Primary Questions from Hon. Joseph Zacharius Kamonga (7 total)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakamilisha Ujenzi wa Chuo cha VETA Shaurimoyo – Ludewa ili kuzalisha Wataalam watakaosaidia kutekeleza mradi wa Liganga na Mchuchuma utakapoanza?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Njombe kinachojengwa katika Wilaya ya Ludewa ni miongoni mwa vyuo vilivyokuwa vinajengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa kuimarisha Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi na Elimu ya Ualimu (STVET – TE). Mradi huu ulikuwa unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambapo mkataba kati ya Serikali na Benki hiyo uliisha muda wake tarehe 31 Desemba, 2019, kabla mradi haujakamilika.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa kukamilika kwa mradi huu, utekelezaji wa mradi huu utaendelea kupitia Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Kazi (ESPJ) kwa utaratibu wa “Force account”. Tathmini ya gharama imeshafanyika ambapo jumla ya shilingi 4,342,678,784.32 zitatumika katika kukamilisha ujenzi huu. Ujenzi wa Chuo hiki unatarajiwa kuanza tena katika Mwaka wa Fedha 2020/2021. Ahsante.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza:-
Kwa kuwa wananchi wa Ludewa hutegemea Ziwa Nyasa kwa shughuli za uvuvi: -
(a) Je, Serikali haioni haja ya kupeleka mradi wa uhifadhi mazingira Ziwa Nyasa ili kutunza mazalia ya samaki ambao wameanza kuadimika?
(b) Je, ni lini Serikali itapeleka fedha pamoja na wataalam kutoa elimu ya kuanzisha mradi wa ufugaji samaki kwenye vizimba ndani ya Ziwa Nyasa ili kuzalisha ajira kwa wananchi na kuongeza kipato?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Ludewa lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara katika kutekeleza jukumu la kulinda, kusimamia, kuhifadhi na kuendeleza rasilimali za uvuvi nchini imekuwa ikitoa elimu kuhusu uhifadhi wa mazingira kote nchini ikiwemo Ziwa Nyasa. Aidha, kwa sasa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuandaa mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya uvuvi ambao utakapokamilika unatarajiwa kubainisha miradi ya uvuvi itakayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa mafunzo katika tasnia ya ukuzaji viumbe maji kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo teknolojia ya vizimba, imetoa mafunzo ya vitendo kwa wananchi 1,885 kuhusu mbinu bora za ufugaji samaki, kilimo cha mwani na uongezaji thamani zao la mwani.
Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imepanga kutoa mafunzo kwa wakuzaji viumbe maji wapatao 3,000 kote nchini wakiwemo wafugaji wa samaki Ziwa Nyasa kupitia Kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbe Maji cha Ruhila – Songea.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -
(a) Je, ni lini wananchi wa Ludewa ambao maeneo yao yamechukuliwa na Serikali kwa muda mrefu kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Liganga na Mchuchuma watalipwa fidia?
(b) Je, ni lini Mradi wa Liganga na Mchuchuma utaanza kufanya kazi ili kuinua uchumi wa Mkoa wa Njombe na Taifa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Jimbo la Ludewa lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi unganishi wa madini ya chuma na makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma uliopo katika Wilaya ya Ludewa, Mkoani Njombe ni Mradi wa Kimkakati na upo katika hatua za awali za utekelezaji. Mradi huu unategemea kutekelezwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa - NDC ambalo litakuwa na 20% na Kampuni ya Sichuan Hongda (Group) Kampuni hii ya China yenye 80% baada ya majadiliano kuhusiana na baadhi ya vipengele katika mkataba wa utekelezaji mradi huu kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ili kuanza utekelezaji wa mradi, mwekezaji aliomba vivutio ambavyo vimeshindwa kutolewa na Serikali kwa sababu vinakinzana na Sheria mpya Na. 6 na 7 za mwaka 2017 ambazo ni Natural Wealth and Resources Contracts (Review and Renegotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hadi sasa, majadiliano na mwekezaji huyu yanaendelea ikiwemo suala la ulipaji wa fidia kwa maeneo yote ya mradi yaliyothaminiwa. Utekelezaji wa mradi huo utaanza mara baada ya kukamilika kwa majadiliano hayo.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali isiingie makubaliano na Chuo cha Ufundi Lugarawa kinachomilikiwa na Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe kwa kupeleka Walimu, vifaa na fedha za ruzuku ili Wanaludewa na Wananjombe wapate mafunzo wakati ujenzi wa Chuo cha VETA Shaurimoyo ukisubiriwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Eilimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa haina utaratibu wa kushirikiana katika kutoa mafunzo kwa pamoja na taasisi binafsi. Hata hivyo, Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na sekta binafsi, zikiwemo taasisi za dini katika utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha taasisi zake za elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa kujenga vyuo katika ngazi za Wilaya na Mkoa na kuvipatia vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa lengo la kuhakikisha kwamba watanzania wanapata elimu bora ya ufundi karibu na maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Njombe, Serikali inamiliki Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Makete chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 160 kwa mwaka. Kwa sasa Serikali inaendelea kupanua Chuo hicho kwa kuongeza madarasa matano yenye uwezo wa kubeba wanafunzi 100 kwa wakati mmoja, mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 72 kwa kila moja na nyumba mbili za watumishi, kila moja ikiwa na uwezo wa kubeba familia mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inaendelea na matayarisho kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Njombe kitakachojengwa katika Wilaya ya Ludewa kupitia fedha za IMF. Aidha, ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kuanza mwezi huu wa Novemba, 2021. Ahsante. (Makofi)
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga minara ya simu katika Kata za Jimbo la Ludewa pamoja na kuongeza nguvu kwa minara iliyopo iwe 4G?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius kamonga Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa Seriakili kupitia Mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF inaendelea kutatua changamoto za mawasiliano katika Jimbo la Ludewa kwa kushirikiana na watoa huduma wa mawasiliano kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Airtel ambao sasa tayari imewasha minara mitatu katika Kata za Madiru Kijiji la Ilawa, Kata ya Madope Kijiji cha Lusitu na Kata ya Mkongobaki katika Kijiji cha Mkongobaki.
Mheshimiwa Spika, kampuni ya tiGo ambayo imejenga minara katika Kata ya Lupanga, Kijiji cha Lupanga, Kata ya Mkomang’ombe Kijiji cha Mkomang’ombe na Kata ya Ludewa Kitongoji cha Ngalahawe ambapo mnara unafika katika Kijiji cha Nindi. Aidha, kampuni ya simu ya tiGo ipo katika hatua za kutekeleza mradi wa kufikisha huduma ya mawasiliano katika Kata ya Lupingu na Mkwimbili ambapo changamoto kubwa imekuwa ni namna ya kusafirisha vifaa vya ujenzi wa mnara na kuvifikisha katika eneo la mradi.
Mheshimiwa Spika, pia Halotel inatoa huduma katika Kata zote za mwambao wa Ziwa Nyasa zikiwemo Makonde, Kimata, Nsele, Ndowa na Igalu. Hata hivyo, Serikali inatambua changamoto kubwa ya mawasiliano inayowakabili wananchi wote wa kandokando ya Ziwa hususa ni Tarafa ya Jua. Kwa upande mwingine, TTCL inatoa huduma katika Kata ya Ibumi japo bado kuna changamoto hasa katika Kijiji cha Masimalavafu. Serikali inatambua kuwa mradi wa uchimbaji wa madini ambao kwa namna moja au nyingine utachangia pato la uchumi kwa nchi yetu. Hivyo, Serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote UCSAF inatumia wataalam wake kwenda kata ya Ibumi na kuangalia namna gani ya kutatua changamoto ya mawasiliano hususa ni katika eneo la uchimbaji wa madini.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na nguvu ya minara kwenda teknolojia ya 4G. Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeanza kutekeleza mradi wa kuongeza nguvu kwenye minara yote nchini iliyokuwa na teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G. Hivyo, minara iliyopo Jimbo la Ludewa itaingizwa katika mradi huo. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kurasimisha, kupanga na kupima ardhi katika Miji Midogo ya Mawengi, Lugarawa, Luilo na Manda – Ludewa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 89 lililoulizwa na Mheshimiwa Joseph Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Wizara kupitia Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi iliikopesha Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kiasi cha shilingi milioni 405 kwa lengo la kupanga na kupima na kurasimisha miji midogo ya Mlangali, Mavanga, Ludewa na Mudindi ambapo jumla ya viwanja 7,911 vimepangwa na viwanja vingine 2,120 vimekamilika katika utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa maelekezo wataalamu wa ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa kuanza kukusanya takwimu muhimu kwa ajili ya kupanga na kupima katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali italipa fidia wananchi waliotwaliwa ardhi yao kwa ujenzi wa viwanda maeneo ya Liganga na Mchuchuma?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa uwekezaji Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Zacharius Kamonga, Mbunge wa Ludewa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mradi Unganishi wa Mchuchuma na Liganga unatarajiwa kutekelezwa kwa ubia kati ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kwa niaba ya Serikali na Kampuni Binafsi, ambaye ni mbia. Katika kutekeleza mradi huo, Serikali imetenga fedha katika bajeti ya mwaka 2022/2023 kwa ajili ya kufanya uthaminishaji upya na hatimaye kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi huo kwa mujibu wa Sheria.