Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Issa Ally Mchungahela (7 total)

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, ninayo maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikipoteza pesa nyingi sana, hasa kwenye miradi na miradi ya maji ikiwapo hasa huu mradi wa Chipingo. Hii imetokea mara nyingi kutokana na watendaji ambao sio waaminifu wakishirikiana na wakandarasi kuhujumu Taifa kwa kutotimiza majukumu ya mikataba yao. Je, Serikali ina tamko gani kuhusiana na suala hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sina shaka na utendaji wa Wizara hii; Mheshimiwa Aweso pamoja na timu yake wanachapa kazi sana lakini wale watendaji wenu kule wanawaangusha. Je, Mheshimiwa Waziri au Naibu Waziri anakubali kuambatana na mimi kwenda kuangalia hali halisi mkajiridhisha kisha mkatatua changamoto hii kwa umakini kabisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge Issa Mchungahela kutoka Jimbo la Lulindi, kama ifauatvyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara kwa sasa hivi tumekuwa tukifanya jitihada za kuona kwamba watendaji wanaendana na kasi ya hitaji la Wizara yetu kwa sababu, madeni yote na miradi ambayo imekuwa ya muda mrefu awamu hii tunaelekea kuikamilisha.

Mheshimiwa Spika, hivyo, napenda kumtoa hofu Mheshimiwa Mbunge kwa hawa watendaji ambao wanakiuka maadili yao ya kazi na kuweza kuwa wahujumu katika shughuli zao tayari tunawashughulikia na tayari tuna mkeka mpya wa Wahandisi ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao kadiri ambavyo tunahitaji watuvushe.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na suala la kuambatana, Mheshimiwa Mbunge aondoe hofu. Hiyo ndiyo moja ya majukumu yangu na ninamhakikishia baada ya kukamilisha ziara yangu kwenye maeneo mengine, basi na hata huko Masasi pia nitakuja na nitajitahidi kufika kwenye majimbo yote kuona suala la maji linakwenda kupata muarobaini.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Imekuwa ni changamoto kubwa sana kwenye masuala ya pembejeo hasa muda. Mara nyingi sana kwamfano jimboni kwangu kumekuwa na changamoto ya kuchelewa pembejeo kila muhula na hili jambo linajirudia mara kwa mara. Je, Serikali inaona jinsi gani ya kuweza kulitatua tatizo hili kwa haraka hasa hususan katiak msimu huu wa mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Mchungahela kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la uchelewaji wa upatikanaji wa pembejeo una mahusiano ya moja kwa moja na upatikanaji wa fedha. Kw ahiyo tumebadili mifumo, sasa hivi tunatumia bulk procurement system ili tuweze kupata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu. Tunaamini kwamba kuanzia msimu unaokuja kwa maeneo ya Lindi, Mtwara wanaolima korosho mtaona mabadiliko ya upatikanaji wa pembejeo.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, naomba nijenge maswali yangu kupitia kwenye hoja tatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya ulinzi wa nchi hii; pia barabara hii ni muhimu sana kwa usafirishaji wa mazao ya ufuta na korosho katika kata zilizopo pembezoni mwa Mkoa wa Mtwara; barabara hii ni muhimu vile vile kwa usafirishaji wa ufuta na korosho kutoka katika maeneo ya nchi jirani ambayo mazao hayo hayana masoko kule:-

(i) Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami? (Makofi)

(ii) Je, Serikali ina commitment gani kwamba barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami na lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela yote mawili kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, naomba tu nitoe taarifa kwamba barabara hii ni barabara ambayo inafunguliwa. Kwa hiyo awamu ya kwanza ni kuifungua barabara hii yenye urefu wa kilometa 365 na ikishafunguliwa ndipo utaratibu wa kuijenga kwa kiwango cha lami utaanza kufanyika.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetambua umuhimu wa barabara hii, kwanza ni barabara ambayo ni muhimu sana kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama, lakini pia ni barabara muhimu sana kwani ikishafunguliwa itafungua uchumi na itaboresha maisha ya wananchi wengi ambao wanaishi katika kata ambazo amezitaja.

Mheshimiwa Spika, barabara hii inatoka Mtwara hadi Ruvuma na ni barabara ambayo inaambaaambaa na Mto Ruvuma. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya hatua ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha changarawe, hatua za ujenzi kwa kiwango cha lami zitafuata kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, hali inayoonekana Manispaa ya Iringa yaani inafanana moja kwa moja na hali iliyopo kwenye Halmashauri ya Masasi. Kwa sababu ni kata 18 kama ilivyo, lakini hali kadhalika vituo vya afya viwili na hali ni mbaya kabisa.

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Mchungahela.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu je, ni lini Serikali itatuwezesha kuwa na vituo vya afya zaidi, maana yake vituo viwili vya afya ni vichache?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchungahela, Mbunge wa Jimbo la Lulindi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri ya Masasi Vijijini katika mwaka wa fedha kuna fedha ambazo zimetengwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kujenga vituo vya afya. Kwa hiyo, naomba nimuhakikishie kambwa pamoja na bajeti yetu 2021/2022 kutenga fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya kwa mapato ya ndani lakini pia kwa fedha za Serikali Kuu tutaendelea kutenga fedha kuhakikisha jimbo hilo pia linapata vituo vya afya.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikifuatilia suala hili kwa muda mrefu sana na majibu yamekuwa ni hivihivi. Naomba Serikali itoe commitment ni lini watalipa deni hili.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na kutokuwa na umakini hasa hasa katika ulipaji wa madeni ya ndani, Serikali haioni sasa ni muda wa kulipa riba katika madeni haya ya ndani pia kama vile wanavyolipa madeni ya nje na riba.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mchungahela maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la riba, mikataba ilikuwa haionyeshi kwamba kutakuwa na riba pale ambapo kunapokuwa kuna ucheleweshaji lakini siwezi kutoa commitment ya hilo jambo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu lini watalipwa nataka nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na kweli amekuwa akifuatilia yeye na Wabunge wa Mkoa wa Lindi na Mtwara na baadhi ya maeneo mengine ya nchi yetu kuhusu hawa waliogawa miche. Niwahakikishie kwamba mwaka ujao wa fedha watalipwa watu wote waliosambaza miche na sisi Wizara ya Kilimo tumeshamaliza zoezi hili na tumepeleka hazina.

Mheshimiwa Spka, vilevile waliokuwa watumishi wa umma kwa maana ya Wakurugenzi na Madiwani kwa kuwa kulikuwa na mikataba halali, haki zao zitalipwa na haziwezi kudhulumiwa kwa kuwa tu ni mtumishi wa umma. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Naibu Spika, hii barabara ya Tandahimba ni barabara ya muda mrefu sana imeahidiwa kwa muda mrefu sana tangu wakati wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Serikali itakuwa imeamua lini kufanya kwa vitendo kutimiza ahadi zake kwa sababu barabara hii ni ya muda mrefu sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ally Mchungahela Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii imeahidiwa muda mrefu lakini Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba barabara hii tayari Serikali imeshaanza kutekeleza kwa vitendo ambapo kilometa 50 zimeshajengwa na katika bajeti tunayoenda, bado tunaendelea tumetenga Billioni tatu kwa ajili ya kuanza barabara hii ya Mnivata kwenda Tandahimba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara bajeti itakapoanza kutekelezwa barabara hii itatangazwa na itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Spika, hali ya kufunga mpaka huu kwa muda mrefu imesababisha mkwamo mkubwa wa kiuchumi kwa wananchi katika eneo hili.

Je, hivi Serikali haioni sababu ya kufungua mpaka huu kusudi wananchi wanufaike na zile fursa zilizoko katika eneo lile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge kama ataangalia zaidi katika jibu langu la msingi nimesema kwamba, ufunguaji wa kituo hiki unategemea zaidi makubaliano ya nchi mbili baada ya kukaa na kuangalia namna ya kuweza kufungua kituo hiki kwa ajili ya kuwapatia huduma wananchi. Nimesema Serikali inaendelea kufuatilia hali hii ili kuona namna bora ya kuweza kukaa na jirani zetu, ili kuweza kuwafungulia.

Mheshimiwa Spika, kikubwa afahamu tu kwamba, lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma katika mpaka huu katika hatua za uingiaji na utokaji na hali ya ulinzi na usalama inaendelea. Hivi tunavyozungumza vipo vikosi vyetu ambavyo vinaweka amani na utulivu katika eneo hilo na huduma nyingine zinapatikana. Ninakushukuru.