaletewa fedha kupitia mfuko wa TARURA nina imani katika maeneo haya na wananchi wataona ma- caterpillar yamepita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto ya daraja, jana Naibu Spika amesema katika Jimbo lake kuna watu watano wamepoteza maisha, roho inamuuna sana. Kila mwaka zaidi ya watu 20 wanapoteza maisha katika Kata ya Loya ili mtu aweze kuja kupata matibabu katika Kijiji cha Loya kutoka Mwamabondo lazima avuke mto. Kila mwaka akinamama wajawazito, watoto wanaoenda shule wanapoteza maisha zaidi ya 20 kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imekuwa likipigiwa kelele Daraja hili la Loya tangu mwaka 2013. Nimejaribu kupitia Hansard za Wabunge waliopita mwaka 2013 mpaka 2015 Mbunge aliongea, 2020 Mbunge alizungumza na baadaye akaamua kuwa maji yamemfika shingoni akaamua kwenda kuwadanganya wananchi akawaambia kuna fedha imetengwa ya kuja kujenga daraja.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya kupita kuwa Mbunge nilikuja kufuatilia fedha hizi sijaona fedha yoyote iliyotengwa. Niiombe Serikali, kwa haya madaraja ambayo ni kiungo ya kijiji na yenye huduma kwa wananchi muda wote niiombe Serikali iwekee kipaumbele, tuna hitaji Daraja la Loya lijengwe kwasababu limeanza kupigiwa kelele zaidi ya miaka 10. Niombe Serikali iweze kusaidia katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya TAMISEMI 2021/ 2022 sijaona wametutengea fedha za kuweka vifaatiba katika kituo chetu cha afya. Tumejenga majengo mazuri, Serikali imewekeza fedha nyingi, tunashindwaje kuweka vifaatiba ili wananchi wetu waanze kutumia yale majengo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, majengo yamekaa kila siku tunapeleka wanafunzi wanakwenda kukalia, yanakuwa machafu nyoka wanaingia kwenye majengo. Niiombe Serikali, kwa hivi vituo ambavyo vimekamilika, wapeleke vifaatiba ili wananchi waanze kupata huduma. Vile vile tuna majengo mengi ya zahanati lakini kwenye bajeti hii wametuwekea kila jimbo angalau watapata zahanati mbili. Nina maboma zaidi ya 10 yapo, wananchi wameweka nguvu zao wanahitaji wapate huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwananchi anapochangia hela yake ya kwenda kujenga kitu, ana malengo nacho kwasababu amepata shida kwa muda mrefu. Kwa hiyo, yale majengo naomba Serikali itanue wigo wa kuongeza bajeti ya kujenga haya maboma. Sisi kazi yetu tunanyanyua maboma lakini Serikali mnapokuja na Mpango wa zahanati mbili mbili, kwa hiyo, nitachukua zaidi ya miaka 20 kumaliza maboma yangu. Niiombe Serikali, kwenye bajeti hii watuongezee ili wananchi wanapotoa nguvu zao basi waone matokeo kwa uharaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru, niachie wigo na wenzangu waendelee kwasababu niliomba tu dakika tano na wewe umenipa. Ahsante, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niwe mmoja wa wachangiaji katika mjadala huu wa Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga mkono hoja kwa sababu tangu asubuhi Mheshimiwa Waziri amewasilisha bajeti yake ya Wizara ya Maji na nimepitia alhamdulilahi Jimbo langu la Igalula nimeona vijiji vingi. Namshukuru sana Naibu Waziri na Waziri wake, kweli Jimbo la Igalula tunakwenda kwenye mapinduzi ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki iliyopita kupitia Bunge lako hili Tukufu katika maswali ya nyongeza niliuliza Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria unaotekelezwa kwenye Jimbo langu la Igalula katika Kata za Goweko, Igalula, Nsololo na Kigwa. Nikasema mradi ule utekelezaji wake umesimama na nikaiomba Serikali iweze kunipatia fedha kwa sababu umesimama kutokana na kutokuwa na fedha. Kwa Serikali Sikivu ya Chama cha Mapinduzi niliweza kuletewa shilingi bilioni moja ili mradi ule uanze utekelezaji wake wa kupeleka maji katika Jimbo langu la Igalula.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna changamoto katika mradi huu. Nimshukuru Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Tabora ameweza kuuzungumzia. Mradi wa Ziwa Victoria katika Mkoa wetu wa Tabora Jimbo la Igalula halikuwepo katika mpango. Wakati kampeni tulivyokuwa tunanadi sera alipokuja Hayati Dkt. John Pombe Magufuli tulimuomba Jimbo la Igalula liingizwe katika mpango wa kupelekewa maji ya Ziwa Victoria naye alipokea na akatoa maagizo na ule mradi ukawekwa katika mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi ule ni mkubwa sana, unakwenda takriban vijiji 16 vilivyoko katika maeneo hayo na una vituo 100 lakini tangu tumeubariki mradi ule mpaka saa hizi na malengo ya kukamilika mradi kufikia mwezi Desemba, 2021 sasa hivi tuko mwezi wa tano nikuambie kupitia Bunge hili mradi ule umekamilika kwa asilimia 10. Tumekuwa tukifanya ziara mbalimbali kuuliza kwa nini mpaka saa hizi tunakwenda taratibu na wananchi wana hamu na shauku ya kupata maji kutoka Ziwa Victoria, wanasema tatizo ni fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekwenda kwa Mheshimiwa Waziri mara nyingi sana, mradi ule ni wa kiasi cha shilingi bilioni 11 mmetupelekea shilingi milioni 900 ya kwanza mkatuongezea shilingi bilioni moja na kwenye bajeti hii nimeona mmeweka shilingi bilioni 1.4 kwa maana kwamba huu mradi utakwenda kukamilika baada ya miaka mitatu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hebu aliangalie Jimbo la Igalula kwa sababu tangu tumeumbwa hatujawahi kufungua maji yanayotokana kwenye koki. Kwa hiyo, wananchi wa Jimbo la Igalula, kupitia kata hizo nne watafurahi sana huu mradi ukikamilika kama ulivyopangwa Desemba, 2021. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu nina changamoto kubwa sana ya maji na mlifanya juhudi za makusudi kututolea maji ya Ziwa Victoria kuyaleta Tabora, ni umbali mkubwa sana lakini mlitambua kuwa ardhi na eneo letu la Mkoa wa Tabora upatikanaji wa maji ya kuchimba kwa kutumia visima ni mgumu sana. Nimwombe Mheshimiwa Waziri katika kuibua vyanzo vya upatikanaji wa maji hebu tubuni mbinu mbadala kwa haya maeneo ambayo yamekuwa yana changamoto ya uchimbaji wa visima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimboni kwangu mimi naishukuru Serikali imechimba visima vingi lakini vinafanya kazi kwa miezi miwili, mitatu ni kwa sababu ardhi yetu ina miamba haina maji. Vilevile mmekuwa mnapoteza fedha nyingi, mkandarasi mnampa tenda ya kuchimba visima anawaambia eneo hili lina maji akienda kuchimba anasema maji yalikimbia yakahamia upande mwingine sasa fedha inapotea, haileti tija kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali tubuni vyanzo vingine, kwetu tuna majaluba mengi sana, kuna mikondo mingi ya maji yamekuwa yanaleta mafuriko kwa nini tusiyavune haya maji tukatengeneza mabwawa makubwa. Tukiweka bwawa pale katika Kata yetu ya Kizengi ninyi wenyewe mashahidi wakati wa masika kabla hatujatengeneza barabara ya Chaya - Nyaua ilikuwa kila mwaka barabara inakatika eneo la Kizengi kwa sababu ya maji mengi lakini tungebuni pale yale maji yasiende barabarani yakategwa yangeweza kusaidia hata katika shuhuli za kilimo siyo tu matumizi ya binadamu. Katika eneo letu hasa Mkoa wa Tabora Jimbo la Igalula naomba Wizara ibuni vyanzo vingine vya upatikanaji wa maji maana yapo kwa sababu kila msimu mvua inanyesha na maji yanakuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mradi katika Kata yangu ya Tura alishawahi kuja Waziri wa wakati huo Mheshimiwa Prof. Mbalawa Machi, 2019. Alivyokwenda kwenye Kata ya Tura alikuta kuna bwawa ambalo liliachwa na mkoloni ambalo linatumiwa na Railway Station akasema hiki ni chanzo kizuri pale pale akatoa shilingi milioni 300 ili wananchi waanze kutumia maji katika Kijiji kile cha Tura. Wakaahidi baada ya miezi mitatu maji yataanza kutumika katika Kijiji cha Tura leo mwezi wa 18 maji wananchi wa Tura wanayasikia kwenye redio tu, hawajawahi kutumia maji yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sisi tumeenda kufanya ziara pale tukimuuliza mkandarasi anakuambia tulipewa shilingi milioni 300 mradi wa shilingi milioni 800, kwa hiyo tunasubiri shilingi milioni 500 zingine ili tuweze kuukamilisha. Sasa tunakuwa tunamlaumu mtaalamu, engineer tunaanza kumpigia kelele lakini ukija kuangalia tatizo lingine huku fedha Serikalini hazijatoka. Niiombe Serikali ule mradi ni mzuri sana, ni bwawa kubwa sana lina maji mengi tukiutengeneza vizuri hata wananchi wangu wa Vijiji vya Kalangasi, Malema, Kizengi, Maguliati na Migongwa wanaweza kupata maji kwa sababu ni chanzo kikubwa ambacho waasisi wetu walituachia. Katika bajeti hii nashukuru vijiji vyangu vingi umeniwekea fedha lakini kwenye hii miradi inayoendelea hasa ya Ziwa Victoria na ule mradi wa Tura, naomba aniongezee fedha ili niweze kukimbia na wananchi waweze kuona matunda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini namshukuru Mheshimiwa Waziri amenipa visima sita katika Kata za Mmale, Mwaokoyesengi, Migongwa, Mbulumbulu na Misole. Kwa hivi visima amasema atanipa shilingi milioni 156 huyu mkandarasi anayekuja wamlipe baada ya kutumia maji ndani ya miezi sita asije akaniachia mashimo halafu akaondoka na fedha zikaondoka. Anapokuja kuchimba visima katika haya maeneo ambayo umeniainishia tuone tija ya wananchi wetu ya upatikanaji wa maji kwa sababu tunajua kabisa upatikanaji wa maji kule ni tatizo asije akachukua hizi fedha kwa sababu wamezileta akadhani ni gombania goli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Waziri yeye ni mkali asimamie haya, wamekuwa wakichimba wanaacha visima havitoi maji na ushahidi upo. Kila siku mnatenga hela za ukarabati wakati visima havitoi maji na penyewe mpaangalie, haiwezi kuwa kila siku tunakarabati kisima halafu hakitoi maji wawaambie visima vinavyotoa maji viko wapi? Katika Jimbo langu la Igalula labda bomba moja au mawili ndiyo yanayotoa maji lakini kwenye takwimu za Waziri unaweza kukuta zaidi ya mambo 40 lakini hayatoi maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji ni uhai maana binadamu kila siku lazima atumie maji, akila chakula atatumia maji, ni lazima tuliangalie hii sekta katika kipaumbele chake. Nakuomba Mheshimiwa Waziri mradi wangu wa Ziwa Victoria wananchi wa Igalula, Kata za Kigwa, Goweko, Nsololo na mimi nimekuwa nikikuambia kila mara mzee nisaidie na kweli nisaidie nipelekee maji kwenye vile vituo 100 ambavyo umeviandika kwenye bajeti hii wananchi wanasubiri maji kwa hamu ili akina mama wapumzike kuamka alfajiri na kwenda kutafuta maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo na mimi niunge mkono hoja, ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia Wizara hii ya Ujenzi na Uchukuzi ambayo imewasilisha hotuba yake leo asubuhi. Kwanza nianze kwa kuipongeza Serikali na Wizara kwa ujumla kwa kujenga Barabara ya Chaya - Nyahua ambayo ilikuwa ni kero kwa wakazi wa Mkoa wa Tabora, lakini nishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuikamilisha kwa asilimia 100 ambayo ilikuwa katika Jimbo langu la Igalula, wananchi wa Igalula wanashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii imetoa fursa kwa watumia barabara hasa wa Mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mwanza badala ya kupita Igunga sasa wanapitia Jimbo la Igalula. Nitoe wito wanapopita katika Jimbo la Igalula tuna migahawa mizuri sana wakifika Tula pale kuna mama mmoja anaitwa mama Tausi, wakifika wapite pale kuna kuku wa kienyeji, anajua kuwapika vizuri. Vile vile wakipita Kizengi pale kuna mgahawa mmoja unaitwa Tula Mgahawa, basi mambo yanakuwa mazuri. Naibu Spika nawe karibu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya shukrani zangu hizo nirudi, mkandarasi amemaliza ujenzi wa barabara, Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi nilikwishamwandikia barua ya kumwomba majengo yale ya Kizengi. Naomba wakimaliza na wakakabidhi mradi, basi naomba yale majengo waikabidhi halmashauri yangu ili tuweze kufanyia utaratibu mwingine hasa tuweze kupata kituo cha afya kwa sababu Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi imetuelekeza tutajenga vituo vya afya kwa kila kata. Kwa hiyo, wakinikabidhi yale majengo nitayatumia kwa ujenzi wa kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nichangie baadhi ya mambo kidogo, pamoja na mazuri wanayoyafanya Serikali lakini bado tunachangamoto ya upatikanaji wa barabara. Kuna Kamati iliundwa ya Mapitio ya Barabara, sasa hii kamati ilivyoundwa ilikuwa inaenda kuzitambua barabara ambazo zinatekelezwa na TARURA, lakini mpaka leo kamati hii imekwishamaliza kazi, lakini hatujui hizi barabara ni lini zitaingizwa kwenye mfuko wa upatikanaji wa fedha wa barabara.


Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, kwangu kuna barabara ambazo ni uchumi, ni muhimu sana katika maeneo yangu, zinaunganisha wilaya na wilaya, lakini zingine zinaunganisha mkoa na wilaya nyingine ndani ya mkoa mwingine. Kwa mfano, kuna Barabara ya Makibo – Msololo – Goweko - Kamama mpaka Nyahua. Hii barabara ina zaidi ya kilometa 80, tunapoisema barabara hii ni muhimu sana kwa sababu inatoka katika Wilaya ya Sikonge inakuja katika Wilaya ya Uyui. Tukisema itekelezwe na TARURA haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzoni tulikuwa tumeweka utaratibu mzuri wa kuainisha hizi barabara, tunazipandisha hadhi TANROAD wanafanya utaratibu mzuri wa kuweza kuzitengeneza, lakini utaratibu ule Wizara waliukataa, wakasema hizi barabara zitekelezwe na TARURA. Leo wilaya yangu inapata bajeti ya TARURA 1.2 bilioni, ukisema utekeleze hii barabara yenye kilometa 80, tutakuwa tunawaonea TARURA. Niombe Serikali ni ile ile, TARURA ni ile ile, niombe Waziri atakapoongeza fedha kwenye Mfuko wa TARURA hata kwa emergency, basi atakuwa ameokoa wananchi wa Kata ya Jimbo la Igalula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Barabara ya Sikonge inakuja Igalula inatokea Goweko, nayo barabara ni nzuri sana kwa uchumi wa wananchi wa Sikonge na wananchi wa Jimbo la Igalula, Wilaya ya Uyui. Leo Mheshimiwa Kakunda akiwa anataka kwenda kufanya ziara kwenye kata moja inaitwa Makibo, lazima afike Tabora Mjini, baadaye arudi tena huku Makibo, ni kilometa nyingi sana anapoteza rasilimali mafuta, lakini angeweza kupita hii barabara basi angeokoa mafuta na hizo fedha zingine akaelekeza kwenye miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya barabara kila mahali ipo, lakini hizi barabara ambazo tunazozipigia kelele, Waziri anaweza kusema TARURA wanatekeleza kwa bajeti iliyopo kiuhalisia TARURA hawawezi kutekeleza bajeti hii. Nimwombe Waziri kupitia mafungu yake akipeleka TARURA fedha za dharura kule, basi wanaweza kuzifungua barabara hizi na hatimaye zikafunguka na wananchi wakaweza kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nije kwenye suala lingine ambalo ni kuhusu TRC, kwangu wananchi wanategemea sana uchumi kwa kupitia reli ya kati. Hata hivyo, tulikuwa tuna urekebishaji wa miundombinu ya reli ya kati ambayo walimtafuata mkandarasi akawa anatengeneza reli ya kutoka Manyoni kuja Tula, Malongwe ikaelekea Goweko mpaka Tabora Mjini. Sasa cha ajabu ninachokishangaa tulikuwa na miundombinu ya njia tatu katika Station ya Goweko, huyu mkandarasi badala ya kurekebisha reli akaanza kung’oa tena njia zingine, ameua njia zingine, zile reli hatujui amezipeleka wapi, sasa wananchi wa Kata ya Goweko wanauliza alikuwa anakuja kubomoa miundombinu au alikuja kurekebisha miundombinu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunategemea zile reli kwa kukuza uchumi wa wananchi wetu kwa kukata mabehewa na kupakia mizigo pale, lakini vile vile, train ikiwa inapita pale ikiweka njia mbili upishano wa train na train wananchi wetu wanapata biashara, lakini sasa leo imekuwa njia moja, train inasimama kwa dakika tano, wananchi hawafanyi biashara. Nimwombe Mheshimiwa Waziri tunataka kujua zile reli zimekwenda wapi? Wananchi wanahitaji pale reli ziwe za njia mbili train ipishane, mabehewa yakatwe, ili waweze kupata uchumi na pale sisi tunatengemea sana uchumi wa train. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, station ile pale tunategemea sana katika uchumi na abiria wapo wengi sana, lakini leo cha ajabu tangu shirika limeanza ile station hatuna choo cha abiria, abiria wakija pale wao wameshajisevia kutoka nyumbani wakifika pale hakuna huduma nyingine itakayoendelea. Kwa hiyo, tunaingiza fedha nyingi kupitia station ile, tunashindwa kujenga hata choo cha shilingi mbili na tuna kampeni nzuri ya choo bora, lakini station yetu kupitia Wizara yetu inashindwa kujenga choo. Niiombe Serikali yangu, Wizara yangu wakajenge choo pale gharama yake ni ndogo sana ili wananchi na abiria wanaowasafirisha wapate huduma nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna changamoto nyingine, Serikali imeleta umeme ambao ni Sh.27,000/=, lakini station ile imekuwa giza miaka yote na umeme upo, lakini mpaka leo tunashangaa kwa nini train zikipita usiku wananchi wanapata adha, pale kuna uwizi unaotokea wakati wananchi wanasubiri abiria iweze kuja pale, giza limekuwa kubwa Sh.27,000 mimi Mbunge wao nitalipa wakafanye wiring.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Naibu Spika, naam, muda umekwisha, jamani!

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi niwe miongoni mwa watu ambao watachangia Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza anianze kwa kumpongeza Waziri kwa kazi nzuri yeye na Naibu wake, Katibu Mkuu kwa kweli wanafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wananchi wetu wanapata mwanga ingawa kuna changamoto. Lakini pia niwapongeze viongozi wa REA, DG wa REA naye anafanya kazi nzuri kuhakikisha anasambaza umeme na sisi tunajivunia kuwa na DG huyu kwa sababu umeme kweli umefika katika vijiji mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo bado tuna changamoto nilipochaguliwa na wananchi wa Jimbo la Igalula nilikuja hapa kujua hatma ya vijiji vyangu ambavyo bado havijafikiwa na nishati ya umeme na uzuri Mheshimiwa Waziri alinijibu Bungeni na bado tukafanya naye safari ya kwenda kwa wananchi wangu kuwaambia lini umeme utawafikia wananchi wangu. Hilo nilikushukuru sana Mheshimiwa Waziri, tulifika katika Kijiji cha Izumba, Kata ya Miyenze na ulikuta watu wengi, walikupokea kwa furaha kwa sababu walijua wewe ulikuja na umeme. Lakini matarajio yao hayakuwa kama tulivyokuwa tumetarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka na naomba nikunukuu na siku ile tulikuwa wote wewe Waziri na Naibu wako na Mkurugenzi wa REA naye alikuwepo na Bodi yako yote ya REA ilikuwepo. Uliwaambia wananchi ilikuwa tarehe 16 Machi ukawahakikishia kufikia mwisho wa mwezi wa nne umeme Izumba utakuwa umewaka na ukawahakikishia ukasema leo umekuja na wakandarasi utawaacha pale pale ili waanze kuwasambazia wananchi umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ni mwezi Juni tarehe 2, 2021; wananchi wa Izumba hawajaona nguzo, yule mkandarasi tulivyoondoka na yeye akaondoka, sasa hivi amebaki anakwenda anaondoka. Nikuombe Mheshimiwa Waziri tunamaliza Bunge tarehe 30 ya mwezi Juni, 2021 ninakwenda ziara kule sasa kama nikizomewa ujue umenisababishia wewe ule mzomeo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nikuombe Mheshimiwa Waziri kwa hizi siku chache naomba uniwashie umeme, nikiunganishi kati ya wananchi na Serikali, ninapokwenda kule tena kuwaambia nitaenda kuiambia Serikali wakati Serikali ndiyo niliipeleka kweli Mheshimiwa Waziri utanipa wakati mgumu mwisho wake na mimi nitakuwa upande wa Serikali nikabaki nashangaa kauli ya Serikali haijatimizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri, wananchi wa Kata za Miyenze, Tura, Miswaki na Lutende wote wanahitaji na wanamatumaini makubwa ya kupatiwa umeme, naomba uwasaidie kwa sababu ulitoa kauli hiyo kwa bashishi kubwa na wao wakakupigia makofi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali kutupelekea umeme, mkandarasi amekwenda kwenye baadhi ya vijiji ameenda kuwashirikisha Waheshimiwa Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji wakisema jiandaeni umeme unakuja. Lakini mkandarasi anasema mimi nitaleta umeme, nitasambaza kilometa moja tu kwenye kijiji.

Mheshimiwa Spika, mimi niiombe Serikali pamoja na nia njema ya kupeleka umeme, msitupelekee mgogoro mwingine ambao utazalika ndani ya mgogoro mwingine kwa sababu unapopeleka kilometa moja na mkaweka idadi ya watu labda 20 wataunganishiwa wakati watu ambao wapo tayari kuunganishiwa umeme zaidi ya 20.

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali kama yule mkandarasi mnampa mkataba wa kilometa moja muwe mna fedha za ziada anapomaliza kilometa moja TANESCO anaanza kazi ya kuunganishia wateja wengine ambao waliobaki. Leo unaponiambia mji kama wa Kata ya Tura unapeleka nyumba 20 nani umpelekee nani usimpelekee, Mji katika Kata ya Miyenze unapeleka nyumba 20 nani umpelekee na nani usimpelekee; wale wote ni wapiga kura. Niiombe Serikali itusaidie hii scope iongezwe kidogo kutoka kwenye kilometa moja basi angalau kwenye kijiji ifike hata kilometa tatu au nne itakuwa imetusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna changamoto moja ambayo Serikali maana kwamba Wizara na TANESCO wanacheza ngoma mbili tofauti. Leo Serikali inatuambia mwananchi akilipa shilingi 27,000 anaunganishiwa nishati ya umeme. Lakini ukienda kwenye uhalisia sivyo mwananchi analipa shilingi 27,000 unakuta nishati ya umeme iko zaidi ya kilometa moja huyo akilipa shilingi 27,000 kweli kiuhalisia atapata umeme?

Mheshimiwa Spika, ukienda TANESCO anakwambia sina bajeti, siwezi kupeleka umeme kwa sababu inahitaji nguzo zaidi ya kumi, sasa TANESCO hujampa fedha na amepokea fedha ya mteja, unapotoa kauli kama Waziri kusema shilingi 27,000 wananchi wanataka kweli kulipa shilingi 27,000 wapate umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe Serikali hebu kuweni na dawati maalum la kutoa elimu. Ile shilingi 27,000 ukomo wake uko wapi, je, kama kuna ziada muda gani wa kusubiri ili ninyi mjipange muweze kufanya hiyo kazi ya kumuunganishia umeme, kuliko sasa hivi imekuwa vurugu match. Leo hii Kata ya Goweko kuna umeme jazilizi ambao umepelekwa kule mradi ambao nilikuomba Mheshimiwa Waziri. Lakini wamepeleka kwa idadi ya nguzo 35 zimekamilika, lakini wananchi bado na wameshalipa shilingi 27,000 wanasema sasa sisi tunafanyaje, wameenda TANESCO wanaambiwa sisi hatuna bajeti. Nikuombe Goweko pale tuongezee nguzo zingine kwa sababu ulisema hii kauli na wenyewe wanaisimamia hata kama ipo nje ya ule mkataba mimi nikuombe sana nisaidie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nirudi sasa kwenye sekta ya mafuta; kwanza niipongeze Serikali kwa jitihada zake za kuchukua jukumu la kuweka vinasaba, niipongeze sana, mlipoipeleka TBS kule mmefanya uamuzi mzuri na sisi kama Wabunge tulitoa hilo kwa sababu kuiona kampuni inanufaika kushinda Serikali na ndiyo maana tukasema hivi vinasaba tuviweke wenyewe. Nikiri tu ni mdau mzuri wa mafuta katika sekta hii naomba nishauri jambo moja. EWURA wanafanyakazi nzuri sana, lakini wao nao wana changamoto, leo EWURA amekuwa akienda tu sehemu kama kuna makosa, haulizi hata kosa limetokana na nini yeye kazi yake ni kufungia tu kituo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa sijui ndiyo wamesoma professional ya kufunga tu, lakini wao hawajikagui kama wana upungufu, wenyewe wanaona wafanyabiashara ndiyo wana mapungufu. Mimi nitoe ushahidi kidogo juu ya EWURA wanavyofanya leo tunasema vinasaba viwekwe kwenye mafuta, lakini mafuta yaliyowekewa vinasaba na ambavyo havijawekewa vinasaba kwa mteja wa kawaida hajui kitu chochote, hata mwenyewe sijui mafuta yapi yamewekewa vinasaba na yapi hayajawekewa vinasaba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo akija yeye na machine yake ndiyo anaiamini kama Msahafu au Biblia akiweka pale ikikataa anasema hii ina vinasaba kidogo haijafikia kile kiwango. Sasa hicho kidogo nani aliweka? Na ikiwekwa inaoneshaje kama imewekwa kidogo? Nikuombe Mheshimiwa Waziri na hili naomba ulichukulie u-serious hawa jamaa wanasumbua sana wafanyabiashara yaani wamekuwa wao ndiyo miungu watu wakifika pale funga kiri hapa kuwa nimekuta kuna kosa na kama nataka nifanye biashara na kiri haraka haraka nikulipe faini yako tuachane kisalama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini unakuta muda fulani wameonea ukichukua yale yale mafuta ukaenda kupima machine nyingine inaleta kipimo tofauti ya kwao ya kwanza, wamepima na wamekufungia na wamekudhalilisha imesema inamakosa, umeenda kwingine ipo sawa ukirudi huku wanasema aisee kanuni ya fidia hamna wewe endelea kufanya biashara. Badilisheni hizi kanuni la sivyo wajiangalie na wao na siye tutakuja siku moja wakaja wakakutana na magumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hapa watu wamesema vituo vya vijijini vipunguziwe masharti ni kweli, leo mnaruhusu watu kulala na petrol mnashindwa kumruhusu mtu haraka haraka aweke mafuta pale nje pump moja mnaweka mavibali mengi, yaani kibali kukamilisha kupata shell ya mafuta yaani uwe na siyo chini ya shilingi milioni 30. Sasa kwa mwananchi wa kijijini ukimwambia milioni 30 anaipata wapi? Kuna teknolojia zimekuja nyingi kuna kontena linatembea yaani ukiweka kontena…

SPIKA: Ahante sana.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Spika, huku ndiyo kulikuwa panoge, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi hii kuwa miongoni mwa watu ambao watachangia bajeti kuu ya Serikali, iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha. Kwanza nianze kuipongeza Serikali, nimpongeze Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, kwa muda mchache ameleta bajeti yenye matumaini makubwa kwa wananchi, kwa sababu wananchi wetu walikuwa na kero kubwa sana juu ya maendeleo yao sasa hata kodi zetu ambazo tunakwenda kuzilipa zitaleta tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanachi walitaka hatima ya maboma ambayo wanayaanzisha yaweze kukamilika, pia kwenye bajeti hii imejipambanua wazi kabisa kuwa maboma yetu yanakwenda kukamilika na watu wataanza kupata hudama, hongereni sana Serikali. (makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watanzania wanahitaji kulipa kodi, lakini waione kodi yao inafanya kazi. Leo tumeleta mpango wa kufuta baadhi ya kodi na kuongeza baadhi ya kodi, lakini inahitajika elimu iongezeke zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunaishukuru Serikali kwa kupunguza tozo au faini ambayo ilikuwa ilikuwa inatozwa kwa watu wa boda boda wanashukuru sana, na tumekuwa tunapokea simu hasa mimi kutoka jimboni wanasema mmetupunguzia faini lakini mmeongeza fedha kwenye mafuta, ukiangalia uhalisia fedha kwenye mafuta haijaongezwa ni utaratibu wa kawaida ambao ulikuwa tangu zamani, na wananchi wanaona mafuta yamepanda zaidi kwa kipindi hiki kifupi, basi wanajua fedha sasa Serikali imepunguza faini imekuongeza kodi kwenye mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali, tunapokuwa tunafanya hivi vitu basi tuongeze na wingo wakutoa elimu. Kwa mfano watu wa mamlaka inayohusika na upandishaji wa bei za mafuta, basi wanapokuja kupandisha au kushusha wanatakiwa watoe taarifa kwa wananchi ili waweze kujua tumeongeza kwa sababu gani au tumepunguza kwa sababu gani, ili tuweze kupunguza haya mengine ambayo wananchi wanashindwa kuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze kwa kupunguza faini kutoka shilingi 30,000 mapaka shilingi 10,000, mmewasaidia sana boda boda na Mheshimwia Waziri ulisema hapa unahitaji boda boda wasiwe ndio chanzo cha mapato ya Serikali, unahitaji Polisi wafanye kuwaelimisha boda boda ili wesiwe miongoni mwa wavunja Sherika. Nikupongeze sana, maana Polisi walibadilika kuwa mungu watu. Sisi kwetu kule boda boda ndio ambulance ya kupeleka wangojwa, ili mgonjwa aweze kukaa vizuri kwenye pikipiki lazima ubebe na mtu mwengine wa kumshikilia, ukikutana na Polisi anawaza tu yeye kutoza faini, sasa ilibadilika kuwa ni kero kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kuipunguza hii imetusaidia sana. Na mimi niiombe na nimuombe Waziri wa Mambo ya Ndani, Polisi wetu watusaidie sana kuwapa watu elimu. Unajua kuna mazingira mengine hayahitaji hata faini, unaweza kukutana na mtu amevunja taa kwa bahati mbaya wakati huo huo umekutana naye anakwambia gari lako bovu, ukumwambia nimevunja sasa hivi anakwambia hamna lete nikupige faini, wakati ilikuwa ni kitendo cha kuweza tu kumwambia, changamato hii nenda kairekebishe, hilo litatusaidia sana na litatupunguzia malalamiko kwa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa Madiwani, niipongeze Serikali kwa kulibeba jukumu hili ambalo lilikuwa ni kero kwa madiwani wetu. Madiwani kero kubwa ilikuwa ni kupata ile stahiki yao kwa wakati, ilo sasa Serikali mtakwenda kulifanya kwa utumilifu, kwa uhakika mkubwa kwa sababu Serikali ikipanga jambo lake na likiingizwa kwenye bajeti basi haliwezi kukwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Madiwani walikuwa hawahitaji kulipwa ile pesa kwa wakati tu, bali walikuwa wanaomba waongezewe posho, kiukweli sisi wenyewe tunajua tukirudi kule majimboni tunakuwa sisi wenyewe ni madiwani, wananchi wote wakiwa na matatizo basi kabla hawajaenda sehemu yoyote basi wanamkimbilia Diwani, wanamkimbilia Mbunge, wanakimbilia sehemu zengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali. Kwa kuwa tulimebeba hili jukumu basi tuone namna gani ya kuwasaidi hawa Madiwani. Na pia tumepata changamoto nyengine, kuna muongozo ulikuja kule kuna Madiwani wamekuwa wakikatwa posho zao, leo tunakwenda kulalamika kumkata Diwani shilingi laki moja na ishirini eti kwa sababu anakaa Makao Makuu ya Halmashauri, hiyo imeleta changamoto sana, majukumu ya Diwani ni yale yale, ni sawa sawa na mbunge anaetoka Kongwa, anaetoka Bahi ukamkata usimlipe per diem, hiyo sasa siyo sawa kwa sababu wale wadiwani wanaposafiri kwenda pale wamebeba dhamana ya wananchi wao kutoka kwenye kata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali, tuwaangalie madiwani wanamajukumu makubwa sana kama tulivyo sisi, tunapokwenda kuwapunguzia posho zao. Kwanza posho ni ndogo, unaenda kupigana nae kwa shilingi laki moja, anafanya kazi kubwa, anapitisha mapato yote ambayo yanatekelezwa katika halmashauri. Kwa hiyo, niombe Serikali itusaidie hili nalo litoe muongozo, kwa sababu wamekuwa wakigombana na wakurugenzi, wakurugenzi wanaosimamia sheria, inakuwa imeleta tabu. Kwa hiyo, niiombe Serikali iweze kutusaidia katika hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lengine kuhusu tozo za simu. Serikali imekuja na nia njema sana katika kukusanya kodi kwa kupitia simu zetu, niiombe Serikali. tumekuwa tukifanya miamala tunalipa mara mbili mbili, leo ukitaka kutuma milioni moja kwanza wewe unaetuma unakatwa shilingi elfu nne, yaani unatuma kwa mtu akapate hela wanakatwa elfu nne, akifika tena yule mtu kabla hajaitoa anakatwa elfu nane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali kama mnataka kuitoza vizuri hii kodi, wale makampuni tunahitaji waendelee ku-survival katika ufanyaji wa biashara, basi kama inakatwa ile ya kutumia iwe ya Serikali, ile nyingine iwe ndio iwe makato ya kampuni na wale wengine watoa huduma, kwa sababu unakuta milioni kuituma na kuitoa zaidi ya shilingi 12,000. Serikali inaenda kupata haifiki hata elfu tatu, sasa zingine zote zinapotelea hewani hewani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe Serikali. Tumekuja na mpango mzuri lakini kuna sehemu kuna linkage hasa hii mitandao ya simu, imekuwa kero kwa sababu wanaongeza tu yaani makato yamekuwa yanaongewa kiaina aina tu hata haieleweki. Leo wanakwambia kufikia 5599 ikifika tu na kamili ile wanaongeza tena 300 zaidi ya ile kilichokuwa. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie hili suala, na ndio maana tulikuja hapa kwenye uchangiaji wa sekta ya mawasiliano, tulisema tuimarishe shuirika letu la TTCL, haya yote hayatokuwepo, lile shirika ni la Serikali asilimia mia moja, haya makampuni mengine yapo kibiashara na hii tukiimarisha shirika letu linaweza kutusaidia hata tozo zenyewe za makato yakapungua, watu wakapiga simu vizuri, Serikali ikapata fedha zake vizuri bila ya hata kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Serikali, kwa kuwa imekuja na mpango huu mzuri tuangalie na sehemu zinapo-link haya matatizo yanayotokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja, nakushkuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia angalau dakika tano nami nitoe mchango wangu katika Mpango huu wa Serikali. Awali ya yote nianze kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kupambana kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma nzuri. Fedha hizi zilizoletwa katika historia nilikuwa naona mikopo mingi inakwenda kwenye miradi ya Kitaifa, lakini mkopo huu umekwenda kuwagusa wananchi wa chini zaidi hasa wa vijijini. Tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi nyingi, tunakwenda kujenga madarasa, shule na mbiundombinu mbalimbali ya afya; lakini tujiandae na mambo mengine ambayo yatajitokeza hususan kwa watumishi wetu. Kwa hiyo, naiomba Serikali katika mpango wao ambao utakuja kwenye bajeti ijayo, iangalie namna gani ya kutusaidia kuongeza watumishi hasa katika Sekta ya Elimu. Madarasa ni mengi, idadi ya wanafunzi ni kubwa lakini idadi ya walimu ni ndogo. Kwa hiyo, naiomba Serikali ije na mpango huo wa kuweza kuongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kuchangia Mpango. Serikali yetu katika Mpango wake ambao ulikuja mwaka 2020, wa miaka mitano, ilituelekeza itakwenda kujikita kwenye Sekta ya Kilimo, nami wananchi wangu wengi ni wakulima. Mpaka sasa hivi, Serikali imekaa kimya, haijatoa mwongozo wa nini kinakwenda kutokea juu ya ongezeko la bei ya mbolea. Tumekuwa na kigugumizi, hatujapata bei elekezi mbolea ni shilingi ngapi? Tunakwenda kwenye msimu ambapo mvua kwenye baadhi ya mikoa imeshaanza. Leo hii tunapokea simu kutoka kwa wananchi, wanauliza nini kilichotokea? Nasi hatuna majibu.

Naiomba Serikali isimame mbele, itoe mwelekeo na dira kwa wakulima kwa sababu msimu umeshaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mbalimbali ya kuisaidia Sekta ya Kilimo, naishukuru Wizara ya Kilimo inaendelea kupambana, lakini kuna mpango walikujanao wa kuwakopesha wakulima matrekta. Katika mkoa wangu na Jimbo langu wapo wananchi ambao walikopa. Ile mikopo ilikuwa ni kichefuchefu. Yamekwenda matrekta hayalimi hata nusu eka kwa siku, lakini wamekwenda kukopeshwa, na wale waliowakopesha kupitia Wizara ya Kilimo hawafuatilii changamoto gani wanazozipata kwenye kukusanya madeni. Wamekwenda TAKUKURU, eti TAKUKURU wakakusanye madeni. Sijawaji kuona aliyekopesha ni mwingine, anayekwenda kukusanya ni chombo kingine cha Serikali tena kikubwa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, yale matrekta ambayo yalikuja kule, wananchi wameyapaki. Agizeni vyombo vyenu mkachunguze.

MWENYEKITI: Aina gani Mheshimiwa, hayo yanayolipa nusu eka kwa wiki.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, yanaitwa Ursus yametoka NDC. Yale matrekta nusu eka hayalimi. Kwa hiyo, naiomba Serikali, wananchi wangu wameyapaki, hawayatumii tena, wanahitaji wavunje mkataba. Wale jamaa wanapigiwa simu hawapokei. Nendeni mkachukue trekta zenu, mkataba uishe. TAKUKURU hawataki kuwaona huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tusaidie wakulima wetu katika maeneo yetu, lazima kama Serikali tuone namna gani ya kuweza kuwasaidia hususan kuwaletea zana bora za kilimo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)