Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Michael Constantino Mwakamo (6 total)

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naitwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge kutoka Kibaha Vijijini. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, najua TASAF ilianza awamu ya kwanza kwa kuwapatia walengwa miradi ya uwekezaji kama majengo mbalimbali zikiwemo kumbi za maonyesho. Katika Jimbo la Kibaha Vijijini, wazee walipewa mradi huu awamu ya kwanza; je, TASAF wana mkakati gani juu ya kuwafanyia ukarabati jengo ambalo walipewa katika awamu ya kwanza ambalo sasa limechakaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia nafasi hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge, awamu ya kwanza ilijikita zaidi katika ujenzi wa miundombinu na si Kibaha Vijijini tu bali katika halmashauri nyingi sana katika nchi yetu ambazo majengo haya au miradi hii ilifanyika. Sasa baada ya awamu ya kwanza kuisha na kwenda awamu ya pili na sasa tuko awamu ya tatu phase II, ni kwamba majengo haya na miradi hii yote ilikabidhiwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri husika. Na ni wajibu wa Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha kwamba wanatunza majengo haya na wasiwaachie tu wale walengwa peke yao; ni wajibu wa Wakurugenzi kuhakikisha sustainability ya miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge kuelekea katika halmashauri yake na kuhakikisha tunakwenda kuangalia miradi hiyo na kuwaagiza Wakurugenzi ili kuhakikisha kunakuwa na sustainability.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri juu ya ujenzi wa barabara hiyo, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeshafanya upembuzi yakinifu wa kilometa hizo 100 ambazo zinatokea Makofia kuendelea Kisarawe, je, ni lini Serikali italipa fidia wananchi hawa ili kupisha ujenzi huo uendelee kwa sababu ni wa muda mrefu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa barabara hii; na kwenye majibu yake anakiri kwamba ametenga pesa ya kufanyia ukarabati wa muda wakati wakisubiri tukipata pesa, naomba niifahamishe Serikali kwamba kwa sasa barabara hii haijafanyiwa ukarabati huo kwa miaka mingi. Kwa kuwa pesa hizi zimepangwa mwaka huu wa bajeti, je, Serikali haioni sasa ni muda sahihi kutafuta fedha za haraka kuzifanyia ukarabati barabara hizo kwa sasa kwani kipande cha kutoka Mlandizi kwenda Mzenga kina mashimo makubwa utadhani mabwawa ya kuvulia samaki? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimwa Michael Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kila hatua inayofanyika ndiyo ujenzi wenyewe wa barabara ya lami unavyoendelea. Barabara hii haitaanza kujengwa mpaka kwanza fidia ya wananchi hawa ambao bahati nzuri tayari wameshatathminiwa watakapolipwa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Mwakamo kwamba wananchi hawa watalipwa fidia pale tu ambapo Serikali itapata fedha. Jitihada kubwa zinafanywa na Serikali kuhakikisha kwamba tunapata fedha ili tuweze kuwalipa hao wananchi ambao tayari wameshaainishwa.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili kwamba barabara hii haijafanyiwa matengenezo; naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia Bunge hili naomba kumuagiza Meneja wa Barabara Mkoa wa Pwani aweze kutembelea barabara hiyo na kuangalia upungufu uliopo aweze kuikarabati kwa sababu fedha imetengwa ili wananchi waendelee kupata huduma ya barabara hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa ahadi ya barabara hizi imetolewa pia kwenye Jimbo la Kibaha Vijijini kwenye Mji wa Mlandizi na tayari kuna barabara ya kilometa moja imeanza kutekelezwa na miezi sita sasa haijalipwa chochote. Je, Serikali haioni ni muda sahihi sasa kumalizia ile fedha ili mkandarasi amalizie ili hata ile kazi ambayo ameshaanza kufanya isiharibike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara zote ambazo wakandarasi wako site zitaendelea kulipwa fedha ili ziendelee kukamilika, ikiwemo hii barabara ambayo umeitaja hapa.

Kwa hiyo, haitakwama kwa sababu ninaamini kabisa kwamba, sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kupitia TARURA tunapitia zile certificates ambazo wakandarasi wanazileta kwetu na tunazitolea fedha. Kwa hiyo, na hili tumelisikia na nikuhakikishie kwamba, itaisha kwa wakati kama ambavyo iliahidiwa na viongozi wetu wakuu, ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri yenye mikakati ya Serikali juu ya watumishi wao, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Jimbo la Kibaha na majimbo mengi nchini kuna watumishi ambao wamechelewa kulipwa mafao yao kutokana na waajiri kutokupeleka michango yao kwa wakati. Je, Serikali inawasaidiaje watumishi hao, kwani waajiri wao wamefanya kinyume na utaratibu wa sheria?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuanzia mwaka 2016 mpaka 2020, kulikuwa na maelekezo mbalimbali ya Serikali juu ya upandishwaji wa vyeo, kuna watumishi ambao wamestaafu wakiwa na barua mkononi lakini wameshindwa kulipwa kutokana na barua zao walizo nazo. Lakini pia kuna watumishi walichelewa kupandishwa vyeo kwa sababu ya waajiri kuwasahau kwenye kuingiza kwenye mfumo.

Je, Serikali inawasaidiaje watumishi hao ili waweze kupigiwa hesabu zao kulingana na haki na sheria ilivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, Mheshimiwa Costantino, kwa kufuatilia vizuri sana haki za wananchi wake katika Jimbo la Kibaha Vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la kwanza ambalo ameuliza ni utaratibu gani tunaochukua kwa wale waajiri ambao wanachelewesha michango lakini pia wanaosababisha fedha zile zisiweze kulipwa kwa wakati, hasa hizi za pensheni. Tumekwisha kuchukua hatua mbalimbali kwa mameneja wa mikoa wa PSSSF, lakini pia hata kwa NSSF kwenye maeneo ambayo tunagundua kwamba kuna uzembe wa ukusanyaji wa michango. Tumekuwa tukichukua hatua kali kwa wakurugenzi wa PSSSF Mikoa, lakini pia complying officers ambao tumekuwa tukiwaagiza kwa wakati wote watoe taarifa ya wadaiwa sugu kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu waajiri wanapochelewesha michango ni pamoja na kukwepa kodi, kwa sababu kuna PAYE kwenye mshahara wa mfanyakazi, kuna fedha inayopaswa kuinia katika Mfuko wa WCF, kuna fedha inayopaswa kulipwa kama Skills Development Levy, lakini vilevile kuna fedha ambayo ni ya mafao ya mfanyakazi, anapomaliza wakati wake wa kazi itamsaidia kwenye maisha yake. Kwa hiyo tunachukua hatua kali, na sheria inaelekeza na tumekuwa tuna kesi mbalimbali ambazo zinaendeshwa kwenye mahakama mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kuagiza kwamba mameneja wetu wa mikoa na complying officers waweze kufuatilia michango.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili kwa kifupi, ni kwamba swali hili liko Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma, kwa wafanyakazi ambao ni wa Serikali. Nikuombe Mheshimiwa Mbunge, mimi pamoja na wewe tuweze kuiona ofisi ile na tuweze kufuatilia madai hayo ili waweze kupata haki na stahiki zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naitwa Michael Constantine Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini.

Naomba niulize swali la nyongeza; kwa kuwa Kibaha Vijijini kuna scheme ambayo inaendelea kujengwa lakini hijaaza uzalishaji na tatizo kubwa ni mifugo kuingia na kufanya uharibifu.

Je, Serikali itatusaidiaje kuondoa tatizo hilo kuhamisha wafugaji wale kwenda kwenye eneo la ufugaji la NARCO ili wakulima wa eneo lile walime kwa uhakika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hili ni jambo specific na ni jambo linahusu sehemu moja, nitamuomba baada ya hapa tukae tukutane ili tukae na wenzetu wa Wizara ya Mifugo ili tuweze kulijadili na kulitatua kw apamoja. (Makofi)
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kwenye majibu ya msingi ya Mheshimiwa Waziri hajaeleza na wala hajaitaja Ranchi ya Ruvu iliyopo pale Vigwaza kama imeshatengwa, sasa kwa kuwa kuna migogoro mingi ya wakulima na wafugaji kwenye Mikoa ya Pwani na maeneo mengine ya jirani kama Wilaya ya Chalinze na Kibaha Vijijini; Je, Serikali haioni huu ni muda sahihi sasa kupanga na Ranchi ile ili kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji kwenye maeneo hayo?

Swali la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri anafahamu kwamba migogoro mingi ya wakulima na wafugaji inapelekea watu wengi kupata ulemavu wa kudumu na wengine kufariki na kwa sababu ipo Ranchi hiyo ninayoitaja ya Ruvu ambayo haijafanyiwa; Je, Waziri haoni kwamba ni muda sahihi wa kufika kwenye maeneo ya Mkoa Pwani hasa Wilaya hizo za karibu kuwaelimisha wafugaji wadogo kwenda kuomba na kupata utaratibu wa kukaa kwenye Ranchi hizo kuondoka kwenye Bonde la Ruvu ambalo lina migogoro? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru na kumpongeza sana lakini pili kwanini Ranchi ya Ruvu haikutamkwa katika majibu haya. Ranchi ya Ruvu katika maelekezo ya muda mrefu uliopita ya Serikali haikupangwa kwa ajili ya vitalu vya muda mrefu. Ranchi ya Ruvu na Ranchi ya Kongwa hazikupangwa. Kwa hivyo, baadaye kwa utashi na maelekezo ya viongozi wetu wakuu na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutaka kuona tunatatua changamoto ndiyo uamuzi wa kukata vitalu vya muda mfupi ukafanywa kwa hivyo Ranchi ya Ruvu ikapangiwa ikatwe vitalu jumla ya 19 na hivi sasa ninavyozungumza jumla ya Ng’ombe zaidi ya Elfu Tisa katika vitalu hivi vidogo vidogo vilivyopo katika eneo nzima la Ranchi Ruvu vimeshagawiwa kwa wafugaji, hili ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni namna ya kuweza kuwatoa wale wafugaji walioko katika maeneo ya Bonde la Mto Ruvu na labda kuwapa nafasi huku. Serikali jambo hili inalifanyia kazi siyo peke yake katika Mto Ruvu lakini vilevile na mito mingine kama Kilombelo, Ruaha na mingineyo. Maelekezo ya Serikali ni kwamba iko Kamati ya Mawaziri Nane inayofanya tathmini ili tutakapotoka na majawabu, tutatoka na majawabu ya pamoja yatakayokwenda kutatua kabisa tatizo hili la muda mrefu la wafugaji, wakulima na watumiaji wengine wa ardhi. Ahsante sana. (Makofi)