Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Vincent Paul Mbogo (4 total)

MHE. VICENT P. MBOGO aliuliza:-

Jimbo la Nkasi Kusini lina Kata 11 na Kituo cha Afya kimoja pekee:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Vituo vya Afya hasa katika Tarafa ya Chala, Kate, Myula, Sintali na Ninde?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi, ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018 hadi mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali imejenga na kukarabati Vituo vya Afya vya Nkomolo na Kirando kwa gharama ya shilingi milioni 900. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetoa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi tatu na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi. Vilevile, Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma matatu ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kusogeza zaidi huduma za afya kwa wananchi, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi inakamilisha utaratibu wa kuingia makubaliano ya utoaji wa huduma za afya (service agreement) na Kituo cha Afya cha Mzimwa kinachomilikiwa na Taasisi ya Kikatoliki Abei kwa ajili ya wananchi kupata huduma za afya ikiwemo upasuaji wa dharura ambapo wananchi kutoka Tarafa za Myula na Sintali ni miongoni mwa watakaonufaika na mpango huo. Aidha, Halmashauri imetenga eneo katika Tarafa ya Chala kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kituo cha afya kupitia fedha za mapato ya ndani katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kujenga na kupanua vituo vya kutolea huduma za afya katika Jimbo la Nkasi na nchini kote kwa awamu kwa kuwa shughuli hizi ni endelevu.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro kati ya Hifadhi ya Lwafi iliyopo Nkasi Kusini na wananchi wa Vijiji vya Mlambo, King’ombe, Tundu na Kata ya Wampembe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba la Lwafi liliwahi kuwa na mgogoro wa Kijiji cha King’ombe ambapo baadhi ya wananchi wake walivamia eneo la hifadhi kwa ajili ya shughuli za kilimo. Hata hivyo, mgogoro huo ulitatuliwa na Serikali baada ya kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo wananchi kupewa elimu na kuonyeshwa mipaka halisi.

Mheshimiwa Spika, aidha, mgogoro huo ulikwisha, lakini kuna mgogoro mwingine kwa sasa ambao ni kati ya Msitu wa Hifadhi ya Loasi yaani Loasi River Forest Reserve na Vijiji vya Mlambo, King’ombe na Tundu, ambapo wananchi walivamia msitu huo kwa ajili ya makazi na shughuli za kilimo. Serikali imefanyia kazi mgogoro huo kupitia mapendekezo ya Kamati ya Mawaziri Nane ambapo maamuzi ya mgogoro huo yameshatolewa na utekelezaji wake utafanyika katika bajeti ya mwaka 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa rai kwa Mheshimiwa Mbunge na wananchi wanaozunguka eneo hilo kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhimiza, kulinda na kutatua migogoro hiyo inayohatarisha uwepo wa maliasili zinazowazunguka.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa maji wa Mji Mdogo wa Chala ambayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni za mwaka 2020?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vicent Paul Mbogo Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji mdogo wa Chala unapata maji kutoka Mto Kauzike na Bwawa la Ntanganyika na hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Mji huo ni asilimia 56. Aidha, katika kuhakikisha huduma ya maji katika mji wa Chala inaboreshwa mwaka 2020/2021 ulitekelezwa mradi wa maji ambao umehusisha kuchimba kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 153,600 kwa siku na kiasi hiki kimeongeza upatikanaji wa maji zaidi ya lita 300,000 kwa siku. Hivyo kazi itakayofanyika kuanzia mwezi Julai, 2021 ni ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji, ujenzi wa nyumba ya mtambo wa maji, ufungaji wa pampu na ulazaji wa bomba mita 500 kwenda kwenye tanki lililopo la lita 150,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji wakati wote, hivyo mpango wa muda mrefu katika mji wa Chala ni kutumia mabwawa madogo na ya ukubwa wa kati ambapo kwa sasa utafiti wa kubainisha maeneo yanayofaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa mawili (2) katika Mji Mdogo wa Chala unaendelea na unatarajiwa kukamilika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2021/2022.
MHE. VINCENT P. MBOGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga masoko ya samaki katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika hususani Kata ya Kala Mpasa, Wampambe, Kizimbi na Naninde ili wavuvi wapate maeneo ya kuuzia samaki badala ya kulazimika kwenda kuuza nchi za jirani za Zambia, Congo na Burundi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kujenga miundombinu ya uvuvi katika maeneo mbalimbali ikiwemo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika. Miundombinu ya Mialo na Masoko ni muhimu katika kuhakikisha kuwa na mazao bora na salama, kupunguza upotevu wa mazao na kusaidia ukusanyaji wa taarifa na mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, pamoja na umuhimu huu, ujenzi wa masoko unahitaji rasilimali ikiwemo ardhi na fedha. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ipo tayari kujenga Soko, katika Wilaya ya Nkasi kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, namuomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kuandaa eneo katika Wilaya ya Nkasi, ili kuwezesha hatua za ujenzi wa soko kuanza pindi fedha itakapopatikana. Ahsante.