Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Daniel Baran Sillo (4 total)

MHE. SILLO D. BARAN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa bado mgogoro huu unafurukuta katika vijiji nilivyovitaja, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kufanya ziara ili wananchi wapate kutatua migogoro hii?

Mheshimiwa Spika, swali la piliā€¦

SPIKA: Kwa nini Waheshimiwa mnamgombea Mheshimiwa Waziri kama mpira wa kona aje majimboni kwenu?

Endelea Mheshimiwa swali la pili.

MHE. SILLO D. BARAN: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mwaka 2019 ulitokea uharibifu wa mazao ya wananchi katika vijiji nilivyovitaja ambao ulisababishwa na wanyama hasa tembo, je, ni lini Serikali itawalipa kifuta jasho wananchi hawa ambao mashamba yao yameathirika?

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Sillo juu ya kuongozana na mimi maana ni majukumu yangu ya kazi, hivyo hilo niko tayari baada ya Bunge lako hili Tukufu tutaenda naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza ambalo ameuliza juu ya uharibifu wa wanyama wakali; Serikali inawajali sana wananchi wake na inatambua kwamba kuna uharibifu wa wanyama wakali ambao wamekuwa wakiwasumbua wananchi hasa wale ambao wanakuwa wamepanda mazao yao na wanyama wakali hususan tembo huenda katika maeneo hayo na kuharibu.

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua hilo ilianzisha Mfuko ambao huwa tunalipa kifuta jasho au kifuta machozi. Kifuta machozi au kifuta jasho ni kwa ajili ya kuwapoza wale ambao wanakuwa wameathirika na changamoto hii ya wanyama wakali. Hivyo, hadi Machi, 2020, Serikali ilikuwa imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 5.9 kwa ajili ya kifuta machozi au kifuta jasho kwa wananchi hawa ambao wamekuwa wakiathirika na changamoto ya wanyama wakali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kuhakiki madai yote ambayo wananchi wameathirika na changamoto hii ya wanyama wakali na itaendelea kulipa kadri inavyopata taarifa.
MHE. SILLO D. BARAN Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pamoja na majibu hayo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umeshakamilika, je, ujenzi wa barabara hii unaweza ukaanza kwenye bajeti ijayo ya mwaka 2021/2022? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pilli, kwa kuwa barabara hii inafanana na barabara ya Magugu kwenda Mbuyu wa Ujerumani kupitia Daraja la Magara ambalo limejengwa na Serikali kwa thamani ya shilingi bilioni 13 hadi Mbulu; je, Serikali ipo tayari kuanza ujenzi wa barabara hii pia ili kuchochea maendeleo katika eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Sillo Baran, Mbunge wa Babati Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Dareda hadi Dongobesh yenye urefu wa kilometa 54 kwenye maeneo ya escarpment ambayo tulijua yana changamoto yameshajengwa kilometa 10. Pia tumekamilisha usanifu wa kina mwaka huu, kwa hiyo, tusubiri bajeti; siwezi nikasema sasa hivi lakini nadhani litajitokeza kwenye bajeti lakini kwa maana ya kukamilisha usanifu wa kina maana yake tuna mpango wa kujenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami na hiyo tu ni hatua za kuelekea huko.

Mheshimiwa Spika, ameuliza barabara inayoanzia Mbuyu wa Mjerumani hadi Daraja la Magara. Barabara hii pia ipo kwenye mpango na itakamilika kufanyiwa usanifu wa kina Septemba mwaka huu. Kwa hiyo, tayari pia ipo kwenye mpango kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya upungufu wa watumishi iliyoko Wilaya ya Korogwe ni sawa sawa kabisa na iliyoko Jimbo la Babati Vijijini hasa Sekta za Afya na Elimu. Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hili la watumishi hawa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tuna upungufu wa watumishi lakini kama ambavyo nimetangulia kusema kwenye jibu la msingi, Serikali imeendelea kutenga ikama kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kuandaa na kuomba vibali vya ajira kila Mwaka wa Fedha ili kuendelea kuongeza idadi ya watumishi katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Kwa hivyo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Baran kwamba katika Wilaya ya Babati pia tutahakikisha tunaipa kipaumbele katika ajira za Mwaka wa Fedha ujao ili angalau tuendelee kuboresha idadi ya watumishi katika halmashauri hiyo.
MHE. DANIEL B. SILLO: Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri yanayotia moyo, lakini naomba niulize swali moja tu dogo la nyongeza.

Je, Serikali ipo tayari kuongeza wataalam wa afya katika Kituo cha Afya cha Ufana ambacho kipo jirani na Bashnet ili wananchi wa Bashnet wapate huduma ya afya wakati wanasubiri kujengewa kituo cha afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daniel Baran Sillo, Mbunge wa Babati Vijijini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo tayari kuongeza watumishi katika kituo cha afya katika ajira hizi za watumishi 2,726 zilizotangazwa, ahsante sana. (Makofi)