Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. George Ranwell Mwenisongole (4 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kusimama katika Bunge hili Tukufu la Kumi na Mbili, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwanza kwa kutuwezesha kufika hapa salama na kutuwezesha sisi kushinda uchaguzi mgumu uliopita.

Mheshimiwa Spika, vile vile napenda niwashukuru wananchi wa Jimbo langu la Mbozi Mkoa wa Songwe na Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniamini na kunichagua mimi kuwa Mbunge. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja. Hotuba hii ya Mheshimiwa Rais sio tu ni dira kwetu sisi Wabunge, nafikiri ni mwelekeo kwa miaka mitano ijayo kwa Taifa letu. Kuna jambo moja ambalo ningependa nijikite ambalo nikuhusu kilimo. Chama chetu Cha Mapinduzi kwa nia njema kabisa kilileta hii sera ya ushirika kwa nia ya kumsaidia mkulima mmoja mmoja ili awe na uhakika wa masoko na bei yake.

Mheshimiwa Spika, katika maeneo mengi vyama hivi vya ushirika nahisi sijui vina mapepo au vimevamiwa na majambazi, sielewi! Sijaona mahali ambako vyama vya ushirika vimefanya vizuri. Ukienda Kagera, ukija Mbozi, ukienda Mbinga kote ni malalamiko hayo hayo yanayofanana. Kwangu mimi kwenye Jimbo langu la Mbozi vyama hivi vya ushirika sisi kule tunaita AMCOS, huwa wakulima wanapeleka kahawa. Kule kwetu Mbozi, sisi kahawa ndiyo kama dhahabu, sisi hatuna zao lingine tunalotegemea zaidi ya kahawa. Sasa wakulima wakishapima kahawa yao, hawa viongozi wa AMCOS wanachofanya, wanakwenda benki kuchukua mkopo bila wale wakulima wengine kwenye vyama vile vya msingi kujua kwamba wale viongozi wamechukua mkopo. Matokeo yake sasa benki inapokuja kufanya malipo inafyeka yale malipo na kuwafanya wakulima waishi katika hali ya umaskini. Hii hali imeendelea kwa kipindi kirefu sana.

Mheshimiwa Spika, napenda nishukuru juhudi ambazo zimeanza kuchukuliwa sasahivi naOfisi ya TAKUKURU ya Mkoa, ingawa zimekuja kwa kuchelewa lakini bado hatua zaidi, ningependa tunapozidi kufikiria hili suala liingie kisheria. Hawa watu sio tu wafilisiwe nyumba zao, wafikishwe mahakamani na kufungwa. Nafikiri tukiamua kuwa wakali katika hili suala la ushirika na hawa viongozi ambao wanataka kuua ushirika, nafikiri tutakuwa tumemsaidia sana mkulima, kwa sababu kwa muda mrefu sana hawa viongozi wamekuwa wanaishia TAKUKURU tu, wanapewa ratiba ya kurudisha fedha zao, wengine wanahama miji, lakini bado hatujapata solution ya kudumu ya kuokoa maisha ya hawa wakulima ambao bado wanaishi katika hali ya umaskini. Kwa hiyo, napenda kuunga hoja hii ya hotuba ya Rais, lakini hili suala la viongozi waAMCOS ni lazima tuje na solution ya kudumu ili kuhakikisha kwamba wakulima wa chini wanalindwa kutokana na mazao yake.

Mheshimiwa Spika, kingine napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Rais, wakati wakampeni alikuja kwenye Jimbo langu la Mbozi na mimi binafsi pamoja na watu wengine tulimweleza shida ya wafanyabiashara pale Mlowo, Vwawa na Tunduma wanavyopata shida na TRA. Rais alikuja tarehe Mosi Oktoba, siku ya Alhamisi. Siku ya Jumatatu yake tarehe 4 alimtuma Kamishna waTRA aje pale Mbozi. Kinachotokea, TRA badala ya kuwa rafiki wanachofanya wakikutana na mfanyabiashara wanamkadiria makadirio ya juu kwa mapato yake, kodi ya juu sana kuliko uwezo wake ili tu akae nao mezani waweze kupata kitu chochote.

Mheshimiwa Spika, matokeo yake ni kwamba TRA imekuwa kama ni fimbo kwa wafanyabiashara na hili ni suala ambalo limekuwa kinyume na maono ya Mheshimiwa Rais. Rais wakati anazindua hili Bunge alisema kwamba angependa TRA na wafanyabiashara wawe marafiki, lakini mahali popote unapokutana na mfanyabiashara, adui yake mkubwa ni TRA. Kwa kweli hili ni suala ambalo kama kweli unataka kumsaidia mfanyabiashara na kuinua mapato ni lazima hawa maafisa wasio waaminifu wa TRA, washughulikiwe.

Mheshimiwa Spika,kwa hiyo kwa kusema hayo machache, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nianze kwa kuungana na Wabunge wenzangu kuipongeza sana Wizara ya Maji kwa juhudi kubwa walizozifanya kusambaza maji vijijini. Vilevile napenda niwapongeze RUWASA Mkoa wa Songwe hasa Meneja Injinia Charles Pambe kwa kazi kubwa anayoifanya, ingawa nasikitika kusema kwamba RUWASA, Mkoa wa Songwe hatuna gari, wamekuwa wakifanya kazi kwa kuazimaazima gari. Vilevile nimpongeze meneja wa RUWASA, Wilaya ya Mbozi Bw. Gratius Haule kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Wilaya ya Mbozi. (Makofi)

Mheshiniwa Naibu Spika, pamoja na juhudi hizi kubwa za Wizara ya Maji kusambaza maji huko vijijini juhudi hizi zinaweza zikawa bure kama Serikali haitaingilia gharama za kuunganisha maji vijijini. Katika ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi inasema kwamba kufika mwaka 2025 asilimia 85 ya wakazi wetu vijijini lazima wapate maji, lakini kwa gharama hizi ya shilingi laki nne laki tano kuungainishiwa maji, hivi mwananchi maskini wa kijijini hizi laki nne laki tano anapata wapi? (Makofi).

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wakulima mwananchi ataamua ni bora anunue mifuko ya mbolea kuliko kuunganishiwa maji, lakini kama gharama hizi zikishushwa zikawa sawa kama umeme wa REA ambao kuungaishiwa ni Shilingi elfu 27 tunaweza tukafikia sio tena asilimia 85 itakuwa ni asilimia 100. Ushauri wangu Mheshimiwa Waziri ni huu, wananchi waunganishiwe bure halafu wakate gharama za kuunganisha bure wanapokuja kulipia gharama za maji kila mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo kama wananchi wote wataunganishwa bure maji, halafu wakaja kuwakata mwisho wa mwezi wanapolipa bili yao ya maji, tunaweza kufika sio tena asilimia 100 hata asilimia 150, lakini bila kufanya hivyo hizi juhudi zote zitakuwa bure kama hatutaweza kushusha gharama za maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine Mheshimiwa Waziri kwa masikitiko makubwa wananchi vijijini wanalazimishwa kununua vifaa vya kuunganisha maji kwenye mamlaka za maji. Sasa nataka niulize hizi mamlaka za maji zina maduka ya kununulia vifaa vya kuunganisha maji? Kama sio udalali! Kwa sababu maduka hayo hayo wananchi ambao wangeenda kununua ndio hayo hayo ambayo hao Maafisa wa Maji ndio wanakwenda kununua hivyo vifaa. Sasa kuna sababu gani ya msingi kulazimisha wananchi kununua vifaa vya kuunganisha maji kwenye mamlaka za maji, kwa nini wasiende kununua kivyao wao wa-deal tu na gharama za kuunganisha maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ushauri wangu ni huu, kama kweli tuna nia yakutaka kusambaza maji na kuhakikisha maji yanafika kwa kila mwananchi ndani ya nchi yetu ya Tanzania, ni lazima gharama za kuunganisha maji ziwe ndogo. Kwa kufanya hivyo tutaweza kabisa kumaliza tatizo la maji ndani ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nikushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Kusema kweli ninaongea kwa uchungu sana kwa sisi watu wa Mkoa wa Songwe na kwa ujumla na mikoa hii ya kusini. Kiuhalisia niungane na Mbunge wa Newala ambaye ameongea kwa uchungu sana na ninashangaa kuona hata Wabunge wenzangu sijui mnaogopa nini kuongea ukweli katika hili jambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi Wabunge wa Mikoa hii ya Mbeya, Songwe, Liwale, Lindi tukiuliza hii barabara tunaambiwa barabara zenu zitajengwa kadri fedha zitakavyopatikana. Tukiuliza barabara, tunaambiwa barabara zenu Serikali inaendelea kutafuta fedha, lakini kuna baadhi ya mikoa hayo majibu hawayapati, wanaambiwa Mkandarasi amechelewa, barabara zenu hela ziko tayari, inakwenda kujengwa siku fulani. Sasa mimi nataka Waziri atuambie kuna kigezo gani mnatumia kugawa hizi fedha kwenye mikoa? Kwa nini mikoa mingine Wabunge tunapewa majibu kama haya? Hata sisi tunalipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya mambo ambayo amenifurahisha Mheshimiwa Rais Mama Samia, ni juzi alipofuta Sherehe za Muungano. Kwa mara ya kwanza aliamua kuzigawa zile hela za Muungano pasu kwa pasu; Bara na Visiwani. Sasa ninyi wasaidizi wake mjifunze kwamba hii keki ya Taifa hata mikoa yote igawanywe sawa. Ameshawapa somo! Sisi kwetu hii barabara ya Mloo - Utambalila mpaka Kamsamba upembuzi yakinifu uko tayari, usanifu wa kina uko tayari, nyaraka za tenda ziko tayari, lakini miaka yote kutenga fedha tenda itangazwe tunapigwa dana dana, lakini mikoa mingine barabara inatengewa usanifu wa kina, inatengenezwa kwa haraka kabisa. Hii siyo sawa mimi sioni kama sisi tunatendewa haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hili naomba Waheshimiwa Wabunge tuungane, hii keki ya Taifa tugawane sawa mikoa yote. Hata huko nako kuna Watanzania. Kwako pale, kuna barabara ile ya Mbeya mpaka Tunduma tumeambiwa itajengwa njia nne za pembeni; ni stori tu, hakuna. Tusipoangalia mpaka 2025 haitajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge ambao mikoa yetu haipewi kipaumbele katika hii bajeti, tuungane tuhakikishe tunambana Waziri atuambie aje na majibu halisi, kwa sababu kule nako kuna Watanzania.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa. Nataka kumwongezea kaka yangu George anayeongea hapa…

NAIBU SPIKA: Subiri kwanza, huongei kabla hujatambuliwa na Kiti. Haya sasa unaweza kusimama. Mheshimiwa Condester Sichalwe.

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. nataka kumwongezea taarifa Mheshimiwa

Mbunge wa Jimbo la Mbozi kwamba barabara pia anayoiongelea ya Mloo – Kamsamba – Chitete - Utambalila yenye kilometa 145.14 ni miongoni mwa barabara ya kimkakati kabisa katika mkoa wetu wa Songwe. Kwa hiyo, tunashangaa ni kwa nini Serikali haijatuingizia kwenye bajeti?

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni miongoni mwa barabara ambayo itatusaidia kuinua kipato sana kwenye mkoa wetu wa Songwe na ukitegemea ndiyo barabara ambayo inatoa mazao kupeleka nchi za jirani na kusambaza mkoa wote wa Songwe na sehemu nyingine.

NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa. Mheshimwa George Mwenisongole unapokea taarifa hiyo?

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kichwa na miguu na mikono naipokea hii taarifa. Hii barabara ndiyo uhai wa mkoa wetu. Kahawa yote inayolimwa Mbozi inapita kwenye hii barabara. Mchele wote, mpunga wote wa Kamsamba unapita kwenye hii barabara na ni kiunganishi kati ya mkoa wetu, Mkoa wa Katavi mpaka Tabora. Kama hii barabara itawekewa lami, malori hayana haja ya kupita Iringa kwenda Dodoma au Tabora, yote yatakuwa yanapita njia ya huku.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nashindwa kuelewa, kila kitu kiko tayari; nyaraka za tender ziko tayari, usanifu wa kina uko tayari, upembuzi yakinifu uko tayari, shida nini Mheshimiwa Waziri kututengea fedha? Kwa kweli tunahitaji majibu katika hili suala.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kusema hayo, mimi nikushukuru sana. Niungane na Mbunge wa Newala aliyesema anaunga hoja mkono kwa shingo upande, tusubiri majibu ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Nianze mchango wangu kwenye hii Wizara kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Spika, nimeingiwa na hofu sana baada ya kuisoma hii bajeti. Nimeingiwa na hofu kwa sababu hii ni bajeti ya kwanza tangu tutoke kuinadi Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2020 kwenye Uchaguzi ambao ulitupa ushindi wa kishindo sana kutoka kwa wananchi. Tuliwajaza matumaini makubwa sana wakulima na Watanzania masikini waishio vijijini kuhusu bei za mbolea na uhakika wa masoko; lakini katika hii bajeti ambayo nimeisoma zaidi ya mara tatu, sijaona hata mstari mmoja ambao unasisitiza kwamba Serikali itaweka mkazo kupunguza bei za mazao ya mahindi au kahawa. Sijaona mkazo wowote katika hii bajeti kuelezea uhakika wa soko la mahindi.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi kule kwetu Mbozi, debe la mahindi ni shilingi 3,000/=, gunia ni shilingi 18,000/= lakini mfuko wa mbolea ni shilingi 70,000/=. Sasa unategemea hawa wakulima ambao tumetoka tu kwenye uchaguzi wakatupa kura, watatuelewa vipi? Tunarudi tena mtaani hakuna solution ya bei za mbolea! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kati ya vitu ambavyo Bunge hili linaweza kufanya ni kuishinikiza Serikali at least kutoa bei elekezi za mbolea. Shilingi 70,000/= kwa mfuko wa mbolea ni kubwa mno, huwezi kulia eka. Tutakuwa hatuwatendei haki wakulima masikini ambao wametuamini wakatupa kura zao, lakini miezi sita baadaye, Bajeti ya Kilimo ambayo walikuwa wakiisubiri, haina majibu ya matatizo yao. Kwa kweli hili ni suala ambalo ni lazima Mheshimiwa Waziri aliingilie na kulitilia mkazo sana kuhakikisha bei ya mbolea na uhakika wa haya masoko unakwenda kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine, nimpe pole Mheshimiwa Waziri, kwa sababu kama Wabunge wenzangu walivyoongea, uzoefu unaonyesha fedha za bajeti ya maendeleo zinatengwa nyingi, lakini zinazokuja ni chache. Sasa sijui kuna miujiza gani ya hizo baiskeli na pikipiki alizowaahidi Maafisa Ugani? Sijui atazipata vipi wakati fedha za maendeleo hazipati? Sijui atajigawa vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli hili ni suala ambalo kama kuna kitu ambacho Bunge hili linaweza kufanya, shilingi bilioni 200 ambazo ni bajeti nzima ya hii Wizara, ni hela ndogo sana kwa Serikali ambayo inakusanya zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwezi. Sasa kuna ugumu gani kupeleka hizo hela zote? Kwa nini kila mwaka hii Wizara hela inazoomba kwa maendeleo huwa hazikidhi vigezo vyao? Kwa nini hawapelekewi hela zao zote wanazoomba? What is billioni 200 kwa hii Serikali ambayo inakusanya zaidi ya shilingi trilioni moja kwa mwezi? Kwa nini wasipelekewe zote? Ugumu uko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tuje na jawabu kuhakikisha hii bajeti, fedha zote walizoomba wanapelekewa kama kweli tuna nia ya kutaka kumsaidia mkulima masikini wa kule kijijini.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nataka niongelee hivi vyama vya msingi, AMCOS. Ni kweli kabisa kwamba vyama vya AMCOS ni Sera ya CCM na vilikuja kwa nia nzuri ya kutaka kumsaidia mkulima, especially wa kahawa kule kwetu Mbozi. Kwetu Mbozi hivi vyama vya ushirika vimegeuka kuwa kaburi kwa wakulima. Kwanza vinachukua mikopo benki bila wanachama wao kujua, unapofika wakati wa malipo, benki inakuja inakata hela zao na kuwafanya wakulima wale masikini kushindwa kupata malipo yao.

Mheshimiwa Spika, mpaka dakika hii ninapoongea hapa ndani ya Bunge lako Tukufu, kuna AMCOS zaidi ya tisa ndani ya Wilaya ya Mbozi hazijalipa wakulima wao. Watu wameshindwa kupeleka watoto wao shule, wameshindwa kulima, wametiwa umasikini wa ajabu na Serikali ipo, inaona.

Mheshimiwa Spika, siku moja nilishangaa hapa, posho zetu sisi Wabunge zilichelewa kwa siku mbili tatu, kulikuwa hakukaliki humu ndani. (Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge)

Mheshimiwa Spika, lakini wakulima wangu mimi Mbozi hawajalipwa mwaka sasa fedha zao za AMCOS na hakuna anayeshtuka.

SPIKA: Mheshimiwa Mwenisongole, hapo unamchokoza Spika. Unajaribu kuonesha kama kuna inefficiency hapa ndani, kitu ambacho siyo kweli. Futa hiyo kauli yako.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, okay, nafuta, lakini msisitizo wangu…

SPIKA: Hakuna cha lakini, unafuta halafu unaendelea kuchangia.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, okay, nafuta.

SPIKA: Eeh, endelea.

MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, point yangu ninayotaka kusema ni kwamba, suala hili la wakulima wa AMCOS kutokulipwa, nataka nitilie mkazo, kwa sababu hawa ni watu ambao wamepeleka mazao yao, wamepima, lakini mpaka leo hii hawajalipwa. Katika hali hiyo, suala hili hatuwezi kumsaidia yule mkulima.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, ninachoomba ni kwamba utakapokuja kuhitimisha bajeti, uje na majibu ya kuhakikisha kwa nini hawa AMCOS mpaka sasa hivi bado hawajalipa fedha zao?

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)