Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Zacharius Kamonga (12 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa neema na rehema zote, niwashukuru pia wananchi wa Jimbo la Ludewa na chama changu Chama Cha Mapinduzi (CCM). Nimshukuru pia Mheshimiwa Rais na Serikali yake yote kwa kazi nzuri ambazo zimekuwa zikifanyika na sisi kule Ludewa tumekuwa tukiziona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Ludewa kwa kuniamini na kunituma nije niseme hapa Bungeni kwa niaba yao na vilevile sisi Wanaludewa tumezisoma vizuri hotuba zote za Mheshimiwa Rais na tukajitahidi kuzitafsiri ziendane na mazingira yetu ya Jimbo la Ludewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza na eneo la uwekezaji kwenye miradi mikubwa ambayo inaweza ikaongeza mapato ya Taifa letu. Mwaka 1996 Baraza la Mawaziri kupitia Waraka wa Baraza la Mawaziri Na. 06/96 wa mwaka 1996 waliridhia miradi ya Mchuchuma na Liganga iweze kuanzishwa na viwanda vikubwa vijengwe kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2011, NDC kwa maelekezo ya Serikali na Baraza la Mawaziri waliunda Kampuni ya ubia Tanzania-China International Mineral Resources Limited. Kampuni hii ilikwenda Ludewa na kufanya uthamini kwa nia ya kuwekeza kwenye huu mradi wa Mchuchuma na Liganga, baada ya kufanya upembuzi yakinifu na kujiridhisha eneo lile lina mali za kutosha.

Upande wa Liganga kuna chuma ambapo kampuni hii ingeweza kuzalisha zaidi ya tani milioni 2.9 kwa mwaka na kwa makaa ya mawe wangeweza kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na ajira za moja kwa moja milioni sita na laki nne na ajira zisizo za moja kwa moja milioni 33. Lakini cha kushangaza ni kwamba mradi huu umekwama.

Mheshimiwa Spika, Wabunge watangulizi wangu wamejitahidi kupambana miradi ianze, lakini hatujaweza kufanikiwa. Wananchi wa Ludewa wana imani na Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli na wanamwalika sana aweze kwenda kutembelea miradi hii mapema iwezekanavyo kwani Wabunge wengi hapa wamekuwa wakilalamika fedha TARURA. Mimi nikuhakikishie Serikali ikiamua kuwekeza kwenye miradi ile tutapata fedha nyingi ambayo itatatua changamoto ya fedha na changamoto ya ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile upo mradi wa Chuo cha VETA ambao ulianzishwa pale Shaurimoyo ambao nao umekwama kwa muda mrefu sana. Tulikwenda kufanya ziara Desemba na Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa na ninamshukuru Rais kwa kutuletea Mkuu wa Mkoa mahiri, Engioneer Marwa Rubirya, tulikwenda naye, watu wa VETA waliahidi Januari wangeweza kuanza kujenga chuo kile, lakini cha kushangaza bado hakijafanikiwa. Kwa hiyo, tunaomba chuo kile kijengwe ili miradi hii inavyoanza na sisi wananchi wa Ludewa na Wananjombe tuweze kupata ajira kwenye miradi ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye Sekta ya Maji; namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Maji, nilipata nafasi nikateta naye, akanihakikishia kwamba mambo yatakwenda vizuri. Pale Ludewa kuna mradi ulitengewa shilingi bilioni saba, lakini kwa miaka mitatu zimeletwa milioni 180 tu, kwa hiyo pana mkwamo mkubwa. Tarafa ya Masasi ina changamoto kubwa ya maji, pale Lupingu walitengeneza mradi wa maji ila umesombwa na maji kwa hiyo kuna changamoto.

Na vilevile pale Kiogo kuna wanafunzi huwa wanakwenda kuchota maji kwenye Mto Ruhuhu kwa hiyo wanaliwa sana na mamba. Manda Sekondari kuna changamoto kubwa ya maji na wataalam wamejitahidi kufanya upembuzi yakinifu Kata ya Mawengi na maeneo mengine…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Kamonga.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, ahsante. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa maoni yangu kwenye Mpango huu wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa. Nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa wasilisho zuri la Mpango na hasa vipaumbele sita vya Taifa letu kwa ajili ya kuleta maendeleo. Wananchi wa Ludewa wanaipongeza sana Serikali ingawa wana mashaka bado sababu wakati wa awamu ya nne hii miradi ya Mchuchuma na Liganga walishaandaa hadi eneo kwa ajili ya uzinduzi. Mheshimiwa aliyekuwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alishaandaliwa kwa ajili ya kwenda kuzindua Miradi ya Mchuchuma na Liganga lakini bahati mbaya mpaka sasa muda mrefu umepita.

Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya kuwa Serikali imeingiza miradi hiyo kwenye kipaumbele na imeweka mpango, lakini bado wananchi wana mashaka na hilo. Mimi kama kiongozi wao nimeendelea kuwapa moyo na kuwaaminisha kwamba Serikali ya sasa ni Serikali ya vitendo, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri tuwe pamoja kwenye hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo wananchi ambao wameathirika na Mradi wa Mchuchuma na Liganga nao wamesubiria fidia kwa muda mrefu sana takribani bilioni 11 ni pesa chache sana kwa Serikali iwapo dhamira ya kuwafuta machozi wananchi hawa ili waweze kuondoka kwenye maeneo haya wakafanye shughuli zao katika maeneo mengine. Toka miaka ya sabini wamezuiwa kabisa kuendeleza maeneo haya na fidia hawalipwi, kwa hiyo wananchi wanaona kama Serikali imekuwa katili kwao, hawa ni wananchi wa Nkomang’ombe na wananchi wa Mundindi na Amani ambao wanalinda mali hizi kwa muda mrefu sana. Kwa hiyo naomba hili la fidia litekelezwe, kwa sababu tunavyozidi kuchelewa thamani ya ardhi inazidi kupanda, tutaingia mgogoro mkubwa sana na wananchi iwapo hatutachukua hatua mapema. Kwa hiyo, hil ni muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa kuwa Wilaya hii ina miradi mikubwa miundombinu yake bado ni changamoto kubwa. Barabara inayoanzia Itoni kwa Mheshimiwa Deo Mwanyika, Lusitu mpaka Ludewa na kwenda Manda takribani kilometa 211.44. Tunashukuru Serikali imetutengenezea lami kwa kiwango cha zege, lazima tuwe waungwana tukubali na tushukuru, kilometa hamsini ambapo thelathini zimekwisha kukamilika. Kwa hiyo tunaomba barabara hii ikamilike yote kwa sababu Serikali hii imetuletea meli kule Ziwa Nyasa ambazo zinatoa mchango mkubwa sana kuinua uchumi wa mwambao, lakini bahati mbaya meli zile zinakosa mzigo wa kutosha kwa sababu barabara hizi hazijaunganishwa. Kwa hiyo uchumi huu na miundombinu yake lazima viwe na mawasiliano kwa sababu sekta moja ya uchumi inaweza kutoa mchango kwenye sekta nyingine. Sambamba na hilo wananchi wa mwambao wanaomba kuwe na kituo cha meli kwenye Kata ya Makonde ili iweze kusaidia hali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Wabunge wengi hapa wamechangia kwamba wananchi wengi Watanzania ni maskini sana na wanaishi vijijini zaidi ya asilimia 75. Kwa hiyo tukijitahidi kutafuta masoko ya mazao kwa maeneo ya vijijini, tunavyosema uchumi jumuishi, uchumi shirikishi tutawagusa wananchi ambao wanaajiriwa kwenye sekta ya kilimo. Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wanatoka maeneo vijijini kama mimi ambako kuna wakulima wengi, wamezungumzia mazao yanakosa masoko. Kwa mfano wilaya yangu wanaongoza kwa kulima mahindi, nitatoa takwimu chache, kwa mwaka 2019/2020 tani zilizozalishwa zilikuwa 110,800 lakini ambazo kwa makisio zinatosha kwa matumizi ya chakula ni tani 46,852, tani za ziada ni 63,239 na ambazo mnunuzi mkuu wa mahindi kwa kule ni hawa wanaitwa NFRA.

Mheshimiwa Naibu Spika, NFRA walikwenda wakanunua tani 709 tu. Kwa hiyo unakuta tani zaidi ya 62,000, mahindi ya wananchi yalioza kwa kukosa soko, kwa hiyo ni muhimu Serikali ikaona haja sasa ya kutafuta wawekezaji waweze kufungua viwanda kwa ajili ya kuzalisha vyakula vya mifugo, viwanda kwa ajili ya kusaga nafaka na kwenda kuuza katika maeneo mbalimbali ili kuweza kuongeza soko kwa wakulima.

Mhehimiwa Naibu Spika, wananchi wengi wa Jimbo la Ludewa na maeneo mengine wanalalamikia sana changamoto ya vijana kuhitimu vyuo vikuu na kukosa ajira. Kwa hiyo, tunavyozungumzia katika Ilani ya Uchaguzi kuzalisha ajira 8,000,000 wanaona kama ni chache sana, kwa hiyo wanaamini sekta mbalimbali hizi kama zitaanzishwa za viwanda na mikopo ya vijana kama ambavyo Mheshimiwa Nyamoga amezungumzia, tunaweza tukafungua soko la ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kwenye utumishi wa umma kuna pengo kubwa sana katika ile Seniority, kwa hiyo unakuta wako Principal Officer lakini wale Juniors hakuna, kwa hiyo kuna kupindi fulani tutazalisha tatizo kwenye utumishi wa umma na tutalazimika wakati mwingine kutengua baadhi ya kanuni za utumishi wa umma na sheria. Kwa mfano inakwambia ili mtu awe Mkuu wa Idara lazima awe amefanya kazi miaka saba, sasa itafika kipindi tutawakosa hawa watu, kwa hiyo lazima tuangalie na athari ambazo zinaweza kutoka hapo mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili watumishi wa umma muda mrefu kidogo hawajapandishiwa mishahara yao. Bahati nzuri aliyekuwa Rais wetu Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli apumzike kwa amani huko aliko, wakati akiomba kura aliahidi kwamba awamu hii anakwenda kutatua tatizo la ajira. Kwa hiyo ili kumuenzi, tumsaidie mama yetu mama Samia Suluhu Hassan kuweza kuajiri vijana ambao wengi hawana kazi. Hapa kwa kwakweli tutakuwa tumeongeza tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile na hii hoja ya kupandisha mishahara, nayo Mheshimiwa Rais wetu alikuwa ameshaahidi kwamba safari hii atapandisha mishahara na hili ni kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, Sheria ya mwaka 2002 inasema mtumishi wa umma atapanda daraja kila baada ya miaka minne wengine, wengine miaka mitatu, kwa hiyo kupuuza sheria wakati ipo wakati mwingine sio hekima sana, ni heri kuifuta. Kwa hiyo tuangalie hiyo, tuweze kuangalia watumishi wa umma kama ambavyo alama za Chama Cha Mapinduzi ni jembe na nyundo; jembe ni wakulima na nyundo ni wafanyakazi. Kwa hiyo tuwaenzi kwa sababu hata kwenye alama ya Chama cha Mapinduzi watumishi wa umma wamo na hawa wafanyakazi wamo.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hata wafanyabiashara kero zao bahati nzuri mama ameanza kuzishughulikia…

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sijui ni kengele ya pili, au ya kwanza?

NAIBU SPIKA: Ya kwanza, malizia mchango wako.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi nimshukuru Mheshimiwa Waziri William Lukuvi na Mama Mabula, walezi wangu hawa, wamenilea vizuri na nawaheshimu sana, walitoa ufafanuzi kwa swali alilouliza jirani yangu Mbunge wa Nyasa, Mheshimiwa Stella Manyanya kuhusiana na ile capital gain tax.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri na wewe ni Mwalimu wangu pale Law School, sheria inayoanzisha kodi hii ni Sheria ya Kodi ya mwaka 2004, Sura 332 na kuna sheria nyingine ambazo zinasimamia ambayo ni Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura ya 334, rejeo la mwaka 2002.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ambazo zipo kwenye kodi hizi ni kwamba ili mwananchi aweze kuhamisha umiliki wa ardhi yake ambayo amenunua au amepewa kama zawadi, anakwenda Ofisi zaidi ya moja, Ofisi za Ardhi zinahusika katika kufanya uthamini, TRA wanakwenda kukadiria kodi. Kwa hiyo ile ya mwananchi nenda hapa, nenda hapa imekuwa kama usumbufu, kwa hiyo kama wangeachiwa Wizara ya Ardhi kwa sababu Serikali ni moja, hii kodi wangeweza kuisimamia vizuri, nina imani sana na Mheshimiwa Lukuvi na Mama Mabula.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Kamishna wa TRA amepewa mamlaka makubwa sana kwenye hii kodi, kwa hiyo hii nayo inachanganya sana wananchi. Pia ina mlolongo mrefu na kupoteza muda wa mlipakodi, ile nenda sijui kafanye valuation, kwa hiyo wananchi wengi wanabaki na nyaraka wanajenga bila kubadilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo hayajapimwa vile vile kodi hii haitozwi, kwa hiyo kuna maeneo mengine katika miji mikubwa ambayo hayajapimwa transaction kubwa zinafanyika, lakini watu hawalipi kodi. Kwa hiyo kuna maeneo ya kuangalia na hata asilimia yenyewe kumi ni asilimia kubwa sana. Mtu ameuza nyumba milioni 100, asilimia kubwa, akiambia asilimia 10 anaondoka anaenda nyumbani na nyaraka. Kwa hiyo hapa tunaweza tukaangalia kuna mambo ambayo yanaweza yakarekebishwa ikiwa ni pamoja na elimu kwa mlipa kodi na vilevile kuboresha namna ya ukusanyaji. Mwananchi asisumbuliwe kuambiwa nenda hapa, nenda hapa, nenda pale, kuwe na mtu mmoja anasimamia kama ni wa Wizara ya Ardhi, afanye uthamini yeye kwa sababu ana watalaam, akusanye yeye kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono pia Waheshimiwa Wabunge waliozungumzia ile kodi ya majengo (Proper tax) ile wangerejeshewa halmashauri ili kuweza kuongeza mapato. Kwa sababu wana wataalam wa GIS wanaweza wakaweka vizuri mifumo ya ukusanyaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa wasilisho zuri na mpango mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hilo wananchi wa Jimbo la Ludewa wamenituma niombe mambo machache yaweze kufanyiwa kazi kwenye sekta ya barabara za vijijini na sekta ya afya. Kwa kuanzia na barabara za vijijini, mara zote tafiti zimekuwa zikituonyesha kwamba wananchi wengi wa Tanzania wanaishi maeneo ya vijijini na tatizo kubwa ni umaskini ambao unawasumbua. Kwa hiyo, ningependa kumwomba Waziri wa mwenye dhamana Ofisi ya Rais, TAMISEMI aweze kuwaongezea fedha watu wa TARURA ili zile barabara za vijijini ziweze kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina changamoto kubwa sana kule Jimboni kwangu Ludewa, kuna barabara inaanzia Lusitu inakwenda Madilu, Ilininda mpaka Mundindi; msimu huu wananchi wanatumia gharama kubwa sana kuweza kukodi bodaboda, barabara hazipitiki kabisa. Barabara hii hasa inayoanzia Madilu mpaka Ilininda halijapata matengenezo kwa miaka zaidi ya nane. Wananchi wa Ludewa wamekuwa wakijitolea sana kuchimba hizi barabara kwa majembe ya mkono, lakini wanakatishwa tamaa baada ya kuona Serikali haiwaungi mkono kwa kutenga fedha na kufanya ukarabati wa mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika, kuna eneo la Kigasi – Milo - Ludende mpaka Amani; barabara hii nayo ni muhimu sana, wananchi wa maeneo hayo ni wakulima, wana mazao mengi yanapaswa kupita kwenye barabara hii, lakini ina changamoto kubwa sana msimu wa mvua haiwezi kabisa kupitika. Mwaka huu nimelazimika mara kadhaa kwenda kushirikiana na wananchi kwa ajili ya kwenda kufanya matengenezo. Kwa hiyo, wananchi wanajihisi kama Serikali imewaacha, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri, naomba eneo hili liweze kuangaliwa na barabara hii ipewe fedha na kuweza kutengenezwa kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna ile Kijiji cha Masimavalafu, kuna Mto Ruhuhu ambapo panahitajika kivuko, ambako inakuwa ni rahisi sana wananchi kwenda Hospitali ya Peramiho kuweza kupata matibabu. Kwa hiyo katika eneo hili tungeomba hata kama kuna kivuko kimeachwa sehemu, tupewe sisi kitusaidie pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia na sekta ya afya; naomba sana hawa wananchi tunaowahamasisha waweze kuwa na hizi bima za afya, wanavyokwenda hospitali waweze kupata dawa na matibabu stahili yanayohitajika. Maana imekuwa ni changamoto kubwa sana, wataalam wanajitahidi kuwahamasisha wananchi wanakuwa na bima za afya lakini hawapati huduma kwa kiwango kile ambacho kinakubalika. Kwa hiyo, naamini sana Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake wote wawili wanaweza wakasimamia eneo hili tukaboresha ili wananchi waweze kuona kwamba Serikali inawathamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, napenda kushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hii ya Wizara nyeti ambayo inawagusa wananchi moja kwa moja. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri, Mheshimiwa William Lukuvi, kimsingi huyu ni mlezi wangu, kwa sababu miaka 10 ambayo nimefanya kazi kwenye sekta hii, amenitumia vizuri sana na nimejifunza mambo mengi sana. Kwa hiyo, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile namshukuru Mheshimiwa Angeline Mabula, naye amekuwa kama mzazi na mlezi wa karibu, kwa kweli niwapongeze, mnafanya kazi nzuri sana. Nampongeza Katibu Mkuu, Mary Gasper Makondo, bosi wangu wa zamani, naye anafanya kazi nzuri sana. Naweza kusema ni Katibu Mkuu wa kwanza ambaye ame-practice kwenye sekta hii kwa muda mrefu. Kwa hiyo, anaisimamia vizuri na anaifahamu sana. Kamishna Mathew na Makamishna wenzangu wote, maana mimi niliachia hicho cheo cha Ukamishna Mkoa wa Dodoma. Kwa hiyo, nawashukuru sana, tupo pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi, naomba Serikali iangalie Wizara hii kwa jicho la karibu sana, kwa sababu ardhi ni rasilimali namba moja. Mheshimiwa Waziri wa Fedha anajua, ni mchumi mzuri kwamba number one resource ni ardhi. Migogoro mingi siyo wakati wote inatokana labda na matatizo yaliyomo kwa wataalam, wakati mwingine ni kutokana na ardhi yenyewe kuwa ni kitu cha thamani. Kitu cha thamani lazima kigombaniwe. Changamoto za wataalam zipo, lakini na ardhi yenyewe nayo ni tatizo kwa sababu ni kitu cha thamani, kwa hiyo, inahitaji umakini zaidi na bajeti ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukiangalia wakati huu; nampongeza Mheshimiwa Waziri na Serikali wameanzisha Ofisi za Mikoa, maana yake huduma zimesogea jirani na wananchi. Kwa hiyo, wananchi wanapata hati kwa gharama nafuu zaidi na gharama ya muda, gharama ya fedha tumeweza kumwondolea mwananchi wa hali ya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali, lakini niombe sasa Serikali iweze kuongeza fedha kwenye hii Wizara kwasababu nayo itakuwa na fursa yakukusanya zaidi iwapo itapewa vitendea kazi. Nitatoa mfano mmoja, pale Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Mkoa, nina maana ya Ofisi ya Ardhi Mkoa, ina vitengo vinne ambavyo vinafanya kazi tofauti kabisa. Kuna watu wa Mipango Miji, kuna Kamishna wa Ardhi, kuna Wathamini na kuna wale Wapima. Sasa kila mmoja unakuta anahitaji aweze kusafiri kwenda kusimamia kazi, kuna miji mipya huko inakua, inatakiwa itangazwe kwenye magazeti ya Serikali ili ipangwe, lakini wanashindwa kutokana na vitendea kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Wizara hii iweze kuongezewa fedha ili ofisi zile za mikoa ziweze kuboreshwa na kuwa na vitendea kazi vya kutosha; kama vyombo vya usafiri na vifaa vya kupimia ardhi, maana sasa hivi teknolojia imekuwa kubwa. Vile vile wakiongezewa fedha za kutosha wataweza kuboresha hii mifumo ya ardhi; Kuna mfumo unaitwa ILMIS, kuna mfumo unaitwa Land Rent Management System na mifumo mingine ambayo inahitaji uwekezaji mkubwa wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mifumo hii itawezesha Wizara kupunguza muda ambao mwananchi anapata huduma, kwa sababu kila kitu kikiwa kwenye computer ni mouse click mwananchi anahudumiwa. Kwa sababu kitu ambacho kinawakwaza sana wananchi kwenye hii sekta ni upotevu wa muda, kwa sababu sekta hii ina mambo mengi. Kuna mtu anaandaa michoro ya mipangomiji, kuna mtu mwingine anaenda kupima na kuweka beacon, kuna mtu anafanya uthamini kwa ajili ya fidia na mtu mwingine anamilikisha. Kwa hiyo, kuna milolongo mingi ambapo hakuna mlolongo ambao unaweza ukauacha kisheria na kila kitu kipo kwa nia njema. Kwa hiyo, wakiongezewa fedha, waweze kuboresha mifumo hii ya umilikishaji ardhi na utunzaji wa kumbukumbu tutaongeza sana tija kwenye sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile Wizara hii ina upungufu sana wa watumishi, kwa hiyo, naomba Serikali iweze kuangalia namna ya kutoa kibali ili watumishi waweze kuajiriwa. Kwa mfano, mahitaji ya watumishi kwenye sekta hii; nilikuwa nasoma hotuba ya bajeti, inaonekana ni 4,847 lakini watumishi waliopo ni 2,378. Upufungu ni watumishi 3,114, lakini wenzetu wa Utumishi wa Umma wametoa kibali cha kuajiri watumishi 36 tu. Kwa kweli hapa tutaendelea kulaumu Wizara hii kwa sababu hatuwawezeshi kuajiri watumishi wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri tuna vyuo vikuu; tuna chuo kinafundisha pale Morogoro, ni chuo kizuri, kinatoa wataalam wa ngazi ya Cheti na Diploma ya Upimaji, kuna chuo Tabora nacho kinatoa mpaka ngazi ya Diploma, kuna Chuo Kikuu cha Ardhi, kuna Chuo Kikuu cha Dodoma, kuna Chuo cha Mipango na vyuo vingine, vinatoa wahitimu hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka pale Jiji la Dodoma tulikuwa na watoto wanakuja ku-volunteer wakati mwingine wanafika mpaka 50, 60 na wengine tumewafundisha kazi, ni wazuri. Kwa hiyo, kuendelea kuwatumia wakiwa wanajitolea ni risk sana kwa Serikali. Kwa hiyo, napenda kutoa ushauri kwa Serikali, iweze kuwaajiri hawa na wengine ambao wapo mtaani ili waweze kusaidia kuongeza kasi ya upangaji ardhi, upimaji na utoaji hati za umiliki wa ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile napenda kuzungumzia kipengele cha upimaji, upimaji shirikishi na urasimishaji. Wabunge wengi wameonekana hawajaridhika sana na kipengele cha urasimishaji. Hii kurasimisha maana yake ni kufanya makazi ambayo hayakuwa rasmi yawe rasmi. Sasa mazoezi haya huwa yanakuwa na migogoro na malalamiko mengi sana kwa sababu wananchi tayari wameshaendeleza maeneo yao, namna ya kuwapanga kwa kweli ni lazima itokee migogoro mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ile ya upimaji shirikishi ni njia ambayo inasaidia sana kuepusha matatizo ambayo yanatokana na uhitaji mkubwa wa fedha kwa ajili ya fidia. Kwa hiyo, kama fedha hamna, maana yake wataalam watakubaliana na wananchi, wanawapimia viwanja, halafu wanagawana viwanja. Viwanja vingine vinakuwa vya wenye ardhi na vingine vinakuwa vya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachotakiwa tu, wale wananchi kwa sababu tunawapa viwanja vingi, tuweke tu utaratibu wa kuwasaidia kuuza ili wapate kipato ambacho kinaendana na bei ya soko. Vinginevyo wananchi hawa watakuwa na viwanja vingi na hawana cha kufanyia. Kwa hiyo, tungeweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia kuuza ili wapate fedha halali ya haki ambayo inaendana na bei ya soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naipongeza Wizara kwa kuanzisha huu mfuko wa kukopesha fedha kwenye Halmashauri. Sasa Wizara iende mbali zaidi, iangalie pia na haya makampuni binafsi ambayo yanatambulika na Bodi za Mipango Miji na Upimaji. Kama nao wanaweza kuwakopesha hata kwa interest kidogo ili wabadilishe mfumo wa utendaji wao wa kazi, kwa sababu inaonekana hawana mitaji na ni Watanzania, wamesajiliwa na vyombo vinavyokubalika, kwa hiyo, wakipewa mikopo hii hata kwa riba kidogo, tutakuwa tunatengeneza ajira ndani ya nchi yetu na vile vile tunaongeza kasi ya upimaji na sasa hivi upimaji wao kwa kiasi kikubwa unategemea fedha za wananchi. Ndiyo maana utakuta takwimu zinaonesha makampuni binafsi yanawadai wananchi zaidi ya shilingi bilioni 70. Sasa kwenda kupima kutegemea hela ya wananchi ni changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naomba kule kwangu Ludewa, nami nina miji midogo mitano ambayo imetangazwa tokea mwaka 2001 ila bado haijapimwa; na wananchi wa Ludewa wanaamini kwamba Mbunge wao ni mtaalam mbobevu kwenye Sekta ya Ardhi. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri na wataalam wako mniondoe aibu hapa ili tuweze kuwapimia wananchi. Kuna Kijiji cha Lugarawa, Mawengi, kuna Manda pale, kuna Beach Plots, kuna Kijiji cha Amani ambako miradi ya Mchuchuma na Liganga inakwenda, kuna Kijiji cha Mavanga na Mawengi. Kwa hiyo, maeneo haya bila kusahau Kata ya Mlangali pale, ni maeneo ambayo yameshaiva kimji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Nashukuru sana Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu aliwapokea Madiwani wangu, walikwenda pale Wizarani wakapata mafunzo. Kwa hiyo, wana ari ya kupokea hii huduma ya mipango miji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, naunga mkono hoja, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia mipango hii ya maendeleo ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu. Niwashukuru pia wale wote ambao wameweza kutambua juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kueleza kwamba asilimia 75 mpaka 80 ya Watanzania wanaishi kijijini na ni maskini. Tushukuru Serikali kwa kutuingiza kwenye uchumi wa kati ila pia tuiombe iongeze fursa, kazi ya Serikali ni kuandaa mazingira mazuri ya biashara ili watu waweze kupata kipato na pato la Taifa liweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo pia nimshukuru dada yangu, Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana, amezungumzia changamoto ya bei ya mbolea. Ni kweli; kwa mfano kule kwetu Ludewa mfuko mmoja wastani unauzwa kati ya 56,000 mpaka 65,000 na kwa ekari moja mkulima anatumia mifuko siyo chini ya minne ambapo mavuno yake anapata sanasana roba kumi. Sasa akija kuuza hizi roba kumi, roba moja shilingi 40,000, kwa hiyo anapata mapato ya shilingi 400,000 wakati amewekeza gharama zaidi ya shilingi 400,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie namna sasa, nashukuru Mheshimiwa Waziri wa Kilimo amekaa na wataalam wa kilimo na kuweka mikakati. Hii ni ishara njema na nimwombe yale ambayo ameahidi aweze kuyatekeleza kwa sababu Wabunge wengi humu tunatokea maeneo ambapo wananchi wetu ni wakulima na wanategemea hasa jembe la mkono. Kwa hiyo naamini atawatoa jembe la mkono wakulima wale ambao asilimia kubwa wako vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na vituo vya utafiti, lakini vituo hivi vijengewe uwezo zaidi ili viweze kutoa taarifa nzuri na taarifa hizi zisibaki kwenye makabrasha, wawashirikishe wataalam wa kilimo kwenye halmashauri zetu, zinaweza kusaidia katika kuongeza tija. Vile vile kwenye ile mikoa yetu ambayo inajishughulisha na kilimo kungekuwa na vituo ambavyo vinafanya uchunguzi wa udongo, zile maabara. Kwa sababu mwananchi anaweza akawa anatumia mbolea ambayo saa nyingine haihitajiki kwenye udongo wa eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulivyokuwa kwenye Mkutano wa RCC Njombe, watu wa madini waliwasilisha taarifa kwamba Wilaya ya Ludewa ina leseni 104 za madini ambazo hazitumiki zimekuwa zikihuishwa tu. Kwa hiyo waliomba kwamba kwa kuwa eneo hili linaweza kutoa ajira nyingi kwa Watanzania na Wanamkoa wa Njombe na kanda nzima ile ya nyanda za juu; leseni hizi ziweze kufutwa, maeneo haya yagawiwe kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuongeza kipato chao na kipato cha Taifa kiongezeke. Namshukuru Mheshimiwa Waziri, aliahidi kwamba atalishughulikia na atafanya ziara Ludewa; nimshukuru sana. Wananchi wa Ludewa wanamsubiri kwa hamu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile wanaomba kwenye eneo la makaa ya mawe pale kuna leseni kubwa mbili ambazo zote zimeshikiliwa na Serikali. Sasa si halmashauri mapato pale ni hafifu sana, milioni 800 na sisi tulitamani Mheshimiwa Waziri wa Madini angetumegea kidogo halmashauri pale tuweze kuwekeza kwenye uchimbaji ili pato letu la halmashauri liinuke, tuweze kuhudumia wananchi. Tukihudumia vizuri wananchi maana yake watakuwa na kipato kizuri watafungua biashara na Serikali itapata mapato kupitia kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Sheria ya Kodi ya Mapato, TRA. Kuna kodi moja inaitwa Capital Gain Tax; mwananchi anavyonunua au kuuza ardhi hii kodi inatozwa kwa mujibu wa Sheria ya Mapato ya Mwaka 2004. Kodi hii siyo rafiki, wananchi wengi ambao wananunua ardhi wanashindwa kuhamisha umiliki wa viwanja vyao. Kwa hiyo naomba iangaliwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze wewe binafsi Mheshimiwa Waziri, Naibu wako pamoja na wasaidizi wenu wote kwa namna mnavyoisimamia vizuri Wizara hii nyeti iliyotoa ajira kwa Watanzania walio wengi (75%) na kuchangia 24% ya pato la Taifa. Kutokana na umuhimu huo, na mimi naomba kuchangia yafuatayo:-

Kwanza, Serikali iingie ubia na wawekezaji wa ndani na nje ili kuweza kujenga viwanda vikubwa vya mbolea hapa nchini ili isaidie kupunguza gharama kwa wakulima wetu. Mfano toka Ludewa DAP inauzwa shilingi 80,000 kwa mfuko 24/05/2021, CAN mfuko mmoja unauzwa shilingi 58,000 na UREA ni shilingi 55,000.

Pili, kodi za matumizi ya maji kwa watumiaji wa maji ziangaliwe vizuri ili kodi hizo zisiwe mzigo kwa wakulima na hivyo kudidimiza sekta ya kilimo. Wizara ya Kilimo ikutane na Wizara ya Maji na Mamlaka za Mabonde ili kujadili hilo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo; mazao yote ni mazao ya biashara hivyo mtizamo wa kuwa kuna mazao ya chakula na mazao ya biashara unatuchelewesha kuboresha kilimo cha mahindi, alizeti, karanga na ufuta kufanyika kibiashara na kumnufaisha mkulima. Mazao yote haya ni malighafi kwenye viwanda.

Mheshimiwa Spika, Wizara za Serikali zijenge utamaduni wa kukutana na kujadili masuala mtambuka, mfano barabara za vijijini zikiwa bora na zipitike msimu wote hakika zitachangia sana kuinua sekta ya kilimo na viwanda vya uongezaji thamani ya mazao. Wakulima walioko maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao wanakabiliwa na changamoto kubwa za ubovu wa barabara Ludewa. Mfano barabara ya Lusitu-Madilu-Ilininda-Mundindi kuna viazi, chai, kahawa, mahindi, maharage, njegere, mbao na parachichi. Pia barabara ya Kigasi-Milo-Ludende-Amani au Muhoro-Ludende-Mkongobaki-Lugarawa; barabara ya Ludewa- Ibumi-Masimavalafu au Nkomang’ombe-Iwela-Bandari ya Manda na Luilo-Lifua-Liugai na maeneo mengineo.

Mheshimiwa Spika, vyuo vikuu vya kilimo vishiriki kwa vitendo katika kufanya utafiti, ubunifu na kuelimisha wakulima ili kuongeza tija vyuo viendeshe mashamba ya mfano hasa mazao yatakayouzwa nje na kuingiza mapato ya kigeni.

Mheshimiwa Spika, vijana wanaomaliza mafunzo ya JKT wapewe mikopo chini ya uangalizi na waanzishe mashamba ya miwa, alizeti ili kuzalisha sukari na mafuta ya alizeti na karanga.

Mheshimiwa Spika, wahitimu mbalimbali wa vyuo vikuu nao wawezeshwe mitaji ili kujiajiri kwenye kilimo cha kibiashara na kukuza uchumi wa nchi na kujiongezea kipato chao.

Mheshimiwa Spika, Serikali iajiri wataalam wengi wa kilimo na kuwasambaza kwenye kata na vijiji vyetu nao wapewe malengo, wafuatiliwe ili watende kazi kama sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika bajeti hii. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Doto Biteko, Waziri kwa wasilisho zuri. (Makofi)

Vilevile nitumie nafasi hii kutoa pole sana kwa Mwenyekiti wa CCM wa Jimbo la Ludewa kwa kuondokewa na Diwani Viti Maalum mama yetu mpendwa Grace Mapunda.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nianze kwa kusema naamini kwamba rasilimali inafaa kuitwa rasilimali pale ambapo inatumika kikamilifu ili iweze kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa letu. Kama tuna rasilimali halafu tunaziangalia tu hapo inapaswa tutafute jina lingine, sio rasilimali tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo, Jimboni kwangu Ludewa kuna madini mengi ambayo watu wa GST wameweza kuyabaini na hivyo watafiti mbalimbali wamekuwa wakienda kule. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba anajitahidi kufanya vizuri sana, wale watafiti wa madini wanavyokwenda kwenye vijiji wanavamia mashamba ya wananchi bila kulipa fidia na mashamba mengine yanakuwa yako kwenye miliki za vijiji kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Na.5 ya mwaka 1999.

Mheshimiwa Spika, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Ibara ya 24 inazungumzia haki ya kila mwananchi kumiliki mali na mali yake ilindwe na Serikali na pale inavyotwaliwa anapaswa kulipwa fidia. Sasa watafiti wa madini wakienda kule wanavamia mashamba ya wananchi wanaanza kuchimba bila kulipa fidia.

Mheshimiwa Spika, zile fedha wangekuwa wanalipa kama ni kwenye vijiji au wananchi zingesaidia sana hasa kupunguza michango ambayo wananchi wanatozwa kila leo kwa ajili ya madawati, madarasa na vituo vya afya. Kwa hiyo, kama vijiji vingekuwa vinalipwa ile fedha kama fidia ya ardhi yao ambayo wanaichimbachimba kufanya utafiti kwa sababu wanaochukua leseni za utafiti wengine wanachimba madini, wakilipa zile fidia zitasaidia vijiji vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nipongeze Bunge lako Tukufu hasa la Awamu ya Tano ambalo liliweza kupitisha sheria nyingi za kulinda rasilimali zetu. Naomba sasa elimu itolewe kwa wananchi na wapewe maandalizi hasa maeneo ambapo miradi mikubwa inakwenda kuhusu nini sheria hizi zinazungumzia kuhusiana na masuala haya. Kwa mfano, kule jimboni kwangu tunaenda sasa kutekeleza mradi wa Mchuchuma na Liganga lakini wananchi hawajaandaliwa.

Mheshimiwa Spika, wale Waheshimiwa Madiwani pia wanaweza kupewa mafunzo kuhusiana na hii CSR, kwa sababu unakwenda kujadiliana na mtu ambaye ni tajiri, bepari, mwenye uwezo kwa hiyo nao wawe wamejengewa uwezo wazijue vizuri hizi sheria ili waweze kutetea haki zao. Kwa sababu hii CSR ukisoma Sheria ya Kodi ya mwaka 2004, kifungu cha 16 kinatumika katika kufanya assessment ya kodi zingine. Wanaotoza kodi wanaangalia mchango wake alioutoa kwenye hizo CSR kwenye jamii. Kwa hiyo, sio hisani kama ambavyo tunadhani, wale wanasheria wa Halmashauri Waheshimiwa Madiwani na wakuu wa idara wajengewe uwezo ili waweze kujiamini. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba sana tumsikilize mchangiaji hata ninyi mkisikiliza kwa masikio yenu mtaona kuna haja ya kupunguza sauti.

Endelea Mheshimiwa Kamonga.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunilinda. Naomba hizi sheria nzuri ambazo zinalinda rasilimali zetu ziweze kutolewa elimu na wananchi wajengewe uwezo ili kuandaliwa na miradi mikubwa ambayo inakwenda kwenye maeneo yao waweze kujua haki na wajibu wao na waweze kutetea haki zao. Vinginevyo wananchi wataendelea kutembea kwenye ardhi tajiri lakini wao wataendelea kuwa maskini. Kwa hiyo, hivi ni vitu vya muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nimuombe Mheshimiwa Waziri atoe tamko juu ya wachimbaji wadogo ambao waliomba vitalu vya makaa ya mawe pale Ludewa kwa sababu soko ni kubwa, rasilimali hizi zipo tumeendelea kuziangalia tu kwa miaka mingi. Ndiyo hayo sasa tunasema kama rasilimali hazitunufaishi hizo sio rasilimali tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo wako tayari na masoko wanayo, kuna wachimbaji wengine wazalendo kama Kampuni ya Maganga Matitu na kuna vikundi kule niliwatembelea wengine nimeona wanachimba copper kwa kutumia nyundo na tindo. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie namna ya kuwawezesha wachimbaji wadogo ili waweze kukuza mitaji yao, ikiwezekana kuwapa vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti hii muhimu ya Viwanda na Biashara, lakini vilevile nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, bajeti yake imekaa vizuri na inaleta matumaini na pia niipongeze Kamati ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Kihenzile kwa sababu walifanya ziara jimboni kwangu kuangalia miradi mikubwa ile ya Mchuchuma na Liganga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli bajeti inaleta matumaini, tunamuomba tu Mheshimwa Waziri aendelee kuisamimia ili iweze kutekelezwa. Na bahati nzuri nimekaa naye jana kwa muda mrefu kidogo akiwa na Naibu wake na wiki iliyopita baada ya kumuomba aweze kutembelea Jimboni Ludewa aliridhia kwamba atakwenda baada ya kuwasilisha bajeti hii ili aweze kuzungumza na wananchi. Mheshimiwa Waziri nakushukuru sana na wananchi wa Ludewa wanakusubiri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali kadhalika siku chache zilizopita Waheshimiwa Madiwani wa Jimbo la Ludewa walikuwepo hapa Bungeni na waliweza kukutana na Mheshimiwa Biteko, nako walileta mawazo yao mbalimbali Mheshimiwa Waziri aliweza kufafanua vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwashukuru pia Waheshimiwa Wabunge mbalimbali ambao nao wamekuwa wakiona kwamba miradi hii ya Mchuchuma na Liganga ni muhimu sana na ni kitovu kwa uchumi wa nchi yetu. Wabunge wengi sana wamechangia juu ya miradi hii, kwa hiyo, wanaonesha kwamba wanaona umuhimu wa miradi hii. Kwa hiyo naomba sana Serikali iweze kuwa sikivu iwasikilize Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia umuhimu wa miradi hii maana na sauti za Wabunge ni sauti za wananchi moja kwa moja.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Ludewa wanapoona miradi inazinduliwa maeneo mengine wanajisikia wanyonge sana, wanasononeka, wanafadhaika, lakini kwa mpango huu wanakuwa wana imani kwamba miradi hii sasa itakwenda kutekelezwa, hasa hasa suala la fidia kwa wananchi wa Mchuchuma pale vijiji vya Nkomang’ombe, Kipangala, Iwela wanadai fidia na wamesubiria kwa muda mrefu sana. Wananchi wa Kijiji cha Amani na Mundindi wamesubiria fidia hizi tokea mwaka 2015.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kwa fedha hizi zilizotengwa Mheshimiwa Waziri atakwenda kuwalipa fidia wananchi wale mapema iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mzee mmoja alikuwa anaitwa Mzee Machupa, mwaka 2017 aliwahi kuwaeleza wananchi wa NDC kwamba hizi fidia Serikali inashindwa kutulipa wanataka ije ijenge makaburi yetu, tutakufa tutaziacha hizi fedha, bahati mbaya mzee yule Mwenyezi Mungu amemchukua bila kulipwa zile fedha. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana utekelezaji wa jambo hili na kukumbusha ile ziara ya Ludewa kwenda kuzungumza na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na vilevile tutambue kwamba katika madini haya tunazungumzia tu makaa ya mawe na chuma, kwenye chuma cha Liganga ambacho kinaonekana kwamba kuna mashapo ya chuma ambayo ni tani milioni 126, kwa eneo la kilometa 10 tu ambao walijaribu kufanya uchunguzi. Lakini kwa eneo lote linakadiriwa na tani milioni 700 mpaka milioni 1,400 za chuma ambazo ndani yake kuna madini mengine ya titanium, ya vanadium na madini haya ni muhimu sana kwa sababu mengine yanatumika kutengeneza vitu vya thamani sana, kama laptop, computers na ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuna madini mengine ambayo yanathamani kubwa, kwa hiyo, hii ni utajiri mkubwa kwa nchi yetu, ni Serikali haina sababu ya kutoanza miradi hii. (Makofi)

Vilevile miradi hii naomba Serikali izidi kuwasiliana, Wizara za Serikali, kwa sababu uwekezaji huu tunavyosema kwamba ni mradi kielelezo, miundombinu nayo inapaswa iendane na miradi hii. Bahati mbaya sana nilisoma bajeti ya Wizara ya Ujenzi nikaona uwanja wa ndege wa Njombe haumo kwenye mpango, wakati Mheshimiwa Rais wa Jamhuri mama Samia Suluhu Hassan alivyokwenda kwenye...

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Neema Mgaya.

T A A R I F A

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nilikuwa napenda kumpa taarifa kaka yangu Joseph Kamonga, Mbunge wa Ludewa, nilikuwa napenda kumwambia kaka yangu Joseph kwamba Serikali pia itueleze imejiandaa vipi kwenye mradi huu wa Liganga na Mchuchuma kuwatayarisha wananchi wetu wa Ludewa kuupokea mradi ule, kuwapa elimu namna gani ambayo wananchi wataweza kwenda kunufaika na fursa mbalimbali zitakazotokana na mradi huu wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Joseph.

MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii kwa sababu ananikumbusha NDC walianzisha mradi wa kuelimisha jamii unaitwa PAKA. Mradi ule haupo tena, nina imani Mheshimiwa Waziri atatoa taarifa na atasema bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kuwapa elimu wananchi wa Jimbo la Ludewa na maeneo jirani ili waweze kujiandaa na miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo uwanja wa ndege nayo ni sehemu ya uwekezaji, bahati mbaya Wizara ya Ujenzi nimeona wameondoa wakati ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi na wananchi wa Njombe kiasili ni wafanyabiashara kwa hiyo uwanja ule ni muhimu sana na unaendana na miradi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu. Nianze kwa kumpongeza sana Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan hasa kwa kauli yake aliyoitoa akiwa Mwanza kuhusu madini ya Mchuchuma na Liganga. Jana nilikwenda Ludewa Jimboni na kauli ile ilivyotoka nimepokea meseji nyingi sana kutoka kwa wananchi wa Ludewa kwamba sasa Mama yetu kweli ameikumbuka Ludewa kwa kuanzisha miradi hii na wanaomba sana viwanda vijengwe eneo lile lile la Ludewa, ili kuweza kufanya kitu ambacho wachumi wanaita diversification of economy na hizo decentration of industries.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itasaidia sana kupunguza wale vijana wa Mkoa wa Njombe ambao wanahama sana kwenda maeneo ya mbali kutafuta ajira. Kwa hiyo kukiwa na viwanda kule tutapunguza msongamano wa watu kwenye Jiji la Dar es Salaam, Dodoma na Miji mingine mikubwa kama Mwanza na maeneo mengine. Vijana wengine wabaki kule ili na mimi niwe Mbunge ambaye nina nguvu kazi ya kutosha, sio vijana wakishakua wanakwenda kutafuta ajira maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile wameomba sana katika miradi hiyo kuwe na maandalizi ya wale wananchi waweze kupewa elimu waone namna ya kunufaika na hizo fursa; kwa sababu miradi hii inakwenda kunufaisha kwa kiasi kikubwa Taifa letu kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengine wameeleza. Vile vile tukiwaandaa wananchi na ile local content na ile community base inayozunguka mradi ikaweza kupata manufaa na wakati na Taifa nalo linapata manufaa kutokana na miradi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo wananchi wa Ludewa licha ya kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu, wameomba vilevile wasaidizi wake waiangalie Ludewa kwa macho ya karibu. Kwa sababu imeonekana kuna miradi yake mingi ambayo inakwama; kuna daraja la Ruhuhu limekwama kwa takriban miaka sita. Jana nilikwenda kule Mwenyekiti wa Kijiji alinipeleka pale, wamelima sana mpunga bonde la Ruhuhu, soko lipo Ruvuma kwa sababu Kyela ni mbali, lakini wale wachuuzi wanashindwa kwenda kwa sababu kuna kivuko pale toka mwezi Septemba, 2020 hakifanyi kazi na daraja hilo ndio toka mwaka 2016 limekwama. Kwa hiyo haya yanaweza kusaidia kuleta tafsiri nzuri ya uchumi jumuishi, uchumi shindani iwapo na wananchi wote wanaweza kupata manufaa. Kwa hiyo naomba hilo liweze kuangaliwa kwa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulisema hapa pia mradi mwingine ambao umekwama kwa muda mrefu ule wa VETA. Miaka karibu 10, ulichimbwa msingi, wamezungusha mabati, kwa hiyo wananchi wa Ludewa wanajiona wao ni losers wakati wote. Kwa hiyo hili la Mama kuweza kutaja jana kwamba Serikali sasa imepania kuanza kushughulikia Mradi wa Mchuchuma na Liganga limeleta faraja kubwa sana kwa wananchi wa Ludewa na wamekuwa na Imani kubwa sana na Serikali hii na kimsingi mimi sina sababu za kutounga mkono bajeti hii. Kwa hiyo naunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono kwa sababu nimeangalia vile vile kuna maeneo kama ya sekta ya afya, kuna changamoto ile ya watu kwenda kupata dawa. Mtu anakuwa na bima ya afya, anakwenda hospitali lakini walikuwa wanachelewa kupata dawa. Kwa hiyo sasa naona kwa bajeti hii inakwenda kumwangalia mwananchi wa chini ili aweze kupata matibabu ambayo ni ya uhakika. Ila tu niiombe Wizara ya Afya waangalie pia baadhi ya sheria ambazo wamezitoa kwenye Vituo vya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sheria inazuia Kituo cha Afya kumwandikia mgonjwa baadhi ya dawa. Sasa sisi ambao tupo maeneo ya pembezoni, kuna mwananchi anatakiwa kutembea kilometa 140 kutoka Mavanga mpaka Ludewa kwenda kufuata matibabu. Kwa hiyo kama kuna Kituo cha Afya pale Jirani, Daktari aliyopo Kituo cha Afya sasa hivi tunashukuru Serikali imetuletea qualified Doctors, kwa hiyo wangeruhusiwa, lazima tuangalie intension of ile legislation, ile dhamira ya kuweka ile sheria ya kuzuia. Miaka hiyo kulikuwa hakuna wataalam kwenye Vituo vya Afya, sasa hivi tunao. Kwa hiyo miongozo ya aina hiyo kwa kweli tuweze kui-review na kuweza kuruhusu Vituo vya Afya kuandika dawa kwa sababu kuna wataalam wa kutosha. (Makofi)

Mheshiwa Naibu Spika, nipongeze pia agizo moja liliwahi kutolewa na Mheshimiwa Ardhi, Mheshimiwa William Lukuvi kwamba kwenye maeno ya hii miradi mikubwa ya mikakati kama kwenye SGR kufanyiwe mipango ya matumizi bora ya ardhi ili sasa mindset zetu ziweze kubadilika. Zibadilike kwa sababu watu wengi wanavyoona kwamba reli imetoka bandarini na kwenda maeneo mbalimbali, wanadhani iko maalum kwa ajili ya kusafirisha mizigo inayotoka viwandani peke yake au inayotoka nje ya nchi, kumbe maeneo yale ya ardhi ya pembezoni kufanyiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi kama ilivyoelekezwa katika Sheria ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi Na. 6 ya mwaka 2007, wananchi wanaweza kutenga maeneo kwa ajili ya kilimo, mifugo na vile vile kuzalisha mazao yakasafiri kupitia reli hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii itasaidia sana kuinua kipato cha wananchi na wanaoishi kandokando ya Reli. Wataweza kuzalisha mazao ya kutosha, kunaweza kukawa hakuna mwingiliano wa matumizi ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, matokeo yake hii reli itapata mzigo wa kutosha, kwa sababu kilimo nacho kinatoa mazao kwa ajili ya viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kuangalia lile eneo la malipo ya mbele wakati mwananchi anamiliki ardhi premium. Eneo hili lilikuwa linawasababisha wananchi wengi sana wanashindwa kuchukua hati miliki za ardhi kwa kushindwa gharama. Kwa hiyo kitendo cha kupunguza ada hii ni ukombozi mkubwa sana kwa wananchi hasa wa hali ya chini. Kwangu kule Lugarawa wananchi wale wameanza kufanya mambo ya urasimishaji na Mlangali na maeneo mengine. Naamini nao watamudu kupata hati miliki bila kikwazo. Kwa kweli hii nipende kuipongeza sana Serikali na tuangalie pia maeneo mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge wameendelea kuyalalamikia na kushauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi baadhi ya Wabunge wamezungumzia kwenye ile kodi ya Majengo. Ni vema sana tukaziangalia halmashauri zetu ambazo vyanzo vingi vya mapato vilichukuliwa. Kwa hiyo tujitahidi sana kuwaajiri wale vijana waliosoma GIS ile Geographical Information System. Wale wanaweza kukusanya taarifa za majengo yote wakayaweka kwenye mifumo ya kompyuta, ukiwa pale ofisini unaweza ukaona kila jengo na kuweza kujua kirahisi uweze kutoza kodi kiasi gani. Vijana hawa wanasoma katika Vyuo vya Ardhi, kuna Chuo cha Ardhi Tabora na Chuo cha Ardhi Morogoro na vyuo vingine ambavyo vinatoa mafunzo kama hayo wanaweza kusaidia sana kuboresha ukusanyaji wa kodi ya majengo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile nilichokuwa namwomba Mheshimiwa Waziri waangalie hiyo asilimia 15 kupeleka kwenye halmashauri ni changamoto haitoshi, wangefikiria kuongeza ongeza kidogo, kwa sababu Wakurugenzi wengi ukiwaangalia ukiwakuta kama hana ugonjwa wa moyo, basi ana presha au ana kisukari au tatizo lingine. Inakuwa hivyo kwa sababu wana matatizo mengi sana lakini hawana fedha. Kwa hiyo eneo hili tungeliangalia, hata halmashauri zingeachiwa asilimia 50, ingesaidia hata kujenga madarasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetembelea baadhi ya madarasa kwenye jimbo langu, yana hali duni sana. Unakuta darasa ni la vumbi. Nilikwenda Shule ya Msingi Liunji, nashukuru Serikali ilipeleka fedha pale, lakini ndio maana naomba sasa halmashauri zifikiriwe kuongezewa mapato. Wakurugenzi wataweza kumudu changamoto ndogo ndogo za madarasa na vituo vya afya. Nitatoa mfano kwenye jimbo langu, kuna kata saba ambazo zimejenga vituo vya afya lakini wanashindwa kumalizia. Wakurugenzi wangekuwa na fedha mambo yangekuwa mepesi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nirudie kumpongeza sana na kumshukuru Rais mpendwa kwa hoja yake ya jana ya Mchuchuma na Liganga. Wananchi wa Ludewa wanampenda, wanamwombea na wanamkaribisha sana Ludewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia bajeti hii ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Kalemani na Naibu wake, Mheshimiwa Stephen Byabato. Bahati nzuri Waheshimiwa Madiwani kutoka Ludewa walikuja, Mheshimiwa Kalemani aliwapokea, alizungumza nao, alisikiliza changamoto za Ludewa, kwa hiyo, nampongeza na namshukuru sana. Halikadhalika Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Byabato, naye nampongeza anatupa heshima sana wanafunzi tuliomaliza Chuo Kikuu cha Tumaini pale Iringa. Hongera sana Mheshimiwa Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Serikali kwa bajeti nzuri ya Wizara ya Nishati kwa sababu umeme siyo anasa ni maendeleo. Nadhani kila mtu anaelewa, kwa hiyo, ni vema sana kuhakikisha kwamba hii mipango ambayo inatekelezwa inapewa fedha za kutosha ili wananchi waweze kupata umeme wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halikadhalika niishukuru sana Serikali tulipata mkandarasi, kule Jimboni kwangu Ludewa kuna kata zile za mwambao ambazo zina mazingira yenye changamoto sana kutokana na uwepo wa Ziwa Nyasa na milima mikali sana. Hata hivyo, nashukuru kwenye Kata za Lupingu, Lifuma na Makonde tayari mkandarasi ameshapeleka nguzo za umeme, kwa hiyo, wananchi wanamuomba tu aongeze kasi zile nguzo wameziona vya kutosha sasa wanatamani kuona umeme. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba utusaidie hapo. Halikadhalika tumempata mkandarasi mwingine kwa ajili ya kata zilizosalia; Kata za Ibumi, Lumbila na Kilondo, tunashukuru sana Serikali kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, sambamba na pongezi naomba Mheshimiwa Waziri afahamu kwamba kuna kata tano za kule Ludewa zina changamoto sana ya umeme; Kata hizo ni Milo na Mawengi. Kata hizi mbili zina mradi ambao ulikuwa unasimamiwa na mzalishaji binafsi ambaye alikuwa chini ya Kanisa Katoliki. Tumshukuru sana Baba Askofu Alfred Maruma huko aliko apumzike kwa amani, alitusaidia sana kupata umeme kwenye Kata za Milo na Mawengi kabla maeneo mengi nchini hayajapata umeme. Kwa bahati mbaya ule umeme sasa hivi unasumbua sana. Kwa hiyo, naomba Serikali iingilie kati ili wananchi wa Kata za Milo na Mawengi waweze kupata umeme wa uhakika kwa sababu kata hizi mbili zina wakazi wasiopungua 21,000, hospitali kubwa ya Milo ambayo iko chini ya Kanisa la Anglican, shule za sekondari na zahanati ambazo zinahitaji umeme.

Mheshimiwa Spika, pia kuna umeme ule wa Lugarawa ambao unahudumia vijiji 20 kwenye Kata za Lupanga, Madilu, Lugarawa, Mlangali, Lubonde na Madope. Nako huku kuna wakazi wasiopungua 51,000 na umeme huu pia ulikuwa chini ya mzalishaji binafsi unakuwa wa mgao zaidi ya saa 12 vilevile mzalishaji anashindwa kuuza umeme kwa maelekezo ya Serikali kwa sababu gharama zake za uzalishaji ziko juu. Kwa hiyo, wananchi 51,000 katika vijiji 20 kupata umeme wa mgao wa saa zaidi ya 12 na wakati mwingine mitambo ile inazima kwa muda mrefu inakuwa siyo sawa. Mheshimiwa Waziri niombe kwanza tuwashukuru wale wazalishaji binafsi kwa sababu walitusaidia sana lakini Serikali iweze kuingilia kati kwa sababu tayari TANESCO wameshaingia mkataba mdogo kununua umeme kwa kampuni ile ya Madope basi inunue umeme wote ili shughuli ya kusambaza na changamoto nyingine ziweze kufanywa na Serikali. Wananchi hawa wa vijiji 20 ndiyo waliokichagua Chama cha Mapinduzi, kwenye kata hizi zote wamechagua madiwani wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwanye Wizara hii ya Fedha. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa bajeti nzuri na pia Naibu wake na wataalam wote.

Mheshimiwa Spika, nilikwenda pale Hazina kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa walikuwa hawakupata zile fedha, nilivyowaona tu wasaidizi wa Mheshimiwa Waziri waliweza kutoa fedha zile kwa asilimia 100. Kwa hiyo, naomba niwe muungwana, nianze kwa kuwashukuru watumishi wa Hazina na naomba sana na awamu ijayo kwa sababu Ludewa na Njombe kuna muda mrefu sana wa mvua muda wa kufanya kazi unakuwa mchache sana, huu mwezi wa tano mpaka wa kumi ndio muda wa kufanya kazi. Ndiyo maana juzi nilimuona hapa Waziri wa Ujenzi baada ya kuona zile barabara zimesimama kwa sababu kule Hazina walikuwa hawajafanya malipo kwa mkandarasi muda mrefu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, naomba sasa nijikite kwenye hoja ambazo nilikuwa nimejipanga kuzisema kwenye Wizara hii. Niliwahi pia kuzungumzia ile kodi inayoitwa Capital Gain Tax, kodi ambayo inalipwa kwa mwananchi ambaye ameuza ardhi. Kodi hii Serikali inakosa mapato mengi sana kwa namna tu ambavyo sheria zimekaa na namna ambavyo inakusanywa. Kwa hiyo, nina mapendekezo machache ya kuboresha. Moja, naomba sana Wizara ya Fedha ikutane na wataalamu wa Wizara ya Ardhi watafute namna kodi hii iwe inakusanywa na ofisi moja, sanasana Wizara ya Ardhi. Kwa sababu mwananchi akishauza ardhi yake anakwenda kwa Afisa Ardhi anaambiwa aende TRA, wakati uthamini wa kodi wanafanya watu wa Ardhi, kwa hiyo, kunakuwa na mizunguko mwananchi nenda pale nenda pale. Kwa kweli tunampotezea muda sana mwananchi na ili wananchi waone raha kulipa kodi ni muhimu sana ikawa ina mazingira rafiki ya kuweza kuikusanya. Kwa hiyo, tuangalie namna mamlaka moja ikusanye kodi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nachoweza kusema ni kwamba ile asilimia 10 ya kodi hii inayokusanywa mwananchi akishafanyiwa uthamini kwa ajili ya kulipa ile kodi ya kuhamisha umiliki wa ardhi, kama umeuza kiwanja milioni 70 akiambiwa asilimia 10 milioni 7, mwananchi anachukua nyaraka zake anaondoka haji tena. Kwa hiyo, hata tukifanya sampling tukasema wananchi ambao wamenunua ardhi hawajaweza kubadilisha wafike tutagundua kwamba kodi nyingi sana hapa iko nje ambayo Serikali ingeichukua tungeweza kuipeleka kwenye miradi na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile hata namna hii ya kuwa na makisio ya kodi kwa mtu kuonana na mteja moja kwa moja tungeangalia namna ya kupunguza mifumo hii. Kwa sababu tuna wataalamu wanamaliza vyuo vikuu wanaweza kututengenezea mifumo ya computer ambayo tukitengeneza mwongozo mzuri wanaingiza tu data kwenye mifumo hii kodi inakadiriwa, lakini tukimpa mtu binafsi madaraka ya kukadiria kodi, saa nyingine mtu anaweza akakadiria kodi kubwa ili kutengeneza mazingira ya majadiliano kidogo na mwisho wake mazingira ya rushwa lakini ikiwa mtu akifanya mouse click kodi imekuja, kidogo inajenga trust kwa mwananchi. Kwa hiyo, tuondoke kwenye ule mfumo wa manual twende kwenye mifumo ya computer. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile nizungumzie maeneo ambayo hayajapimwa. Ukisoma Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura ya 334, inasema kodi hii inapaswa itozwe kwenye ardhi iliyopimwa tu, lakini kuna maeneo mengi ambayo hayajapimwa, kuna miamala mingi na mikubwa ambako tungeweza kupata kodi nyingi sana. Kwa hiyo, tuangalie maeneo haya ikiwezekana turekebishe sheria ili ituruhusu tukishirikiana na Wenyeviti wa Mitaa, tukawapa hata posho kidogo Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, watatusaidia kupata mapato mengi sana ambayo yatalisadia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Kibaigwa na sehemu nyingine unakuta mji mkubwa watu wanauziana petrol stations, majengo na ardhi kwa fedha nyingi. Kwa hiyo, unakuta kodi hii maeneo mengine Wenyeviti wa Mtaa wanakusanya na hawatoi risiti. Kwa hiyo, nafikiri ni eneo ambalo tunatakiwa tuliangalie.

Mheshimiwa Spika, maeneo ya vijijini kuna vikundi vinaanzishwa ambavyo vinachukua hadi tenda labda ya kufyeka barabara au kujenga mifereji, vikundi vya akina mama na vijana. Sasa vikundi hivi wanavyotaka kwenda kulipwa malipo yao wanaambiwa wawe na mashine za EFD, halafu wanatambuliwa kama wakandarasi. Mimi nafikiri hili eneo tungeangalia kwa sababu wale wanajikimu tu kwa zile kazi za kufyeka na kutengeneza mitaro miwili/mitatu. Kwa hiyo, kuwaambia wale wawe na EFD machine ambayo inauzwa Sh.590,000 na kuwawekea kama ni sharti la muhimu, nafikiri tungeangalia kwa sababu wale akina mama na vijana wanajikimu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, vilevile tuendelee kutoa elimu hasa kwa wale wajasiriamali wa vijijini kwa sababu kuna malalamiko kwamba wanakadiriwa kodi kubwa sana. Kwa hiyo, nipongeze sana juhudi za Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kuonesha kwamba eneo hilo sasa anakwenda kuliangalia kwa karibu. Vilevile Mheshimiwa Waziri nimemsikia mara kadhaa ameonesha naye ana dhamira ya kusimamia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siku moja nilikaa na wananchi pale Jimboni kwangu Ludewa, kundi la wafanyabiashara, wakaniambia kwamba suala la ulipaji kodi kiserikali mwananchi anapaswa awe mzalendo na anatambua umuhimu wake. Hata kwenye Imani, ukisoma Marko 12:17 wale Mafarisayo walimuuliza Yesu, je, ni halali kwa wananchi hawa kwenda kupeleka mapato kwa Kaisari? Kwa hiyo, aliwajibu pale, mpeni Kaisari yaliyo yake Kaisari. Kwa hiyo, hata misingi ya kiimani inatambua umuhimu wa kulipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia wale maaskari waliambiwa watosheke na mishahara yao, wasichukue zaidi na wasimsingizie mtu mashtaka. Kwa hiyo, haya mazingira ya Afisa wa TRA kukadiria kodi yeye binafsi na siyo mfumo yanajenga mazingira, hasa maeneo ya vijijini kwa mwananchi kukadiriwa kodi kubwa ili kuwe na negotiation na kuwe na malipo ya pembeni. Kwa hiyo, kukiwa na mfumo kwa kweli wananchi wanapenda sana kulipa kodi kwa sababu kwa sasa hivi wanaziona kodi zao zinakoenda; wanaona miradi ya maendeleo inafanyika kwa hiyo, wanapenda kulipa kodi. Kwa hiyo, tukitengeneza mazingira rafiki wananchi watalipa kodi bila shida yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kusisitiza kwamba wale wafanyabiashara wa vijijini huwa wanaambiwa wanunue zile mashine za EFD. Sasa ile mashine Sh.590,000/= wanaambiwa watarejeshewa lakini unakuta inachukua miaka mitatu mpaka minne kumrejeshea. Mtaji wa mwananchi wa kijijini unaweza ukakuta Sh.1,000,000, sasa ukimwambia mashine Sh.590,000/= kidogo tungetafuta namna nyingine ama Serikali ingekuwa inaziagiza nje na kuhakikisha zinapatikana kwenye ofisi za TRA ili bei ipungue kuliko kuacha wananchi waendelee kununua mashine kwa gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, nashukuru sana ila nimuombe tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha pale Hazina akipitapita yale malipo ya Barabara ya Lusitu – Mawengi yafanyike. Ile barabara imejengwa kwa miaka sita haiishi na chanzo kikubwa ni kucheleweshwa malipo kwa mkandarasi, hivi sasa amendoka site.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia mpango huu. Nianze moja kwa moja kwa kuishukuru sana Serikali, kuanzia Rais wetu, Mheshimiwa Waziri Mkuu na viongozi wote kwa miradi mingi ambayo imeelekezwa kwenye Jimbo la Ludewa. Wananchi wa Ludewa walikuwa wanaliwa sana na mamba Mto Ruhuhu, hawakuwa na daraja, wamelilia kwa miaka sita, nashukuru sana, sasa daraja lile limekamilika na wananchi wanaweza kufanya shughuli zao na hawaliwi tena na mamba. Kwa hiyo, naishukuru sana Serikali, ni jambo ambalo limewafurahisha sana wananchi wa Ludewa na wameahidi kuiunga mkono Serikali kwa nguvu zao zote na uwezo wao wote aliowajaalia Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa daraja lile limekamilika, kwa hiyo, wanaomba pia ile meli ambayo inapita Ziwa Nyasa kuanzia Itungi kwenda Nyasa nayo iweze kuanza safari zake. Kwa sababu kwa muda wa miezi mitano sasa, toka mwezi Mei, ilikuwa matengenezo na wananchi wanatumia usafiri wa mitumbwi na maboti; hivyo, wengi wanazama kwenye maji na kupoteza mali zao. Kwa hiyo, wanaiomba sana Serikali, huu uchumi ambao tumesema umekua kwa asilimia 4.8 na robo hii 4.7 nao wanatamani kufanya shughuli ili uchumi wao uweze kukua. Kwa hiyo wanaiomba sana Serikali meli ile ianze safari zake mara moja, maana katika Ziwa Nyasa, Wilaya ya Ludewa ina kata nane; kuna kata ya Kilondo, Lumbila, Lifuma, Makonde, Lupingu, Iwela, Manda na Ruhuhu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kata zote hizi nane zinategemea sana usafiri wa maji kwa sababu maeneo haya yana changamoto sana za barabara. Kwa hiyo, jambo hili linarudisha nyuma jitihada za wananchi katika kujishughulisha na uchumi ili nao waweze kuongeza kipato chao na kulipa kodi ili uchumi wa nchi yetu uweze kukua zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, upande wa sekta ya kilimo kuna changamoto moja kwamba hizi sheria zetu nyingine zimekuwa kama zinadidimiza wananchi. Kuna Sheria ya Matumizi ya Rasilimali za Maji; Sheria Na. 11 ya Mwaka 2009. Sheria hii imeanzisha utaratibu kuwa, mtu yeyote anayetaka kutumia maji, anatakiwa apate kibali ambalo siyo tatizo; lakini sambamba na kibali hicho, kuna tozo ambazo zimeanzishwa. Sasa wananchi wa Mkoa wa Njombe na hasa Ludewa Kata ile ya Madilu na Madope wanalima sana viazi vya umwagiliaji. Sasa sheria hii inawarudisha wananchi kwenye kilimo cha kutegemea mvua, kwa sababu mwananchi ananunua ma-roll yale ya mabomba, anatafuta maji, anachimba mtaro, anaingia gharama kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inamwanzishia kodi ya shilingi 250,000 na gunia moja la viazi unakuta linauzwa shilingi 12,000. Kwa hiyo, ili upate hizo 250,000 unahitaji siyo chini ya gunia 23. Kwa hiyo, tozo hii naiomba sana Serikali, kwani inakuwa inawarudisha wakulima kwenye kutegemea kilimo cha mvua. Hii iko sana maeneo ambayo yana miradi ile ya umeme wa maji. Hizi jumuiya na haya mabonde yanakwenda kutoa elimu, yanaanzisha jumuiya za watumia maji. Kule kwangu wananchi wanalia sana na hii tozo ya shilingi 250,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwenye sekta hiyo hiyo ya kilimo, Wabunge wengi wamezungumzia changamoto ya mbolea. Nitatoa mfano wa bei chache ambazo ziko kwa Njombe. Mbolea aina ya DAP ilikuwa inauzwa shilingi 55,000 mwaka 2020, lakini sasa hivi inakwenda kwa shilingi 97,000 mpaka shilingi 106,000; na hii mbolea ni muhimu sana kutokana na virutubisho ambavyo vinahitajika kwenye udongo. Kwa hiyo, kuna mbolea nyingine ambayo ni muhimu ya UREA, nayo imetoka kwenye shilingi 55,000 mpaka shilingi 80,000 au shilingi 90,000. Kwa hiyo, imepanda karibia mara mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mbolea nyingine ambayo inahitajika zaidi aina ya CAN, nayo kwa sasa inauzwa kati ya shilingi 60,000 mpaka shilingi 72,000 kwa Mkoa wa Njombe. Kwa hiyo, kwa hali hii, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba Serikali ina kila sababu ya kutoa ruzuku kwenye mbolea ili bei iweze kushuka irejee kwenye hali yake ya mwaka 2020 au pungufu zaidi ili wakulima waweze kulima mazao yao kama kawaida, kwa sababu imekuwa ni kilio kikubwa sana. Kwa hiyo, naomba Serikali ichukulie katika uzito wa pekee ili tuweze kumnusuru huyu mkulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kwenye sekta hii ya kilimo, naishukuru sana Serikali ilitoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa mahindi. Bahati mbaya sana mfumo uliotumika mwaka huu wa kutumia vikundi vya ushirika umewaumiza sana wale wakulima wenye gunia tano, sita saba au 15, wengi hawajauza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda Kijiji kimoja cha Mkongobaki kufanya mkutano, nikajaribu kuuliza pale wakulima mmoja mmoja ambao waliweza kuuza mahindi. Kwa kweli katika Kata ile ya Mkongobaki nilipata mwananchi mmoja tu. Kwa hiyo, zile tani nyingi hazieleweki zilikwenda wapi? Wakulima wanalia mahindi yanaoza, sasa hivi watoto wanaripoti Vyuo Vikuu, masomo ya mahindi hakuna. Kwa hiyo naomba hapa napo paangaliwe mfumo ule, ama tungeweza kuwaandaa wananchi kwa kuwapa elimu ya kutosha au tungetumia mfumo wa soko la miaka yote, tusingepitia kwenye hivi vikundi. Kwa Ludewa, wananchi; mkulima mmoja mmoja wameumia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niishukuru Serikali kwenye miradi ya umeme. Miradi ya umeme kwa kweli vijana wa kileo wanasema Serikali imeupiga mwingi sana. Kule kwangu Ludewa kuna vijiji ambavyo havina umeme kabisa ambavyo ni vitatu. Naomba Serikali iweze kuviingiza kwa wakandarasi hawa REA. Kuna Kijiji cha Ndoa, Kijiji cha Kimata na Kijiji cha Kitewele. Vijiji hivi havijaingia kwenye Mpango ili wananchi hawa nao waweze kuona wananufaika na uchumi huu ambao uko chini ya Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ameelekeza fedha nyingi kwenye Mpango huu kwa ajili ya miradi ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, kuna hii miradi ambayo ya umeme ya wazalishaji binafsi. Kuna Kampuni ya Madope, inazalisha umeme kwa ajili ya vijiji 20. Kwa hiyo, umeme huu umekuwa na changamoto ya mgao wa masaa zaidi ya 12 kwa muda wa miaka miwili sasa. Naishukuru Serikali na Waziri wa Nishati, Bodi ya REA imekwenda kule na wameona changamoto hizi.

Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba ile tathmini waliyoifanya ya kutatua hizi changamoto ziende haraka ili Kata ya Mlangali, Lubonde, Madilu, Madope, Lupanga na Lugarawa waweze kupata umeme wa uhakika na wa bei nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwenye kipengele cha uchumi shindani na hii miradi vielelezo, kuna huu mradi wa Mchuchuma na Liganga, nashukuru sana Mheshimiwa Rais alishatolea maelekezo kwamba miradi hii ianze, amechoka sana kuisikia; na ninafikiri ametambua kwamba miradi hii itatoa ajira nyingi sana. Ajira za moja kwa moja zaidi ya milioni nane pale zitapatikana. Wale wote watalipa kodi Serikalini, Serikali itaongeza mapato nao watapata kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hoja unayoizungumza ya mabilionea, sisi pale tuna makaa ya mawe ambapo leseni zake zote zimeshikiliwa na NDC halafu uchimbaji haufanyiki. Kwa hiyo, wangepewa wachimbaji wadogo, nina imani (namwona Mheshimiwa Biteko ananisikiliza vizuri) na sisi Ludewa tungezalisha mabilionea. Naomba wananchi wale waweze kulipwa fidia wakati Serikali inaendelea na majadiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, nakushukuru sana. (Makofi)