Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joseph Zacharius Kamonga (4 total)

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ina uhaba mkubwa wa walimu kwenye shule zake za msingi, jambo linalosababisha wazazi kuchangishwa kati ya 15,000 mpaka 20,000 kwa ajili ya kuajiri walimu wa kujitolea kwenye Kata ya Mlangali, Mavanga na Lugarawa. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha kwenye shule za msingi za Wilaya ya Ludewa ikiwa ni pamoja na kuwaajiri wale walimu waliojitolea kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, shule 23 za sekondari zilizopo Jimboni Ludewa hazijafanyiwa ukaguzi muda mrefu. Je, ni lini Wizara itatoa maelekezo kwa wadhibiti ubora wa elimu walioko pale Ludewa waweze kufanya ukaguzi huo kuliko kuendelea kusubiri wakaguzi kutoka kanda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna changamoto ya uhaba wa walimu katika maeneo mbalimbali nchini. Na kama mnavyofahamu hivi punde tu Mheshimiwa Rais aliagiza kwamba, wale walimu 6,000 ambao wa kuziba nafasi utaratibu wake uweze kufanyika mapema. Lakini kama mnavyofahamu mwaka jana mwezi wa Novemba Serikali ilitoa kibali cha kuajiri walimu zaidi ya 13,000. Tunaamini kati ya wale 13,000 walimu karibu elfu nane walikuwa tayari wameshasambazwa shuleni na walimu 5,000 walikuwa wanaendelea na mchakato.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika magawanyo huu sasa na hawa 6,000 watakaopatikana hivi punde watakwenda kutatua tatizo lile la upungufu wa walimu katika Halmashauri zetu ikiwemo na Halmashauri au Wilaya ya Ludewa.

Mheshimiwa Spika, hili la wazazi kuchangishwa, naomba tulibebe. Tutashirikana na wenzetu wa TAMISEMI tuweze kuangalia namna gani jambo hii linaweza likachukuliwa hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili amezungumzia suala la ukaguzi wa shule, Wizara inaendelea na kuimarisha Kitengo hiki cha Wadhibiti Ubora, ambapo hatua tofauti zimeweza kuchukuliwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018/2019 mpaka hii 2020/2021. Wizara imeweza kufanya mambo yafuatayo; kwanza, tumeweza kusambaza Wadhibiti Ubora 400 katika Halmashauri zote nchini.

Pia katika kipindi cha mwaka 2018/2019 hadi 2020/ 2021 jumla ya ofisi za Wadhibiti Ubora 100 katika Halmashauri zetu zimeweza kujengwa na mpaka hivi navyozungumza tunaendelea na ujenzi wa ofisi 55 na ukarabati wa ofisi 31. Sambamba na hilo, Wizara yangu tumeweza kununua na kusambaza magari 83 kwenye Halmashauri tofauti tofauti.

Mheshimiwa Spika, lengo la kufanya hayo yote ni ili kuimarisha Kitengo chetu hiki cha Udhibiti Ubora hasa katika Halmashauri zetu. Kwa kufanya hivyo, tunaamini kutokana na ongezeko la shule nyingi ambazo zinahitaji kukaguliwa za msingi na sekondari tutaweza sasa kuzifikia shule hizo kwa umakini mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sasa Wadhibiti wetu wa Ubora hawa wa Wilaya watakwenda kufanya ukaguzi katika shule hizi za msingi na sekondari katika maeneo waliopo badala ya kutumia wale Wadhibiti Ubora wa Kanda ambao walikuwa wanakagua hizi shule katika kipindi kilichopita. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Ziwa Nyasa lina Kata zisizopungua nane; Kata ya Ruhuhu, Manda, Iwela, Lupingu, Lifuma, Makonde, Kilondo na Ruhila. Je, ni lini Serikali inakusudia kupeleka vifaa vya uvuvi kama engine za maboti kwa vikundi vya wavuvi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningetamani kufahamu ni lini Serikali itapeleka kituo cha kufanya utafiti wa samaki na viumbe maji huko Wilayani Ludewa maana kata hizi zina wakazi wasiopungua 28,000 ambao wanatumia ziwa hili kama swimming pool na njia tu ya usafiri. Ningependa kufahamu commitment ya Serikali juu ya kupeleka kituo cha utafiti wa samaki?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamonga, Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, juu ya kupatikana kwa vifaa vya uvuvi katika makundi ya vijana kwenye Kata za Ruhuhu, Manda, Makonde na kwingineko katika Jimbo lake la Ludewa naomba nimhakikishie kwamba katika mwaka wa fedha huu ambao leo tunaendelea kujadili bajeti yake, Serikali imejipanga kuhakikisha vijana wote waliopo katika maeneo hayo na wenyewe wanaweza kuwezeshwa kupata vifaa vya kufanyia shughuli zao za uvuvi.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni kituo cha utafiti; Ziwa Nyasa ni katika maeneo ambayo Shirika letu la Utafiti la Uvuvi (TAFIRI) litakwenda kufanya utafiti kule na uwezekano wa kuweza kupata kituo kidogo pale kwa ajili ya utafiti kwenye eneo la Ziwa Nyasa upo na naomba nichukue jambo hili nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itafanya jitihada ya kuhakikisha kituo kinapatikana pale ili na Ziwa Nyasa wakati wote liwe linatazamwa na kuangaliwa kwa karibu. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; wananchi wa Ludewa wangependa kufahamu kwa kuwa wamesubiria fidia hizi kwa muda mrefu. Je, kwa nini Serikali isitenganishe majadiliano na mwekezaji na suala la fidia ili wananchi wa Jimbo la Ludewa waweze kulipwa fidia mapema?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; ningependa kufahamu ni lini Serikali itaanza kutoa elimu ya kuandaa wananchi wanaoathirika na miradi ili waweze kunufaika na miradi hii? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Jimbo la Ludewa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika mradi huu fidia kwa wananchi iliyothaminiwa jumla ya bilioni 11.037 katika majadiliano au katika mkataba ambao tuliingia na kampuni hii Situan Honda ilikuwa yeye kama mwekezaji atakuwa na wajibu wa kulipa fidia eneo hilo ambalo atakuwa analitumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema baada ya majadiliano na mwekezaji huyu tutaangalia sasa kama tutafikia muafaka maana yake yeye atakubaliana kulipa fidia, lakini utekelezaji wa mradi huu lazima uanze mwaka 2021/2022, aidha tumekubaliana na mwekezaji huyu au hatujakubaliana lakini mradi huu lazima uanze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshaeleleza na ni utekelezaji ambao unaenda kufanyika katika mwaka wa fedha ujao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la elimu katika eneo hili, ni kweli Serikali imekuwa ikiweka fedha kwa ajili ya kuelimisha wananchi namna ambavyo watashiriki katika ujenzi wa mradi huu kwa maana ya local content kwamba wao watafanya nini au watashiriki vipi katika mradi huu mkubwa wa Mchuchuma na Liganga. Kwa hiyo fedha zinatengwa kila mwaka na elimu inaendelea kutolewa kwamba sasa mradi huu ukianza naamini elimu zaidi itatolewa ili wananchi wa eneo hili waweze kushiriki katika utekelezaji wa mradi huu kikamilifu.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Moja, namwomba Mheshimiwa Waziri aweze kutupa Mpango wa Serikali: Ni kwa muda gani chuo hiki kitakuwa kimekamilika na kuanza kutoa mafunzo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Ludewa kwa umoja wao wamechangia fedha na nguvu zao kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya wanafunzi watakaokuwa na ufaulu mkubwa wa Darasa la Saba.

Je, ni lini Serikali katika kutambua jitihada za wananchi na kuunga mkono juhudi zao? Ni lini Wizara itatuma watalaamu kwa ajili ya kwenda kusajili shule ile ili watoto waweze kuanza kusoma pale?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante; naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kamonga Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Kamonga pamoja na wananchi wa Ludewa na vilevile Watanzania wengine walioko kwenye Mikoa ya Rukwa, Geita pamoja na Simiyu, kwa sababu katika maeneo ambayo vyuo vya mikoa vinaenda kujengwa ni pamoja na maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la muda, tunatarajia ndani ya miezi minane kutoka leo vyuo hivi vinakwenda kukamilika kwa sababu fedha hizi zina muda maalumu wa utekelezaji kuhakikisha kwamba miradi hii inafanyiwa kazi sawa sawa. Kwa hiyo, niwahakikishie tu, Mheshimiwa Rais ametoa fedha hizi kwa kuhakikisha katika kipindi hiki kifupi huduma hizi zinaweza kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili, anazungumzia Shule ya Sekondari; nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Ludewa kwamba taratibu za kufuata zipo wakati wa kufanya ukaguzi na kusajili shule hizi. Namshauri Mheshimiwa Mbunge kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri kuweza kuandika barua kupeleka kwenye idara yetu ya Udhibiti Ubora iliyokuwepo katika Wilaya ile ya Ludewa na wataalamu wetu wale wakishapata tu barua na maombi hayo, mara moja wanatakiwa kwenda kwa ajili ya kufanya ukaguzi ili kutengeneza ithibati iwapo viwango vile vimethibitika kuwepo, basi usajili huo utapatikana. Ila kwa vile amelizungumza suala hili hapa Bungeni, tutakwenda kulifanyia kazi kuhakikisha kwamba wiki ijayo wataalamu hao waweze kwenda kwenye eneo hilo la shule ili kuweza kupata usajili ili vijana wetu kama Januari shule hii inaweza kufunguliwa, iweze kufunguliwa na wanafunzi waweze kupata huduma. Ahsante. (Makofi)