Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Michael Constantino Mwakamo (4 total)

MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Makofia kupitia Mlandizi hadi Vikumbulu Kisarawe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Makofia – Mlandizi – Vikumbulu yenye urefu wa kilometa 135.97 ni barabara ya mkoa inayounganisha Wilaya za Bagamoyo, Kibaha na Kisarawe. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina pamoja na uhakiki wa mali zitakazoathiriwa na mradi sehemu ya Makofia – Mlandizi – Maneromango yenye urefu wa kilometa 100 umekamilika. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza baada ya kupata fedha ambazo Serikali inaendelea kutafuta.

Mheshimiwa Spika, wakati ujenzi kwa kiwango cha lami ukisubiri upatikanaji wa fedha, Wizara yangu inaendelea kuihudumia barabara hiyo ili iweze kupitika majira yote ya mwaka ambapo katika Mwaka huu wa Fedha wa 2020/21 jumla ya shilingi 1,524.000.07 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii. Ahsante.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA - K.n.y. MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua migogoro ya mipaka ya kiutawala baina ya Mikoa, Wilaya na Vijiji hapa nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Constantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua migogoro ya mipaka ya kiutawala baina ya Mikoa, Wilaya na Vijiji hapa nchini Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kusambaza Matangazo ya Serikali kwa maana ya Government Notices au GN yanayoonesha mipaka ya Wilaya na Mikoa kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini; kKuunda vikundi kazi na kuvipeleka kwenye maeneo yenye migogoro ya mipaka ili kutatua migogoro; kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Matumizi Bora ya Ardhi nchini kwa kuhakikisha Vijiji, Kata na Wilaya zinaandaa na kutekeleza Mipango ya matumizi ya ardhi, kutoa elimu kwa umma kuhusu Sera na Sheria za ardhi, kusimamia upimaji wa viwanja na mashamba katika Halmashauri, kurasimisha makazi na kumilikisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ili kutatua migogoro ya mipaka ya kiutawala baina ya Mikoa, Wilaya na Vijiji hapa nchini.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia watumishi waliostaafu kupata mafao yao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ulianzishwa rasmi tarehe 1/ 8/2018 kwa Sheria Namba 2 ya Mwaka 2018. Mfuko huu ni matokeo ya kuunganisha mifuko minne ya awali (LAPF, GEPF, PPF na PSPF) ambayo ilikuwa ikihudumia watumishi mbalimbali wa Umma na kuufanya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kubaki ukihudumia sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati, mipango na utekelezaji wa Serikali katika kuhakikisha watumishi waliostaafu wanapata mafao yao kwa wakati ni kama ifuatayo: -

(i) Kutengeneza mifumo mbalimbali ya TEHAMA ili kuweza kuwatambua wanachama wake na kulipa mafao stahiki pale wanapodai mafao;

(ii) Kulipa malimbikizo mbalimbali ya mafao ya wanachama yaliyopaswa kulipwa na mifuko iliyounganishwa na yale yaliyopokelewa kipindi ambacho mchakato wa kuunganisha mifuko huo ulikuwa unaendelea; na

(iii) Kuandaa ofisi mbalimbali nchini kote na kuweka misingi bora itakayowezesha utoaji wa huduma bora kwa wanachama wake ikiwa ni pamoja na kuimarisha mifumo ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha wastaafu wanalipwa kwa wakati, waajiri wanakumbushwa kufuata kikamilifu utaratibu ulioainishwa katika Sheria namba 2 ya Mwaka 2018 ambapo inaelekeza ipasavyo maandalizi ya taarifa za wastaafu kabla ya malipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifuko imeendelea kuboresha mifumo yake ambapo matarajio ni kuwa waajiri nao wafuate vizuri utaratibu ulioainishwa kisheria ili kupunguza ucheleweshaji wa kulipa mafao kwa wastaafu.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -

Je, ni Ranchi ngapi nchini zimeshawapokea wafugaji na kuwapatia nafasi ya kufuga kwenye Ranchi hizo kama Serikali ilivyotoa maelekezo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Michael Costantino Mwakamo Mbunge wa Kibaha Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) imetekeleza maelekezo ya Serikali kwa kutenga jumla ya vitalu vya muda mrefu 116 katika Ranchi 11 za NARCO na kuzikodisha kwa wafugaji wadogo 116. Ranchi hizo ni Kikulula (Kagera) vitalu 2, Mabale (Kagera) vitalu 7, Kagoma (Kagera) vitalu 18, Kitengule (Kagera) vitalu 10, Missenyi (Kagera) vitalu 11, Mkata (Morogoro) vitalu 7, Dakawa (Morogoro) vitalu 2, Mzeri Hill (Tanga) vitalu 9, Usangu (Mbeya) vitalu 16, Kalambo (Rukwa) vitalu 13 na Uvinza (Kigoma) vitalu 21. Jumla ya eneo la vitalu hivi ni hekta 322,525.

Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kutatua migogoro ya wakulima, wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi nchini hasa baada ya wafugaji kuondolewa kwenye hifadhi za misitu na mapori ya akiba, Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) ilianzisha utaratibu wa kugawa vitalu vya muda mfupi ambapo jumla ya vitalu 128 vimekodishwa kwa wafugaji wadogo 128 kutoka katika Ranchi 10 za NARCO. Ahsante sana.