Supplementary Questions from Hon. Vincent Paul Mbogo (6 total)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri. Ukanda wa Ziwa Tanganyika akina mama wengi wanakufa kwa kutokupata huduma za afya, hasa upande wa ambulance boat kwa sababu kule miundombinu ya barabara hakuna, usafiri wao ni ndani ya maji na vijiji vipo vingi sana ndani ya Ziwa Tanganyika ambavyo vinatumia usafiri wa boti. Ni lini Serikali itapeleka ambulance boat kwa ajili ya kuokoa akina mama wajawazito? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba katika mwambao ule wa Ziwa Tanganyika kuna changamoto ya usafiri pale ambapo tunapata dharura za wagonjwa na hususan akina mama wajawazito ambao wanahitaji kwenda kwenye vituo vya rufaa kwa ajili ya huduma za upasuaji. Serikali imeendelea kuweka mipango ya kuhakikisha kwamba maeneo hayo ambayo yana changamoto kubwa za usafiri, hasa ambulance kwa maana ya ambulance boats, tunaendelea kuangalia utaratibu mzuri zaidi wa kutenga fedha kadri zitakavyokuwa zinapatikana ili tuwezeshe ufanisi wa rufaa katika maeneo hayo ili tuendelee kuokoa maisha ya wananchi katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo kwamba suala hili kama Serikali tunalichukua, tutalifanyia kazi na kuona namna bora zaidi ya kupata ambulance boat ili iweze kusaidia wananchi katika Jimbo la Nkasi Kusini. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuweza kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Nkasi ina kadiriwa na changamoto kubwa sana ya maji, ni lini Seikali itatoa maji Ziwa Tanganyika ambacho ndiko chanzo kikuu cha uhakika kuweza kutatua changamoto Wilayani Nkasi?
Swali la pili; Wilaya ya Nkasi katika Tarafa ya Nkate upo mradi wa maji ambao umekaa muda mrefu sana Tarafa ya Nkate ambao unahudumia vijiji vya Ntuchi, Ntemba, Siriofu na Ifundwa, mradi huu Mkandarasi hajalipwa ili aweze kumaliza mradi huu na ipo kesi ambayo anatuhumiwa mahakamani, naomba Wizara hii iweze kushughulikia kesi ya Mheshimiwa Felix Mkandarasi atoke ili aweze kumalizia mradi huu umekaa muda mrefu wananchi wanahangaika na maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo Mbunge wa Nkasi Kusini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, lini Serikali itatumia maji ya Ziwa Tanganyika kwa ajili ya kulisha katika Mji wa Nkasi wote. Serikali ya Awamu ya Sita katika vipaumbele vyake cha kwanza ni kuhakikisha kumtua ndoo kichwani mwanamama, kwa hivyo nataka nimhakikishie kazi kubwa imefanyika katika maji eneo la Ziwa Victoria kuyatoa na kuyapeleka Mikoa mbalimbali ikiwemo Tabora na kwingineko, kwa sasa kwenye bajeti hii ya 2021/2022 Serikali inaendelea kutafuta fursa ya kuona namna ya kuweza kusaidia na kwa hivyo hili la Ziwa Victoria naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge linaweza kuwa ni moja ya sababu ya kuweza kulifanyia kazi ili kuondosha hii adha inayowapata wananchi wa Nkasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili juu ya mradi uliokwama wa Kata ya Nkate jambo hili naomba nilichukue na mara baada ya kikao hiki kuisha tuje tulizungumze tulielewe tatizo lake ni nini na baadaye tuweze kulitatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Uchumi wa blue unafanana na mazingira mazuri kabisa sawa sawa na Ziwa Tanganyika. Je, Serikali ina mpango gani kama inavyofanya kwenye mazingira ya Bahari ya Hindi rasilimali zinavyopatikana baharini, vivyo hivyo na rasilimali zinapatikana Ziwa Tanganyika. Ni lini Serikali mnakuja na mkakati maalum swali namba moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali namba mbili dagaa Ziwa Tanganyika ni zao la kipekee ambalo ndio linasababisha uchumi wa Mikoa mitatu Kigoma, Rukwa na Tanganyika. Serikali ina mpango gani na zao hili na pia kwa sababu linavuliwa ndani ya Mikoa mitatu, libadilishwe jina sio dagaa wa Kigoma waitwe dagaa wa Ziwa Tanganyika ili kuweza kutangaza Ziwa Tanganyika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua kwanza fursa hii, kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbogo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, la kwanza naomba kwa namna ya kipekee nimpongeze yeye na Wabunge wote wa Mkoa wa Kigoma, Katavi na Rukwa kwa kuona umuhimu wa Ziwa Tanganyika na mazao yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Rais Samia Suluhu Hassan, moja ya mkakati ni hili la uchumi wa blue na ni kipaumbele kama Taifa letu na ndio maana katika bajeti ya mwaka huu, Serikali ya Awamu ya Sita imeweka jumla ya kiasi cha shilingi milioni 800. Kwa kusudio la kwanza ni kuhakikisha kwamba tunafanya stock assessment. Ziwa Tanganyika halijawahi kufanyiwa stock assessment kwa mara ya kwanza sasa tunakwenda kufanya stock assessment, ya kujua ni kiasi gani cha Samaki migebuka na dagaa tulionao katika eneo lile. Hii itatusaidia sana kwenye mkakati wa uchumi wa blue, ili kuweza kuvutia uwekezaji na watu kuweza kujua kwamba akiweka fedha yake itakwenda kumlipa kwa kiasi gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini hili la pili la ushauri la kwa nini dagaa hawa wasiitwe dagaa wa Ziwa Tanganyika? Nataka nimhakikishie yeye na Waheshimiwa Wabunge wote tumeuchukua ushauri huu. Isipokuwa kibiashara wewe unafahamu ya kwamba katika marketing strategy dagaa hili limetambulika kwa miaka mingi sana kama dagaa la Kigoma.
Kwa hiyo, ikiwapendeza sisi tutakaa nao tutashauriana nao badala ya kuwa dagaa la Kigoma, tutasema kwamba liitwe dagaa la Tanganyika. Kwa dhumuni jema lile la kwamba wanavuliwa kwenye Mikoa yote mitatu, Rukwa, Katavi na Kigoma kwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na dagaa hizi ni mali sana hazijawahi kushuka bei hivi sasa inauzwa mpaka shilingi 30,000 kwa kilo na haijawahi kushuka chini ya shilingi 20,000. Ahsante sana.
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nina swali moja la nyongeza. Jimbo la Nkasi Kusini Tarara ya Kate, huduma za kimahakama wanatumia godown; upande mmoja magunia, upande mmoja Mahakama inaendelea.
Mheshimiwa Spika, nilimpigia simu Mheshimiwa Naibu Waziri, akafika, tukatembelea Tarafa ya Kate yeye mwenyewe akajionea mazingira magumu, jinsi gani huduma za haki za kimahakama zinatolewa katika mazingira ambayo siyo mazuri. Ni godown, wakiweka dawa kwenye mazao, Mahakama haikaliki, ni harufu tupu: Je, ni lini serikali inakuja kujenga jengo la kisasa Tarafa ya Kate? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa
Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vincent Mbogo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana masuala haya kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupata eneo sahihi la kupata huduma za haki. Ni kweli kabisa nilitembelea Kate, na nilikuta ni kweli wanatumia godown ambalo ndiyo linakuwa kama Mahakama.
Mheshimiwa Spika, vile vile nilimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba hili jambo tumelichukua na kwa sasa hivi katika ule mpango kazi ambao Mahakama imejiwekea, tunamwahidi Mheshimiwa Mbunge, katika kipindi hiki tunachoendelea nacho mpaka kufika 2025, Makao Makuu yote ya Tarafa nchini tunakwenda kujenga majengo ya Mahakama ya Mwanzo. Kwa hiyo, kwa sababu Kate ni Tarafa, inaenda kupata upendeleo wa pekee katika kipindi kijacho cha fedha. Ahsante. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Nina swali moja;
Kwa kuwa robo tatu ya Pori Tengefu la Lwafi la Wilayani Nkasi halina wanyama na wananchi wameshaingia wanafanya shughuli zao za kiuchumi; na mipaka hiyo tangu 1948 kipindi cha ukoloni iliwekwa, lakini baadaye ikaja ikabadilishwa ikasogezwa kwa wananchi.
Je, Mhesimiwa Waziri haoni kuwa ni kukwamisha juhudi za wananchi wa Wilaya ya Nkasi wanaojitafutia riziki zao?
Je, ni lini tutakuja kupitia upya ili mipaka irekebishwe, wananchi wameongezeka ili wapate maeneo ya kulima? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vicent Mbogo, Mbunge wa Nkasi, akiwakilishwa na Mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Khenani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Wilaya ya Nkasi haina uhaba wa maeneo, isipokuwa kuna changamoto ya mtawanyiko. Wananchi wanaishi pale ambapo wanahitaji kukaa, kitu ambacho tunaipa mzigo Serikali kupeleka huduma kwa wananchi tukiendelea kuwaruhusu waendelee kutokomea kwenye maeneo ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoelekeza Serikali ni kwamba wananchi wapangwe kwa kuangalia matumizi bora ya ardhi ili kuwepo na miundombinu inayowezesha huduma bora za wananchi ziweze kuwafikia wananchi. Hili swali analolisema kwamba robo tatu ya Lwafi haina wanyama. Ili eneo lihifadhiwe vizuri na ili liwe na madhari nzuri ni pale tu ambapo litaachana na shughuli za kibinadamu. Ndiyo maana yale maeneo ambayo tunayatunza vizuri wanyama huwa wanarudi taratibu na uhifadhi unakuwa ni endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nataka niwaambie tu wananchi wa Nkasi kwamba maeneo ambayo tunayahifadhi mengine tunayachukua yakiwa hayastahili kuwa hifadhi; lakini yanapotunzwa kwa muda mrefu uoto wa asili unarudi, madhari inarudi na wananyama wanaanza kurudi. Kwa maana nyingine wanyama wanatoweka baada ya shughuli za kibinadamu kuingilia maeneo ya hifadhi. (Makofi)
MHE. VINCENT P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa sababu niliomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Kala Kijiji cha Mpasa ambapo kuna biashara kubwa sana ya Samaki inafanyika. Ukanda wa Ziwa Tanganyika kuna uhalifu wa mara kwa mara hasa Kata ya Kizumbi;
Je, ni lini Serikali itajenga kituo cha polisi Kata ya Kizumbi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo Mbunge wa Nkasi Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunashukuru kwamba Mheshimiwa Mbogo amekuwa akitoa ushirikiano kwa Wizara yetu na wakati mwingine kupitia halmashauri yake amekuwa akitenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo hiki. Nimuahidi tu, baada ya kumaliza kituo hiki kadri hali ya fedha itakavyoruhusu maeneo tete kama ya Kizumbi tutaweza pia kuyajengea kituo cha polisi ngazi ya kata. Nashukuru.